Abdul Sykes na yeye alikuwa anavuta sigara " clipper" kama Nyerere?
Laki...
Hii ni taazia ya Prof. Bavu kwa bahati mbaya umeleta habari za Abdul Sykes, Julius Nyerere na Sigara Clipper.
Hapa si mahali pake lakini nitakujibu.
Swali lako kwanza umekosea kuliuliza.
Kuwa Abdul anavuta sigara gani si swali ambalo nitalijibu na barza itakuwa imeelimika.
Kuna mtu kasoma ile makala yangu na alipoona kuwa Mwalimu baada ya kuona rafiki yake Hamza Mwapachu yamemsibu maradhi na akafariki na sababu ni uvutaji, yeye akaamua kuacha sigara ili kulinda afya yake.
Huu ulikuwa uamuzi wa busara.
Sasa nataka nikueleze kitu ambacho siku zote kikiwataabisha viongozi wa TANU pamoja na Abdul Sykes.
Hii ilikuwa usalama wa Nyerere kuwa vipi watamlinda maadui wasimuue.
Ajabu hawa viongozi hawakufikiria kuwa uvutaji wa sigara wa Nyerere pia ni moja ya tishio kwa maisha ya Mwalimu.
Wao walichokiogopa zaidi ilikuwa Nyerere kulishwa sumu.
Mwalimu alikuwa akiwa Iringa basi chakula chake popote pale kilikuwa kinasimamiwa na Abbas Max na walichokuwa wakifanya ni Abbas Max kubadilishana sahani na Nyerere baada ya chakula kishatengwa dakika ya mwisho wanataka kula.
Mwalimu alikuwa akimuuliza Abbas Max ana uhakikika gani na ''ujanja,'' ule?
Abbas Max alikuwa akijibu kuwa hakuna mtu anaeweza kufikiri hata kwa mbali kumdhuru yeye Iringa nzima kwani wote wale walikuwa ni ndugu zake na ikiwa Mungu apitishie mbali limemkuta la kumkuta basi koo zitamalizana kwa visasi.
Alikuwa akimwambia Nyerere kuwa hakuna atakaeweza kupenya katika ngome ile yao ya Wahehe.
Tabora Mwalimu katika mkutano wa Kura Tatu mwaka wa 1958 alikuwa akipikiwa chakula chake na Jaffari Iddi na yeye alilishwa yamini kuwa hatomdhuru Nyerere.
Nimekutangulizia mkadama huu ili ujifunze kufikiri mbali zaidi na uulize maswali yenye maana.
Sasa hata nikikuambia kuwa Abdul Sykes alikuwa anavuta Pall Mall taarifa hii ina maana gani kwako na kwa wasomaji?
Iko siku Nyerere katika ''retreat,'' nyumbani kwa Abdul Sykes baada ya kula chakula cha mchana walipomaliza kikao Nyerere akashikwa na tumbo kali sana akawa amelala kwenye sofa anaugulia.
Taharuki kubwa ikatokea kwa haraka watu wakadhani Nyerere kalishwa sumu.
Mama yake Mwalimu alikuwapo uani na akina mama wengine ambao ndiyo walikuwa kila pakiwa na kikao pale kwa Abdul wanakuja kupika.
Bi. Mugaya Nyang'ombe, mama yake Mwalimu alipoona hali ya mwanae akawa analia ana hakika mwanae katiliwa sumu kwenye chakula inabidi wanawake wenzake pamoja na mama yake Abdul Bi. Mruguru bint Mussa wamtulize.
Swali kubwa likawa nani anaweza kumtilia sumu Nyerere nyumbani kwa Abdul Sykes kwani kwenye nyumba ile Nyerere alikuwa kazungukwa na nduguze watupu?
Hii ilikuwa siku za mwanzo za TANU na Nyerere keshakwenda UNO.
Yaliyobakia ni historia.
Ndugu yangu Laki wewe unauliza habari za sigara.
Nikikuambia alikuwa anavuta Sigara Kali....