Stan Laurel na Oliver Hardy

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
STAN LAUREL NA OLIVER HARDY

Hii nimeikuta kwenye group moja.

Imenirudisha nyuma zaidi ya miaka 60 utotoni.

Tukiwaita hawa wachekeshaji Chale Mnene na Chale Mwembamba.

Chale Mnene Oliver Hardy tulimpa jina Chale Ndute.

Hawa walikuwa wachekeshaji wakubwa sana Marekani na ulimwenguni.

Tukiangalia senema hizi Mnazi Mmoja zikionyeshwa bure.

Kwetu ilikuwa furaha kubwa sana.

Tulikuwa watoto tukikusanyika hapo karibu ya maghrib jua linakaribia kuzama.

Watu wenye biashara zao wao wanakuwa weshafika mapema na kutandaza chini walichokuja kuuza ziwe karanga, korosho, machungwa, embe za pilipili nk. vile vitu ambavyo watoto wanapenda.

Kiza kikiingia wanawasha vibatari vyao na utaviona vimezunguka uwanja nzima vimetuzingira watazamaji senema.

Senema inaanza na kulikuwa na utulivu mkubwa wala hatuchokozani kwani tuliipa hadhira hii heshima ya juu kabisa.

Kwetu senema ilikuwa burudani kubwa ya aina yake isiyo na kifani.

Naukumbuka sana Mtaa wa Lumumba siku hizo ni barabara moja tu inapita katikati ya nyumba za wenyeji zinazoangaliana.

Baada ya Uwanja wa Mnazi Mmoja ni Titi Street barabara ya vumbi na nyuma yake ni Soko la Kisutu watu wakillita Soko Mjinga.

Kuangaliana na soko hili ulikuwa Msikiti wa Badawy.

Chale Ndute na mwenzake wamenirudisha utotoni katika Dar es Salaam ile ya miaka ya 1960.

Wakati naandika makala haya nimepigiwa simu rafiki yangu wa utotoni Abdallah Mkwanda maarufu kwa jina lake la Ingemar Johansson amefariki.

Ingemar Johansson alikuwa bingwa wa ngumi kutoka Sweden.

Nimecheza mpira katika uwanja huu na Mkwanda na alikuwa inside left mzuri na mguu wake wa kushoto hodari wa kupiga mashuti nje ya box na kufunga magoli.

Wengi wenzangu nawakumbuka wametangulia mbele ya haki kama Jumanne Masimenti, Rashid Vava, Garincha, Guy (Ghalib) mfupi hana kimo mabeki wakimuogopa kumfuata kwani alikuwa na kipaji cha juu cha "dribbling."

Kumfuata Guy akiwa na mpira ni kujitafutia kuadhirika makusudi.

Binafsi nikimuusudu Guy na hakika sikupata kumfikia uchezaji wake.

Kaka yake Guy, marehemu Hamidu Hamza alikuwa right wing hodari wa Cosmopolitan.

Hii ilikuwa mwaka 1966 timu yetu ilikuwa Everton baadae ikawa Saigon na jezi zetu zilikuwa bluu na bukta nyeusi.

Nakumbuka tukiwa tumekaa pembeni ya uwanja tunavaa kabla ya mazoezi tukipenda kuimba nyimbo za Kizungu.

Katika hili nilikuwa naingoza.

Mkwanda hakupenda nimshinde lakini bahati mbaya yeye alikuwa anajua nyimbo moja tu ya Jim Reeves, "I Wont Forget You."

Takriban mika 20 hivi Mkwanda afya yake haikuwa nzuri lakini hakuacha kuja Msikiti wa Mtoro kusali na kila nikienda pale tulikuwa tunaonana.

Tukionana pia kila nilipohudhuria Khitma ya Saigon inayosomwa kila mwaka.

Ingemar Johansson hakuacha kuhudhuria kila khitma ya Saigon inayomwa kila mwaka kuwarehemu wenzetu waliotangulia mbele ya haki na mimi nikitokea Tanga nilipokuwa nafanyakazi ikawa fursa yetu ya kuonana.

Ingawa alikuwa hawezi kuzungumza lakini macho yetu yakikutana nilikuwa najua kuwa rafiki yangu alikuwa ananitambua ila ulimi wake ulikuwa umefungika.

Allah amrehemu rafiki yangu Abdallah Mkwanda na wote waliotangulia.
Amin.

https://www.facebook.com/
 
Nro Leo tanzia hii umeiingiza kiufundi zaidi, RIP Mkwanda Allah akufanyie wepesi huko uendako.
 
Sahihisho: asante kwa habari za Kisutu si sawa kukubishia sisi hatukuwa huko. Kwetu walikuwa wanaitwa George mnene na George mwembamba kwenye senema za Orofea.
 
Sahihisho: asante kwa habari za Kisutu si sawa kukubishia sisi hatukuwa huko. Kwetu walikuwa wanaitwa George mnene na George mwembamba kwenye senema za Orofea.
LGF,
Umeniongezea taarifa sikuwa najua kuwa sehemu nyingine Stan Laurel na Oliver Hardy walipewa majina ya George.

Ahsante sana.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…