Simulizi: My family

Simulizi: My family

Tajiri Sinabay

JF-Expert Member
Joined
Dec 25, 2024
Posts
1,333
Reaction score
3,619
TekTok-20250214-193428_1079x1385.png

Simulizi: My Family
Sehemu ya kwanza
Mtunzi: kijana Masikini

UTANGULIZI.
Wamakonde tunasema "nnume alage mmahe anyete"
Yaani "Mwanaume apambane hadi kukonda ili mwanamke anenepe"

Simulizi hii ni zawadi ya valentain day kwa mtu mmoja humu jamii forums,
Kama olivyo kwa konde boy ndivyo ilivyo kwa wamakonde wote tukipenda tunakuwa mazuzu.
Hivyo nimejitoa kwa hali zote ili kuhakikisha ninaileta simulizi hii.


MWANZO
Upepo unaovuma kutokea mashariki mwa mkoa wetu huu wa mtwara,
unaufanya mtumbwi wetu kuzidi kwenda kwa kasi huku mimi na rafiki yangu Edo kissy tukiendea na maongezi ya hapa na pale huku kila mmoja wetu akiwa na hamu ya kufika bandarini.

"Aliyesema hii kazi ya uvuvi ililaaniwa na mtume mimi namkubalia, yaani hela tulizopata tangu hili bamvua limeanza zinaweza kufika laki saba na.. huko, lakini hadi leo sijanunua hata kitu cha elfu kumi nikaweka pale na hela pia sina"

Aliongea Edo huku akitenganisha samaki katika mafungu mawili, wakubwa sana na wakubwa wastani.

"Hahaha.... ndiyo hivi hivi walivoishi wazee wetu hadi leo tunawalaumu kiwanja kilikuwa elfu nane, tisa na hawakununua kwa wingi, ila hata hivyo mwanangu umezidi matumizi makali"

Niliongea huku nikikaa vizuri ili kupata balansi ya kuongoza mtumbwi kwa sukani la mbao, kama ilivyo kwa vyombo vingi vya baharini nahodha/muongozaji hukaa nyuma hivyo hivyo kwenye mtumbwi.

"Chupi mwanangu.. ndiyo maana mzabzab kwenye bodaboda yake kaandika MJINI HELA TUNAPATA TATIZO CHUPI"

"Sasa kama unajuwa shida ni chupi kwanini uanze kusingizia mitume? Hahaha!"

"Ah sema Kim wewe unaweza yaani inakaribia miezi sita sasa uko na demu mmoja tu halafu wala huwazi, sijuwi Qashy Lilith kakulisha nini yule mchaga! maana sura hana, shepu hana, rangi hana yupo yupo tu, au unapagawa na chaji na waya za USB anazo kuhonga?"

"Halafu mwanangu unapenda kumkanyagia shemeji yako kinoma, hivi itafika siku ukamuheshimu"

"Aaa kwahiyo umemaindi?"

Aliongea Edo huku akisindikiza maongezi yake kwa kicheko na kuinua uso wake akinitazama.
"Kim, Kim, Kim.."

Aliniita Edo kissy kwa jina la Kim ambalo ni ufupisho wa jina langu la Kijana Masikini.

Edo kissy ni rafiki yangu ambae ni kama ndugu kwangu, kwani tumekuwa marafiki kwa muda mrefu lakini pia tumekuwa pamoja kikazi takribani miaka mawili sasa katika kazi yetu ya kuvua Samaki kwa kutumia Mshipi na ndoano"

" Toa maji, toa maji tutazama ujue"

Niliongea wakati nikijitahidi kuuweka sawa mtumbwi huu ambao tumeutweka kwa tanga kwani umeanza kuingia maji kutokana na kasi kubwa ya upepo, unaoingia kwenye tanga.

"Poa sema usijaze sana upepo"

Alinijibu Edo na kuanza kutoa maji kwa kopo la plastiki.

"Ila si unajua inabidi tuwahi kufika ili tuwahi kuuza Samaki kwa bei angalau, tukichelewa itakua kama jana hapa"

"Poa, halafu vipi na yule mwalimu wako wa jana mliishia wapi kwani, mbona tangu asubuhi hujamzungumzia?"

Aliniuliza Edo kuhusu realMamy ambae ni mwalimu mgeni katika shule ya msingi kata ya Rahaleo iliyopo manispaa ya Mtwara Mikindani, shule ambayo ipo karibu na nyumba ninayoishi"

"Ah alinipigia simu jioni eti akasema anataka nimfundishe kuogelea, mi nikaona hana mada"

"Hana mada kivipi sasa wakati anataka ajue kuogelea"

"Sasa walimu wenzake si wapo pale wanaojua kuogelea, tena hadi wakike wanaojua wapo kwanini asiwambie wamfundishe?"

"Sasa mwenyewe si kakuchagua wewe, kwa hiyo ukamjibu vipi?"

"Ah mi nimemwambia kwamba sina ujasiri wa kuingia kwenye maji na wewe halafu tukatoka salama"

"Hahahaha! Doh Kim unazinguwa kwahio ye akasemaj.."

"kwanza tuachane nae bhana toa joshi hiyo tuingie bandarini"

Nilikatisha maongezi ya Edo huku nikimuamrishe aifungue joshi (kamba ambayo inaweza kubadili muelekeo wa tanga) na ailegeze ili tuingie katika bandari yetu ya Kianga.

"Poa ila mwanangu usiniangushe, ujue hilo ni zali, hiyo ndio ndizi chini ya mndimu hiyo"

"Halafu Edo mimi kila siku nakwambia mimi najiona wa thamani maumbile yangu sio ya kumuonyesha kila mwanamke"

"Kim acha ufal* hayo ni maneno ya kike, maneno hayo waongee wakina Atoto sio dume kama wewe na bichwa lako kama beberu wa sauzi afrika uongee upuuzi kama huo, nipe mimi namba zake basi nikuoneshe mwanaume anatakiwa awe je"

"Shida yako Edo unafanya sifa kwenye mambo ya wanawake, Kumbuka hakuna mtu amewahi kupewa ubingwa wa kut* *ba, Zaidi na zaidi ni kujiongezea matatizo tu"

Niliongea huku nikifungua abdelemani (kamba inayoingiza na kutoa upepo kwenye tanga) ili kushusha tanga (tanga ni kitambaa au laikoni ambalo hutumika kukusanya upepo kwa kuwekwa juu ya mlingoti).

"Leo tumewahi naona sokoni pamechangamka kwahiyo hawa Changu tutaweka wangapi wangapi?"

"Hao wakubwa weka watano, hao wa saizi utaweka kumi, hao kolekole kwa sababu siyo wakubwa sana tutaweka wawili wawili, kitoweo utajuwa wewe tuchukuwe samaki gani"

Nilimjibu Edo huku wote tukishuka kwenye mtumbwi kwani tumefika bandarini ambapo kina cha maji ni kidogo kiasi cha kutuwezesha wote kusimama.

Mimi na Edo tunafanana kwa maumbo wote tukiwa ni warefu na wembamba wastani japo yeye ananizidi kidogo kwa urefu. Lakini pia mimi namzidi Edo kwenye umri kwani nina miaka ishirini na minane yeye ana miaka ishirini na sita.

Muonekano wa bandari hii ulikuwa ni wa kupendeza kwani ulipambwa na mchanganyiko wa watu walio onekana kuwa bize na pilikapilika za hapa na pale.
Huku wavuvi wenzetu wengi nao wakifika kitoka baharini.

Tukaweka vitendea kazi vyetu sawa na kubeba samaki wetu kwenye mifuko . Tukaanza kutembea kutoka kwenye maji kuelekea kwenye soko la bandari yetu hii ya kianga ili kuwauza.

"Kumi na sita.. kumi na sita.. Kumi na sabaa... Kumi na sabaa.. Wapi kumi na nane..?"

Tuliendelea kuzisikia sauti za wanadishaji wa samaki na makelele ya watu wengine huku tukikaribia mnadani.

Tukafika mnadani na kumkabidhi mnadishaji wetu samaki, akaanza kuuza samaki huku Edo akikusanya pesa mimi nikiwa ni muangalizi wa samaki kwani kama sio kuwa makini hata mnadishaji wetu anaweza kutuibia, kwani wanadishaji wengi wa samaki katika soko hili na hata masoko mengine akili zao zimeathiriwa na matumizi ya vilevi kupita kiasi, hivyo sio ajabu muda wowote wakafanya mambo yanayoharibu uaminifu.
Tuliuza samaki wetu na kuanza kutoka katika eneo hili la soko.


"Oya Kim tupa jicho kule mwisho"

Aliongea Edo huku tukielekea sehemu ambayo wamama na wadada wafanya biashara za vitafunwa viburudisho na vinywaji wamejitenga ili kufanya biashara zao.

"Mh mwanangu we kwa kupenda madem utashika namba moja kwa mkoa"

Nilimjibu baada ya kutazama aliko ashiria na kumuona msichana mmoja mzuri wa umbo sura hadi rangi, akiwa anaongea na simu.

"Sasa mwanangu wanawake si ndo wametuzaa kwanini nisiwapende"

Aliongea Edo huku akibadili muelekeo na kuelekea upande ambao yupo yule binti na kuniacha mimi nikielekea sehemu yenye vitafunwa.

"Enhee hafadhali Kim nimekuona hivi wewe wa kunipikisha mimi chakula kingi halafu usitokee"

Aliongea ephen_ muuza sambusa ambae anaishi Mtaa wa Magomeni, Mtaa ambao upo mbali usawa unaofika hata kilomita moja na mita mia saba kutoka kwenye pwani hii ya Kianga. Japo mimi naishi mtaa wa mbali na kwa kina Ephen lakini tumekuwa na mazoea kupitia biashara yake, kwani mimi ni mpenzi sana wa sambisa na yeye anajuwa kuzipika vizuri pia.

"Hi! kwa hiyo uliniwekea kweli?"

Nilimjibu huku nikimshangaa kwani swala la chakula tuliliongea jana katika hali ya utani na sikuwahi kufikiria kama angeliweka akilini.

"Sasa si uliniambia mwenyewe"

"Ah sasa mimi nakuja vipi kwenu usiku wakati wewe unaishi na wazee wako, mimi naingia kama nani kwa mfano?"

"Kwahiyo uliponiambia nikuwekee hukujua kwamba naishi na wazee au ulikuwa unanitoa akili?"

Aliongea Ephen huku akizungusha macho yake ambayo ni makubwa kiasi yaliyopamba uso wake wa duara.

" A aa... basi chibonge wangu usifike huko nisaheme nimekosea ila leo nakuja kweli, kwanza unajuwa kuukaanga vizuri mchele, isije nikakataa msosi hom halafu ukanilisha mnyoma? (ubwabwa usioiva)"

"Ahaa kumbe ndio maana hukuja uliogopa nitakulisha chakula kibichi, kwahiyo unamaanisha mimi sijuwi kupika si ndiyo? Sawa asante, tena wala usije isije ukapata ugonjwa wa tumbo kwa mipango ya mungu huko akasema ni chakula changu"

"Hahaha! Kwahiyo nije au nisije?"

"Bhanae nunua unachotaka kununua uondoke"

"Sawa nanunua ila nijibu kwanza nije?"

"Sitaki"

Alijibu huku akiuvesha uso wake hisia ya makasiriko na kuyafanya mashavu yake kuzidi kuonekana makubwa.


"Hahahaha.... Mtoto akililia wembe mpe umkate.."

Aliongea kwa sauti ya juu Miss Natafuta Mama muuza juisi za matunda na kuwafanya wamama na wadada wanao fanya biasha katika fukwe hii kuangua kicheko.

"Ephen mwaya usiwaze hakuna mkate mgumu mbele ya chai, ila hapa ni mjini ukimpenda mtu funguka, funguka bibi usije ukakosa fungu uliloandikiwa upo.."

Aliongea tena Miss Natafuta kwa lafudhi ya kutania na kimfanya Ephen aokote kokwa kavu ya embe dodo na kumrushia ili kumpiga. Vicheko vikazidi kutawala eneo hili kwani miss alikuwa ni kituko haswa.

"Kwahiyo miss unataka kusemaje kuna mtu mjini hapa ananipenda na mimi wala sijuwi?"

"Kha! hapo ni kumsukuma mlevi tu"

"Kim ujuwe unaniharibia siku na huyo mpumbavu mwenzio"

"Basi Ephen ngoja nimwite Edo akuletee Samaki mmoja ukampikie shemeji yangu supu"

Nilinunua kila nilichokihitaji na kuanza kuondoka kuelekea alipo akiendelea kuongea na yule dada ambae ni mgeni machoni mwangu.

