Simulizi: Tajiri Kijana

Simulizi: Tajiri Kijana

AK Mastori

Member
Joined
Jul 26, 2024
Posts
5
Reaction score
6
SURA YA 1 - SAPRAIZ YA NGUVU
likua maajira ya saa tatu usiku kwenye jengo la gorofa la hostel ya wanaume katika chuo kikuu cha Mbezi Beach.

“Bilal, nenda gorofa ya kwanza chumba namba mia moja na nne uniletee laptop yangu!”

Kijana mwenye kiduku aliamrisha baada ya kufungua mlango wa chumba cha wakina Bilal na kutupa shilingi elfu moja sakafuni kabla ya kugeuka na kuanza kuondoka.

“Nimesahau, pia ukishuka ninunulie maji kutoka super market ya hapo chini.”
Yule kijana mwenye kiduku aligeuka na kutoa elfu moja nyengine na kuirusha chini kwa ajili ya Bilal kumnunulia maji.

“We kiduku! Kwanini mnapenda sana kumtuma tuma Bilal awafanyie vitu vyenu? Mda wote mnakuwaga na kazi ya kumnyanyasa tu.”
Rafiki wa kutoka chumbani kwa wakina Bilal waliuliza kwasababu walikua wamechoshwa na rafiki yao kutumwa tumwa.

“Hahaha! Bilal anaishi chumbani kwenu na wala hamjamsoma tu hadi leo? Huyu mtu ukimpa buku mbili tu unaweza kumuamrisha ata kula kinyesi,” Kiduku alijibu kwa dharau huku akiondoka na kucheka.

Sura ya Bilal ilibadilika kwa hasira na aibu huku akijitahidi kuyapotezea yale aliyoyatamka Kiduku. Baada ya hapo, aliinama kuokota zile pesa zilizorushwa na Kiduku huku akijiwazia, "Hapa nimeshatengeneza buku na inatosha kabisa kula wali maharage kutoka kwa mama ntilie wa site ya ujenzi iliopo jirani na chuo, silali na njaa tena leo, asante Mungu."

“Bilal..usiende! Kama hauna pesa za kutosha tutakuazima, na wala huna haja ya kuturudishia.” Kiongozi wa chumba chao alishindwa kujizuia na kujikuta akimwambia hivyo Bilal ili asidhalilike. Bilal alitikisa kichwa chake kabla ya kutabasamu na kusema, “Asante, lakini usijali ni sawa tu..”

Kisha Bilal akageuka na kuanza kutoka nje ya chumba chao. Mda huu, wavulana wote wa chumbani kwake walimuangalia Bilal akiwa anaenda huku wakitikisa vichwa vyao kwa kumhurumia.

Bilal hakuwa akifurahia kutumwa tumwa na wanafunzi wengine na alitamani na yeye kufurahia maisha ya chuo kama wenzake. “Ingependeza kama na mimi ningekua nasoma bila ya kuwa na hofu ya vitu vyengine.” Aliwaza.
Lakini kiuhalisia, Bilal alikuwa maskini sana. Ingawa wale vijana wa chumbani kwake walikua wakiishi nae vizuri kulingana na hali yake, hakutaka wamhurumie. Alikuwa anahofia kwamba itafika siku watamchoka tu na maisha yake ya chuo yatazidi kuzorota.

Ukiacha na hawa aliokuwa akiishi nao chumba kimoja, Bilal hakuwa na marafiki wengine wa karibu chuoni hapo isipokua wachache sana waliokua wakisoma kozi moja, kwani wanafunzi wengi walikua ni watoto wa kitajiri. Kilikuwa ni chuo cha gharama kuliko vyote katika wilaya hio, na yeye alikua akisoma kwa ufadhili tu kwasababu ya ufaulu wake mzuri.

“Bilal, nimemskia Kiduku akisema unashuka kwenda chini, si ndio?”

Mara hii, kijana mtanashati alievaa vizuri alikuwa akizungumza huku akitoka kutoka kwenye chumba cha jirani na Bilal.

Jina lake lilikua ni Daniel Mushi na alikua ni kiongozi wa chumba cha wakina Kiduku. Alikua ni kijana anaependwa na wanafunzi wa kike kwa sababu licha ya uzuri wake, Daniel pia alikua ni mtoto wa kitajiri. Hata hivyo, Daniel alikua akimdharau sana Bilal kwa kuwa alihisi ni kijana anaetia aibu tu kutokana na hali yake ya kimaisha.

Bilal hakuelewa kwanini huyu kijana anaemdharau hivi anamuongelesha, hivyo akatikisa kichwa kuitikia, “Ndio, naelekea chini.”

Daniel alitabasamu kabla ya kumpatia Bilal boksi lilijojaa vitu.

“Nina rafiki yangu mmoja yupo kwenye vimbweta vya mapumziko vya jirani na jengo la sheria, mpelekee hili. Utamkuta kavaa jinzi jeusi na tishet ya bluu bahari. Hii hapa buku tatu kwa ajili yako.”

Daniel alikua anapenda kuchezea wasichana na vimbweta hivyo ndio alikua anapenda kukutana nao. Pia alikua na marafiki wengi ambao ilikua ndio tabia yao hii.

Bilal hakuwaza sana kuhusu hili na alikubali kwa kuwa alikua kashazoea kutumwa tumwa.
Alichukua hilo boksi na shilingi elfu tatu akaanza kushuka ngazi. Alivyogeuka tu, alihisi kumsikia Daniel akicheka kwa mbali..

Bilal alishuka ngazi kwenda kuchukua laptop na kumnunulia maji Kiduku kabla ya kuanza safari ya kimbwetani kupeleka boksi alilokabidhiwa na Daniel.

Vimbweta vya mapumziko vya jirani na jengo la sheria vilikua maarufu kwa wapenzi wa chuoni hapo kukutana maajira ya usiku. Walivipa jina lililokua maarufu la vimbweta vya mahaba.

Bilal alivyofika vimbwetani hapo akaona mtu alievaa jinzi jeusi kwa mbali akiwa na binti wa kike. Walikua wamekaa chini kwenye bustani, eneo linalomulikwa vizuri na mwanga wa mwezi, wakipiga stori na kucheka pamoja. Bilal akaanza kuwafuata.

Alipowakaribia, Bilal alishtuka sana baada ya kuona sura ya mwanaume na mwanamke hao waliokuwa wamekaa hapo.

Ilikua ni kama kapigwa na shoti ya umeme.

Alikua ni Sheila!

Macho ya Bilal yakawa mekundu ghafla na boksi alilobeba likadondoka chini.
Sheila alikua ni mpenzi wa Bilal walioachana siku tatu tu zilizopita, tena ilikua ni Sheila alietaka wavunje uhusiano wao.

Wakati wanaachana, Sheila alimwambia anataka tu kuwa mwenyewe kwa muda ili atafakari mambo, lakini imekua siku tatu tu na tayari alikua na mwanaume mwengine, tena kwenye vimbweta vya mahaba!

Wawili hao nao walivyomuona Bilal anawafuata sura zao zilibadilika ghafla.

“Bilal..unafanya nini hapa? Wewe, wewe...usinielewe vibaya. Nipo na John kwasababu...”

Sheila alianza kupanik hapo hapo, akiwa anajiskia aibu kwa mazingira aliokutwa. Aliinamisha kichwa haraka na kuangalia chini kwa kutojua namna ya kumkabili Bilal.

Kijana John Rugemalila, ambae pia alikua ni mtoto wa kitajiri, alitupia macho kwenye boksi lilodondoshwa na Bilal kabla ya kuanza kucheka kwa nguvu.

“Duh! Kweli Daniel anajua kuwafanya watu wapumbavu. Nilimuomba aniletee hivi vitu na sikutegemea atakutuma wewe uvilete. Hii inafurahisha, inafurahishsa sana!”

Bilal alijua kuwa John, ambae ni mtoto wa kitajiri, ni rafiki wa karibu wa Daniel. Familia yao inamiliki migahawa mingi na alikua akitumia gari aina ya BMW 3 series chuoni. Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kukunja tu ngumi zake kwa hasira wakati akiskiliza maneno ya John.

Ilikuwa wazi kwamba Daniel alimfanyia hivi maksudi. Zaidi ya hayo, Bilal alianza kuhisi na kuamini kuwa Daniel alihusika katika yeye kuachana na Sheila, haswa baada ya kuona rafiki wa karibu wa Daniel yuko na Sheila siku chache tu baada ya mahusiano yao kuvunjika.

“Sheila, najua huna hisia na mimi lakini huna haja ya kuwa na mvulana wa namna hii baada ya mahusiano yetu kuvunjika. Unajua ni wanawake wangapi kawabadili huyu kabla ya wewe?” Bilal aliongea kwa sauti.
Alimpenda sana huyu dada, sana.

Shelia aliudhika na kauli ya Bilal iliotaka kumtia hofu na wasiwasi. “Bilal, unadhani wewe ni nani? Nani kakupa haki ya kunifundisha nini cha kufanya na kutofanya? Nimeshaachana na wewe na sasa naweza kuwa na mtu yoyote ninaetaka kuwa nae!”

“Pia...” Sheila alikua kashajawa na hasira mda huu. Akamtazama Bilal kabla ya kuendelea kumuuliza, “Kwani umekuja hapa maksudi? Embu potea”

‘Kofi!’

Baada ya kumaliza kuzungumza, Sheila alimsogelea Bilal na kumpiga kofi kali shavu la upande wa kulia.
John alicheka zaidi baada ya kuyaona haya. Kisha akamshika kiuno Sheila huku akiendelea kucheka na kuzungumza. “Hahaha. Sheila, kwanini unamfukuza huyu kapuku? Muache tu abaki atutazame tunavyofurahi!”
Sheila akatabasamu kiuchokozi. “John, nishapoteza hamu yote baada ya kumuona huyu mpuuzi hapa! Labda wakati mwengine...”

Baada ya hapo, Sheila akautoa mkono wa John kutoka kiunoni kwake.

Bilal hajui hata aliwezaje kutembea kutoka kwenye vimbweta hivyo. Akili yake ilikua kama imeganda na haifanyi kazi wakati huo.

“Kila kitu ni pesa tu. Nisingekua katika hali hii kama ningekua tajiri.“ Alijiwazia.
“Hahaha…”

Baada ya kufika hostel kwake, Bilal alisalimiwa na vicheko vya wanafunzi wenzake kwenye korido.

Daniel alikua kashika tumbo lake huku akicheka kwa nguvu zaidi. Ilikua dhahiri kwamba aliwaelezelea wanafunzi wenzake kuhusu tukio lote kwani yeye ndio aliolipanga.

“Hahaha. Bilal, uliona nini ulivyoenda kupeleka boksi uliloagizwa na Daniel?” Kiduku alimuuliza akiwa na tabasamu usoni mwake.

“Dah! Umepoteza demu mwenye umbo zuri sana mzee” Daniel aliendelea kuchochea huku akicheka.
Bilal alikunja ngumi kwa hasira na macho yake yalikua mekundu karibu kudondosha chozi. Alitamani amuue Daniel mda huo huo na yeye ajiue ili asiwe kwenye aibu hii tena.

“Kwanini? Kwanini unanifanyia hivi lakini Daniel? Nimekukosea nini?” Bilal alizungumza kwa sauti ya chini lakini yenye hasira.

Daniel aliendelea kucheka kabla ya kumjibu, “Sikia we mpuuzi, mimi sikuogopi kabisa. Hujui katika maskini wote wa darasani kwetu wewe ndio wa kutupa? Sheila ni msichana mrembo na ni hasara mtu kama yule kuwa kwenye mahusiano na mwanaume wa aina yako. Shukuru tu nimekutoa kwenye ramani na sasa anafurahia maisha na kijana anayeweza kumhudumia. Alafu nimekumbuka, hivi unajua John ameweza kumpata Sheila ndani ya nusu siku tu wakati wewe umehangaika karibu mwaka mzima kabla ya yeye kukukubalia? Tafuta pesa mzee.”

Kila mtu aliekuwepo alikua anamcheka Bilal mda huu na hamna aliejali hisia wala utu wake kabisa.
Bilal akaanza kumkimbilia Daniel kwa ajili ya kumpiga baada ya hasira kumzidia. Matokeo yake, yeye ndio alioishia kupigwa na marafiki wa Daniel na hakuweza hata kumgusa.

Wakati fujo hizi zikiendelea kukua, watu wa hostel hio walishaanza kujaa eneo hilo. Marafiki wanaokaa na Bilal chumba kimoja pia wakafika na baada ya kuona mwenzao anapigwa wakakimbilia kuamuru ugomvi na kumrudisha mwenzao chumbani kwao.

Bilal alifunika uso wake na shuka yake ya kujifunikia huku akiendelea kulia akiwa kitandani kwake.
“Kwanini? Kwanini mimi tu ndio wa kuonewa na kuvunjiwa heshima? Kwanini? Kwani sina hisia hata kama mimi maskini? Kwahio maskini ndio hatutakiwi kuwa na hisia? Yani mimi moyoni mwao sio mtu kabisa, kwanini unaniweka katika hali hii Mungu? Dua zangu huzisikii? Huoni ninavyodhalilika?”

Bilal aliendelea kusononeka moyoni na kushindwa kuzuia machozi kuendelea kububujika kutoka machoni mwake. Alishindwa kabisa kupoteza mawazo ya yaliyomtokea usiku huo.

Hajui hata ni muda gani alipitiwa na usingizi akiwa kajikunyata chini ya shuka yake akilia.
Bialal alilala usingizi mzito sana usiku huo, huenda kwasababu ni kutokana na kuchoka na mawazo na vilio vya yote yaliyomkuta.

Alipoamka asubuhi iliofuatia, hakukuwa na mtu chumbani kwao. Bilal alijua kiongozi wa chumba chao hakutaka aamshwe ili apumzike baada ya matukio aliyoyapitia usiku uliopita. Baada ya kushika simu yake, alishtushwa kuona kuwa kuna simu nyingi zimeingia na meseji ambazo hakuzijibu.

Kilichomshangaza zaidi, simu na meseji zote zilikua zikitoka kwenye namba za kigeni.

Kwakua hakuwa na salio kwenye simu yake, alishindwa kuipigia ile namba iliokuwa imepiga mara nyingi. Hivyo akaanza kupitia meseji zilizokua zimeingia.

Alishtushwa kuona meseji kutoka benki ya CRDB ikimtaarifu kuwa kiasi cha shilingi za kitanzania milioni arubaini na laki nne kimewekwa kwenye akaunti yake.

Kabla hajamaliza kustaajabu akapokea simu kutoka benki hio ikimtaka afike katika tawi la karibu kwa ajili ya mahojiano. Aliamka haraka haraka na kuvaa tishet na jinzi aliokua kavaa jana yake na kutoka mbio. Alisahau hata kuoga na kupiga mswaki.

Akiwa njiani, bado alikua haelewi nani anaweza kukosea na kuweka kiwango chote hicho kwenye akaunti yake. Mawazo na maswali yalijaa kichwani mwake na yote yalikosa majibu. Wakati akiendelea kuwaza, simu yake ikaita tena. Kuangalia ilikua ni ile namba ya kigeni. Aliipokea kwa haraka kabla haijakata, baada ya kupokea aliskia sauti ya kike ambayo haikuwa ngeni kwake ikimuongelesha.

“Bilal, assalamu alaikum. Ni mimi dada yako Aisha!”

“Dada! Waalaikumu salaam. Vipi mpo salama?” Bilal alishindwa kuzuia furaha ya kusikia sauti ya dada yake na kujikuta akitokwa na chozi. “Mama yupo wapi? Mpo wapi? Mbona hamjanitafuta miaka yote hii?” Maswali mfululizo yalitoka kinywani mwa Bilal.

Ilikuwa ni mwaka wa pili tangu mama na dada yake waondoke nchini kwenda katika falme za kiarabu kutafuta maisha bora. Wakati wanaondoka, familia yao ilikua katika hali duni sana. Mama yake alimnunulia simu ndogo ya kiswaswadu kwa ajili ya kuwasiliana nae lakini kwa bahati mbaya aliibiwa na kushindwa kurejesha laini kwani haikusajiliwa kwa jina lake na hakuwa na kitambulisho cha taifa muda huo, ingawa kwa sasa alikua ameshapata simu janja kutoka kwenye posho za chuoni na pesa anayotengeneza kwa kufanya shughuli za kutumwa. Pia, laini ya mama yake ilifungiwa baada ya kukaa kwa muda bila ya kutumika huko nje ya nchi. Hivyo hakuwa na taarifa zozote za ndugu zake.

“Embu punguza maswali kwa kasi basi mdogo wangu, nitakujibu vipi haraka hivyo? Nimekumiss dada yako.” Aisha alimjibu huku akiwa na furaha kuweza kuongea na mdogo wake kwa mara nyengine.

“Kiukweli huwezi kuamini nitakachokwambia, lakini mdogo wangu dua zetu za miaka yote zimejibiwa. Tumefanikiwa kukutana na baba yetu mzazi Bilal. Baba yuko hai. Na taarifa kubwa itakayokusapraiz ni kwamba baba anatokea kwenye familia yenye utajiri mkubwa sana huku Abu Dhabi. Wana uwekezaji kwenye makampuni makubwa duniani kote. Ni stori ndefu sana kuielezea kwa sasa lakini jua tu wewe ni kijana tajiri sana huko, sidhani kama kuna kijana anaekufikia kwa utajiri huko. Sasa mdogo wangu mimi naingia kwenye kikao huku, tutaongea vizuri nikipata nafasi.”

Bilal alishtuka na maelezo haya. Upande mmoja alitamani kuamini lakini kuzingatia na maisha waliyokulia na changamoto walizopitia alihisi dada yake anamtania tu.

“Dada acha masihara yako bwana. Kweli unataka tupoteze muda na salio kuongea hadithi za abunuasi wakati tuna mambo ya msingi chungu nzima ya kuongelea?”
Bilal alimjibu.

“Sikutanii Bilal. Kwanza nimetuma pesa ya matumizi kwenye akaunti yako kiasi cha dola elfu kumi na tano. Kwa kiwango cha kubadilisha fedha cha huko utakua umepokea kwenye shilingi milioni arubaini. Benki watazuia hio pesa kwa ajili ya kujiridhisha kuwa hutakatishi fedha hivyo kuna maelezo na vithibitisho nimekutumia kwa whatsapp uwaelezee ili uweze kutumia hio pesa. Naingia kwenye kikao sasa, tutaongea baadae.”

Bilal hakuamini alichosikia. “Kwa hio hizi pesa ni zangu?” alijiwazia. Kuhamaki alikua kashafika kwenye tawi la benki ya CRDB. Baada ya kuingia kuhojiwa na kutoa maelezo ya pesa ile, benki ilijiridhisha na kuondoa zuio kwenye akaunti yake.

Alivyotoka, akaingia kwenye atm kujiridhisha. Akajiaribu kutoa laki nne iliotoka bila ya changamoto yoyote. Aliruka ruka pale kwenye atm kufurahia hadi watu wakamshangaa. Ndipo aliporudi hostel za chuo na kwenda moja kwa moja chumbani kwao. Akajitupa juu ya kitanda huku akitazama juu na kusema kimoyo moyo:
“Mimi Bilal Hassan, mtoto niliyekulia kwenye umaskini..leo hii ni tajiri? Asante Mungu kwa kujibu dua zangu!”

Sura ya pili itaendelea
Whatsapp: 0746260961
 
SURA YA 2 - MTEJA V.I.P
Baada ya kufuatilia, Bilal alikuja kugundua kwamba baba yao alipoteza mawasiliano na mama yao baada ya kuondoka Tanzania kurudi nyumbani kwao uarabuni mwaka 2003. Alikuja Tanzania kwa ajili ya kutafuta fursa za biashara kabla ya kukutana na mama yao wakina Bilal na kumpenda. Baada ya biashara kuyumba, alilazimika kurudi kwao. Teknolojia kipindi hicho ilikua duni kwa yeye na mzazi mwenzake kuweza kuendelea kuwasiliana mara kwa mara. Baada ya kutajirika alivyorudi kwao, alijitahidi kuwatafuta bila ya mafanikio yoyote lakini hakusita kuacha kuendelea kuwatafuta.

Kwa bahati nzuri, alikua akipendelea kuwekeza sana Tanzania na kuchukua watanzania kwa ajili ya kufanya kazi kwenye makampuni yake huko uarabuni kukiwa na upungufu wa wafanyakazi wa nchini kwao kutokana na mapenzi aliokuwa nayo ya nchi hio baada ya kutembelea na kuishi humo kwa kipindi kirefu miaka ya nyuma.
Alikutana na mama yao wakina Bilal tena kwenye moja ya miradi yake ya ujenzi walipokwenda kufanya kazi huko miaka miwili iliopita.

Hawakumtafuta mapema zaidi kwasababu baada ya baba yake kufuatilia na kumuona yupo kwenye chuo bora na cha kitajiri kutokana na akili zake, aliamua kumuacha ajifunze uhalisia wa namna watoto wengi wa kitajiri walivyoharibika kiutu huku akiandaa mpango wa namna gani ataingia kwenye biashara zake. Alihisi akimjulisha mapema kuwa wao ni matajiri sana angeharibika na kushindwa kumaliza chuo.

Hata hivyo, dada yake hakuacha kulazimisha wao kumtaarifu Bilal na baada ya yeye kuingia kwenye biashara za baba yake na kutajirika pia ndio ikawa ngumu kumficha mdogo wake hivyo akamtafuta.
Baada ya kuyajua haya, Bilal alijiridhisha kuwa yeye kapata bahati kubwa sana na kweli ni mtoto anaetokea kwenye familia ya kitajiri sana kwa upande wa baba yake.

Alikua na shauku sana.

Hakuacha kuwaza matukio yaliyomkuta siku chache tu zilizopita alipodhalilishwa na kipenzi chake Sheila. "Yani ungenivumilia kwa wiki moja tu nyengine saa hizi ningekua natimiza ndoto na mahitaji yako yote ya kipesa bila ya kuwaza. Huyo John wako na Daniel sijui watajiskiaje huko mbeleni watakapojua ukweli wangu kwa namna walivyonidhalilisha," alijisemea mwenyewe.

Alikua anatoka kupokea bahasha ndogo kutoka kwa dada yake katika ofisi za DHL simu yake ilipoita. Alipoitoa mfukoni aliona ni kiongozi wa chumba chao ndio anampigia.

"Hello kaka!"

"Bilal, upo sawa? Nimekutafuta hostel sikuoni, chuo chote haupo."

"Ah nipo sawa usiwaze. Nimetoka tu kutembea ninyooshe miguu."

"Umetutisha. Sio kawaida yako kutoonekana mida hii chuoni. Sasa, si unajua leo ni siku ya kuzaliwa ya Naomi? Kaniagiza nikuulize kama utahudhuria sherehe yake leo usiku, ana mambo mengi na alikupigia hukupokea kwahio kashindwa kuwasiliana na wewe ingawa anasema alishakwambia kuhusu hii sherehe wiki iliopita!"

Aliposikia maneno haya, Bilal aliangalia simu ilioita wakati yupo ofisi za DHL na kushindwa kuipokea akagundua ilikua ni kutoka kwa Naomi.

Naomi alikua ni mwanafunzi mwenzake wanaosoma kozi sawa. Alikua ni binti mrembo na moja ya marafiki wake kwa kuwa hakupenda kuona anavyodhalilishwa mara kwa mara. Ukiacha Sheila, Naomi ndio binti wa kike mwengine pekee aliekua na urafiki na Bilal.

Bilal alikua anakumbuka kualikwa kwenye sherehe na Naomi wiki iliopita, lakini, hakujibu chochote wakati anaalikwa kwasababu alikua katika hali mbaya kiuchumi na hakutaka kujihusisha na anasa yoyote.

Kwa sasa, alikua na uwezo mkubwa kiuchumi. Aliamua kufanya maamuzi ya kuishi kama mwanafunzi wa kawaida tu kwanza asiekua na shida kwa marafiki zake wa karibu. Hivyo akaamua kuhudhuria sherehe ya siku ya kuzaliwa Naomi.

"Lakini nitahitaji zawadi si ndio kaka?"

"Sio lazima Bilal, uwepo wako tu utamridhisha."

"Sawa."

Baada ya kukata simu, Bilal akawa kajipa jukumu la kumtafutia rafiki yake zawadi. Aligeuka na kuona kibanda kinachouzwa juisi. Alikaa kwenye viti vya kibanda hiko na kununua glasi moja ya juisi ya embe iliochanganywa na passion ili awaze vizuri zawadi gani itamfaa Naomi. Akiwa anakunywa juisi yake, alifungua ile bahasha aliopokea kutoka kwa dada yake. Ilikua na kadi ya benki na kikaratasi kilichoandikwa "Tumia uwezavyo, pin ni 3219. Nakupenda - Aisha."

Bilal hakujua kadi aliokua kaishika mkononi mwake ina thamani kiasi gani. Ilikua ni JP Morgan Reserve Card! Hii ni kadi iliotengenezwa mahususi kwa ajili ya matajiri wakubwa duniani. Kadi hii ni moja kati ya kadi nyengine takriban elfu tano pekee zilizowahi kutengenezwa na benki hio. Haina kikomo cha pesa unachoweza kutumia kwa siku na kama kiwango cha manunuzi unachofanya kinazidi pesa iliopo kwenye akaunti yako, kadi hii inaweza kufidia kiwango chochote na ukalipa baadae. Kadi hii pia huwezi kuipata kwa kufanya maombi tu benki, inabidi ualikwe na mteja anaemiliki kadi hii ndio uweze na wewe kuomba kupata.

Bilal aliwaza tu kwamba itakua ni kadi iliowekwa kiasi kikubwa cha pesa basi lakini hakujua uhalisia wa ukubwa huo. Wakati akiendelea kunywa juisi yake, aliskia wadada watatu waliokaa jirani na yeye wakizungumzia duka la brand ya Gucci lililopo jirani na namna gani wana bidhaa nzuri. Hapo hapo akapata wazo la kumnunulia pochi Naomi hivyo akaelekea kwenye duka hilo baada ya kumaliza juisi yake na kulipia.

Hili lilikua ni duka la kifahari maarufu linalouza bidhaa za brand ya Gucci pekee. Lilikua maarufu pia chuoni kwao kutokana na ujirani wake na chuo chao. Wanafunzi wengi walipendelea kuonyesha ufahari wa utajiri wao kwa kushindana kununua vitu vya bei ghali hapo.

Bilal hakua na shaka ya kuingia dukani hapo kwasababu bado alikua ana salio limebaki kutoka kwenye pesa aliotumiwa na dada yake wiki iliopita. Pia, alikua katoka kupokea kadi ya benki ambayo alikua na uhakika ina pesa nyingi.

Alikua bado ndio anajifunza kuzoea maisha ya kawaida ya kutokua na shida za pesa. Tayari alishaongezeka ujasiri tangu agundue kuwa familia yao ni matajiri. Lakini hakutaka kubadili aina ya maisha aliokua akiishi haraka. Aliona itakua ni kujionesha tu na wale wasio na uwezo watakua wanaumia kama ambavyo yeye alikua akiumia kipindi wanafunzi wenzake matajiri walipokuwa wakifanya sifa zao.

Baada ya kuvuta pumzi kubwa alipofika nje, Bilal alifungua mlango wa duka hilo na kuingia ndani.

"Habari kaka, karibu. Naweza kukusaidiaje?"

Binti mzuri wa mauzo dukani hapo alimkaribisha Bilal kwa upole, ingawa alikua na taswira ya dharau baada ya kuangalia mavazi aliyokua kayavaa Bilal.

Alikua kashazoea wateja wanaoingia hapo huwa wana taswira na muonekano wa kitajiri hususani kwa namna wanavyovyaa na kujipodoa. Hakuelewa kwanini kijana wa namna hii anaweza kuingia kwenye duka kama hilo.
"Asante, ngoja kwanza niangalie bidhaa zenu." Bilal alijibu. Hii ilikua mara yake ya kwanza kuwahi kuingia kwenye duka la kifahari la namna hio kwahio akaona azunguke kutazama na kujua bei za mavazi ya kifahari haswa yale wanayoringia baadhi ya wanafunzi wenzake chuoni.

Yule dada wa mauzo akamuangalia Bilal kwa sura ya kubeza akidhani amekuja tu kumsumbua na hana uwezo wa kumudu kununua bidhaa yoyote dukani hapo.

"John mpenzi si utaninunulia pochi leo?"

Sauti ambayo Bilal alikua anaijua iliongea. Bilal alipogeuka, akashtushwa kuona wapenzi hao wawili ambao walikua wameingia dukani hapo. Haikua mwengine bali ni Sheila na mpenzi wake mpya John. Sheila alikua kashika mkono wa John kwenye kiwiko kwa mikono miwili akimuegemea kwa upande huku John akiwa kaweka mkono alioshikwa mfukoni.

"Habari Boss Rugemalila, huyu ni mpenzi wako? Ni mrembo sana."

Yule dada wa mauzo aliekua akimhudumia Bilal alivyowaona wawili hawa ghafla akachangamka na kuwakaribisha kwa bashasha na tabasamu kubwa.

Kila mfanyakazi wa dukani hapo alijua John Rugemalila ni kijana anaetokea kwenye familia ya kitajiri na alipenda kufanya manunuzi hapo mara kwa mara. Hii ndio sababu dada huyo wa mauzo akamkimbilia mara moja alipomuona.

"Ndio Recho, huyu ni mpenzi wangu Sheila. Nimemleta leo aangalie mzigo uliopo kwasababu nataka kumnunulia pochi."

Sheila alitabasamu kwa furaha. Alijiskia fahari kuona yupo na mtu anaejulikana kila wanapokwenda. Aliashiria pochi moja kwa kidole na kumwambia John "Nataka pochi hii kipenzi."

Pochi alioashiria Sheila ilikua ndani ya kabati la kioo la kipekee kando na bidhaa nyengine. Kabati hilo lilipambwa kifahari zaidi kuliko yale mengine yaliyokuwepo hapo.

Recho akatabasamu na kusema, "Hii ni pochi ya Gucci Zumi Crocodile, ndio pochi ya bei kubwa tulio nayo kwa sasa. Bei yake ni dola elfu thelathini na mbili tu kama unalipia kwa kadi ya nje au kama ni kwa fedha za nchini ni shilingi milioni themanini na saba."

"Nini?"

Sheila alishtuka kusikia bei hio na kushindwa kujizuia kuuliza kwa sauti ya nguvu.

John nae akadakia haraka huku akitabasamu na kusema, "Recho, kama sijakosea, pochi hii imepewa jina hili kutokana na msanii Zumi alietembea nayo kwenye maonyesho Ufaransa. Pia ina bei kubwa kwasababu imetengenezwa kwa kutumia ngozi ya mamba na ndio maana inaitwa crocodile, pochi zote za Gucci za crocodile ni za ngozi halisi ya mamba na ni imara sana."

Recho alifurahishwa na ujuzi wa John kuhusu pochi hii. "Kumbe unajua mengi kuhusu pochi boss Rugemalila? Sikujua hili."

John alitikisa kichwa chake na kusema, "Napenda kufuatilia brand kubwa haswa kwenye mitandao ya kijamii. Si unajua inabidi niende na fasheni. Nilitazama video ya uzinduzi wa pochi hii huko mitandaoni."

Baada ya hapo, John alimtazama Sheila na kumwambia, "Mpenzi una jicho zuri sana la vitu vizuri. Lakini uwezo huo sina, tutafute pochi ya dola elfu moja hadi elfu mbili tu."

John alikua radhi afe kuliko kununua pochi ya milioni themanini na saba.

Sheila aliongea kwa kunung'unika, "Mbona mchumba wa Emmy kamnunulia pochi ya dola elfu sita?"

John akajibu, "Basi itabidi usubiri hadi mwezi ujao nikipewa pesa ya matumizi."

Muda huu, watu waliosikia mazungumzo ya Recho na John tayari walishalizunguka lile kabati lenye pochi ya bei kubwa kuliko zote. Kila mtu alionekana kuvutiwa na maelezo aliosikia na ikawa ndio gumzo la hapo dukani.
Bilal alivyoona yule dada wa mauzo kampuuza na kumuacha mwenyewe, alipoteza hamu ya kununua zawadi dukani hapo na alikua tayari kuondoka kwa kuwa hakutaka wakina Sheila na John wamuone.

Wakati akielekea kutoka, dada mwengine mdogo zaidi alimjia ghafla mbele yake na kumsalimia, "Habari kaka, mbona huna raha? Niambie naweza kukusaidiaje leo dukani kwetu?"

Alionekana kuwa ni binti ambae alikua mfanyakazi mpya kwa namna alivyokua na shauku ya kuridhisha wageni.
Bilal alipenda ukarimu wake hivyo akasimama kumjibu, "Salama, ningependa kumnunulia rafiki yangu wa kike zawadi ya siku ya kuzaliwa." Alijibu.

"Sawa boss. Ngoja nikutaftie kitu kizuri umfurahishe mwenzako leo. Utaridhika. Pia tuna huduma ya kulipa kwa kadi ya benki kama huna pesa taslimu boss hivyo usisite kama pesa uliotembea nayo haitoshi." Yule dada aliendelea kumkirimu Bilal vizuri kwasababu ndio alikua mteja wake wa kwanza dukani hapo.

"Tena kweli bora umeniambia, nimeacha kadi yangu ya CRDB hostel. Hapa nimetoka kupokea kadi nyengine DHL lakini sijaitumia bado, naomba nikuoneshe uone kama itafaa." Bilal alitoa ile kadi ya JP Morgan aliotumiwa na dada yake na kumpatia dada wa mauzo.

Yule dada wa mauzo alitoa macho kwa kushangaa alipoiona kadi ile.

"Hii ni Reserve card ya JP Morgan?" Dada huyo akauliza huku akimtazama Bilal kwa kutoamini. "Huyu kaka ana muonekano wa kawaida sana, anawezaje kuwa na kadi ya aina hii?" Aliwaza.

Bilal hakuelewa kwanini yule dada kashangaa sana. "Kwani hio kadi ina nini? Mimi nimetoka kuipokea hata sijaitilia maanani."

Yule dada ndio akamuelezea uadhimu wa kadi ile Bilal. Akamalizia kwa kumuonesha meseji za kundi lao la chuo alichomaliza ambapo walikua wametoka kufanya utani tu kuhusu kadi hio asubuhi yake wakiiongelea kadi hio na mwisho wote kukubaliana hamna mtu anaeimiliki kwa nchi hii.

Bilal ndio alizidi kuchanganyikiwa pia, alibaki kujiuliza, "Kwani familia yetu ina utajiri kiasi gani haswa?"
"Boss, kwa hadhi ya kadi hii siwezi kukuonesha hizi bidhaa za kawaida. Ngoja nikuletee pochi yetu ya bei kubwa kuliko zote kwanza uone kama utaridhika nayo." Yule dada akaondoka haraka haraka kwenda kuleta pochi hio.
Wakati huo huo, Sheila na John walikua bado wapo dukani hapo wakiangalia pochi nyengine huku wakionekana kufurahia siku yao.

Yule dada wa mauzo akafungua loki ya kabati lenye ile pochi ya Gucci Zumi Crocodile na kuitoa pochi hio.
Recho hapo hapo akamfokea kwa hasira, "Amina, unafanya nini?"

Amina akageuka na kumjibu, "Kuna mteja nataka kumuonesha pochi hii!"

Recho akaendelea kuongea kwa hasira, "Nyie wageni mna tabu, unadhani hii ni pochi unayoweza kumuonesha mtu yoyote tu? Kwani unataka kumuonesha nani?"

Amina aliangalia upande alioko Bilal na kusema kwa heshima, "Nataka kumuonesha kaka yule pale."

John na Sheila pia wakageuka upande alioashiria Amina wamuone huyo mnunuzi kabla ya kuanza kucheka kwa nguvu pamoja.

“Hahaha!”

Hawakuamini walipoona anaezungumziwa ni Bilal. Wangeweza, wangejitupa sakafuni wagare gare kwa kicheko walichokua nacho.

"Unaongelea nini we dada? Yule kijana ndio anataka kuona pochi hii?" John aliuliza huku akimnyooshea kidole Bilal. Huu ulikua ni utani mkubwa sana kwake.

John alimuangalia Bilal kwa dharau sana hadi Bilal akaanza kujiskia aibu, hususani kulinganisha kile kikundi kilichokua kinashangaa pochi hio sasa chote kilikua kinamshangaa yeye.

Recho nae alikua kakunja sura akiendelea kufoka, "Amina! Kweli unaamni kijana huyu anaweza kumudu kununua pochi yoyote humu? Unafanya utani?"

Amina akajibu, "Hapana dada unakosea, huyu kaka anaweza kuingia kwenye chama chetu cha wateja muhimu cha VIP."

"Hahaha!" John akacheka tena kwa nguvu. "Mteja VIP? Huyu ni kapuku maarufu chuoni kwetu!"

Sheila pia akamtazama Bilal kwa karaha huku akisema, "Bilal, hivi hujiskii aibu? Toka hapa haraka sana."

Hahaha…

Bilal alitazama kikundi cha watu kilichokuwa kimemzunguka sasa kikimsema na kumcheka kwa dharau. Amina nae pia alikua anaanza kuhisi amejiingiza katika matatizo kwa namna ambavyo Recho alikua akimsema.

Bilal akaanza kutembea kwa hasira akiwa kimya kuelekea kwa Amina, akaichukua pochi ile kutoka mikononi mwa Amina na kuelekea kwenye meza ya malipo ya duka hilo. Akaweka pochi hio na kadi yake juu ya meza kisha akasema,

"Nataka kulipia pochi hii sasa hivi!"

**************************************
Baada ya Bilal kuweka pochi na kadi ya benki mezani, Sheila na John watajibu vipi mapigo?

Kwa muendelezo, whatsapp kupitia namba 0746260961.
 
Story yanko nzuri mkuu.ila unatukatisha moyo tunaokulipa kwenye app yako kupata story halafu hautumi story.this is very very bad.am very dissapointed
 
Tembea uone maana Gucci wana pochi wamemuuzia kardashian takribani USD250,000 kwa bongo ni zaid ya millioni 500
Nimeshatembea mno Mkuu mtandaoni....na ninaelewa ila Kwa aina ya story na maisha halisi hiyo ni pesa ndefu mno kuitaja basi angesema pochi aliambiwa 1.something......eti milion 87 hahaaaaaaaaa wamekuja ku a kina Ambani haaaaaaaa
 
Nimeshatembea mno Mkuu mtandaoni....na ninaelewa ila Kwa aina ya story na maisha halisi hiyo ni pesa ndefu mno kuitaja basi angesema pochi aliambiwa 1.something......eti milion 87 hahaaaaaaaaa wamekuja ku a kina Ambani haaaaaaaa
Ndugu yangu tembea uone mengi hio amesema ni kidogo sana amini hilo kuna mahali ukienda ukisikia bei zake utajua duniani ww ni msindikizaji
 
Hakuna uhalisia pochi milion 87...hapo ndio nimeishia kusoma
Zipo za hiyo bei kabisa, Nenda Italy ndo utajua binadamu tunatofautiana.
Hiyo ni Gucci yenyewe og kabisa ndio bei zake.
Ina mpaka signature.
Sio hiyo mitambara yenu ya kichina huko mnauziwa 30000. Gucci 30k uliona wapi?
Yaani mwajuma ndala ndefu ana gucci ya elfu 10 unataka na kim avae Gucci ya 10000.
Akili zenu zina matobo sana.
 
Back
Top Bottom