Simulizi za vitabu

Simulizi za vitabu

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
KITABU NILICHOSOMA: WATU MASHUHURU KATIKA UHURU WA TANGANYIKA
Na Hafidh Kido

1145425

Hafidh Kido akipokea kitabu kutoka kwa Mwandishi
KATIKA jamii tuliyonayo hatuna budi kusoma maandishi yoyote kwa bidii ya ajabu kabisa, kwa sababu dunia imepoteza lengo la kujifunza. Elimu tunayopewa tunapunjwa, taarifa au maarifa mengi tunatakiwa kujiokoteza wenyewe.
Mfumo wetu wa elimu unabinywa ili uendane na sera za nchi, kila siku mitaala inabadilishwa na kile tunachofunzwa si kile tunachokwenda kukifanyia kazi ndani ya jamii.

Hivyo, nimeanzisha ukurasa huu kwa lengo la kuonyesha vitabu nilivyosoma. Kisha nitavichambua kwa lengo la wegine kuokota nilichopata au kuvitafuta vitabu husika nao waelimike. Vitabu ndiyo masanduku ya fikra.

Tufikiri pamoja.

Leo, ninafungua pazia na uchambuzi wa kitabu cha nguli wa historia nchini na Bara la Afrika: Mohammed Said. Ambaye ni mwandishi wa vitabu vingi vya historia ya umajumui wa Afrika na Tanganyika kabla ya kuitwa Tanzania.

Kitabu maarufu alichoandika ni ‘Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes: Historia iliyofichwa kuhusu harakati za waislam dhidi ya ukoloni wa waingereza katika Tanganyika.’

Mbali ya vitabu vingine chekwa, Mohammed Said ameamua kuwarahisishia wasomaji wake kwa kuandika vitabu vidogo vidogo vyenye kurasa chache, kimoja ni ‘Watu Mashuhuri katika uhuru wa Tanganyika.’

Katika kitabu hicho chenye kurasa 28, mwandishi amewazungumzia kwa kina wanamajumui watatu ambao kwa kiasi kikubwa walishiriki harakati za uhuru wa Tanganyika wakishirikiana na watu wengine wakiwemo ukoo wa Sykes na Mwalimu Julius Nyerere.

Watatu hao ni Tewa Said Tewa, Sheikh Abdallah Rashid Sembe na Zuberi Mtemvu. Hawa ni wazee wenye asili ya Pwani. Makuzi yao ni kati kati ya miji, wawili wakitokea Dar es Salaam au Mzizima na mmoja; Sheikh Sembe akitokea katika kitovu cha Mji wa Tanga, Barabara 14 Ngamiani.

Mwandishi amefanikiwa kugusa maisha ya watatu hawa kwa kina kiasi kwamba unaweza kuhisi kama unazungumza nao kwenye kurasa za kitabu, inatokana na namna alivyofanikiwa kuzungumza nao wakati wa uhai wao na kueleza mchango wao katika harakati za kudai uhuru, kila mmoja kwa umuhimu wake.

Ni nadra sana kuona mwandishi wa kitabu anaelezea tawasufi ya watu aliopata kuzungumza nao, akachota elimu kutoka kwao; huku wengine wakidhihirisha mahaba yao na kufunua hadi siri walizozihifadhi ndani ya vifua vyao kwa miaka mingi.

Mwandishi katika ukurasa wa tatu anaanza kuzungumzia maisha ya Tewa Said Tewa, anamweleza namna alivyomfahamu kwa uzuri, wakati huo mwandishi akiwa mtoto bado. Maisha yake wakati wa harakati za uhuru na baada ya uhuru akiwa Waziri, akiwa balozi nchini China na kiongozi wa chama cha dini ya Kiislamu (East African Muslim Welfare society- EAMWS) ambacho hiki ndiyo asili ya BAKWATA.

Amemweleza Tewa Said Tewa, namna alivyomwingiza Mwalimu Nyerere kwenye siasa, alivyomshika mkono na kumuonyesha vipembe vya Dar es Salaam na kumkutanisha na wazee maarufu waliomuombea dua njema.

Hadi mauko yanamkuta, Mzee Tewa hakujulikana sana. Si tu na jamii ya kitanzania bali hata watoto wake aliowazaa kuna baadhi ya mambo makubwa aliyoyafanya hawakuyajua. Mwandishi ameeleza kwa kina habari hii ya kusikitisha.

