Simulizi: Uhuru wa Watumwa

Simulizi: Uhuru wa Watumwa

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
9,189
Reaction score
16,128
Na James Mbotela.



MUHTASARI WA MAISHA YA MWANDISHI​

Mwandishi wa kitabu hiki, ni mzaliwa wa Frere Town, Kisauni, Mombasa. Baba yake ni Myao, akiitwa Mbotela ambaye alikuwa mmoja wa vijana wale waliookolewa baharini na Wazungu wa manowari za Waingereza zilizokuwa zikizuia biashara ya watumwa. Huyo baba alipenda sana kusafiri na Wazungu wa misheni pamoja na Wazungu wa kampuni katika safari zao za miguu kwendea nchi za bara. Alikuwa ni mmoja wa wale walioandamana na Bishop Hannington, Uganda. Na safari yake ya mwisho, yeye na wenziwe waliandamana na Mzungu wa biashara akiitwa Dick, kuelekea nchi za Wakikuyu na Wamasai. Mbotela alikuwa mchukuzi wa bunduki ya Bwana Dick, nao wote wawili waliuawa na Wamasai siku moja katika matata yaliyotokea huko Kedong Valley.

Mama yake mwandishi alikuwa Mnyasa wa ukoo “Kamtunda” akiitwa Halima, na alipobatizwa aliitwa Ida Halima. Yeye pia alikuja kutoka Mpanda, na chombo chao kiliwateremsha Unguja kwanza. Mwisho waliletwa Frere Town kwenye wajoli wenzao, na hapo ndipo alipopata kuolewa.

Mtoto wao alizaliwa Frere Town. Hajui lugha ya wazazi wake, basi kwa asili yeye ni Mnyasa, lakini kwa kawaida ni Mswahili wa Mombasa hasa. Baba yake alifariki akali mtoto yuko skuli, na mama yake alikuwa mtu wa shamba akitumainia kiserema chake.

Mama yake mjane, alipata taabu sana hata asiweze kumtunza mwanawe. Juma akaanza kuwa mtoro, ala apatapo, akikosa yuashukuru. Mama yake alimpeleka kwa mjomba wake, Mlenga, akakae huko.

Mwandishi alibatizwa akaitwa James Juma Mbotela (Juma yaani, alizaliwa Ijumaa, na Mbotela ni jina la ukoo, naye mwenyewe aona fahari sana kwa hilo jina la mababu). Basi huyu James Juma mwana wa Mbotela ingawa alikuwa maskini, lakini aliendelea sana na kusoma.

James Juma alimaliza masomo yote yaliyowekwa kuwa- fundisha watoto. Akashinda Scholarship iliyowekwa na Bishop wa Mombasa, Bishop Peel, akaingizwa kusoma katika Buxton High School.

Mama yake James alifariki mwaka wa 1904 wakati huo James yuasoma.

Katika mwaka wa 1903 Chama cha “Industrial Mission Aid Society” kilituma Bwana na Bibi Harrison waje Frere Town kufunza watu kazi, chini ya msaada wa Church Missionary Society. Ndipo Wazungu hao walipomtunuka James Juma. Baada ya Bwana Harrison kukaa Frere Town miaka miwili, alishikwa na homa mbaya, na daktari akamruhusu arudi Ulaya akapate afya njema. Walitaka waende na James Juma, mwishowe Bishop Peel akakubali, ndipo alipoandamana na Wazungu hao mpaka kwao Ulaya Uingereza, naye hakutaka kurudi Afrika hata kidogo. Na huo ni ushuhuda wa kutosha kuwajulisha kuwa alikuwa na raha kweli kweli!

Kwa vile alivyokuwa amekwisha onja utamu wa masomo, hakukaa bure Uingereza. Aliendelea kusoma katika L.C.C. School, West Hill School, Wandsworth, na sehemu nyingine katika Wandsworth Technical Institute. Nyakati za ruhusa alitem- bezwa mahali pengi, akapata rafiki wengi sana. Alipokuwa Uingereza alijaribu kuongeza maarifa katika kazi ya ukarani aliyokuwa akiifanya katika Buxton High School. Kwa neema ya Mwenyezi Mungu, aligeuzwa kuwa mwalimu Mwinjilisti!

Mwisho wa mwaka wa 1906 alirudi Afrika na Wazungu wale wale aliotoka nao Frere Town. Lakini mambo huendelea yakigeuka. Juma akawa Mwinjilisti, kwanza katika nchi za Wakikuyu, pili katika nchi za Wamasai, katika kabila lile lile lililomwua baba yake. Tatu alikuja akawa mkaaji kabisa Ukambani, pamoja na Wazungu wale wale.

Alimwoa Grace David mwezi wa March mwaka 1908 katika kanisa la Kambui, Kikuyu, ambaye alizaliwa Seychelles.

Watoto wake wote walizaliwa Ukambani, waume wanane na msichana mmoja. Na wawili, binti mmoja na mtoto wa kiume, walifariki dunia, mmoja mwenye umri wa miaka kumi na mmoja, na mwingine umri wa miaka tisa.

Mwalimu huyo James Juma alikuwa mtu wa mashughuli mengi. Alikuwa mwalimu wa skuli, mhubiri Injili, mfasiri lugha, fundi wa kujenga na wa kufanya na kuchoma matofali.

Sasa watoto wake wamepata elimu ya kutosha, maana wengine ni walimu, na wakulima, na mmoja ni mkalimani.

Yule Juma, mwana mmoja wa baba na mama, mpaka sasa ana wajukuu ishirini na wanne.
 
1. KWAO MPANDA

VIZALIA vya Mateka walikuwa wakipenda sana kuuliza, na kuelezwa na baba zao, jinsi kulivyo huko, baba zao walikotoka. Kila jioni, Juma alikuwa akikaa jamvini kando ya baba yake, akimsikiliza vile aimbavyo nyimbo za kwao Mpanda. Huyo baba alipenda sana kuzungumza na mwanawe habari za kwao. Basi Juma alimwuliza baba yake amweleze mahindi ya kwao yalivyo, naye baba yake alimwambia hivi: “Mwanangu, huku pwani hakuna mahindi ya haja, mahindi yako Mpanda. Ukichomewa hindi moja la kwetu, huliishi kulila! Nikifikiri kwetu, machozi hunilengalenga. Mashamba ya kwetu si kama haya tulimayo hapa. Ya kwetu ni makubwa sana, huwezi kutupa jiwe kwa teo likafika mpakani kwa shamba. Hapo mwivi aibapo mahindi shambani, hatumsikii wala hatuwezi kujua. Wakati wa mavuno hatuwezi kuvuna mahindi yote jinsi yalivyo mengi. Maghala ya vyakula huwa yamejaa vyakula vya mwaka jana. Vile vya magha-

lani huondolewa vikachomwa moto, na vile vipya hukusanywa vikatiwa humo.” Vile Juma aambiwavyo, huwa ameyatia moyoni sawasawa, huku akiwaza akisema, “Ningependa kuiona nchi hiyo na hayo yaliyomo.” Akamwuliza baba yake, “Je, hizo njugu nyasa za kwenu baba, zikoje, ambazo huku zaitwa karanga ?”

Baba yake akamjibu akisema, “Hizo hazionekani kuwa ni kitu kwetu. Mama zenu huzitumia sana katika mboga, ndizo nazi za Mpanda. Mno mno huliwa na watoto. Wapewapo hizo njugu hutulia sana. Hapo kina baba na kina mama waendapo mashamba ya mbali, watoto huachwa mjini walinde mji, na wasikiapo njaa huenda ghalani kutoboa madundu ya njugu, waziangalia zimiminikavyo chini. Halafu huzichukua, wakazi- menya, wakazikaanga na kuzila.”

Juma aliuliza, “Je, hapo baba na mama warudipo kutoka mashambani hawatawapiga”? Baba yake akamjibu, “Watoto hawawezi kupigwa kwa jambo kama hilo, hicho chahesabiwa kuwa ni chakula cha watoto na matumbili. Sisi twaona ajabu kwa kuwa huku pwani, hizo njugu zauzwa.” Kisha Juma akauliza habari ya samaki wa huko Mpanda.

Baba yake akamwambia, “Huku pwani hakuna samaki wakubwa na wenye mafuta kama wa kwetu. Sisi sote tuliopo hapa hatuwezi kwisha kumla samaki mmoja wa Mpanda.”

Juma alipendezewa sana kusikia habari ya kusifia hao samaki wa kwao, pia kwa vile yeye mwenyewe alikuwa mvuvi. Na kila aletapo smaki nyumbani baba yake humwambia, “Samaki wa pwani ni wadogo sana”. Baba yake akaendelea na kusema, “Samaki wa kwetu wachomwapo, makaa ya moto huzimika kwa ajili ya mafuta mengi ya samaki. Kisha, hapo tuchomapo samaki mmoja, ni lazima tuwaite majirani waje kutusaidia kumla.”

Juma aliposikia vile, alikuwa hafai kwa kucheka kwingi. Alijua hivyo aambiwavyo ni kweli, kwa sababu vijana vizalia wengi walikuwa wakiambiwa hivyo na wazazi wao Mateka. Ndipo Juma akataka aelezwe jinsi muhogo wa huko kwao ukuavyo. Baba yake akamwambia, “Ukitaka kuula muhogo wa kwetu, muhogo ambao wewe mwenyewe umeupanda; wakati wa kuung’oa ni lazima ualike watu waje wakusaidie kung’oa. Tena siku hiyo, mama yako huwa ametengeneza togwa ya mtama ya kunywewa na wale wang’oaji wa mihogo. Tena atengeneze na pombe. Hiyo pombe hunywewa mihogo ikiisha ng’olewa. Basi huwa hivi: uamkapo asubuhi hiyo ya kung’oa mihogo uchukue kigoma ukipige, ndiyo mbiu hiyo. Ye yote asikiaye hujua kama leo kwa Mzee Mponda kwang’olewa mihogo, kwa sababu yeye Mponda alikuwa mkulima mkubwa mno wa mihogo. Na mihogo ing’olewapo, huimbiwa.”

Baba yake aliposema vile, Juma alimwambia, “Tafadhali, baba, niimbie huo wimbo wa kung’olea mihogo”. Baba yake akasema, “Siwezi kukuimbia, kwa maana mama yako hana togwa ya kunipa, wala hana pombe. Kama nikiuimba huo wimbo, nitaingiwa na mori niende nikang’oe mihogo ya watu. Wewe na mama yako mtaniona kuwa nina wazimu, kumbe, ni vile nilivyofikiri kwetu Mpanda. Wewe sikiliza habari yake tu, usiwe na haja na huko kuimbiwa.” Baba yake akaendelea na kumwambia, “Wanaume wale waliokuja kung’oa mihogo, ni wale waliooa. Mihogo ya kwetu haipandwi, wala haichimbwi na wavulana.”

Juma aliposikia vile alimwuliza baba yake, “Mbona huku nina shamba langu la mihogo nami ni mtoto tu”?

Baba yake akamjibu, “Huku ni Uzunguni, twashika hayo tuambiwayo na hao waliotuleta huku.

“Sikiliza basi nikumalize hiyo habari ya mihogo. Ile mihogo ya Mzee Mponda ilipong’oka iliwaangusha hao waliokuwa waki- ing’oa. Haiwezekani kung’olewa mingi, shina moja hung’olewa asubuhi, na jingine saa za jioni, kwa jinsi ilivyo mikubwa! Ukiiona utadhani ni pembe za ndovu. Hao waing’oao, siku ya pili yake huwa na mavune.”

