SoC01 Subira

SoC01 Subira

Stories of Change - 2021 Competition

Kitumba_

Member
Joined
Aug 21, 2018
Posts
30
Reaction score
21
Sifa njema zote za mstahiki Mwenyezi Mungu Sub'hana wa Ta'ala, Rehma na Amani zimshukie kiongozi wa Ummah, Mtume wetu Muhammad Swallallahu alaiyhi wasallam.

Kwenye mafundisho (ya dini) tunaambiwa, kwa kila mwenye kutia nguvu na kujiwekeza katika kuwafanyia mema wamzungukae na atarajie malipo kutoka kwa Mungu. Ukishughulika na kila lenye kuunganisha watu kuwa kitu kimoja, mapenzi kama vile kutoa salamu, kupeana mikono wakati wa kukutana na mengineyo wataipata radhi yake. Ni vyema vijana tukajishughulisha na haya.

Tuweke pembeni kila lenye kudhoofisha mapenzi haya kama vile kudhaniana vibaya, kusengenya, kufitini na mengineyo. Dhana mbaya ni njia nyepesi ya kueneza uadui, chuki, kutengana na familia na kuvunja undugu baina. Vilevile tusilale, tushughulike na kujitafutia riziki huku tukiusiana katika upendo.

Fahamu ya kwamba, miongoni mwa mambo makubwa yenye kuokoa ni kusubiri, SUBIRA!...kwa mitihani tunayotahiniwa na Mwenyezi Mungu.

SUBIRA yako hii iende sambamba na neema, fursa alizokuneemesha Mwenyezi na kuipa mgongo dunia yenye kujali kupata tu. Elewa ya kuwa subira ni miongoni mwa ibada ngumu lakini zenye fadhila kubwa kabisa.

Subira ni siri na ufunguo wa fanaka, furaha, amani, salama na mafanikio yote katika ulimwengu huu wa mapito na ule wa milele.

Katika Qur'an mfano, Mola wetu anasema, "Enyi mlioamini! Jisaidieni katika mambo yenu kwa subira na swala, bila shaka Allah yuko pamoja na wanaosubiri" (2:153).

(2:155), anaendelea kwa kusema, "Na tutakutieni katika misukosuko ya (baadhi ya mambo haya) khofu na njaa na upungufu wa Mali na watu na wa matunda, na wapashe habari njema wanaosubiri.

Hapo vijana tayari tumearifiwa kwamba kila mmoja wetu ataonjwa na MwenyeziMungu kwa mitihani mbalimbali na hakuna njia ya kuliepuka hilo. Hatuna tegemeo wala kimbilio wakati wa misukosuko au masaibu ila katika kusubiri na kuswali.

Riziki, fursa au neema uliyonayo sasahivi huo ni mitihani kutoka kwa muumba na iko siku utaulizwa kuhusiana na neema hiyo. Wengine tunaohangaika kuipata riziki, neema fulani, na hatupati, vile vile ni mitihani kutoka kwa Mungu.

Endapo utachakarika pasi kukata tamaa, ukasubiri juu ya maamuzi yake yeye, basi malipo makubwa yataandaliwa kwa ajili yake, lau atalaani mitihani hiyo, hapo utakosa radhi yake.

Ni yupi ambaye unamuona wewe kafanikiwa, halafu hakupitia changamoto?, mitihani?. Kuna amepata kumsikia Raphael Obonyo. Huyu ni miongoni mwa wajumbe wa bodi ya benki ya dunia. Kijana mdogo. Alizaliwa na kukulia katika kijumba kisichoeleweka huko Korogocho, Kenya. Mtoto wa mpishi wa Cafeteria mjini Nairobi. Alikutana na masaibu kila kuitwapo leo katika heka heka sake za kuipata elimu.

Raphael Obonyo alikua na subira. Alipomaliza masomo yake chuo kikuu cha Nairobi kwa mbinde alirudi Korogocho na kuungana na vijana wenzake huku akiwapa elimu juu ya biashara ndogondogo. Akasota nao kweli huku tegemeo lake likiwa ni muumba pekee. Akawagusa vijana wengi wa Kogorocho. Hapo neema ikamshukia. Obonyo safari yake ya mwangaza ilianza baada ya kuupata ufadhili wa Ford Foundation kwenda United States kusomea master's.

Hivyo basi inafaa tuwe na mu'amala mzuri baina yetu na jamii, makundi maalumu. Tunafaa tumsaidie yeyote kwa chochote ulichokuwa nacho. Kidogo ulichonacho wewe ni kikubwa akitamaniacho mwengine. Vijana tuwekeze nguvu zetu katika yale yenye kugusa wengi.

Fanya mema kwa kutarajia malipo kutoka kwa Mungu utatunukiwa na kuyapata mafanikio endelevu. Na yeyote mwwnye kufanya mema kwa ajili ya maslahi yake binafsi basi hatapata chochote. Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kumfanyia wema mwenzake hali ya kutajia rehma na fadhila kutoka kwa Mungu.

Wapo watu ambao hutumia unyonge wa watu wengine kwa manufaa yao binafsi, bila kujali maisha ya walio chini yao. Hali hii mwishowe husababisha hasara tupu katika maisha ya mtumiaji vibaya. Kila mtu anfaa kupewa haki yake kiukamilifu bila ya kudhulumiwa kwani dhulma ni giza.

Ukarimu unapatikana katika tabia njema ambayo anatakiwa ajipambe nayo yeyote. Mtu anatakiwa awe mwepesi wa kukirimu wengine wakati wanapokuwa katika hali ya kuhitaji msaada.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom