Simulizi ya kipelelezi: Nani Muuaji?

Simulizi ya kipelelezi: Nani Muuaji?

Bishop Hiluka

JF-Expert Member
Joined
Aug 12, 2011
Posts
7,147
Reaction score
14,699
NILIKUWA na uwezo mkubwa sana wa kiakili na nilikuwa naongoza darasani kwa kushika nafasi ya kwanza tangu nikiwa darasa la pili shule ya Bronx English Medium Primary School.

Nilikuwa nazijua nchi zote huru duniani kwa majina na miji yake mikuu na hata majina ya viongozi wakuu wa nchi hizo, na hii ilitokana na uwezo mkubwa wa kukumbuka mambo niliokuwa nao. Kumbukumbu hizo zilikuwa zikinijia kichwani kwangu mfano wa mtu aliyekuwa akitazama filamu.

Mtaalamu mmoja wa afya ya akili na saikolojia wa hospitali ya mkoa, ambaye pia alikuwa rafiki wa Baba, aliwahi kusema kuwa nilikuwa na tatizo la ‘hypermnesia’ yaani uwezo usio wa kawaida wa kukumbuka mambo hata yaliyokuwa madogomadogo au ya kijinga.

Ilikuwa ikinitokea pindi ambapo watu walinitaka nikumbuke kitu fulani kilichotokea huko nyuma, nilivuta kumbukumbu zangu na picha ya tukio ilinijia na kukumbuka kwa urahisi mno mfano wa mtu aliyebonyeza ‘rewind’ yaani kitufe cha kurudisha nyuma matukio ya filamu kama ilivyo kwenye deki ya video.

Hata hivyo, akili yangu ilikuwa ni zaidi ya deki ya video kwa sababu sikuhitaji kubonyeza kitufe cha kurudisha nyuma au kupeleka mbele matukio ili niweze kukumbuka mambo yaliyotokea muda mrefu uliopita. Na sikuwa na vitufe vya aina hiyo kichwani kwangu kwa sababu kumbukumbu zangu zote zilinijia ndani ya akili yangu nilipoamua kukumbuka jambo.

Endapo mtu angeniambia, “Christopher, niambie mama yako alikuwa mtu wa aina gani,” ningeweza tu kuvuta hisia ili kurudisha nyuma kumbukumbu zangu kwenye matukio tofauti yaliyomhusu Mama na kisha kuelezea jinsi alivyokuwa kupitia matukio hayo niliyoyaona akilini kwangu.

Kwa mfano, ningeweza kurudisha nyuma kumbukumbu zangu hadi siku ya tarehe 7 ya mwezi wa 7 mwaka wa 2012 wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 5 na miezi 3 na siku 28.

Siku hiyo ilikuwa ni Jumamosi, mimi na Mama tulikuwa tumekwenda Mbamba Bay kumtembelea Bibi, mama yake mdogo Mama. Ilikuwa alasiri ya siku hiyo ambapo Mama alinipeleka kutembelea mwambao wa Ziwa Nyasa na kushuhudia ufukwe wa mchanga unaovutia.

Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kushuhudia maji mengi yakiwa yamekusanywa pamoja, na Mama aliniambia kuwa hilo ni ziwa linaloshika nafasi ya tatu kwa ukubwa kati ya maziwa yote yaliyopo katika bara la Afrika na linazihudumia nchi za Tanzania, Malawi na Msumbiji na wananchi wa nchi hizo na wageni wengine wamekuwa wakinufaika kwa uvuvi wa samaki na viumbe wengine waishio majini kwa chakula na biashara.

Mama alikuwa mnene kiasi na mweupe kiasi mwenye haiba ya kuvutia. Hakuwa mrefu wala hakuwa mfupi bali alikuwa na kimo cha wastani, mashavu yake yalikuwa ya mviringo mfano wa chungwa na nywele zake zilikuwa nyingi za singa na nyeusi fii. Alikuwa akiniambia kuwa zile nywele alirithi toka kwa baba yake ambaye alikuwa na asili ya Ethiopia.

