jmushi1
Platinum Member
- Nov 2, 2007
- 26,329
- 25,263
Tambwe atishia CHADEMA
na Kulwa Karedia
na Kulwa Karedia
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa siri ya kuwapo mpango wa kukamatwa viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa kuhusishwa na kifo cha aliyekuwa mbunge wa Chadema, marehemu Chacha Wangwe.
Siri hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Propaganda, Tambwe Hiza, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Itirya.
Tambwe alisema viongozi hao wa juu, watakamatwa baada ya miezi mitatu, kwa madai ya kuhusika na kifo cha Wangwe.
Tambwe alitumia mkutano huo kuzungumzia kifo cha Wangwe na kukihusisha moja kwa moja na viongozi wa Chadema.
Kutokana na hali hiyo, Tambwe amewataka wananchi wa Tarime kuacha kumpigia kura mgombea wa Chadema, Charles Mwera, kwa madai kuwa chama hicho hakina dola na viongozi wake watasambaratika.
Katika hatua nyingine, CHADEMAimemwaga zaidi ya baiskeli 20 zenye thamani ya sh milioni 2.6 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Tarime, ikiwa ni sehemu ya kurahisisha usafiri kwa mawakala wake, ili waweze kuwafikia wanachama kirahisi katika kampeni zinazoendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi baiskeli hizo, makao makuu ya chama hicho mjini hapa jana, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi, Msafiri Mtemelwa, alisema hiyo ni moja ya hatua ya kukabiliana na mbinu chafu zinazofanywa na wapinzani ambao wamekuwa wakipita na kutangaza kwamba chama hicho hakina uwezo.
Tumeamua kuwawezesha viongozi wetu wa kata ambao tunaamini kwamba wao ndio wako karibu zaidi na wapiga kura wetu... hivyo tumeona vyema kuwapatia baiskeli hizo ili ziwawezeshe kuzunguka maeneo mbalimbali wakati huu wa kampeni, alisema Mtemelwa.
Alisema hiyo ni moja ya hatua ya kuwajengea uwezo ambao utawawezesha kuwafikia kirahisi watu walioko maeneo ya vijijini, ambako usafiri wa magari umekuwa mgumu, kutokana na hali halisi ya kijografia iliyopo wilayani hapa.
Huu ni mwanzo, tumejipanga vya kutosha kukabiliana na mbinu chafu zilizoandaliwa na baadhi ya wapinzani wetu ambao wanaonekana sasa wanaweweseka kwa kuandaa mbinu za kutaka kutuvurugia mwenendo wetu wa kampeni...naamini lengo letu litatimia tu, alisema Mtemelwa.
Alisema mbali ya baiskeli hizo kutolewa sasa, pia zitatumika katika uchaguzi wa serikali za vitongoji mwaka ujao, hatua ambayo alisema itakuwa imewajengea uwezo wa kusambaza ujumbe maeneo mbalimbali kwa wanachama wao.
Naye Katibu wa chama hicho, Wilaya ya Tarime, Joseph Anthony, aliwapongeza viongozi wa chama hicho kutoka makao makuu kwa hatua ya kutoa baiskeli hizo ambazo alisema zitatumika kama zilivyokusudiwa kwa nia ya kurejesha jimbo ambalo lilikuwa likishikiliwa na marehemu Chacha Zakayo Wangwe.
Alisema baiskeli hizo zitatumika zaidi maeneo ya vijijini ambako ndiko kuliko na wapiga kura wengi, ambao wamekuwa hawafikiwi kwa usafiri wa magari na badala yake husababisha chama kukosa kura kutoka kwa wanachama wake.
Kuhusu kampeni zinazoendelea hivi sasa, Mtemelwa alisema zinaendelea vizuri licha ya vikwazo mbalimbali ambavyo wamekutana navyo, hasa kutoka kwa Jeshi la Polisi ambalo limekuwa likishindwa kuwachukulia hatua baadhi ya watu ambao huripotiwa kwao.
Alisema mara baada ya kufanya mazungumzo ya kina na viongozi wa jeshi hilo jana, wanaamini kwamba hali itabadilika na kuona haki inatendeka kwa kila chama ili kufikia malengo yaliyokusudiwa hadi siku ya uchaguzi Oktoba 12, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Chama cha TADEA, na UPDP, kimelaani vurugu zinazoendelea katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime na kwamba endapo hali ikiendelea hivyo, kuna hatari ya uchaguzi huo kutofanyika au kuwa uwanja wa mapambano.
Wakizungumza katika mkutano wa pamoja kwa nyakati tofauti uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl, jijini Dar es Salaam jana, Rais wa Tadea, Lifa Chipaka, alisema kuwa vurugu hizo zinachochewa na wanasiasa wenyewe wawapo kwenye mikutano ya kampeni.
Alisema kuwa kila chama kimekuwa na kauli za uchochezi, lakini alilaani kitendo cha Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Mtikila kupigwa, huku baadhi ya viongozi wa CHADEMA, wakiipongeza hatua hiyo.
Mimi nimeshangazwa sana na kauli ya Zitto Kabwe, kusema kipigo cha Mtikila ni sawa, kwani amezidi kuropoka, hii si sahihi, hatutarajii vyama vya upinzani vishabikie mmoja wao kupigwa, alisema Chipaka. Naye Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa, alisema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Tarime kuwa kama Zanzibar ilivyochafuka mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, ambapo zaidi ya watu 30 waliuawa na wengine kukimbilia Kenya kutokana na machafuko ya kisiasa. Sisi hatutaki taifa lipoteze amani, lakini ndiyo maana tunakemea hali hiyo.
Yanayotokea Tarime yasipodhibitiwa, yatatokea tena sehemu nyingine. Sasa hii ni hatari, alisema Dovutwa.