"Edo ni saa ngapi kwani"

Niliongea huku nikiwakaribia kwani Edo ndiyo alikuwa na kopo tunalohifadhia simu zetu ndogo tukiwa baharini.

"Ni saa tisa na dakika kumi na sita, halafu simu zenyewe sijui zimepatwa na nini laini zote zimekaa Emergency"

"Labda ni hitilafu za kimtandao"

"Hitilafu za kimtandao wapi mbona huyu dada ana tunashea nae mitandao lakini yeye kweke simu inafanya kazi vizuri tu"

"Basi labda maji yaliingia kwenye kopo tutaangalia vizuri tukifika nyumbani. habari dada"

"Salama Kim mambo vipi"

"Safi, mbona unanifahamu halafu mimi sikujuwi"

"Hata mimi sikufahamu pia jina lako kaniambia Edo hapa"

"Ahaa. Edo vipi mmeshamaliza maongezi hapa tuondoke?"

"Ndiyo, kwani leo hatuogi huku huku?"
"Tutaoga nyumbani bhana kuchukuwe begi tuondoke"
" basi poa naita boda na kabisa tutembee, best sisi tunakwenda tutawasiliana"

"Poa hata mimi sina muda mrefu hapa naondoka"
Akapiga hatua na kutuach mdada huyu ambae sijalijua jina lake.

"Edo nilitaka kusahau mpelekee Ephen Loba wawili hao akapikie ugali"

"Poa, sema yule dogo kavu kinoma anajiona kama yeye ndio mwenye hii mtwara, yaani kama angekuwa mtoto wa mbunge yule, sijuwi kama asingejenga barabara ya kweke akawa anapita mwenyewe tu"

"Hahahaha.. acha makasiriko bhana, wewe unataka kila mtu akuchekee tu, peleka Samaki hao mimi nakusubiri huku mbele"

Niliongea na kuanza kupiga hatua kufata barabara yenye uelekeo wa nyumbani.
Edo akafika na bodaboda tukapanda wote kuelekea chikongola anakoishi yeye.
Tukafika getoni kwa Edo kwenye nyumba ambayo amepanga ambapo kuna wapangaji wengine. tukamlipa bodaboda na kuingia getoni kwa Edo ili tugawane pesa zetu tulizozipata katika mauzo ya Samaki.

"Huu mwaka wewe Mchaga wa kuchovya usipojenga sijuwi!"
Aliongea Edo huku akiweka mfuko mdogo wa laikoni wenye pesa juu ya meza iliyopo humu chumbani kwake, kisha akaitoa simu kubwa (smart phone) ndani ya dro la kabati.

"Eee kila mtu ashinde mechi zake, sio mimi nitoe mjengo halafu udhanie utakuja kukaa bure, nakupangisha"

"Hahahaha! Kum**make nakubali mkata wa kupanga nahamishia vitu vyangu na hela silipi"

"Kama hulipi si nakufukuza, ulale bure kwani patakuwa ni kwa Babako mzee Chiyano"

"Nasemaje wewe ukijenga mimi na kaa humo humo na silipi. Oya ona hata hii simu kubwa laini moja iliyomo imekaa Emergency"

"pengine ni mtandao tu haujatulia. Hii pesa yote ipo laki tatu na elfu ishirini na sita, naigawa kila mmoja laki moja na thelathini, hamsini tutaweka kwenye akiba hii kumi na sita tutanunua chambo"

"Poa, sema naona kwa huu mwendo tutachelewa sana kupata boti ya kwetu, hapa chakufanya siku kipato kikiwa kikubwa ni bora sisi tugawane nusu ya Mali halafu nusu tuwe tunaiweka akiba, ili hadi huu upepo wa neema unaisha tuwe tunamiliki angalau mashine"

"Ni wazo zuri sio mbaya tukifanya hivyo na kama ungeshauri mapema tungekuwa mbali sasa"

Nikabeba kila kinachonihusu na kumuaga Edward au Edo kissy kama anavopenda kujiita mwenyewe.
Nikatoka ndani na kuita boda ili kuelekea nyumbani Rahaleo ambako nimepanga.

Ni mwendo wa kama dakika tano tu tukafika nyumbani nikamlipa boda boda na akatembea.
Nikawasalimia wapangaji wenzangu waliokaa barazani na kuzama ndani ya nyumba hii ambayo ina vyumba saba na vyote vikiwa na wapangaji.
Nikaoga na kubadilisha nguo.

"Yes hapa niko bomba"
niliongea huku nikikitazama kioo kirefu kilicho wekewa fremu za mbao, ambacho kinaonesha jinsi jinzi yangu ya bluu na shati ya kijivu na weusi ilivyonikaa vizuri.

Nikaitotoa smart phone yangu kwenye chaja ili kumpigia Mzabzab aje achukuwe Samaki ampelekee mpenzi wangu Qashy ambae anauza vifaa vya simu katika duka lake lililopo Soko kubwa Mtwara, lakini pia awapelekee wazazi wangu ambao wanaishi Likonde.
Nikashangaa kuona nayo emekaa alama inayoashiria kutokuwepo kwa muunganyiko wa mtandao.
Nikatoka ndani ili kuwauliza wapangaji wenzangu juu ya tatizo hili.
Nilishangaa kiona wenzangu wote simu zao mtandao unafanya kazi vizuri tu.
Nikamuomba simu KENZY ili kumtafuta Mzabzab.

"Namba unayoipigia haipo"
Ilijibu sauti ya kike kwenye simu na kuniacha na mshangao, kwani hii ninamba ninayoitumia kila siku kuwasiliana na Mzabzab.

"Hivi leo kuna ishu ya namba kufunguwa na mitandao"
Nilimuuliza kenzi huku nikimrejeshea simu yake.

"Mh sijasikia vipi kwani?"

"Namba zangu na za rafiki yangu yule Edo hazifanyi kazi, lakini pia nampigia yule boda anaefataga kitoweo najibiwa namba haipo"

"Inawezekana"

Nikaingia ndani na kubeba Samaki wangu ambao nimewaweka katika mfuko wa kitambaa.
Nikaita boda na kuelekea sokoni dukani kwa Qashy.

Nikafika dukani kwa Qashy na kumkuta kijana ambae amemuajiri kumsaidia kazi.
"Vipi dogo mbona umepoa sana"
Nilimuongeleshaa kijana huyu anaeitwa Mshamba hachekwi huku nikiingia dukani.

"Ah bro hapa hakuna hata ninachokielewa nilikuwa nakusubiri wewe tu hapa pengine utaniweka sawa"

"Kukuweka sawa kwenye lipi?"

"Sista Qashy ameondoka sijuwi ameelekea wapi, lakini ondoka yake imeniacha na maswali mengi sana kichwani"

Akakaa kimya kidogo huku akiangaza macho kwenye mlango ili kuona kama kuna mtu anaingia

"Katika siku ambayo nimewahi kumuona Daa Qash amekasirika sana ni leo. asubuhi alikuja akiwa katika hali ya kawaida kabisa hadi ilipofika mchana. tulipokula chakula cha mchana akapita jamaa mmoja muuza Ice cream hawa wanaobeba mgongoni, ni mcheshi sana huyo jamaa halafu ni mtanashati.
Akafika hadi hapo mlangoni na kutunadishia Ice cream zake, Daa Qashy akajibu sawa tumeona, yule jaama akasema Anti ndiyo hata huniungishi au unaogopa na mimi nitafungua goli nikapumzika kama wewe? Daa Qashy akasema usiwaze swahiba nitakuungisha kesho, yule jamaa akasema poa ila kwa sababu leo nimeuza sana mapema na sasa namalizia tu nakuachia hii moja ila ni deni kesho ni lazima uniungishe. Yule jamaa aliongea hivyo huku akitua kibegi chake cha Ice cream na kumpa Sista Ice cream ya strawberry, Daa Qashy akashukuru na kumuahidi atamuungisha akipita kesho"

Mshamba Hachekwi aliongeabm kwa sauti ya chini huku akionekana kuwa na wasiwasi mkubwa sana.

"Baada ya yule jamaa kuondoka Sista akaanza kula ile Ice cream huku tukipiga stori, ameimega sijuwi ni mara moja au mara mbili vile nikamuona anaweka mkono mdomoni huku akitoa sauti ya kugumia kama mtu anaetaka kutapika, akatoka nje haraka sana huku mimi nikiwa namshangaa, zikapita kama dakika kumi hivi, akarudi akiwa amekasirika mno, wakati huo mimi nilikuwa nahudumia wateja, baada ya wateja kuondoka akaniita kwa majina yangu na kuniambia, muda wowote wowote kuanzia sasa mimi naondoka na hii inaweza kuwa ni mara ya mwisho mimi na wewe kuonana labda kwa mapenzi ya mungu. Kama sitowahi kuonana na Kim mwambie ninampenda sana, lakini najuta kwanini niliipenda pesa kabla yake, pia mwambie yeye ndiyo mmliki halali wa vitu vyangu vyote kuanzia sasa hivi ila mwambie asihangaike kunitafuta"

Akaingia mteja dukani na kukatisha maongezi ya Mshamba Hachekwi.

"Samahi Mama kuna tumepatwa na dharura hapa tunajiandaa kufunga"

Niliongea na Mteja huyu Kama vile mimi ni mtowa huduma wa hapa.
Mama huyu akaondoka kisha Mshamba Hachekwi akaendelea kinipa simulizi hii ambayo inaingia kichwani mwanangu kwa shida sana.

"Mwambie hawezi kuniona kamwe kwa jitihada zake, ikiwa mungu atatujalia maisha marefu tutaonana mwambie nampenda sana. Sasa ninaondoka hapa naenda kufanya jitihada ili niweze kumuona ila kama nikishindwa kumuona Naomba umwambie yote niliyokueleza"

Mshamba Hachekwi akakaa kimya kidogo na kuendelea

"Baada ya kuongea maneno hayo akaingia mzee wa makamo hivi na kumuita Daa Qashy waongee nje, Daa Qashy akavuta pumzi ndefu na kuitoa huku akisonya akainuka kwenye kiti na kwenda nje, mimi nikainuka pia na kusimama upande huo huko ili nione wanaenda wapi, wakasimama hapo kwenye huo mkokoteni wakwanza kuongea alikuwa ni Daa Qashy, sikusikia wanaongea nini kutokana na makelele kama unavyoona hapa lakini kwa lugha ya miili yao tu ilionesha kama kuna kitu Sista anampinga yule mzee, baada ya maongezi ya kama dakika mbili hivi yule mzee alionekana kukasirika, akatembea kwa hatua za haraka akienda kule kwenye kijiwe cha bodaboda. Daa Qashy akasimama kwa sekunde kadhaa akimuangalia yule mzee huku uso wake ukionekana ni kama mtu aloyechukizwa sana, na mwili wake ukiwa unamtetemeka, akairusha chini simu yake kwa nguvu na kupiga hatua za haraka kumfata yule mzee. Wakati huo mimi nikatoka nje ili kuona vizuri kinacho endelea, yule mzee alikuwa wa kwanza kupanda bodaboda na kuondoka, Daa Qashy nae akapanda bodaboda na kumpa ishara dereva aifate pikipiki aliyopanda yule mzee. Muda huo watu walikuwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, mimi nikaenda sehemu aliyotupa simu Sista na kukuta imepasuka kama unavyo iona, baada ya hapo nikachukuwa simu yangu ili nikupigie lakini iligoma mtandao, nikaazima simu ya mshkaji hapo jirani nilipopiga namba yako ilijibiwa haipo"

Aliongea Mshamba huku akininesha simu iliyo kwenye kiti ambacho hukaa Qashy Lilith.

"Ooophwwwwwwww......"
Nilishusha pumzi huku ubongo wangu ukifanya mchakato utakaoamua ni swali lipi liwe la kwanza kumuuliza Mshamba, kwani hadithi aliyonipa imeniacha na maswali ambayo hata idadi yake tu siijuwi.
ITAENDELEA.

Unaruhusiwa kutoa Maksi, kutoa maon,i kutoa ushauri wa kiutunzi na uandishi na hata kukosoa pia.
 
Sema nimependa sana jinsi ulivyowapa watu vitengo 😆😆😆😆😆😆 mimi sijui ningekaa kwenye kukata mkaa 😃😃😃😃😃😃😃
 
Back
Top Bottom