Tafakuri kuhusu elimu, ustaarabu na maendeleo.

Tafakuri kuhusu elimu, ustaarabu na maendeleo.

Shayu

Platinum Member
Joined
May 24, 2011
Posts
608
Reaction score
1,655
Elimu ni msingi kwa taifa lolote lile kuendelea. Maendeleo ya taifa lolote lile yanategemea sana msingi huu. Bila elimu hakuna maendeleo. Kwahiyo ili taifa litoke kutoka katika hatua moja ya ukuaji kwenda nyingine ni lazima izingatie kwa ukaribu sana elimu ya watu wake. Maendeleo ya kiakili ya watu ndio msingi wa maendeleo ya vitu. Kwahiyo ni muhimu kwa serikali kuwekeza katika elimu.

Elimu ambayo itawafanya watu wetu wafikiri na wapende kutafuta maarifa na kuongeza ufahamu wao. Tunataka kutoka tulipo kama taifa ili tupige hatua nyingine ya kimaendeleo na ya kijamii, na katika hili hakuna jinsi zaidi ya kufikiri na kutafuta maarifa jinsi gani tutatoka hapa tulipo. Kama tunavyofahamu tuna changamoto nyingi katika elimu yetu ya sasa ambayo bado haijawafanya watu wetu wawe huru na wenye fikra zinazojitawala.

Naomba tujiulize kwanini taifa linawapa elimu watu wake? ni kwaajili tu ya kuwapa ufahamu ambao utaosaidia kulitoa taifa kutoka hatua moja ya maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi kwenda nyingine. Tunajua kabisa pasipo elimu jambo hili ni gumu sana. Ndio maana nasema elimu ni jambo la kusisitiza sana katika nchi yetu kama tunataka kuendelea kama taifa. Na jambo la elimu sio la mtu binafsi ni jambo la taifa. Kwahiyo ili tuendelee kutoka hatua moja kwenda nyingine jambo la elimu ni muhimu mno. Na hili pia linahitaji umoja hatutaweza kutoka katika hatua moja ya kijamii na kiuchumi pasipo kuwa wamoja.

Kwahiyo ni muhimu kuangalia misingi upya ya elimu yetu na muelekeo wake ni lazima kuwe na dira kama tunataka kutoka hapa tulipo. Tunapozungumzia elimu tunazungumzia kukuza watoto wetu katika mkondo fulani wa mawazo na imani. Kukuza watoto wetu katika uzalendo na utaifa.

Kujenga tabia zao wangali wadogo katika nidhamu na utaifa. Jambo hili ni msingi wa ukuaji wa taifa lolote. Sisi wote tumeunganishwa na kitu kimoja Taifa letu. Hatuwezi kuangaliana kama wageni ni lazima tuangaliane kama watu wa taifa moja wenye malengo sawa na elimu yetu lazima ijenge katika ufikiri huo kwa watoto wetu.
Kwahiyo elimu yetu lazima ituunganishe katika lengo moja na katika mkondo mmoja ambao safari yetu kama taifa itaishia.

Jambo la nidhamu nimezungumza mara nyingi katika maandiko yangu ni muhimu sana. Ili elimu iwe na faida ni lazima iendane na nidhamu. Lakini pili ni muhimu kwetu tukavunja elimu yenye malengo ya faida za kibinafsi lakini tuwe na watu ambao wanafikiri jinsi gani tutaendeleza taifa letu kabla ya kufikiri ni jinsi gani atajiendeleza yeye binafsi na familia yake.


Ni muhimu kujenga jamii ambayo iko pamoja na yenye malengo ya pamoja badala ya jamii ambayo watu wake ni wabinafsi. Mapenzi yetu kwa jamii ni lazima yaibuliwe ili watu waangalie jamii kwanza badala ya kuangalia ubinafsi ili tujenge jamii zetu na kuziendeleza katika roho ya upendo.


Maendeleo na ustaarabu wa jamii yeyote ile msingi wake ni elimu iliyobora. Mawazo haya ambayo yamekusanywa na kuelekezwa katika mkondo mmoja ambao ni maendeleo ya watu wetu na taifa letu ndio msingi haswa wa taifa lolote kunyanyuka.


Kujitegemea maana yake unazalisha kilicho chako na unakula kilicho chako lakini pia unafikiri mawazo yako mwenyewe. Nje ya hapo bado hujajitegemea ni mtumwa ili tusimame kama taifa ni lazima tuzalishe vilivyo vyetu na tufikiri wenyewe. Hapo tutakuwa tumejitawala. Hatuwezi kujitawala pasipo serikali kuwa na uwezo wa kutawala vyema. Ninapozungumzia kujitawala ni uwezo wa serikali kutawala watu wake na kuzuia mgawanyiko wowote ndani ya taifa ambao utapelekea watu wa taifa hilo kutokuwa wamoja na kutozalisha. Lakini pia kufanya maamuzi yake yenyewe yatakayopelekea taifa kupiga hatua kimaendeleo.


Ni wazi kwamba bado tunawategemea wazungu kwa mambo mengi hata kwa mawazo, bado hatujawa huru na bado hatujajitegemea. Sidhani kama ni wakati wetu waafrika wa kupumzika bali ni wakati wa harakati. Kujitegemea ni uhuru, taifa lisilojitegemea halina uhuru. Haliwezi kuamua mambo yake lenyewe.


Tumepata uhuru kujitawala lakini harakati zetu za kujiletea maendeleo na kujitegemea lazima ziendelee ili tusimame wenyewe kama taifa. Taifa letu ni kama mtoto mdogo anayetambaa tunahitaji kusimama. Waambieni vijana wa Afrika mapambano lazima yaendelee ili Afrika isimame.


Mapambano haya sio ya mtutu wa bunduki bali ya fikra. Na ya kujiletea maendeleo yetu wenyewe kama taifa. Waambieni pia vijana ambao watakuwa viongozi wa kesho wawe wazalendo na wenye kufikiri. Wasiendeshwe na tamaa ya madaraka bali fikra mujarabu ambazo zitaleta ukombozi wa watu wetu.

Waambieni waangalie tabia zao na mienendo yao kama inafaa kuwaongoza waafrika na kama wana uwezo wa kuleta nuru katika giza lililo tufunika.


Waambieni ukweli huu binadamu hawezi kuongoza wenzake kama atashindwa kuongoza nafsi yake mwenyewe. Kuishinda nafsi yake dhidi ya tamaa na usaliti.

Waambieni wote ambao wana kiu ya kuongoza waangalie nidhamu zao kwasababu nidhamu ni kionjo muhimu kwa kiongozi yeyote bora.


Kuna wengine wanaotaka madaraka kwaajili ya kujinufaisha wenyewe na kuwafanya sehemu kubwa ya jamii kuwa watumwa wao. Waambieni hao huu sio wakati wao watu wa Afrika wanahitaji maendeleo na usawa.


Waambieni watu wa Afrika na Watanzania; Elimu ndio msingi wa maendeleo ya taifa lolote tutafute maarifa kwa udi na uvumba sio kwasababu ya kupata kazi bali ya kuongeza uelewa wetu na ufahamu wetu ambao utatufanya kujua masuala mengi na katika kufanya maamuzi yenye hekima yatakayolitoa taifa hili kutoka sehemu moja kwenda nyingine na yatakayotufanya tuishi vyema na kufanya taifa letu kuwa endelevu.

Pasipo elimu hatutaweza kulijenga taifa hili na pasipo nidhamu hatutaweza kulilinda taifa hili. Elimu yetu lazima ijenge tabia za watu wetu. Katika uzalendo, nidhamu na uwajibikaji.

Hivi vitu vitatu ni muhimu sana kwa maendeleo yetu kama taifa ni muhimu kuvizingatia sana. Ni muhimu kujenga taifa la watu wamoja na wanaowajibika kwa maendeleo ya taifa lao.
 
Back
Top Bottom