Tafakuri kuhusu Elimu na Utaifa

Tafakuri kuhusu Elimu na Utaifa

Shayu

Platinum Member
Joined
May 24, 2011
Posts
608
Reaction score
1,655
Kuendelea kwa taifa lolote hutegemea sana nguvu kazi iliyo nayo, nidhamu, uzalendo na elimu mahsusi kuleta maendeleo jamii inayo yahitaji kwa ujumla, ili kufanya taifa liendelee.

Misingi ya elimu hii lazima ijengwe katika kuendeleza taifa na si vinginevyo. Ni lazima ijengwe katika misingi ya uzalendo, nidhamu na wajibu.

Taifa linapofundisha mtu si kwaajili yake tu, bali ni kwaajili ya taifa, ni kwaajili ya maendeleo ya wote. Ni kwaajili ya watu wote wapate uelewa utakaosaidia katika ujenzi wa taifa imara. Kuendelea kwa taifa lolote hutegemea sana nguvu kazi iliyo nayo na elimu mahsusi kuleta maendeleo jamii inayo yahitaji kwa ujumla, ili kufanya taifa liendelee. Lakini pia jamii lazima iwe moja katika malengo yao.



Watu wote watakapopata uelewa ndipo ukombozi wa kweli utakapopatikana. Uelewa huu ni muhimu kwa ukuaji wa taifa. Kuishi katika ujinga ni sawasawa na kuishi katika kiza kinene, ni elimu pekee itakayotutoa katika kiza hiki.

Na elimu hii ni lazima iende kwa watu wengi zaidi ili wapate kujielewa. Kwakuwa pasipo kujielewa huku hatutaweza kujenga taifa hili. Ni kwa kujitambua huku pekee tutaweza kujenga jamii iliyobora, pasipo kujitambua huku hatutaweza kuondoa ujinga.

Lakini misingi ya elimu yetu ya sasa haisaidii kujitambua huku kwa watu wetu kwa taifa lao ndio maana watu wanapata maarifa ya kazi lakini ujinga wanaendelea kuwa nao NA UFAHAMU WAO kwa taifa lao unakuwa finyu. Hawajui kwanini sisi ni taifa na wala hawana uzalendo wa kulijenga.

Kujitambua huku ni kufanya mambo ambayo ni yenye faida kwa jamii na kwa mtu husika. Kujitambua huku ni kutumia uwezo wa kiakili kujizuia na kuongozwa na fikra. Ni kujua asili ya binadamu ni fikra na nje ya fikra huwezi kumtofautisha na mnyama. Pasipo kuongozwa na fikra na kuchagua kilicho bora kwa faida yetu kama taifa tutasemaje tumeelimika?

Elimu hii ni lazima iwe na uwezo wa kujenga mahusiano yetu na kufanya taifa liwe na dira moja.

Ni nini faida ya elimu kama sio kutengeneza mwenendo wa binadamu kadiri inavyowezekana kuwa bora na wenye faida kwa umma?

Tuangalie elimu yetu ya sasa ilivyoundwa je ina mjengea mwanafunzi nidhamu na wajibu katika jamii na taifa lake? Je inamjengea uzalendo? Je inatengeneza mienendo ya namna gani kwa wanafunzi? Je inampatia maarifa ya kazi ya kutosha ambayo yameambatanishwa na mapenzi na uzalendo kwa taifa?

Je inaonyesha ubora wetu katika kuzalisha na katika tabia zetu na mienendo yetu?

Elimu yetu lazima ifundishe watu kutumia akili yao wenyewe. Tutafanya mapinduzi makubwa kama watu wetu watakuwa na uwezo huu, elimu yetu ni lazima iwe katika kukuza akili na sio kumwingizia maarifa mtoto kama maji yanavyojazwa kwenye chupa na kufungwa, kwa kufanya hivyo tunafunga ufahamu wao. Ukuzaji wa akili za watoto wetu ndio lengo kuu ya elimu. Tukikuza ufahamu huu ni hatua moja kubwa kwetu kuendelea. Ni lazima iunde watu wetu katika uzalendo,nidhamu na maadili...Ni lazima tutengeneze akili za watoto wetu katika mkondo fulani, akili zilizotawanyika kamwe hazitojenga kitu.

Kutengeneza akili za watoto wetu katika mkondo fulani ndio nidhamu yenyewe ambayo ni muhimu sana kwa ukuaji wa taifa lolote na kujitambua kwake. Watu wetu ni lazima wawe na mwelekeo na taifa lao.

Ni lazima tujielewe sisi ni watu wamoja na elimu yetu tunayotoa kwa watu wetu ni maalum kwaajili ya ujenzi wa taifa hili na ni kwaajili ya ukombozi kwa watu wetu dhidi ya ujinga.

Je ujinga tutautoaje? Ujinga ni kufanya mambo yasiyo sahihi. Kupata maarifa ya kazi tu sio tiketi ya kukufanya wewe uwe umeelimika. Ili tuseme tumeelimika ni lazima tuwe na watu wanaofanya mambo yaliyo sahihi kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla ndio maana nasema ni lazima iunde tabia zao pia. Ili uwe ume elimika ni lazima utumie akili zako vizuri na uwe mwenye manufaa kwa umma. Namaanisha uwe mwenye msaada kwa taifa. Utumike ipasavyo kuleta manufaa katika taifa sio kulibomoa.

Hivi ndivyo tutakavyo jenga taifa kwa kujitolea. Tukitaka kujenga jamii yenye furaha ni lazima tufanye mambo haya. Bila ukombozi huu dhidi ya ujinga kwa watu wetu wengi zaidi, hatutaweza kuendelea wala kuondoa uhalifu nchini. Kwahiyo ni lazima tuwe na watu walioelimika na waliotayari kujitolea kulijenga taifa hili ndio maana mataifa yanawapa elimu watu wao. Lakini wale wanaoitumia vizuri katika uzalendo, wajibu na kujitolea kuona taifa lao likiendelea ndio waliopiga hatua. Sisi elimu yetu imejengwa katika ubinafsi.

''Ni katika kujitolea huku sisi kama taifa tutapiga hatua za kimaendeleo. Kwahiyo ni lazima elimu yetu ibadilike ilenge katika kujenga taifa badala ya kuelimisha watu kwa manufaa binafsi. ''

Suala la ajira kwa watu wetu litamalizwa ikiwa watu wetu watapata maarifa ya kutosha yatakayo -wafanya kujitegemea. Ni katika msingi huu wa kutoa maarifa yatakayomfanya raia kujitegemea nchi yetu itapiga hatua kimaendeleo.Ni lazima elimu yetu ijengwe katika misingi hiyo. Ni lazima tutoe elimu bora itakayowafanya watu wetu kujitegemea na kuwa wazalendo na wawajibikaji kwa taifa.

Pamoja na kuwapa elimu ya stadi za kazi tabia pia ni muhimu kujengwa kwakuwa bila tabia bora hatutakuwa na nguvu kazi nzuri katika taifa letu. Ni lazima tujiulize ni tabia gani tujenge kwa watoto wetu ambazo zitakuwa chachu ya maendeleo yetu kama taifa?

Ni mambo gani watoto wetu wajiepushe nayo na ni yapi wayafuate? ni lazima tuangalie hapa kwakuwa pasipo kujenga tabia bora za watoto wetu baadae ya taifa hili itakuwa gizani.

Kuwaachia vijana wetu kujiingiza katika starehe za kupindukia sio jambo jema kwa ukuaji wa taifa letu. Jambo hili huondoa uwajibikaji na utiifu wa vijana na huondoa uwezo wao wa kufikiri sawa sawa. Kwahiyo maadili ni jambo la msingi kwa ukuaji wa taifa na hatutaweza kujenga maadili hayo kwa kuwaacha vijana kutopea katika starehe.

