Mama mbaroni kwa kutaka kumuuza mwanawe albino
Bei yake ilikuwa milioni 15/-
na Julieth Mkireri, Pwani
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata Mwajabu Said (66) na mama na mtoto wake, Said Omary (40), kwa tuhuma za kula njama za kutaka kumuuza binti wa mama huyo aliyetajwa kwa jina la Kabuyu Dalili (22), mwenye ulemavu wa ngozi (albino ) kwa sh milioni 15.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Absalom Mwakyoma, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa, mama na mtoto wake wanadaiwa kula njama za kuandaa mpango huo na mtu ambaye aliahidi kuwalipa kiasi hicho cha fedha.
Alisema, uchunguzi wa polisi umebaini kuwa biashara hiyo ilipangwa kufanyika Desemba 26, siku moja baada ya Sikukuu ya Krismasi.
Kamanda huyo alisema binti huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kwamba anakusudia kuuzwa kwa kitita hicho cha fedha alikimbilia katika kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wake.
Kwamba baada ya polisi kupewa taarifa hizo, walimtaka binti huyo kubaki kituoni hapo na wao walikwenda kijijini Fukayosi alikokuwa akiishi na kuwakamata watuhumiwa.
Alisema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ili kuwatia mbaroni wahusika waliotaka kumnunua albino huyo.
Je kwa hali hii tutafiaka??