Wakati wote huu baba yake alipokuwa anamweleza, Juma alikuwa anaumia mbavu kwa kucheka. Mama yake aliyekuwa akipika akamwambia mumewe, “Ni afadhali uache kueleza, maana mtoto anaumia mbavu kwa kucheka sana.’ Baba akamjibu mkewe, “Juma ndiye aliyetaka nimweleze habari za kwetu, na sasa anacheka wala hasikilizi!” Lakini Juma alikuwa anasikiliza sawasawa; isipokuwa hiyo habari ilimfurahisha sana, ndiyo sababu ya kucheka.

Baba yake akasema, “Hao wanawake wa Mzee Mponda hualika wanawake wenzi wao waje kuipasua, na kwa vile ilivyo mikubwa tena migumu, haipasuliki isipokuwa kwa shoka. Mihogo ya kwetu huchanjwa kama kuni, halafu huanikwa yakawa makopa, tena hayo makopa hupondwa yakawa unga; unga ufanywao sima ya ujora. Wale wanawake waliokuja kusaidia kupasua hiyo mihogo, hupewa fungu lao ndio ujira wao. Mashina hayo mawili, mihogo yake huliwa kwa siku nyingi. Ukiwaona hao kina mama walivyoibeba utadhani ni mizigo ya kuni.”

Mara Juma akaitwa mekoni kwa mama yake, akaambiwa ateke maji amletee baba yake anawe mikono, kwa kuwa chakula kimekwisha kuwa tayari. Na baba yake aliyeachwa pekee, aliendelea akijizungumza kwa kuimba nyimbo za kwao, mpaka alipoandaliwa chakula.

Siku ya pili yake, baba yake Juma alimwambia mwanawe akae amweleze tena habari za vyakula vya kwao. Akamwambia, “Huo muhogo tulioutaja ni chakula kikubwa sana cha kwetu, tena ni chakula kimtiacho mtu nguvu. Mihogo ya kupika na samaki wa kuchoma, ndicho chakula cha kwetu. Chakula kingine kilicho bora ni sima ya mtama. Hata mpunga pia uko, lakini mpunga mwingi tulikuja uona katika nchi ya Umakua, nchi ya Msumbiji. Mtama hufanywa -boji na pombe. Na kila afanyaye pombe ya kwanza ya mwaka, humpelekea mkubwa wa mji, ili aonje pombe ya mwaka. Ndizi za kwetu zaivia migombani. Ndege huzila watakavyo, hawachungwi, wala ndizi haziuzwi kama tuonavyo huku pwani.

“Kadhalika vyakula vinginevyo ni vile vile. Na mizinga ya nyuki pia ina tofauti. Angalia huu mzinga wetu; tangu nilipoutia hapo katika huo mkanju, sasa ni zaidi ya mwaka nao hauna asali ya haja. Juzi tulipokwenda ondoa, hata hili bunguu la mama yako halikujaa! Kama ni kwetu hatungeiisha kuitoa.” Baba yake akaongeza kumwambia, “Wamwona huyu Mzee Mwambila anavyosumbuka huku na mizinga yake ya nyuki? Kama ni kwetu, angetoshewa na mmoja tu. Huko kwetu mzinga wa nyuki huvunja tawi kwa wingi wa asali. Tena si mno watu kuangika mizinga. Iko miti mikubwa sana, na katika miti hiyo mna mapango, na ndani ya hayo mapango nyuki hukaa wakafanya asali. Hao watafutao asali huenda wakazoa kuko huko mwituni. Tena kuna mafuta ya mbarika ambayo ni bora sana kwetu, yana thamani sana. Watu huzipanda sana ili wapate mafuta ya kujipaka, mwili ung’ae.”

Juma aliposikia vile, alikunja uso kwa vile alivyokuwa hapendi kusikia harufu ya mafuta ya mbono. Baba yake akamwambia, “Mafuta hupakwa sana katika siku za ngoma. Ngoma, ndiyo sherehe kubwa sana huko kwetu. Huyo mkubwa wa kwetu afurahiwapo, huamuru ngoma zipigwe kwa siku nyingi. Kina mama hupika majungu makubwa makubwa ya vyakula aina aina, navyo huletwa kuko huko kwenye uwanja mkubwa wa ngoma kwa mkubwa wetu. Na asiyekuja katika ngoma hizi, hutozwa sana na huyo mkubwa wetu, kwa vile alivyoonyesha madharau. Ijapokuwa wana furaha jinsi hiyo, lakini furaha huisha wasikiapo kama kwa fulani kumekufa mtu. Kifo huko kwetu kilikuwa ni jambo lipelelezwalo sana. Ingawa watu ni washenzi kweli; lakini hapo mtu afapo, wao husema, ‘Mungu ametujia, tena hakupendezewa nasi.’ Watu wote wa mtaa huo uliofarikiwa, na nchi nzima ya huyo mkubwa wetu, huwa wamenyamaza kimya. Na wasemapo, husema kwa kunong’ona. Siku moja huyo mkubwa wetu aliamuru ngoma kubwa ichezwe, na ngoma hiyo ndiyo iliyokuwa yangu ya mwisho kucheza kabla sijakamatwa kuwa mtumwa. Mkubwa wetu akasema ‘Ngoma ipigwe mwezi mzima! Hata hao Wanyasa waliokuwa upande wa pili wa ziwa walikuja kucheza, wale kina Kamtunda. Tulipokuwa tumecheza ngoma siku kumi, tulisikia kwamba kwa Mzee Maonga kumefarikiwa! Tulijua ni kweli kwa kuwa Maonga mwenyewe aliacha kuipiga ngoma ile kubwa iitwayo msondo. Kila mmoja alitoka katika uwanda wa ngoma pasipo kusema na mwenziwe sana sana.

“Maana ya kufanya hivyo, husema, huyo aliyeleta kifo huwa hajatoka, na tukisema sana, tutasikia mwingine amefariki. Kwetu mtu akifiwa, watu hawalii kwa kupiga makelele. Tabia hii twaiona huku pwani. Watu hukaa kimya kwa kitambo kirefu sana, ndiyo matanga yao. Msafiri huvunja safari yake, mkulima huacha kulima mpaka mavuno ya mwaka yaishe. Watu si mno kufa huko kwetu, kama tuonavyo huku pwani. Watoto wadogo hufa wangali wachanga, lakini walioinukia hukua wakakonga. Mchawi huuawa kwa kupigwa mawe au kuchomwa moto. Mwivi hutendwa vile vile kama mchawi, au mtu mbaya ajulikanaye vitendo vyake huuawa vile vile, na watu hawawi na majonzi kwa ajili ya watu wa namna hiyo.

“Wamwona huyo Mzee Chiponda alivyo, kama umepata kufika huko kwake nyumbani, umeona nini ?”

Juma akajibu, “Kwake kuna ngozi nyingi za wanyama mwitu”. Baba yake akamwambia, “Umejibu kweli, maana yeye huko kwetu ni mwindaji mkubwa. Mkubwa wa nchi yetu alikuwa anampenda mno huyo Chiponda. Karibu watu wote wa kwetu walimtumainia huyo Chiponda na upindi wake. Vyakula vya mashambani huharibiwa na wanyama wabaya kama ndovu na nyati. Wanyama hawa waingiapo mashambani, watu humlilia Chiponda aende kuwaua, naye huenda na wafuasi wake. Harudi mpaka awe amewaua kabisa. Vile umwonavyo ni hodari sana. Mshale wake hauanguki chini patupu! Kwa vile alivyokuwa shujaa, alitungiwa wimbo wa sifa sana. Huwinda majira ya mvua na majira ya kaskazi. Atakaye nyama hupata atakavyo, kwa Chiponda haziuzwi. Maadui wajapo kutupiga katika siku zile za ngoma, Chiponda na watu wake huwa wamejificha mwituni kuwavizia”.

Juma moto apendaye kuuliza sana akamwuliza baba yake, “Baba, ni watu gani hao waliokuwa wakija kuwasumbua, nanyi mwasema mlikuwa mwakaa raha kwenu na amani ?”

Baba yake akamjibu, “Liko kabila moja la watu namna ya Wamasai. Sisi twawaita Wamasai wa Mpanda, lakini huko wakaako hatukujui. Wao walikuwa shujaa kwa vita zaidi yetu. Miguu yao ilikuwa mirefu sana ndiyo miguu ya milonjo; tena wembamba na wepesi kwa kwenda wenye nguvu sana. Silaha zao zilikuwa mikuki, sime, ngao, hata mishale na rungu.

“Huja kwa kuibaiba, nao huiba wanawake, watoto na mifugo. Ni watu wenye hasira sana, chakula chao ni nyama ya mawindo. Hawakuwa wakija kila mara, na wajapo walikuwa wakituumiza sana. Nilipokuwa kijana tukichunga, mimi na wenzangu; hao vijana wenzangu walikamatwa bondeni kwenye nyasi zile zi- itwazo mlangamia. Nami niko ukingoni, nikasikia kelele, na lugha yenyewe sielewi. Mara wale vijana walikamatwa, wao na mbuzi zao. Siku hiyo hiyo adui hao walifukuzwa sana, lakini wasiwezekane. Waliepa mishale, wakiikinga kwa ngao zao. Kina Chiponda walipata kumwua mtu mmoja wao, hasa alikuwa jitu, si mtu! Alikuwa amebeba vitu chungu, kitoma cha asali, mkuki, sime, ngao, mkoba wa nyama na shoka na rungu pia. Alipouawa aliachwa wazi aonekane na kila mtu. Hao waliomwua wasema ilikuwa bahati tu, kwa vile alivyotumbukia katika shimo la Mzee Chimwenye, la kutegea nguruwe waliokuwa wakimharibia mihongo yake. Kina Chiponda walipoona mavazi ya jitu hilo, yeye na watu wake walipata maarifa ya silaha na mavazi ya vita. Chiponda alimkosa ndovu siku moja alipokuwa amevaa mavazi hayo. Tena hata hao watu wa mjini kwetu walipata kushikwa ghafula na watu hao walipokuwa vichuguuni, wakiangalia kama kumbikumbi wametoka; wapate kutengeneza mahali pa kuwakamata sawasawa. Kwetu watu waendapo huko vichuguuni, ni lazima watazamie kwa mganga kama pana kisirani. Sultani au mkubwa wa mji huamuru mbiu ipigwe ya watu kwenda kutega kumbikumbi.”

Juma aliposikia kama kumbikumbi hupigiwa mbiu, alianguka chini kwa kicheko. Hata alimwuliza baba yake, “Ehe, hao kumbikumbi hupigiwa mbiu kwa sababu gani?”

Baba yake akamweleza, “Wadudu hao si wazuri wakikamatwa ovyo tu, mtu huwa kiziwi! Tena mwanadamu wa kwanza alitoka vichuguuni, basi vichuguuni mna vizuka, hamwendewi ovyo”! Mkewe aliposikia vile, akamkemea mumewe, akamwambia, “Usimfundishe mtoto mambo ya watu wa- zima. Je, akiota usiku, au akiweweseka au kujiwa na hao wenyewe wa vichuguuni ?”

Baba yake akaendelea kusema, “Mji ulio na watoto wengi kama ule wa Chimwenye huwa una machezo mengi usiku wa mwezi. Kina baba na kina mama huenda kuangalia machezo ya watoto, kwa sababu huko kwa Chimwenye ndiko walikokuwa wakikutanikia. Machezo yao yalikuwa ya kuimba, kubebana, kurukana, na wengine wafanye kuigiza machezo ya vita. Wayakosapo hao kina baba kuwaonyesha. Wavulana na wasichana hucheza pamoja usiku wa mbalamwezi. Machezo mengine yalikuwa ya kuhukumiana, na mengine machezo ya arusi, na mengine huwa matengenezo ya kuposa. Waweza kumwona mwivi ameiba naye anahukumiwa; mchawi amekamatwa, anahukumiwa kuuawa. Basi vile wazee waangaliavyo, waweza kupambanua ya kwamba mwana fulani atakuwa kiongozi wa vita, au mtungaji wa nyimbo, au mwindaji, au mwamuzi. Na wasichana kadhalika; mama mwema hutambulikana na mama mbaya pia hujulikana pale pale, na hivyo wachezavyo wana shibe. Basi usikiapo watu wengine wanatamani kurudi kwao, huwa wakikumbuka mambo hayo mengi ya kwao, na hizo ngoma za kila siku, na chakula cha bure.”

Baba yake alipomaliza kueleza hivyo, Juma aka- mwuliza, “Baba, ilikuwaje ninyi kuacha nchi namna hii, hata mkafika huku pwani? Tena wasema watamani kurudi, lakini huwezi, wala hutakuona tena huko!”

Basi yule baba mwema akamwambia mwanawe, “Mwanangu, nakuona u mchunguzi mno wa mambo, na kama wataka ku- jua yote haya, basi mimi nitaanza kukueleza tokea mwanzo hata mwisho. Nawe, uwe na fahamu sawasawa, uje uwaeleze wanao, nao waeleze wana wao baadaye. Na ukiweza kuwaeleza walimwe-ngu ni bora zaidi.”

Basi kila jioni Juma alikuwa akiisha kazi zake mapema ili apate kukaa jamvini na baba yake asimuliwe. Huyo mama pia alimsaidia mumewe katika kumkumbusha.
 
2. MWAKA WA KUMBIKUMBI

SIKU hizo zilikuwa siku za kumbikumbi kutoka, katika mvua ya mwaka. Ilikuwa wakati wa jioni kama saa kumi na moja huko Mpanda, katika bara ya nchi tuliyotoka. Mvua ya mwaka ilikuwa imekunya vizuri. Sadaka za Mungu wa mvua zilikuwa zimekwisha tolewa mizimuni.

Waganga walikuwa wamekwisha agua ya kwamba watu watapata mvua nzuri. Waliambiwa wapande, walime, kwa sababu mwaka huu ni wa neema.

Mashamba yalipopandwa, ngwe zimekwishalimwa, na mimea mizuri inapepea mashambani; watu walianza kutega kumbikumbi wa mwaka. Katika bara hizo kumbikumbi hutoka mapema sana. Kina baba hutangulia kwenda kutengeneza mashimo ya kuwakamatia, na kina mama huja nyuma na makapu yao kuwazoa mle mashimoni walimoangukia kwa kuchomwa mabawa yao na mienge ya moto, iliyokuwa na kina baba. Wadudu hao walipendwa sana hapo mwaka wao wa kuja ufikapo.

Basi hapo walipokuwa wakifurahia hao kumbikumbi, wakati huo, walisikia kilio pande zote za mji! Hao wenyeji waliingiliwa na watu wasiowajua, nao walikuwa wakikamatwa na kufungwa. Maadui hao, wengine walikuwa weupe na wengine weusi. Nyuso za hao weusi zilikuwa zatisha sana. Basi, wale waliokuwa wakiteka kumbikumbi waliingiliwa kutekwa gha- fula. Hao wenyeji waliokuwa wamekaa kwao katika raha bila hofu yo yote, hawakuwa tayari kujitetea, wala hawakuweza kukimbia mbali. Wanaume kwa wanawake wote waliopatikana, walishikwa na kukazwa kamba za mikono na za miguu na hao watu wengine waliowashinda nguvu. Watu hao ni wale Waarabu waliokuwa wakitafuta pembe na watumwa, wakawauze mbele. Watu hao walivaa vilemba, tena walikuwa na silaha za panga na bunduki. Hao watu weusi waliokuwa nao, walikuwa na mataruma makubwa sasa nyusoni mwao, ambao ni urembo wa kwao. Nao ni wale Wamakua wa Msumbiji, ndio waliowaongoza wale Waarabu wafike Mpanda.

Waarabu hawa walikuwa na msafara mwingine wa watumwa walioshikwa pande zile zile za bara ile wakafungwa na miti mibaya yenye mafundo shingoni mwao, wakiumia sana. Mk- ihadithiwa na hao wenyewe waliofungiwa miti hii mibaya, maumivu yao yasikitisha sana! Na jinsi walivyoshikwa makazini mwao ovyo tu. Wako waliokamatwa mashambani, mitoni wakivua samaki; wako walioshikwa wakiwinda, malishoni, wengine ngomani, wengine visimani, hata nyumbani. Nyumba na ghala zao zilipigwa moto. Chiponda na watu wake pia walishikwa. Kwa vile walivyojulikana kuwa ni wajeuri tena wakali, walifungwa kamba za mikono kwa nyuma.

Wako kina mama waliopokonywa watoto wao wachanga. Huyo Chaliwali, ambaye ni mwenye safari hii, alikuwa mtu mwovu. Aliua watoto wengi kwa upanga wake. Hakutaka wale kina mama wenye wa toto wacheleweshe safari. Ndipo alipowaambia, “Ninyi mwachelewesha safari yangu kwa kutaka kunyonyesha.” Alipoona wale kina mama walia sana alisema, “Haidhuru, mbele nitawalipa ninyi watoto wengine.’ Hao kina mama hawakuweza kunyamazishwa kilio na yale maneno ya Chaliwali. Waliona ni heri kufa kuliko kuishi.

Chaliwali na rafikize wakaongoza safari yao kubwa ya watumwa kuelekea pande za pwani kwa haraka. Walipokuwa wanapelekwa watumwa walikuwa wakichungwa kwa kuen- deshwa mbio kama mbuzi. Walienda wakilia, walijua hawataiona tena nchi yao. Chaliwali hakupendezewa na kilio kile kikubwa cha usiku, na giza limefunga! Akawaambia, “Nyamazeni. Msiponyamaza, nitawakatila mbali vichwa vyenu kwa upanga!” Aliposema vile alikuwa na hasira sana. Mara ile ile akamfunga mtumwa mmoja mnyonge, akawaambia wale watumwa, “Angalieni jinsi nilivyomtenda huyo jamaa yenu. Nanyi, mkiniasi nitawatenda vile vile. Nendeni kimya! Ninyi sasa mmekuwa mali yangu, semeni ‘bwana wetu!’” Watumwa wote wakajibu, “Mfuana wetu! Mfuana wetu!” (Hawakuweza kutamka sawa kwa sababu hawakuelewa na Kiswahili kwa vile isivyo lugha yao.) Humo njiani waliumizwa sana na miti hiyo ya panda waliyotiwa shingoni mwao. Masikio yao yalikuwa yavuma kwa maumivu ya kugongwagongwa kila wakati.
 
3. MSITU WA NDOVU

HUYO Chaliwali na wale wenziwe, na watwana wake ambao ndio askari zake, waliiongoza hiyo safari ya watumwa kwa kuhofia watu wengine. Aliacha njia ya kanuni akaona ni heri apite mwituni. Mnamo siku tatu, waliingia katika mwitu mkubwa mno uitwao, Msitu-wa-Ndovu. Kwa tamaa ya kupata pembe za ndovu, alikusudia kupita huku kupumzisha safari katika msitu huu. Chaliwali akamwambia mnyapara wake Mrere aiongoze ile safari yake, akamngoje huko Ziwa la Ndovu. Yeye atasalia katika huo Msitu wa Ndovu, akitafuta pembe za ndovu. Kwa kuwa usiku ule, huyo Chaliwali aliota ameona mizoga mingi ya ndovu, akasema, “Huenda ikawa bahati yangu nikapata pembe!” Lakini Mrere akamjibu hivi, “Mbona bwana wangu umeota maiti nasi tuko katika mwitu huu wa hatari?” Chaliwali akamngurumia akamwambia, “Kelele! Kefule mtwana we! Mtumwa waahedi! Chup! Nyamaza kimya!”

Mrere akamjibu bwana wake hali amepiga magoti, uso juu, na mikono kichwani, “Ewallah bwana”.

Chaliwali akamwambia, “Wewe timiza amri yangu, tunza watumwa sawasawa. Ukiona hatari njoo uniarifu umtume Mtipia.” Mrere akamjibu, “Ewallah bwana mkubwa! Ewallah bwana wangu nimesikia!” Mrere akamwacha bwana wake akaenda mbele. Kabla hajafika ziwani, alitupa jicho mbele akaona ndovu wengi sana karibu na hilo ziwa! Akairudisha safari polepole, mpaka kwa bwana wake. Chaliwali alipoona safari imerudi upesi alimwuliza Mrere, “Je! Mrere, kuna nini huko?” Mrere akamjibu akamwambia, “Bwana wangu, hao ndovu niliowaona ziwani ni wengi sana. Ukiwaua wote hao pembe zao zitakupa utajiri wa maisha! Hatukukubali kupiga kambi huko tusije tukakutilia fujo, ni heri tukakungojee Bonde la Nyasi za Simba.” Chaliwali akamwambia, “Tunza watumwa nami sitakawia. Mnamo saa tisa nitawasili kambini. Msiende mbele zaidi.”

Mrere akatelemsha wale watumwa Bonde la Nyasi za Simba, akamwacha Chaliwali akiwaza wale ndovu alioambiwa. Chali- wali akawaambia wale Waarabu rafikize, “Na tuwindeni mumu humu mwituni tutafute mizoga; hatuna bunduki za haja za kuwaendea hao walio ziwani. Kisha tujihadharini na upepo wasije wakasikia harufu yetu, tukakosa pembe zetu na hao watumwa.”

Basi walizunguka tu katika mwitu ule, kisha kwa woga mkubwa, nao walikuwa mbali na ziwa.
 
4. BONDE LA NYASI ZA SIMBA

BONDE hilo lilikuwa katika mahali pazuri kati ya milima, na nyasi za bonde hilo zilikuwa ngeni machoni mwa watumwa. Hilo bonde lilizungukwa na msitu wa miti pande zote. Ingawa jua lilikuwa lachoma utosi, papo katika bonde hilo mlikuwa na hewa nzuri ya baridi.

Upande wa mkono wa kulia palikuwa na kisima cha maji mazuri. Kwa mbele zaidi vyaonekana vilele vya milima, vime- tokeza kwa juu zaidi kupita ile miti mirefu ya huo msitu, na njia ya kuifikilia milima hiyo imo humo katika msitu. Watumwa waliburudika kidogo kwa ile hewa ya pale. Wengine walipumzika magogoni, na wengine walijilaza katika nyasi zile nzuri laini.

Mahali hapo ingawa palipendeza, palitisha sana kwa vile zile kingo za mahali hapo zilivyokuwa ndefu. Mtu akipatikana na simba ni shida kupona. Hapakuwa na kinyama hata ki- moja. Palitosheleza kujulisha kuwa ni uwanda wa yule aitwaye Mfalme wa wanyama, walikuwa wakitazama huku na huku kwa hofu, wakidhani mnyama mkali atatokea mara moja! Ilikuwa kama saa sita za mchana, hapo Mrere alipoileta safari katika kambi hii; naye hakuwa na furaha kwa vile alivyongurumiwa na bwana wake, na kwa kufikiri ndovu wale wengi aliowaona. Basi alipokuwa akipumzika hivyo, alijiwa na mawazo mengi. Mrere akamwambia Mtipia ampe tumbako kidogo, yake ilianguka alipokuwa amepiga magoti akiomba msamaha mbele ya bwana wake katika Msitu wa Ndovu.

Mtipia akamwambia, “Ngoja nitie hesabu mali ya watu nisije nikangurumiwa kama ulivyongurumiwa punde kidogo. Omba Mungu umepona baba! Ungeipata wapi tumbako ya kutafuna wakati huu !”

Mrere akasema, “Ah safari hii yetu naiona kuwa mbaya ina matata sana, tena visirani ni vingi. Laiti Mrere ningeweza kufika kwa mganga, ningetazamia.” akazidi kusema, “Leo bwana wangu amenionea bure. Amenitukana, tena ataka ku- niua kwa upanga! Kama nisingalimpigia magoti upesi, wakati huu ningekuwa maiti!” Mrere akamwapiza bwana wake kwa uchungu aliokuwa nao akasema, “Thuu! kufa kuko huko mwi- tuni wewe na hao jamaa zako !”

Mtipia akamwuliza kama ataka tumbako tena ya kuta- funa. Mrere akamjibu. “Basi, hiyo niliyochukua yanitosha, napumzika kidogo nimngojee huyo mwana kulaanika aliye mwituni!”

Mtipia akamwambia, “Huyo aliyekuambia hadithi hiyo kama simba ana hirizi alikupata sawasawa!??

Mrere akazidi kumwambia Mtipia, “Kama simba ana hirizi, mbwa anayo, na paka anayo! Kwa sababu wanyama wote hao niliowataja, kila mmoja hutapika fundo la nyasi. Mkiona fundo la nyasi, basi mwasema ni hirizi ya simba!”

Mtipia akamwambia Mrere, “Nakuona ungali kijana hujavuka bahari.” Lakini Mrere hakutaka kushindwa akesema, “Wasikia Mtipia, simba halali manyasini babu! Analisha tu, alala ma- pangoni. Tena simba, ha,-ee!” Mambo akadakia, “Acheni kumtajataja mdude huyo. Hamwoni tuko mwituni? Wewe Mrere sasa hivi nusura ufe kwa upanga wa Chaliwali, tena watuvutia kisirani. Mwafanya mambo ya kitoto nanyi mwajidai mu watu wazima. Mwasema safari yetu ina visirani, kumbe hivyo visirani mwavileta wenyewe! Mnyama huyu akitajwatajwa hutokea. Ehe! Akitokea mtampinduaje nanyi hamna hirizi yake? Au mwanyeta kwa kuwa hamna pingu kama hizi zetu, kwa kuwa mtaweza kukimbia atokeapo, mtuache sisi tukitafunwa! Vyema, msitucheke sana maana leo ni sisi na kesho huenda ikawa ni siku yenu ya kuteseka!” Mambo akisema hivi, alikuwa amechukiwa sana, na macho yake yalikuwa mekundu, yamemtoka pima kwa woga! Mambo alikuwa mzee, lakini hao waliomshika hawakumwonea huruma, kwa kuwa alikuwa na afya zake, na maungo yake yalikuwa mazuri, hayakuchakaa.

Mrere aliwazuia kina Mambo wasiseme, akawaambia, “Tuk- isikiwa na Chaliwali twazungumza kama waungwana, sijui atatufanyaje.”

Mtipia apendaye ubishi akamwambia, “Mrere mwoga! Ndiyo sababu ukapoteza tumbako yako kwa woga mwingi. Chaliwali amekwisha tuambia saa atakayojia, sasa mwaogopa nini?”

Mrere alijipurukusha kwa maneno mengine, akasema, “Njia hii siyo tuliyokujia bara hizi hata kidogo. Kile kilichofanya tugeuze njia sikijui.”

Mtipia akamwambia, “Mrere mwongo sana wee! Wewe ndiwe uliyesema tupite njia hii; sasa wasemaje? Mbona wapayuka sana? Kama huna neno la kusema, si heri ukajinyamazia ?”

Mambo akayahakikisha yale yaliyosemwa na Mtipia, akasema “Kwa kweli, Mrere ndiye sababu ya njia hii. Nilimsikia akimwambia Chaliwali, ni heri tukapumzike Bonde la Nyasi za Simba.”

Aliposema vile, macho yake yalikuwa yakipesapesa huku na huku, kwa maana alisikia kitagaa kikianguka “kacha” akid- hani ni yule mnyama katokea ghafula. Walipokuwa katika mazungumzo hayo, walisikia sauti kama za watu za safari ijayo. Yeye Mrere alidhani ni wale ndovu aliowaona kule ziwani wamepitia huku. Mrere akawaambia wenziwe, “Nyamazeni! Chaliwali anakuja! Nasikia mishindo, wala hakupata pembe hata moja kwa vile alivyonitukana bure.”

Naye Mtipia akasema, “Hasa! Yafaa vivyo hivyo nisichoke na kuzihesabu!” Pale pale Mrere na Mtipia waliinua macho, wakaona safari kubwa sana ya watumwa kupita ile yao, nayo yatelemkia pale pale Bonde la Nyasi za Simba, imeongozwa na Bwana Ali. Mwenyewe hasa wa safari hii ni Bwana Upate, ndiye aliyekuwa tajiri mkuu.

Lakini Watumwa walimwita Mwinyi Upate. Watumwa hao walitekwa nyara pande za bara za juu zaidi, nao walikuwa wa makabila waliochanganyika. Watu hawa walifungwa ki- tambo, kwa vile walivyokuwa wamekonda sana. Walikuwa wametiwa ile miti mibaya ya shingo, na wengine walikuwa wamefungwa minyororo ya viuno, wamebeba mizigo ya pembe. Hizo pembe hazikununuliwa. Washenzi waliokamatwa na Waarabu walilazimishwa kutafuta pembe na kuzibeba mpaka pwani, wakauzwe pamoja na pembe zao. Ndiyo sababu Waarabu waipenda biashara hiyo, kwa vile ilivyokuwa ikiwapatia faida ya watumwa na pembe pia.

Watumwa hao hawakuweza kutamka Bwana Ali, basi, wal- imwita Pwanali. Pwanali aliagizwa na huyo Bwana wake Mwinyi Upate ya kwamba, akiona watu wengine wanatafuta watumwa na pembe za ndovu, ni lazima awakamate apigane nao, kwa sababu huyo Mwinyi Upate alidai upande wote wa nchi ile, kuwa ni nchi yake ya biashara; wala hana uwezo wa kudai hivyo.

Hapo Mrere alipomwona Pwanali akitelemkia Bonde la Nyasi za Simba na msafara wa watumwa, ile tumbako aliyokuwa akiitafuna aliimeza kwa woga! Alitamani kukimbia awaache hao watumwa aliokuwa nao, lakini Pwanali alimwelekezea bunduki, akimwambia, “Ukivuta mguu tu, umekufa!” Mrere akaona ni heri asikie aambiwayo. Akakaa kitako pamoja na watumwa wa bwana wake. Pwanali akaitulizia macho ile safari iliyopumzishwa na Mrere, akaitamani. Aliona ina watumwa wenye maungo mazuri.

Akatambua ya kwamba wamekamatwa karibu. Pwanali akam- wona Mtipia aliyekuwa twana kubwa kabisa, amesimamia wale walio na pembe, akamwuliza kwa ukali, “Na wewe ni nani? Mbona umethubutu kusimama mbele yangu?” Mtipia aliposikia vile, yeye pia alikaa kitako. Ndipo Pwanali akamwamrisha mnyapara wake, aliyeitwa Kupata, awafunge watu hao wawili Mrere na Mtipia mara moja. Wakachukuliwa wakafungiwa katika gogo kubwa lililokuwa hapo. Halafu Pwanali alimwendea Mrere, akaanza kumsaili na maswali ya mfulizo, “Wewe ni nani? Na safari hii ya watumwa, mwenyewe ni nani? Kisha yu wapi?”

Mrere alimjibu kwa sauti ya kunyenyekea, “Mimi naitwa Mrere. Na safari hii ya watumwa, mwenyewe ni bwana Chali- wali, tumemwacha nyuma yeye na wenziwe wakiwinda ndovu.” Pwanali akamwuliza tena, “Huko aliko ana safari nyingine ya watumwa ?” Mrere akajibu, “La, bwana, isipokuwa watwana wachache tu, na wenziwe watatu. Na mimi aliniagiza kumngojea hapa.”

Sasa Pwanali alijua ya kwamba Mwarabu huyo aitwaye Chali- wali ana cheo kumpita. Pia alijua ni mwana wa mwungwana, kwa vile alivyosafiri na Waarabu wengine rafikize. Basi aliazimia vita na huyo Chaliwali, kisha vita vya kumwangamiza! Pwanali akamwambia Mrere, “Mwevi, na kisha mu waongo. Jueni, hivi sasa mmekuwa mali ya Mwinyi Upate. Msipokubali, mauti yenu yatakuwa papa hapa mlipo.’ Mrere aliwaambia watumwa wa Chaliwali maneno yaliyosemwa na Pwanali. Na wale watumwa wakapaza sauti pamoja wakasema, “Mali ya Mpuana! Mali ya Mpuana! Mali ya Mpuana Pwanaliii!” Wakisema hivyo wenyewe walikuwa wanajidai kuwa wajua lugha ya Kiungwana, ambayo ni Kiswahili.

Pwanali akamwambia mnyapara wake Kupata, “Usichelewe; changanya watumwa pamoja. Kupata akawachukua akawatia katikati ya ile safari ya bwana wake.” Pwanali akamwambia Kupata, “Leo tumepata! Hata Mwinyi Upate akiwaona atafu- rahiwa sana. Na wewe Kupata sasa kazi yako imezidi, tunza watu sawasawa, tukifika pwani utaongezewa mshahara, tena utapewa wake wanne wawe wako mwenyewe.” Kusikia vile, Kupata alikuwa mkali juu ya watumwa. Mara kwa mara huwatisha na kuwatajia watachomwa na msumari wa moto wasipotii.

Jambo hilo lilikuwa linamwudhi Mzee Mambo, kwa kuwa hakutaka maungo yake yateketezwe.

Kisirani hiki, ndicho kile kilichosemwa na Mrere alipokuwa akitafuna tumbako aliyopewa na Mtipia. Mrere akamtupia jicho Mzee Mambo kama amwambiaye, “Umeniloga” kwa vile huyo Mambo alivyosema kabla hawajashikwa na Pwanali. Mtipia hakuwa na neno la kusema hata moja. Alikuwa akiwaza tu, hapo alipofungwa gogoni.
 
5. VITA VYA BONDE LA NYASI ZA SIMBA


 
Back
Top Bottom