Mbali na huyo, mwandishi aligusia maisha ya Sheikh Abdallah Rashid Sembe, amegusia namna Mkoa wa Tanga ulivyokuwa na mwamko wa kimaendeleo. Aligusia biashara za mzee huyu wakati akiuza nazi katika soko la Ngamiani katika miaka ya 1950.

Ushawishi wake na lugha nzuri na faswaha ya Kiswahili, hata Mwalimu Nyerere akawa anamtumia katika mikutano migumu, mikutano inayohitaji ushawishi mkubwa ikiwemo ule wa Tabora kuamua ikiwa TANU iingie kwenye uchaguzi wa Kura Tatu au la.

Vilevile, mzee huyu ndiye aliyeshawishi kuasisiwa kwa TANU mkoani Tanga mwaka 1955, wakati huo mkoa umelala hauna mwamko wa kisiasa. Siasa waliachiwa watu wengine ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa vibaraka wa wakoloni.

Katika siku ya kifo chake Mei 22, 1999 redio iliyorusha taarifa za msiba, ilimtaja Mwalimu Nyerere kama sehemu ya watu wake wa karibu waliotakiwa kupata taarifa hizo. Hii ni kutokana na urafiki mkubwa waliokuwa nao wawili hawa.

Mwanamkakati wa tatu wa uhuru wa Tanganyika, aliyetajwa katika kitabu hiki ni Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu, amemtaja kama mzalendo aliyekuwa na msimamo mkali kwa waafrika.

Mambo makubwa aliyoyafanya akiwa na Mwalimu Nyerere hayawezi kusahaulika, ingawa wengi wamempachika guo la usaliti kutokana na kuanzisha chama cha kupinga harakati za TANU kudai uhuru baada ya kupishana kauli na Mwalimu Nyerere.

Hata hivyo, mwandishi anamtaja Mzee Mtemvu kama mtu mwenye misimamo isiyoyumba. Kilichomgombanisha na wenzie ilikuwa suala la kura tatu mwaka 1958.
Waingereza baada ya kuona waafrika wanataka kushiriki uchaguzi mkuu wa wabunge, na nafasi nyingine za uwakilishi waliamua kuweka sheria ngumu, miongoni mwa sheria hizo ilikuwa ni lazima kupigwe kura tatu yaani moja ya Muasia, Mzungu na Mwafrika.

Ili kuwe na uwiano wa makabila au utaifa kwa wajumbe kwenye baraza la kutunga sheria, kama hiyo haitoshi sheria ilizuia wafanyakazi wa serikali kushiriki uchaguzi lakini pia kwa wagombea walitakiwa kuwa na utajiri wa kiasi fulani cha fedha, ambao kundi kubwa la waafrika hawakua nazo.

Hilo lilikuwa pigo kwa waafrika, Mtemvu akakataa sheria hizo kali na kandamizi kwa kuwa aliamini Tanganyika ni kwa ajili ya Waafrika na si vinginevyo.

Baada ya mvutano, Mtemvu alijitoa katika siku muhimu ambayo mkutano wa Tabora ulipitisha uamuzi wa kushiriki kura tatu. Baada ya hapo akaanzisha chama kipya, African National Congress (ANC). Ambacho kilipachikwa alama ya usaliti, ikawa mtu akiitwa ‘Congress’ maana yake ni msaliti.

Mwandishi anaelezea maisha ya mwishoni mwa Mzee Mtemvu, kama yaliyojaa unyonge na alifafanua namna alivyokuwa akizungumza naye na kumtania wakati akiishi naye jirani jijini Dar es Salaam.

Kurasa hazitoshi, lakini hiki ni kitabu adhimu kwa kila mtanzania anayetaka kuijua historia ya nchi yake. Mwandishi ameamua kukiuza kwa bei ndogo ya Sh 2000, ili walau hata watu wa hali ya chini wanufaike na elimu hii.

Mwisho
 
sasa huyo Sembe wakati wa kifo chake mwaka 1999 redio walitaka Nyerere asikie, wakati huo mbona Nyerere alishakufa?
 
sasa huyo Sembe wakati wa kifo chake mwaka 1999 redio walitaka Nyerere asikie, wakati huo mbona Nyerere alishakufa?

Hapo muandishi amesema mzee Sembe alifikwa na umauti tarehe 22/05/1999 na Kama unakumbukumbu nzuri, je hiko kipindi Mwalimu alikua ameshafariki?

Jibu ni hapana Mwalimu alikua bado yuhai.

NB: Jitahidi kusoma kwa umakini taarifa unayoiona na kuuchangamsha ubongo kwanza kabla haujacomment unachotaka kuComment.
 
Back
Top Bottom