ubongokid
JF-Expert Member
- Apr 30, 2017
- 2,154
- 4,184
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU SHAMBULIO KWA MGOMBEA WA UDIWANI KATA YA TUNGI JIMBO LA KIGAMBONI
Ndugu Wananchi;
Uongozi wa Chama Cha Wafanyakazi Tanzania (Tanzania Labour Party-TLP) Wilaya ya Kigamboni unalaani vikali shambulio lililofanywa dhidi ya Mgombea wa nafasi ya udiwani katika KATA ya TUNGI wilaya ya Kigamboni;
Ndugu SETH NICOLAUS MCHAYUNGU
Shambulio hilo ambalo lilifanyika mbele ya watu katika eneo lake la kazi lilifanywa na vijana walioambatana na MGOMBEA udiwani KATA ya TUNGI kupitia Chama Cha Mapinduzi-CCM ambao pamoja na mambo mengine Walichana Bendera ya Chama Cha Tanzania Labour Party iliyokuwa imetundikwa kwenye BAJAJ YA Ndugu SETH NICOLAUS MCHAYUNGU na kuharibu Bajaj yake hiyo ambayo ilikuwa imepaki kituoni kwa ajili ya kupakia abiria huku wakimpatia vitisho vikali.
Tukio hili sio la kistaarabu na linapaswa kukemewa na kulaaniwa na wapenda haki wote nchini na wapenda amani.
Aidha uongozi wa TLP wilaya ya Kigamboni unalisihi sana Jeshi la Polisi kutokuchukulia kwa wepesi taarifa za matukio kama haya yanapofikishwa kituoni kwani tulishangazwa sana na kitendo cha Askari Polisi wa zamu kutokuchukua hatua baada ya kupewa taarifa ya tukio hili.Hii haileti picha nzuri juu ya utayari wa jeshi la polisi kutoa ulinzi kwa watu wote hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Hata hivyo,tunashukuru sana uongozi wa kituo cha miito cha Jeshi la Polisi Makao makuu kwa utayari waliouonyesha wa kufuatilia tukio hili na kuhakikisha kwamba Ndugu SETH NICOLAUS MCHAYUNGU anapatiwa huduma stahiki baada ya kutoa taarifa kituoni hapo.Ieleweke kwamba raia anapokuja kuleta taarifa ya tukio la uhalifu Jeshi la Polisi lisiichukulie kwa wepesi kwani inaweza kuleta madhara ambayo hayakutarajiwa.
Tunatumaini kwamba Jeshi la Polisi Wilaya ya Kigamboni litachukua hatua stahiki dhidi ya uhalifu huu ikiwamo kuwakamata wahalifu hawa na kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria
Aidha uongozi wa TLP wilaya ya Kigamboni umefikisha Taarifa za tukio hili kwa Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi pamoja msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa KATA ya TUNGI na ni matumaini yetu kwamba hatua stahiki za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya Mgombea huyu wa CCM anayeratibu uhalifu.
Tunawashukuru wote waliotupa pole,ushauri na kututia moyo hasa katika kushughulika na adha hii.
Tunapenda kuwajulisha wakazi na wapiga kura wote wa KATA YA TUNGI pamoja na WILAYA ya Kigamboni kwamba tukio hili halitatuvunja moyo wala kuturudisha nyuma,bali limetupa hamasa zaidi,na nguvu zaidi ya kuhakikisha kwamba tunashiriki kikamili katika KUJENGA jamii mpya inayoheshimu haki za Raia.
TLP-UHAI WA MTANZANIA
TUPEANE FURSA,TUWEZESHANE Tanzania ni Yetu Wote
Asanteni sana
Imetolewa na Uongozi wa TLP
Wilaya ya Kigamboni.
Wilaya ya Kigamboni.