Kwa hiyo, Jumamosi ya sabasaba ya 2012 tulipotoka nyumbani kwa bibi kwenda katika ufukwe wa Ziwa Nyasa, Mama alikuwa amevaa dela la maua ya buluu na kijani na nyeupe, ambalo kwa kiasi fulani lilikuwa limeushika kidogo mwili wake mkubwa na kulichora umbo lake, na alikuwa amening’iniza mkoba wake mzuri wa ngozi wa rangi ya pinki na miguuni alivaa viatu vyepesi vya ngozi

Tulipofika ufukweni tulikuta watu wengi waliopeleka watoto kuogelea, Mama alitafuta sehemu nzuri chini ya mti kandokando ya ufukwe na kuketi juu ya gogo la mti uliokatwa na kisha alifungua kitabu cha hadithi na kuanza kusoma, na ninakumbuka kilikuwa kitabu cha Kiingereza na kiliitwa ‘Second Best’ kikiwa kimeandikwa na Denise Robins.

Mama alipenda sana kusoma hadithi. Muda wote alikuwa akitafuna bazooka ambayo watu walisema kuwa ilikuwa ikikifanya kinywa kutoa harufu nzuri sana.

Mimi pia niliketi kwenye lile gogo kando ya Mama wakati watoto wengine wakiogelea kwenye maji machache kandoni mwa Ziwa Nyasa.

Mama alisoma kile kitabu kwa muda mrefu kidogo na kisha alikifunga wakati jua likikaribia kuzama na kuinuka kisha alilivua lile dela na kuliweka kwenye mkoba na kubakiwa na nguo fupi mfano wa chupi iliyounganika toka sehemu ya juu kifuani. Nguo ile iliyaacha mapaja yake makubwa yaliyonona yakiwa wazi na kuifichua miguu yake mizuri na ilikuwa ya rangi ya samawati.

Halafu akaingia ndani ya maji ya ziwa, akaanza kuogelea huku akilalamika kuwa maji yalikuwa ya baridi sana. Kisha alitoka na kunishika mkono akitaka kunipeleka kwenye maji ili niogelee pamoja naye, lakini sikupenda wazo la kuogelea kwa sababu nilikuwa nayaogopa sana maji, na pia sikupenda kuvua nguo zangu mbele ya watoto wengine, hasa wa kike, kwa sababu nilikuwa na aibu mno.

Mama aliniambia nivue viatu tu na niingie katika maji yaliyopo kandokando ya ziwa bila kuvua nguo kwani nilikuwa nimevaa kaptura na shati la mikono mifupi, alinitaka niyakanyage maji na kutembeatembea kidogo kandokando kwa ajili ya kupata uchangamfu.

Nilikubali na kuingia kwenye maji, nikasimama majini na kufurahia kugusa maji ya Ziwa Nyasa. Na Mama akaniambia, “Umeona? Inapendeza sana, hata ukirudi Morogoro utapata cha kusimulia!”

Kisha Mama aliniacha na kusogea mbele zaidi na kisha akajirusha kwa nyuma na kuzama chini ya maji, akapotea kwa kitambo fulani hata nikadhani kuwa labda wadudu wakali wa ziwani walikuwa wamemmeza.

Nikaanza kupiga kelele huku nikilia kwa hofu na huzuni, Mama akaibuka toka ndani ya maji na kusimama kwa miguu yake huku akinitazama kwa mshangao kisha alipiga hatua taratibu kuja mahali nilipokuwa nimesimama, akainua mkono wake wa kulia na kutawanya vidole vyake kisha akanielekea katika hali ya urafiki huku akisema, “Christopher, usiogope, sogea uguse mkono wangu... Usilie. Nisikilize, Christopher. Hata wewe utaweza kuogelea ukiwa mkubwa.”

Niliacha kulia kisha nikainua mkono wangu wa kushoto na kusambaza vidole vyangu kama alivyofanya Mama na tukakutanisha vidole vyetu kwa furaha na hapo Mama akaniambia, “Usiogope, Christopher. Humu hakuna papa wala nyangumi kama baharini.”

Ingawa nilikuwa na uwezo mkubwa sana wa kukumbuka mambo, lakini nilishindwa kukumbuka kitu chochote kilichotokea kabla sijafikisha miaka 4 kwa sababu kabla ya umri huo sikuwa nikiviangalia vitu katika mtazamo sahihi, kwa hivyo ubongo wangu haukuweza kuhifadhi matukio hayo kwa usahihi.

Pia uwezo wangu wa kukumbuka mambo ulinifanya kuweza kumtambua mtu yeyote niliyepotezana naye kwa miaka kadhaa nyuma hata kama angekuwa amebadilika sana kiasi cha kumchanganya kila mtu asijue ni nani.

Endelea kufuatilia...
 
Asante sana bishop nitaimalizia baaadae nimesoma kidogo ila majina ya humo mmmhh kuna mwalimu shunie
 
Back
Top Bottom