Tumemwaga maji machafu pamwe na mtoto?
Jenerali Ulimwengu Februari 20, 2008
NIMESEMA awali kwamba, pamoja na sifa zote nilizozitaja (na nyingine nyingi) Mwalimu Julius Nyerere hakuwa mwana-demokrasia. Nasema hivyo nikijua kwamba hili linaweza kuhitaji maelezo, nami sina tatizo na hilo.
Kwanza kabisa ni muhimu nieleze ni kwa nini ninahusisha moja kwa moja sudi ya nchi na mtu mmoja, kiongozi mmoja wakati tunajua kwamba nchi hujengwa na watu wengi, mamilioni, na mustakabala wake huundwa na kila aina ya mikondo ya nishati zinazokutana katika mchakato ambao mara nyingi haufuati msitari ulionyooka.
Nimekwisha kuzungumzia kile nilichokiita zama za Bwana Mkubwa na chama-tawala tulizokuwa nazo baada ya Uhuru, na hizi zama zilizikumba nchi zote za Afrika, bila kutofautisha. Leo hii tunaweza kusema kwamba hali imebadilika sana, hasa kutokana na kufunguliwa milango ya siasa inayoruhusu, angalau kidogo, raia kujiunga katika vyama vya siasa wanavyovipenda au kuanzisha asasi za kijamii zinazokidhi matarajio yao.
Lakini, hata hivi leo, nafasi ya kiongozi mkuu bado ni kubwa mno barani Afrika kwa sababu asasi zetu za utawala na uongozi bado ni changa, mifumo yetu ndiyo kwanza tunaijenga na itachukua muda kidogo kabla hatujawekeza matumaini yetu kwenye mifumo, asasi na taratibu zaidi kuliko kutegemea fikra na busara za kiongozi mkuu.
Huko tulikotoka hali ilikuwa ni ngumu zaidi. Hata pale tulipomchagua kiongozi wetu (mara nyingi kwa sababu yeye alikuwa miongoni mwa wachache waliodiriki kutuambia kwamba tunaweza kuungoa ukoloni) bado mtu huyo mmoja alikuwa na nguvu na ushawishi kuliko asasi alizoziongoza. Mara nyingi rais wa nchi ya Kiafrika alikuwa na nguvu na ushawishi mkubwa zaidi kuliko katiba ya nchi, sembuse taratibu nyingine zilizowekwa kwa misingi tuliyofundishwa na wakoloni wakati wakiondoka.
Kwa jinsi hii, viongozi wakuu wa Afrika ambao tunawakumbuka kwa ushujaa wao na uwezo wao wa kuona mbali (Nkrumah, Toure, Nasser, Nyerere, Kaunda) wote hawakuwa wana-demokrasia, kimsingi kwa sababu nyakati hazikuwapa fursa ya kuwa wana-demokrasia.
Kilichohitajika wakati ule kilikuwa ni maendeleo ya haraka ambayo yangetuondoa katika hali mbaya ya umasikini, maradhi na ujinga; hatukuhitaji mabishano na ukinzani wa kisiasa ambao ungetukawiza katika jitihada za kupata maendeleo.
Huo ndio ulikuwa mtazamo wa zama hizo, na mtazamo huo ndio uliozaa urais-ufalme, au kile kinachoitwa imperial presidency.
Tukiangalia kidogo tu, hata leo, tutagundua dalili nyingi zinazoonyesha ufalme huu ndani ya urais, pamoja na kwamba tunatamba kwamba tumeimarisha demokrasia, tumejenga asasi, na nchi zetu ni huru zaidi kuliko zilivyokuwa miongo minne iliyopita.
Tunaweza kusema leo kwamba ilikuwa haiepukiki kuwa na kiongozi wa aina ya Julius Nyerere, ambaye yeye mwenyewe aliwahi kusema kwamba kwa katiba ya nchi angeweza kabisa kuwa dikteta (wapo wanaosema kwamba hivyo ndivyo alivyokuwa). Kwa vyo vyote vile Nyerere alikuwa ndiyo Tanzania, na Tanzania ilikuwa ni Nyerere, si tu wakati akiwa madarakani bali hadi alipoaga dunia
. na labda hadi leo hii.
Katika mazingira kama haya, hata sera nzuri kama zile zilizotangazwa katika Azimio la Arusha na baada yake, pamoja na programu kadhaa za utekelezaji wa sera hizo zilitangazwa na kutekelezwa katika mazingira ambamo fikra za mtu mmoja zilikuwa na uzito mkubwa kuliko ambavyo ingekuwa katika mfumo wa kidemokrasi. Yeye ndiye aliyefikiri; yeye ndiye aliyetunga sera; yeye ndiye aliyeamua vipi zitekelezwe; yeye ndiye aliyeamua nani azitekeleze.
Hii ilikuwa na maana kwamba iwapo jambo alilitia maanani jambo hilo lilishughulikiwa kwa ari kubwa na kila aliyekuwa chini yake; iwapo jambo hakulitia maanani, hata lingekuwa ni la muhimu sana, jambo hilo halikupewa uzito; iwapo alimwamini mtendaji, mtendaji huyo alishamiri; iwapo hakumwamini, mtendaji huyo hakushamiri.
Kama alivyosema Nyerere mwenyewe, madaraka makubwa mno yaliwekwa mikononi mwa Rais, hali ambayo bado tunayo hivi leo, ikiwa ni pamoja na uteuzi wa watendaji hadi ngazi ya wilaya. Baraza la mawaziri likawa (na hadi leo) ni baraza la ushauri kwa Rais. Hakuna kinachofanyika bila yeye.
Azimio la Arusha lenyewe lilikuwa kwa kiwango kikubwa ni azimio la Nyerere, ingawaje lilipitishwa na Halmashauri Kuu ya TANU, na kwa kuungwa mkono na maelfu ya Watanzania, likawa azimio la Watanzania wote. Ukweli ni kwamba hakukuwa na mjadala uliowahusisha wananchi (au hata wana-TANU) katika utungaji wa azimio lenyewe wala katika mbinu za utekelezaji wake.
Mwaka 1968, tutakumbuka, walichomoza wabunge kadhaa waliotaka kufurukuta na kuihoji TANU ndani ya Bunge la chama kimoja. Alichofanya Nyerere ni kuwashitaki wabunge hao (Kaneno, Bakampenja, Choga, Masha, Anangisye, Mwakitwange) ndani ya vikao vya chama. Wakanyanganywa uwanachama wa TANU, na hivyo wakapoteza ubunge.
Huo ukawa ndio mwisho wa kutaka kuhoji cho chote ndani au nje ya TANU. Wengi wa wabunge hao machachari wa wakati huo wamekwisha kufariki (lakini walikuwa wamekwisha kufa kisiasa muda mrefu kabla ya kuaga dunia), ukimwacha Masha, ambaye sasa ni mbunge wa Afrika Mashariki baada ya miaka mingi ya kuishi uhamishoni-laini katika Umoja wa Mataifa.
Hakika ilianza kusadikika kwamba ukipata laana ya Kambarage ujue umemalizika kisiasa, imani ambayo imezidi kujengeka katika miaka ya karibuni.
Utamaduni ulioanzishwa wakati wa Nyerere umeendelea ndani ya chama-tawala kiasi kwamba majadiliano ni nadra sana, na mara nyingi mijadala huzuka ili kumshughulikia mtu fulani, na wala si kusaili hoja wala falsafa. Athari mojawapo ya utamaduni huo ni kwamba hivi sasa, Nyerere akiwa hayupo, hakuna kiongozi hata mmoja, hata wale waliokuwa safu ya mbele kabisa katika kuhubiri Ujamaa leo hii huwezi kuwatambua.
Hali hii ilianza kujitokeza hata wakati Mwalimu akiwa madarakani. Kadri umri ulivyoongezeka na nguvu za mwili kupungua ndivyo kasi ya kusimamia sera na utekelezaji wake ilivyoendelea kupungua, kiasi kwamba chama na sera zake vilianza kuonyesha uzee kadri nywele za Mwalimu zilizvyozidi kuwa nyeupe.
Katika hali ya kutokuwapo na mjadala, sera zilizolenga kumkomboa Mtanzania zikaishia kumletea matatizo ambayo yaliupa Ujamaa jina baya. Serikali ikajiingiza katika biashara isiyokuwa yake kuuza nyama na chumvi; vyama vya ushirika vikavunjwa; serikali za mitaa zikafutwa, na kadhalika.
Leo hii ni vigumu kujua CCM imesimama wapi. Ni dhahiri kwamba sera za Ujamaa zimetupwa, hata vipengele ambavyo vingeweza kuwa na manufaa leo. Katika mkanganyiko uliotokana na utekelezaji mbovu wa sera za awali, viongozi wa CCM wameamua kumwaga maji machafu pamoja na mtoto, lakini kimya kimya.
Hawathubutu kusema kwa sauti kubwa kwamba falsafa yao ni Ujamaa, na wala hawathubutu kusema wazi kwamba wameachana na siasa hiyo. Chama hakina dira wala mwelekeo, na kila kukicha kinafanya kile kinachoonekana kufaa kwa siku hiyo.
Athari nyingine ya hali hiyo ni kwamba ukosefu wa falsafa-ongozi umekivua chama-tawala ile taswira ya kuwa mtetezi wa wanyonge. Uongozi na utetezi wa wanyonge unahitaji falsafa inayowaongoza viongozi wenyewe kwanza, falsafa inayopingana na ugandamizaji wa kila aina, unyonyaji wa kiuchumi unaomdhulumu mtu wa chini (ndani ya nchi) na udhalimu unaofanywa na mataifa makubwa na mitaji yao(nje ya nchi). Utetezi wa wanyonge hauna budi kuandamana na msimamo dhidi ya ubeberu na ukoloni-mamboleo.
Hii ina maana ya kutegemea nguvu ya wananchi walio wengi wanaojiunga na chama, na michango yao, hata kama ni kidogo. Badala yake, tunachokishuhudia ni chama-tawala kugeuka chama cha matajiri wachache ambao ndio wanakibeba kifedha, na vivyo hivyo serikali ya chama hicho kuwa tegemezi kwa misaada ya mataifa ya nje kwa ajili ya maendeleo ya nchi.