Soko la Keko Mwanga lilipo Temeke Jijini Dar es Salaam lina umri wa takribani Miaka 48, tangu lijengwe Mwaka 1976 Wafanyabiashara katika soko hilo wanasema halijawahi kukarabatiwa hata mara moja.
Madai haya yanaweza kuthibitisha kwa namna muonekano wa soko ulivyo:
Kwa mbali kabla ya kufikia soko hili utakaribishwa na moshi unaotoka humo ambao ni wa Mama Lishe, wakaanga samaki na dagaa wanaokaangwa kwa kutumia nishati ya Mkaa na Kuni.
Ukisogea karibu kabisa utapokelewa na mabati yaliyochoka haswa, miundombinu mibovu na uchafu ikiwemo tope linalotokana na kumwagwa kwa maji, kwani miundombinu ya kutoa maji nje hakuna.
Kwanini halifanyiwi ukarabati?
Wafanyabiashara na Mwenyekiti wa soko wanadai kuwa hakuna kiongozi wa eneo hili ambaye hajui changamoto ya uchakavu katika soko hilo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Diwani wamekuwa wakiwaahidi kila wakati wa uchaguzi kuwajengea soko lakini ni ahadi ambazo hazijawahi kukamilishwa na hata kufika eneo hilo hawafiki katika soko hilo.
Hali hii hufanya Wananchi wao kuchanga mara kwa mara ili kukarabati baadhi ya sehemu ambazo ni korofi zaidi lakini kawaida hazidumu.
Athari
Wananchi wa maeneo ya jirani baadhi wanasema hawanunui bidhaa katika soko hilo, hivyo hutumia masoko ya nje na eneo la Keko Mwanga kufanya manunuzi.
Wafanyabishara wamekuwa wakilalamika kusumbuliwa na vifua kutokana na moshi wa soko hilo ambao hakuna miundombinu ya kutoa moshi nje.
Uchafu ni mwingi, vyakula vinavyouzwa vingi havipo katika mazingira ya usafi.
Unaweza kusema wewe haupo kwenye mduara huo kwa kuwa hauishi huko lakini tambua inawezekana mtu akanunua kutoka katika soko hilo akaingia mtaani ukanunua au akapeleka katika soko lingine, wewe unayedai huusiki na soko ukawa mteja.
Nini Kifanyike?
Wananchi wanaomba kufanyiwa maboresho ya soko ambalo ni chakavu kwani kwa sasa wateja wanakimbia hapo na wakati wa mvua ndio kabisa kupata wateja ni ndoto.
Wanaomba madai yao yafikishwe kwa viongozi wa juu zaidi ili waweze kutatua kero hii ya muda mrefu.