SoC04 Somo la kilimo lipewe kipaumbele katika ngazi zote za elimu

SoC04 Somo la kilimo lipewe kipaumbele katika ngazi zote za elimu

Tanzania Tuitakayo competition threads

Kandongu

New Member
Joined
Mar 5, 2018
Posts
4
Reaction score
4
Somo la kilimo (Agricultural sciences) ni miongoni mwa masomo yanafofundishwa katika elimu ya sekondari pekee kama somo ambalo mwanafunzi anachagua kusoma. Kutokana na umuhimu wa somo hili na tija kubwa itokanayo na sekta hii adhimu serikali haina budi kulifanya somo hili kuwa la lazima katika ngazi zote za elimu ili kuweza kuleta mapinduzi makubwa katika nchi yetu.Mada nyingi zilizopo katika somo la Kilimo zinawezesha kabisa wanafunzi kuweza kujiajiri na kuleta tija kubwa sana katika taifa letu la Tanzania.Vilevile serikali haina budi Ili kufikia adhima hiyo serikali na wadau kufanya mambo yafuatayo:

1. Kuongeza idadi ya shule zinazofundisha somo la kilimo ( Agricultural sciences). Serikali ihakikishe shule zote hususan za vijijini ziwe zina walimu wa somo la kilimo na shule mpya zote zinazoanzishwa ziwe na walimu wa somo hili. Mfano Mkoa wa Ruvuma ni mkoa unaoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula lakini haina hata shule 10 zinazofundisha somo la kilimo.

2. Somo la kilimo lipewe uzito sawa na masomo mengine hasa katika mitihani ya taifa. Somo la kilimo limekuwa halitendewi haki hasa katika mitihani ya taifa. Mfano mwaka 2009 katika Shule ya sekondari Maguu wanafunzi waliofanya mtihani wa upimaji kidato cha pili alama za somo la kilimo hazikujumlishwa kati ya masomo tisa yaliyokuwa yakifundishwa, wanafunzi walipewa adhabu kutokana na kutosoma somo la Fizikia.( Rejea necta ftsee 2009 Maguu secondary school). Hali hii ilipelekea wanafunzi wengi kukata tamaa ya kusoma somo hili na kufanya vibaya katika mitihani ya taifa 2011

3. Kuongeza idadi ya tahasusi katika somo la kilimo. Kuna tahasusi moja tu ya somo la kilimo ambayo ni CBA. Hivyo serikali haina budi kuongeza idadi ya tahasusi katika somo la kilimo ili kupanua wigo wa wanafunzi wengi kusoma somo hili. Mfano serikali inaweza kuongeza michepuo ya AGM( Agriculture, Geography na Mathematics),GAB( Geography, Agriculture na Biology EMA( Economics, Mathematics na Agriculture) na NBA (Nutrition, Biology na Agriculture)

4. Kuimarisha maabara na karakana za somo la Kilimo.Serikali ihakikishe shule zote hususan zinazofundisha somo la kilimo ziwe na maabara na karakana wezeshi za kujifunzia na kufundishia. Serikali imeweka mkakati na msisitizo mkubwa sana katika ujenzi wa maabara za masomo ya Fizikia,Kemia na Baiolojia pekee,imeshindwa kabisa kuweka mkazo kwenye ujenzi wa maabara na karakana za somo la Kilimo. Shule nyingi zinazofundisha somo la kilimo hazina maabara na karakana zinazoweza kuwasaidia wanafunzi waweze kusoma kwa vitendo.Walimu wa somo la Kilimo wamekuwa wakitumia madarasa kama maabara. Vilevile shule zenye maabara hazina vifaa vile muhimu kwa ajili ya kufundishia somo la kilimo. Hivyo hata kufanya maswali mengi ya mitihani mingi ya Somo la kilimo (Agricultural sciences 2) kujirudiarudia kila mwaka.

4. Kuongeza idadi ya vyuo vikuu vya kilimo. Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo wanapaswa kuongeza ujenzi na uanzishwaji wa vyuo vingi zaidi vitakavyofundisha masuala ya kilimo. Tanzania ni nchi kubwa sana na miongoni mwa nchi ambayo ina uzalishaji mkubwa sana wa mazao ya kilimo,uvuvi na ufugaji lakini inategemea zaidi Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine kwa ajili ya kufanya utafiti na kupata wataalamu wabobezi wa masuala ya kilimo. Licha ya kuwa na idadi kubwa ya vyuo vya kati vya kilimo na mifugo serikali haina budi kuongeza idadi ya vyuo vikuu vya kilimo na mifugo hususan katika maeneo yanayoongoza katika uzalishaji kama vile mikoa ya Ruvuma,Mbeya,Songwe, Rukwa, Katavi,Kagera,Mwanza na Kigoma.

5. Uanzishwaji wa mashamba darasa katika Shule na Vyuo. Serikali iweke mkakati wa kuanzisha mashamba ya mfano katika Shule na Vyuo ili kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia pindi wanapohitimu masomo yao. Shule nyingi kongwe na zile za vijijini zina maeneo makubwa sana ambayo hayatumiki au hutumika kuwafaidisha watu wachache. Maeneo haya yangeweza kutumika kuanzisha mashamba au bustani za kilimo cha mfano kwa wanafunzi au ujenzi wa mabanda ya ufugaji wa mfano kwa wanafunzi. Hii ingeweza kuwaandaa wanafunzi kujikomboa kiuchumi wakati wakiwa shuleni na vyuoni na mara baada ya kuhitimu masomo yao.

6. Kuongeza idadi ya walimu na wakufunzi katika somo la Kilimo. Serikali iajiri walimu na wakufunzi wa somo la Kilimo kama ilivyo kwa masomo mengine ya sayansi. Idadi ya walimu na wakufunzi wa somo la Kilimo nchini ni ndogo sana.Na wengi wa walimu waliopo wanafundisha kwa mikataba.Hali hii hupelekea baadhi ya shule kusoma somo hili kwa vipindi.Mfano Maguu sekondari ilikuwa na Mwalimu Romanus Milinga aliyekuwa anafundisha kwa mkataba toka 2007-2012 baada ya kuondoka Mwalimu hakuwepo mpaka alipokuja kuajiriwa mwalimu mpya mwaka 2016 lakini mwaka 2022 mwalimu huyo amehama na kuacha wanafunzi wakihaha.Hivyo hali hii haina afya kwa somo Hilo.

Endapo serikali itaweka msisitizo mkubwa sana ufundishaji na ujifinzaji wa Somo la Kilimo nchi ya Tanzania itazalisha wataalamu wengi sana wa masuala ya kilimo na kuacha kabisa kutegemea programu ya BBT (Building Better Tomorrow) ambayo imekuwa ni kama tu suluhisho la vijana waliokosa ajira. Lakini suluhisho ni kuweka mkazo kwenye somo la Kilimo na si vinginevyo.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom