Simulizi: My family 02

Simulizi: My family 02

Tajiri Sinabay

JF-Expert Member
Joined
Dec 25, 2024
Posts
1,333
Reaction score
3,619
Simulizi: My family
Sehemu ya pili
Mtunzi: Kijana Masikini


ILIPOISHIA
"Daa Qashy nae akapanda bodaboda na kumpa ishara dereva aifate pikipiki aliyopanda yule mzee. Muda huo watu walikuwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, mimi nikaenda sehemu aliyotupa simu Sista na kukuta imepasuka kama unavyo iona, baada ya hapo nikachukuwa simu yangu ili nikupigie lakini iligoma mtandao, nikaazima simu ya mshkaji hapo jirani nilipopiga namba yako ilijibiwa haipo"

Aliongea Mshamba huku akininesha simu iliyo kwenye kiti ambacho hukaa Qashy Lilith.

"Ooophwwwwwwww......"
Nilishusha pumzi huku ubongo wangu ukifanya mchakato utakaoamua ni swali lipi liwe la kwanza kumuuliza Mshamba, kwani hadithi aliyonipa imeniacha na maswali ambayo hata idadi yake tu siijui

ENDELEA

"Dah ni nini hiki au Qashy alikuwa sirias"
Niliongea huku nukikumbuka kama majuma mawili nyuma Qashy aliwahi kuniuliza ikitokea yeye amekufa nitaishije bila uwepo wake, nikamjibu sijuwi nitaishije kwasababu haijatokea.
Akaniambia kifo chake kwangu kipo karibu hivo anaomba siku tutoke nje ya mji sehemu ambayo itakuwa na utulivu mkubwa mno ili awe huru kufurahia penzi langu kwa masiku ya mwisho.

Nilimchukulia Qashy kama mtu ambae akili yake haipo sawa pengineni kwa sababu ya mambo ya biashara yake ama ni mambo mengine, nilijaribu kumuuliza maana ya maneno yake lakini alisema atanieleza vizuri siku tukiwa mbali, yaani tukiwa nje ya mji kama alivo taka. alikuwa amelaza kichwa chake kifuani pangu, nikamuitikia kila alichokiongea usiku ule huku nikimchezea nywele zake, nilimshushia mtanange mzito ndani ya usiku ule kuirudisha akili yake katika hali ya kawaida mrembo huyo mwenyewe asili ya kichaga ambae ni mrefu mwembamba na mweupe kiasi.

"Mshamba naomba tufunge hapa twende nyumbani hapa hatutaongea kwa uhuru"

"Sawa bro"
Tukafunga duka na kuchukuwa bajaji, Umbali kutoka soko kubwa dadi kufika nyumbani ninapoishi ni mdogo sana, kwa mwendo wa mguu ni kama dakika nane tu.
Ndani ya muda mfupi tu tukawa nyumbani.

"Halafu bro umesahau samaki kule dukani"
"Tuachane nao twende tudili na hili jambo la msingi"

Tukaingia ndani kisha nikaanza kumhoji Mshamba maswali mengi kuhusiana na utowekaji wa Qashy.

Japo Mshamba alieleza mengi lakini yote yalikuwa yanaendana na maelezo aliyonipa kule dukani hapakuwa na jambo ambalo ni ziada sana.

Ila kitu nilichokigundua mpaka sasa hivi ni kwamba watu wa karibu wa Qashy namba zao za simu zimefungiwa ama zimesitishiwa huduma.

"Mshamba. hapa sasa wewe nenda nyumbani mimi naenda kwa Qashy. Asubuhi kafungue goli kama kawaida ila kama utahisi unahitaji kupumzisha akili basi utabaki nyumbani tu"

"Poa bro nitaangalia hiyo asubuhi nitaamka vipi, ila kuwasiliana ingekuwa ni vizuri zaidi ili mimi pia nijuwe ni nini kitakacho endelea utapoenda kwa Daa Qashy"

"Ni kweli lakini sasa mimi sina muda wa kusajili laini zingine, hii ni saa kumi na dakika thelathini na moja natakiwa niwahi ili pengine tunaweza kupata mwanga wa hiki kinacho endelea"

"Poa bro ila mimi nitapita pale dukani kuchukuwa simu ya Daa Qashy na kuwatoa wale samaki maana hadi kesho wataharibika"

"Kachukuwe samaki tu simu iache humo humo kwa usalama zaidi"

Akaitikia Mshamba hachekwi na kutoka ndani ili kuelekea nyumbani kwao mtaa wa majengo anako ishi na wazazi wake.

Nikatoka ndani na kuingia barabarani kuianza safari ya kuelekea kwa Qashy Mtaa wa kiangu ambako amepanga.

Nikasimamisha pikipiki ambayo ilikuwa inakuja kutokea mbele yangu.

"Nipeleke nangwanda bro"

Dereva bodaboda akaigeuza pikipiki nikapanda.
Baada ya kama dakika mbili tu tukawa tumefika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona. Nikashuka na kumlipa, nikaanza kutembea kuelekea nyumbani kwa Qashy. Nikatembea taratibu mno huku nikiiona kwa mbali nyumba anayoishi Qashy lakini mazingira yalikuwa ni ya kawaida mno, niliwaona watoto wa kike Mama mwenye nyumba wakicheza mdako huku dada mmoja ambae ni mpangaji mwenzake Qashy alikaa kwenye kibaraza anachezea simu.

"Habari Evelyn"
Nilimsalimia Dada huyu anaeitwa Evelyn Salt baada ya kufika alipoketi

"Salama shemeji habari za masiku"
"Salama nashukuru, hivi Habibi wangu yupo ndani?"

"Hapana, alikwenda kazini tangu asubuhi hajarudi, yeye kama kawaida yake kurudi ni jioni sana vipi hujamtafuta kwenye simu?"

"Hapatikani kwenye simu"

"Ahaa ngoja nimjaribu mimi"
Aliongea huku akipangusa simu yake.

"Hii! hivi watu wa nyumba hii leo tuna nini"
Aliongea Evelyn baada ya kujibiwa namba anayopiga haipo

"Mmm vipi?"

"yaani mimi unaponiona hapa hii line nimetoka kusajili sasa hivi laini zangu zote zimezuiliwa huduma, na hata hivyo nimejaribu kurenew zote zime goma, Mama humo ndani nae hivyo hivyo laini pia hadi baba pia nae katoka kwenda kurenew, sasa nashangaa nampigia Qashy nae wanajibu namba haipo! Cha kushangaza zaidi watu wengine mtaani kote huko nilikopita hakuna mwenye hiyo shida"

'Hivi huyu Qashy alikuwa ni nani! Hivi kulikuwa na Qashy Lilith mwingine nyuma ya huyu ninaemfahamu? Halafu kwanini alimwambia Mshamba kwamba aliipenda pesa kabla yangu'

"Kim Babaangu habari"

Ilinitoa mawazoni sauti ya Mama Edina Mama mwenye nyumba hii, nikageuza kichwa na kumtazama mlangoni alipo simama.

"Aa.. Salama Mama Habari za tangu juzi"

"Salama namshukuru mungu. nakuomba tuongee kidogo"

Aliongea Mama Edina huku akizama ndani, nami nikamfata tukapitiliza hadi nyuma,
Mlango wa chumba cha Qashy ulikuwa umefungwa.

Mama Edina akaketi kwenye kiti cha plastiki nami nakaketi kwenye kiti cha pembeni yake.

"Kim.. wewe ni kama mwanangu, mwenzako Qashy nae ni mwanangu pia hivo kila nitakacho kuuliza naomba unipe majibu ya kweli ili nione namna ambavyo naweza kuwasaidia"

Taratibu moyo wangu ukaanza kuongeza kasi ya mapigo yake huku nikimtazama Mama Edina usoni kwani sijuwi anataka kuniambia nini.

"Kim katika siku za hivi karibuni mahusiano yenu yapo katika hali gani?"

"Tupo vizuri tu Mama, vipi kwani kuna tatizo"

"Ndiyo kuna tatizo ndiyo maana nikakwambia nataka unipe majibu ya kweli"

"Sisi tupo sawa tu si unaona hadi juzi nimekuja hapa na wote tulikuwa na furaha tu, tena hadi tukawa tunataniana kama kungalikuwa na shida kati yetu unadhani tungeweza kuwa katika hali ile! Kwani kuna nini Mama hadi uniulize hivo?"

"Unacho kisema kinalandana na ukweli lakini sitaki kuamini kwamba hamuna tatizo kabisa. hujawahi kulala na mwanamke mwingine labda au hata kutongoza mwanamke mwingine?"

"Hapana mamaangu sijawahi kwa hivi karibuni labda zamani kidogo wakati mapenzi yetu hayajafikia kuwa ya wazi"

"Ni kama muda gani na ulimtaka tu huyo mwanamke au ulilalanae kabisa?"

"Kipindi hiko penzi letu lilikuwa na kama mwezi tu, kama inazidi basi ni siku chache, na sikuwahi kulala nae huyo mwanamke, kiufupi ni kwamba tangu niwe na Qashy sijawahi kukutana kimwili na mwanamke mwingine"

"Ahaa nimekuuliza hivo kwa maana, ni kama mwezi huu hali ya Saikolojia ya Qashy haipo sawa, muda mwingi anakuwa ni mtu wa kujiudhi sana na hata uchangamfu wake kwa ujumla haupo kama zamani. mwili wake pia umepungua kiasi Qashy wa miezi mitatu nyuma sio huyu wa leo, sasa kile kitu alichokibeba na kuwa katika hali ile haifai kabisa, inatakiwa awe mtu wa furaha kama anavyoishi siku zote, tena ikibidi furaha yake iongezeke. Ndiyo maana nikakuuliza haya ili kama kuna mahali mnakwaruzana katika safari yenu nione ni kwa namna gani naweza kuwasaidia"

"Umesema kitu alicho kibeba haifai awe katika hali ile ni kitu gani kakibeba?"

Nilimuuliza huku nikimtazama usoni kwa umakini wa hali ya juu.

"Unamaanisha hujuwi kwamba Qashy ni mjamzito?"

"Mjamzito!"

"Eee kwani hajakwambia?"

"Hapana hajawahi kuniambia kwahiyo wewe umejuwaje au amekwambia mwenyewe"

"Hahahah.. eh nyie watoto wa kiume kwenye mambo haya mungu kawafumba pakubwa. kwahiyo mpaka mnalala kitanda kimoja na bado hujuwi tu kwamba ni mjamzito! Yale mapua yake nayo huyaoni kwamba yanazidi kutanuka? Una muda gani sasa hujawahi kumuona Qashy anakula samaki?"

Nikakaa kimya huku nikiyatafakari maneno ya Mama Edina ambayo yamekuja na mshangao mkubwa sana kwangu.
Ubongo wangu taratibu ukaanza kurudisha kumbukumbu za mara nyingi ambazo nimewahi kula chakula pamoja na Qashy na akawa anakwepa kabisa mchuzi wa samaki au kula samaki hata kama kakaangwa.
Kigezo chake kilikuwa ni kwamba amekula sana samaki tangu tumekuwa pamoja hivyo sasa wamemtosha.
Wajawazito wengi huwa na changamoto ya kutapika pindi wanapo kula samaki au kitu chochote chenye shombo kupindukia, hasa ujauzito unapokuwa na miezi michache.

"Vipi mbona upo kimya? Qashy ni mjamzito mimi sijampima wala hajaniambia ila ni mjamzito, tena haupungui miezi mitatu hivyo jiandae kuitwa baba kama hujawahi kuitwa"

"Mh sawa kwahiyo Qashy mwenyewe tangu atoke asubuhi ndiyo hajafika tena?"

"Eee kama alivokwambia Evelyn"

Nikawaza kwenda kufungua chumba cha Qashy lakini nikakumbuka funguo ya chumba chake sijaibeba nimeiacha nyumbani.

"Sawa Mama nitajitahidi kuona ni changamoto ipi inamsumbua ili tuweze kuitatua"

"Sawa ila usimwambie kuhusu suala la ujauzito kwa sababu atajuwa mimi ndiyo nimekwambia kwani nimeshamuona anatapika kama mara mbili hivi kila alipojaribu kula samaki, lakini katika hizo mara mbili zote alijitahidi kujifanya yupo sawa tu ni tumbo tu ndio linamsumbus ila mimi ni mtu mzima naelewa, na baada ya hizo mara mbili amebadilisha kabisa aina yake ya ulaji"

"Sawa Mama nashukuru kwa kunifumbua macho"

Nikamuaga Mama Edina na kutoka ndani huku nikitawaliwa na mawazo mengi.

'Mh mbona nashindwa kabisa kuelewa kabisa haya mambo, kama kweli Qashy ni mjamzito kwanini asiniambie? Kwanini pia aondoke katika mazingira ya namna hii, Inaamaana ndio kaondoka kweli? Lakini pia kwanini karibu kila namba ya mtu wa karibu imefungiwa mawasiliano, aaah haya mambo ni magumu. amesema anajuta kwanini aliipenda pesa kabla yangu , pia nisimtafute siwezi kumuona kwa jitihada zangu, Inaamaanisha ameondoka huku akijuwa kuwa ana mimba! Na hiyo mimba yang..?'

"Jamani shemeji unaondoka bila hata kuniaga?"

Ilinishutua sauti ya Evelyn Salt nikiwa katika msitu mkubwa wa mawazo, nikageuka nyuma na kimuaga kisha nikaondoka.

Nikatembea hadi karibu ya uwanja wa Nangwanda Sijaona, nikasimama chini ya mti uliopo nje ya uwanja huu huku mawazo bado yakiendelea kuniandama, muda huo ilikuwa ni kama saa kumi na moja na dakika kadhaa.

'Mh naanzia wapi kumtafuta huyu mtu, najuwa tu kwao ni moshi, sijuwi ni Mtaa gani kata wala wilaya, sijuwajui wazazi wake wala ndugu yake mmoja, isivyo bahati pia hana rafiki wa kudumu. mh nitaanzia wapi? nadhani teknolojia ndiyo inaweza kunisaidia kwenye hili, Ahaa ngoja nikamshirikishe Joanah pengine anaweza kunisaidia, ni mambo mengi huwa ananisaidia tena mengine huwa ananilaumu kwanini sikumwambia mapema. Joanah anaweza kuwa msaada kwenye hili sina cha kupoteza'

Mwili wangu ukapata nishati mpya baada ya kumkumbuka rafiki yangu Joanah ambae anafanya kazi TIFFANY DIAMOND HOTEL iliyopo karibu kabisa na soko kubwa la mtwara.
ITAENDELEA


Nakaribisha maoni, maswali, ukosoaji.
Nakini pia nakaibisha ushauri wa kiutunzi na kiuandishi.

pia soma hapa sehemu ya kwanza

 
Back
Top Bottom