SoC01 Sisi watu wa Kawaida

SoC01 Sisi watu wa Kawaida

Stories of Change - 2021 Competition

From Chugga

New Member
Joined
Aug 22, 2021
Posts
4
Reaction score
9
Kwanza nianze kwa kusema napendezwa sana na vijana wanaothubutu kufanya vitu tofauti na ilivyozoeleka. Mfano kuna dada mmoja huwa namuona mitaa ya Mikocheni kwa Mwalimu anauza miwa, anakuwa na mkokoteni wake wa miwa na kisu.

Natamani siku moja niongee nae nijue alipataje ujasiri wa kutoka kuuza miwa, bila kujali watu wangemuonaje mtoto wa kike anauza miwa. Tena mara zote ni msafi na amechangamka, hii ni alama kuwa anapenda kazi yake.

Kuna kijana mwingine wa kiume ameanzisha biashara ya kuuza uji, akaboresha mazingira ya kuuzia na uji kuutia vikorombwezo, anauza kikombe kwa sh. 4000/-. Anapata wateja wengi na amezidi kujitangaza vizuri kwa kutengeneza fulana na kurasa instagram.

Kwa upande wangu napenda sana kilimo na maisha ya shambani, kama kwenye tamthilia za kihispaniola. Yaani kuwe na nyumba ndogo ya aina yake, kuku, mbuzi, bata mzinga, na farasi. Natamani sana kuwa na farasi.

Ili kutimiza ndoto yangu nilijiunga na kikundi cha kuweka na kukopa, ikawa kila mwezi naweka kiasi cha sh laki moja kutoka kwenye mshahara wangu wa kima cha chakawaida.

Imani yangu ni kuwa mdogomdogo ningeweza kufikia ndoto zangu, na baada ya kuweka kwa miaka miwili nikaweza kuchukua mkopo wa kwanza na kununua eneo la shamba, Bagamoyo. Kwa bahati nikapata eneo zuri karibu na mto.

Fikra yangu ya kwanza ni kuwa ningeweza kufanya kilimo muda wote wa mwaka, akilini nikaanza kuona nyumba yangu ya kimtindo, imezungukwa na mistafeli, mipera na michungwa.

Upande wa nyuma ningekuwa na banda la sungura, kuku na bata mzinga. Ningeweka sehemu za kupumzikia na rafiki siku za likizo na weekend tukichoma nyama. Nyakati za jioni ningekuwa natembea na farasi wangu, hapa ndipo napapenda zaidi, ningemwita farasi wangu Sisi.

Kilichofuata ikawa kumuweka mtu asimamie kilimo, tuanze na mbogamboga za muda mfupi kama vile hoho na bamia. Ukweli sikutaka kumuweka mtu kutoka kule Bagamoyo, nadhani ni kwa vile nilishasikia sana “habari za watu wa Pwani”.

Nikamchukua kijana mmoja, anaitwa Fikiri, ambaye sikuwa na shaka na uaminifu wake, nikidhani ingekuwa nafasi ya kumsaidia na Mama yake pia, ambaye binafsi nampenda kwa roho yake nzuri. Huyu Mama amenisaidia mambo mengi na sikuona namna njema zaidi ya kumuonesha shukrani zangu kwake.

Tukaanza kazi, nikahakikisha anapata kila kitu, chakula, mbegu, madawa na pesa ya kutumia. Ahadi yangu kwake ni kumfungulia duka, mambo yakienda vizuri, na kuongeza mashamba. Nikamuhakikishia sote tutajenga maisha yetu, ila tuhakikishe kilimo kinaenda vema.

Peleka picha miezi miwili mbele, siku moja ghafla Jumamosi mchana, napokea ujumbe mfupi kutoka kwa Fikiri kuwa ameondoka shambani kurudi kwao. Yaani amnitumia ujumbe yupo njiani tayari. Nikapiga simu yake haipatikani.

Nilichanganyikiwa! Shambani kulikuwa na bamia za kupaliliwa na miche ya hoho iliyokuwa ikisubiri kuwekwa shambani. Nilishamtumia pesa kwa ajili ya kusimamia kazi hizi lakini ndio ameondoka na simpati hewani angalao anipe muongozo.

Ikabidi nihangaike kutafuta msaada, nikampata Bwana Hamadi, ambaye awali alijitambulisha kuwa na utaalamu wa kilimo, nikampa jukumu la kuokoa jahazi. Akanipamba kwa maneno ya faraja na matumaini yakanirejea upya ingawa tayari nilishapata hasara ya pesa za mwanzo.

Hamadi akanitajia anavyohitaji, nikampatia pesa za kutosha kila kitu ili asikwazike. Siku nimemtumia pesa, kesho yake ajabu nakutana nae Shekilango nikiwa naenda kumpokea dada yangu ofisi za mabasi pale Shekilango.

Sote tukashtuka kuonana, akanambia alikuja ili aende Gerezani kununua kifaa cha mashine ya kumwagilia. Nikamuitikia ila moyoni nilipata mashaka, nikawaza anyways muda ungenena. Hata hivyo sikuwa na namna nyingine ya kufanya.

Peleka picha mwezi mmoja mbele tena, Jumamosi moja nikamchukua rafiki yangu tuende shambani. Tulitoka mapema, nikiwa na shauku.

Shambani sasa, sikuamini nilichokuta.... bamia zimemea sehemu ndogo na hakuna kazi yoyote inayoendelea tofauti na maelezo ya Hamadi aliyoniambia kwenye simu. Palikuwa tu na vijana wawili wamesimama hapo, wakasema waliambiwa wanisubiri hapo wanioneshe kazi waliyokuwa wakifanya.

Wakasema walikiwa wanapalilia, nawauliza majembe, wanasema wameyaficha sehemu kwa sababu walitaka kwenda kupata chai.

Mara Hamadi anakuja, ananiambia zile hoho tuliotesha kitaluni zimepitiliza muda wake, hazitafaa tena kuwekwa shambani. Inabidi kupanda mbegu zingine upya.

Eeh Mungu! Nilihisi hasira ya ajabu, hasira zaidi ikaja kwa vile siwezi kumfanya chochote Hamadi. Siwezi kumpiga, maana ni mkubwa kwangu, siwezi kumpeleka polisi najua hana cha kunilipa. Nikaishia kumgombeza tu kwa nini anipotezee muda.

Muda huo nikakumbuka maneno ya rafiki zangu Joh na Victor, Joh hakuambulia chochote kwa shamba la nanasi alilowekeza Kiwangwa. Victor, mara kwanza alipata faida nzuri kwenye shamba lake la bamia na nyanya chungu kule Ruvu lakini mara ya pili aliambulia hadithi tu. Sasa ameamua kuuza viatu kupitia mtandao wa Instagram.

Anyways, bado nina hamu ya kuendesha farasi shambani kwangu. Nikaachana na Hamadi na kupata kijana kutoka Korogwe, mnyenyekevu na anaongea kwa upole sana. Nikavutiwa kumfanya mdogo wangu kabisa.

Tukaanza kazi, nikahakikisha anapata kila kitu na mara ningi jioni tunaongea kwa simu kunipa taarifa ya maendeleo name nina mueleza ninayowaza. Nikamnunulia mashine mpya ya kumwagilia, dawa zote, mbegu na miche ya miti ya matunda.

Katika tathmini ya miezi mitatu ya mwanzo, amepoteza mpira wa kumwagilia, nikamnunulia mwingine na miche imekauka nikanunua mingine na mwisho wa msimu hakuna kilichopatikana. Nikamwambia arudi nyumbani, nipate muda wa kujipanga tena.

Hapa sasa nawaza fikra za kijana ambaye kila siku analia kuwa hakuna ajira, anaomba pesa za kununua chakula na vocha. Wakati vijana haohao wanapata nafasi kama hizi na wanazipoteza au uzitumia vibaya.

Ninaamini kuwa mtu anaweza kupata kikubwa kutoka kwenye kidogo, anaweza kufika anapotaka kwenda endapo atapata mtu wa kumnyanyua na kumpa mwendo. Muhimu ni kuweka fikra na uvumilivu kwa anachokifanya,

Ninaamini hivo kwa sababu, Mathayo, muuza matunda pale Boma alianza na mtaji wa machungwa pekee, mwaka jana lakini sasa anauza na ndizi, tikiti, parachichi na papai. Anaweka kwenye vibakuli vya plastiki, gengeni kwake muda wote ana wateja. Wateja wake wengine ni wafanyakazi wa ofisi za karibu na alipo. Juma lililopita amemleta mdogo wake wasaidiane kwa sababu wateja wamekuwa wengi.

Kwa nini vijana niliowaweka shambani hawakuona fursa ile na moyo niliokuwa nao kusaidiana nao? Sasa mmoja kila mara anapiga simu kuomba sh. 2000! Siku zingine sipokei simu yake. Natamani kumsaidia lakini siafiki suala la mtu kukaa tu na kuomba pesa, hata kama ni ndogo.

Nashukuru Mungu sikuwahi kuwa na tabia ya kuomba, ingawa nimelelewa kwenye umasikini. Ninajituma kujikimu na kuwasiaidia wanaonitegemea hasa wazazi wangu, siwezi kujibebesha mzigo mwingine wa mtu timamu na afya yake, kisa tu kashindwa kuwa mvumilivu kwenye kazi.

Kuna wimbo wa John Legend una kipande kinasema "we ordinary people, we don't know which way to go", yaani sisi watu wa kawaida hatujui njia ya kupita. Ndio utakuta vijana wengi walomaliza waliomaliza vyuo vikuu hawafikirii kuanza kwa biashara za mitaji midogo na baadae kukua kuwa wanavyotamani, wao wanalalamika tu hakuna ajira.

Mara nyingi watu wanaachia fursa zinapita kwa sababu tu akilini mwao wamejiwekea fikra fulani, ofisi kubwa yenye kiyoyozi, gari la kutembelea na safari za Saadani likizo. Bahati mbaya mtu hajui labda ile biashara ya kuuza maziwa ndio mwanzo wa kupata kampuni yake hapo baadae.

Ninachoamini ni kama kucheza karata, unapaswa kutumia ulizozipata kushinda, na huwezi kusema upekue kwenye fungu la karata ujipe zitakazookuwezesha kushinnda.

Mimi si mtu wa kukata tamaa, bado nakusanya picha za kunisaidia kudizaini nyumba yangu ya shamba, tena itakuwa na dirisha kubwa kwa upande ulipo mto na mandhari ya msitu, samani chache za mbao za majahazi, jioni mwanga hafifu sebuleni na banda la farasi upande wa kulia.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom