Soko la Kisasa, Lakini Hali Ni Tofauti
Soko hili limejengwa kwa gharama kubwa na linajivunia muundo wa kisasa na mazingira mazuri.
Hata hivyo, nilipofika ndani, nilishangazwa na upungufu mkubwa wa Wafanyabiashara. Meza zilizopo takriban hamsini (50), lakini ni nane tu zinazotumiwa na Wafanyabiashara, huku nyingine zikibaki tupu.
Wanasema mara nyingi wanamaliza siku nzima bila kuuza kitu chochote. Sababu kuu? Soko hilo lipo ndani mno, na ni vigumu watu kugundua uwepo wake.
Aidha, wateja wengi wanaamua kununua bidhaa kwenye njiapanda ya Mwinyi, eneo ambalo lina mkusanyiko mkubwa wa watu.
Swali la Utafiti Kabla ya Ujenzi
Hali hii inazua maswali kuhusu uamuzi wa Serikali kujenga soko hilo. Je, kulikuwa na utafiti wa kutosha kabla ya mradi huu wa gharama kufanyika? Inaonekana kama soko hili lilijengwa pasipo kuzingatia mahitaji halisi ya eneo hilo au muingiliano wa kijamii unaohitajika kwa biashara.
Hali Mbaya ya Vyoo
Mbali na changamoto ya ukosefu wa wateja, hali ya vyoo vya soko ni ya kusikitisha. Vyoo hivyo, ambavyo vinalipiwa shilingi 300 kwa kila matumizi, ni vichafu sana.
Cha kushangaza, vyoo hivi hutumiwa zaidi na wapita njia na wakazi wa eneo hilo, hususan watoto kutoka mitaa ya jirani. Pesa zinazokusanywa kwa matumizi ya vyoo zinaweza kutosha kuboresha usafi, lakini hali inaonyesha vinginevyo.
Pendekezo Langu
Kama soko hili limejengwa lakini halitumiki ipasavyo kwa biashara, angalau jitihada zifanyike kuboresha usafi wa vyoo na huduma nyingine muhimu.
Soko la Makangarawe ni mfano hai wa miradi ya maendeleo ambayo haikupangwa kwa ufanisi.
Natoa wito kwa mamlaka husika kufanya tathmini ya kina juu ya ufanisi wa soko hili na kuchukua hatua stahiki kwa faida ya wananchi na wafanyabiashara.