Tunahitaji kujenga raia wawajibikaji kwa taifa lao, wazalendo na shupavu. Kwa njia hii pekee tutapata mwelekeo kama taifa. Kujitolea huku kwa vijana kwa taifa lao kutaka kuona likinyanyuka na kupata heshima katika mataifa ni roho ya kweli ya ukombozi. Tunahitajika kujenga roho hii kwa kila raia. Watoto wetu lazima wakue wakitambua wanawajibu huu muhimu ni lazima wawe na mahaba kwa taifa lao. Mwanamke asiyejipenda hawezi kujipamba, Taifa ambalo watu wake hawajawekeza hisia zao kwake litavutiaje?

Kwahiyo ni lazima tujenge upya fikra za watoto wetu katika mwelekeo fulani na katika tabia fulani. Hizi tabia tunaweza kuzijenga kwa kuwapa elimu itakayo wajenga hivyo. Kwakuwa Siamini kama kuachia taasisi kama polisi na mahakama kushinikiza tabia na mienendo ya watu wetu katika tabia tunayotaka inatosha. Ni lazima watu wetu wajielewe wenyewe na kujua wanajenga taifa lao wenyewe. Kwahiyo hii roho ya kutaka taifa lao livutie na kupendeza ni lazima iwe katika kila moyo wa mwananchi.

Uzuri wa taifa hili utatutegemea sisi kutokana na maarifa na stadi zetu za kazi. Kutokana na busara na hekima. Kila mwananchi ni lazima ajitahidi kufanikisha hili, kwakuwa hili taifa ni la kila mmoja wetu, kila mtu ana umiliki nalo ndio maana mtu aliyezaliwa hapa tunamwita mwananchi na mtu yeyote mwenye asili ya hapa kwa vizazi vingi. Ni muhimu kutambua kwa vizazi vingi tumeendelea kuishi katika taifa hili tukipitia katika mambo kadhaa mpaka tulipofikia sasa. Utumwa na ukoloni; na mambo yote magumu ni wakati sasa wa kutafakuri na kulileta taifa hili pamoja. Wakati sasa umefika kwa sisi kuwa wamoja. Ni wakati sasa umefika wa kujifunza kutokana na historia. Ni lazima tuungane tuwe kitu kimoja. Kwa kutopendana kwetu na kwa kutokuwa wamoja tulijikuta katika utumwa na katika ukoloni.

Ukurasa wa umoja na mwelekeo lazima ufunguliwe. Umoja katika malengo ya kujenga jamii bora na endelevu.
Kitabu lazima kifunguliwe sasa, kitabu chenye hadithi nzuri ya kuvutia ya taifa lilinyanyukia kutoka katika utumwa na kutawaliwa, na kujenga jamii bora na zinazovutia dunia haijapata kuona. Kwa ushupavu na matumaini tutafika huko. Mbegu hii lazima ikue, tumaini hili lazima linyanyuke katika kila moyo wa mwananchi. Kwahiyo ni lazima tujenge tabia za wananchi wetu kuelekea huko.

Tungehitaji raia wanaojiongoza wenyewe kutenda yanayostahili kutokana na ufahamu wao na mapenzi yao kwa taifa .
Hapa ndipo umuhimu wa elimu bora unapokuja na ndio maana nasema; elimu ya stadi za kazi peke yake haitoshi pasipo kujenga tabia na nidhamu za watu wetu. Tukifanya hivi taifa letu litakuwa na mwelekeo ni lazima tujenge taifa letu katika uzuri na sio katika ubaya.

Kwahiyo polisi na mahakama havitoshi kujenga jamii bora bila ya kuwepo elimu bora.
Ingawaje vyombo hivi ni muhimu katika kurekebisha tabia za watu wetu na kushinikiza taratibu na sera, ili kujenga jamii bora na zenye amani.

Vyombo hivi vingetumika kidogo kwenye jamii iliyoelimika ili kufanya jamii bora zaidi.
Kwahiyo mtazamo uliokuwepo ya kuwa watu wetu wanapata elimu ili iwafaidishe wao na kuwapatia ajira ni lazima ufutwe ili tuwe na mtazamo wa kuwapa maarifa yatakayowafanya kujikomboa kifikra ili waweze kujenga taifa lao wenyewe na kujitegemea.

Elimu yetu ni lazima iwapatie stadi za kazi zitakazowafanya wajitegemee. Ni ubora wa stadi za za kazi pekee utakaowafanya wahitajike na kuwa wenye manufaa. Ni lazima pia tuwajengee moyo wa kupenda kufanya kazi kwa bidii na bila kukata tamaa.

Habari ya kupasi na kufeli ni lazima tuiangalie upya na kwa umakini. Lengo hapa ni kumuingizia maarifa mtoto na maarifa haya inabidi tuangalie tangia wakiwa watoto katika makuzi yao, tutawajengeaje ufikiri wao. Je tutawasaidiaje watoto wenye ufikiri mdogo kama wakiwepo darasani? Kuwaacha waliofeli ni kutotimiza wajibu wetu. Ni lazima tujenge nidhamu yao na mwelekeo wa akili zao. Pengine walimu wawe na muda wa ziada kwaajili ya wale wenye ufikiri mdogo. Ni lazima vijana na watoto wetu wajue wanaenda shule kutafuta maarifa na akili yao iwe katika maarifa na sio ajira. Wakienda shule katika mtazamo wa kutafuta maarifa watakuwa wabunifu zaidi na watatia juhudi zaidi kupata ufahamu. Vijana wetu wakienda shule kwa mtazamo wa ajira na sio maarifa tutakuwa hatujafanya jambo la msingi. Hawatopata uelewa wa kutosha na hawatotumia nguvu nyingi na akili kuitafuta. Watatumia njia zozote ili wapasi hata kwa kudanganya ili waje wapate ajira na pesa hawatothamini maarifa kama maarifa. Kwa mtazamo huu hatutaweza kukuza ufahamu wao.
Vijana wetu wakiwa na mtazamo huu hawatapenda elimu, itakuwa ngumu na mzigo kwao, na watatumia nguvu nyingi katika kuelewa, elimu yetu itajawa na uwoga na hofu ya kufeli na ya maisha. Ni muhimu kuwaondolea hofu hii vijana kwa kuangalia upya misingi na mazingira ya elimu yetu.

Iwe watu wanaenda shule kutafuta maarifa yatakayokuja kuwasaidia jinsi ya kuishi, na ufundi stadi wa kuzalisha mali.
Katika mwelekeo huu taifa letu litakuwa na tija. Watu wetu wataweza kutawala familia zao na kuwa na mahusiano mazuri miongoni mwao lakini watakuwa na dira ya pamoja kama taifa.

Tunapenda watu wetu wawe na ufahamu na wawe huru. Waweze kujua yaliyo sahihi kwao. Waweze kujenga familia zao katika ubora, na wawe wenye manufaa kwa jamii na kwa taifa.
Wakiwa na elimu hii wataweza kutumia rasilimali za taifa kwa faida ya umma kwasababu elimu yetu itakuwa imeelekezwa kwenye ujenzi wa taifa na jamii na sio manufaa binafsi.
Watatengeneza sheria na kuzitii kwasababu watajua ni mali yao na ni kwa faida yao. Ni katika mtazamo huu tutaweza kulikabidhi taifa hili kwa kizazi kingine likiwa bora na lenye utaratibu na ustaarabu.

Tunapenda watu wetu wawe kwa asilia wenye kupenda maarifa ni lazima tujenge tabia hii na ni lazima tuondoe fikra hizi zilizojengeka kwa miaka mingi mongoni mwetu. Tukifanikiwa tutajenga jamii bora na yenye uwajibikaji.
Ni lazima wafundishwe kulithamini na kulipenda taifa lao na ya kwamba wanapewa elimu ili waweze kuliendesha taifa hili katika ubora.

Ni muhimu kutambua ya kwamba binadamu anapata faida kubwa anapoishi na jamii, nje ya jamii maisha ya binadamu yasingekuwa kama yalivyo sasa.
Tuna wajibu wa kujenga jamii zetu na familia zetu lakini pasipo elimu bora hatutaweza vyote hivi. Ni lazima tujenge familia zetu na jamii zetu katika nidhamu na katika utaratibu.

Elimu yetu pia lazima ilenge kukuza fikra na uelewa wa watu wetu. Na sio tu kumwingizia maarifa kichwani, imfanye aweze kufikiri na kufanya maamuzi sahihi kwa kutumia ubongo wake na sio kuelekeza tu bali kukuza ufahamu na wala sio kukariri. Aweze kufikiri mwenyewe na kuamua yaliyo sahihi.

Elimu hii itamfanya kuwa huru zaidi na bila elimu ya namna hii hatutaweza kujenga nchi ya kidemokrasia. Kwasababu demokrasia inahitaji uelewa wa watu katika kufanya maamuzi sahihi kwa manufaa ya nchi.
Kwasababu demokrasia inawataka wananchi kujiamulia mambo yao wenyewe kwa faida yao wenyewe na hii inahitaji elimu. Bila elimu na hatutaweza kujenga demokrasia.

Demokrasia hii inahitaji nidhamu na jamii yenye utaratibu na mpango. Demokrasia katika jamii isiyokuwa na utaratibu mzuri ni fujo. Ni lazima jamii iwe inajielewa ili demokrasia ifanye kazi vizuri. Ni lazima iwe jamii inayojitambua na inayojua mwelekeo wao. Ni lazima iwe jamii iliyopangwa na kupangika ndipo demokrasia itakapofanya kazi vyema. Jamii hii ni lazima iwe ambayo imeelimika. Bila kuelimika huku demokrasia haiwezi kufanya kazi.

Ni baba anayejua kilicho bora kwa mtoto wake lakini mtoto atakapokua na kupata uelewa hujua anachohitaji. Ni lazima elimu yetu iwafanye watu wetu wapate uelewa huu. Na demokarsia yetu itafanya kazi mpaka pale watu wetu watakapoelimika na kujitambua, kwasasa ni mpaka tumpate kiongozi mzuri atakayesimamia ukuaji huu. Mpaka hapo itakapoonekana watu wetu wanajitambua na wanaweza kujiongoza wenyewe kwa njia za kidemokrasia bila kuathiri mpangilio wa jamii na amani ya nchi.

Ni muhimu sana kama tunataka kujenga taifa la kidemokrasia ambalo pia huhitaji nidhamu ya hali ya juu. Ni lazima tujenge watu wetu katika fikra sahihi.

'' Kama madhumuni ya elimu ni kumuongezea uelewa binadamu na kumfanya kujitambua, kutambua mazingira yake, kutengeneza tabia yake na mahusiano yake na jamii, kumfanya awe na nidhamu na awe mwenye faida kwa umma na kwa jamii, bado kwa kiwango kikubwa, hatujafanikiwa katika dhamira hii kwakuwa dhumuni la kuwa na taifa sio tu ni kupata faida za kimali bali pia kujenga mahusiano yetu na mashirikiano yetu kama binadamu. Na huu ndio msingi wa jamii yenye furaha.
Jamii ambayo inahangaika kwenye kutafuta mali tu bila pia kujenga misingi ya mahusiano yao kamwe haitoweza kuwa na furaha. Kwasababu pesa itakuwa ndio msingi wa maisha yao. Uhusiano wao utakuwa duni na tunaweza kupima mwisho wa jamii hii kwa matendo yake na kuujua. Ni dhahiri sio mwisho mzuri''
 
Back
Top Bottom