Tarehe 21 Agosti ya kila mwaka ni siku ya kimataifa ya kukumbuka wahanga wa ugaidi. Umoja wa Mataifa uliichagua siku hii kwa makusudi, kutokana na changamoto ya ugaidi kuwa kubwa na kuathiri watu wengi duniani. Mwezi Aprili mwaka huu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Gutiérrez alipitisha pendekezo la kufuatilia “maendeleo ya utaratibu wa Umoja wa Mataifa kuziunga mkono nchi wanachama ambazo ni wahanga wa ugaidi”.
Bahati mbaya ni kuwa shambulizi la kigaidi la Septemba 11, 2001 lililotangazwa sana na vyombo vya habari duniani, lilifanya Marekani ionekane kama ni mhanga mkubwa au mhanga pekee wa ugaidi duniani. Lakini ukweli ni kwamba kuna nchi nyingi duniani ambazo ni wahanga wa ugaidi. Watu wa mashariki ya kati wamekuwa ni wahanga wakubwa wa vitendo vya ugaidi, makundi ya kigaidi kama vile IS, Al Qaeda na Al Nusra yamekuwa yakifanya mauaji na kuwaletea taabu watu wa eneo hilo.
Barani Afrika mara kwa mara kundi la Al-Shabaab linafanya mauaji nchini Somalia na Kenya, na hivi karibuni limekuwa linaleta taabu nchini Msumbiji. Nchini Nigeria hadi sasa kundi la Boko Haram linaendelea kuwaletea taabu watu nchini humo na katika nchi jirani, taabu hii pia iko katika eneo la Afrika Kaskazini ambako makundi ya kigaidi yanaendelea na kuwaletea taabu watu wa huko.
China pia imekuwa ni mhanga mkubwa wa matukio ya kigaidi, mashambulizi mbalimbali yalitokea kwenye miji kadhaa ya China, lakini mengi zaidi ya kikatili yalitokea katika mkoa wa Xinjiang, na kusababisha vifo vya watu wa makabila mbalimbali wa mkoa huo, na kuleta hasara kubwa ya mali. Kutokana na kutambua ukweli huo, mwaka 2002 kamati ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuhusu vikwazo dhidi ya kundi la Al-Qaeda, ililiweka kundi la East Turkestan Islamic Movement lililohusika na matukio mengi ya kigaidi nchini China kwenye orodha ya makundi ya kigaidi, lakini kutokana na sababu za kisiasa Marekani imeliondoa kundi hilo kutoka kwenye orodha yake ya makundi ya kigaidi.
Ilichokifanya Marekani ni kuionyesha dunia kuwa kundi la kigaidi ni kundi linalofanya ugaidi dhidi ya Marekani, au linalotishia maslahi ya Marekani na washirika wake. Kama kundi hilo linafanya ugaidi mahali pengine bila kutishia maslahi ya Marekani, au linaunga mkono maslahi ya Marekani basi si kundi la kigaidi. Hali hii ni hatari si kwa Marekani peke yake, bali pia ni hatari kwa dunia nzima.
Mwaka huu “siku ya kimataifa ya kukumbuka wahanga wa ugaidi” inaadhimishwa wakati Marekani inahitimisha vita yake dhidi ya ugaidi nchini Afghanistan. Marekani ambayo pamoja na washirika wake wa NATO imeondoa jeshi lake Afghanistan, imeacha janga kubwa nchini humo. Inaondoka huku ikiwatelekeza maelfu kwa malaki ya waafghanistan ambao ni wahanga wa vitendo vya ugaidi vilivyotokea nchini Afghanistan, na kuwaachia Taliban kazi ngumu ya kuwasaidia watu hao.
Lakini pia kuondoka kwa jeshi la Marekani kumekumbusha somo la siku nyingi kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi, yaani mapambano hayo yasiwe chanzo cha kuongeza wahanga wa ugaidi. Matumizi ya jeshi, yanatakiwa kwenda sambamba na njia nyingine kama vile kuwapatia njia za maisha watu waliojiingiza kwenye ugaidi kama njia ya kujipatia kipato, au kuwapatia njia za maisha watu ambao utaratibu wao wa maisha umevurugwa kutokana na matumizi ya nguvu kwenye mapambano ya kigaidi.
Wakati dunia inaungana kuwakumbuka wahanga wa vitendo vya kigaidi, ni muhimu kuendelea kuwa na sauti moja kwenye tafsiri ya ugaidi na nani ni gaidi, bila kuwa na vigezo viwili. Iwe wazi kuwa ugaidi ni ugaidi bila kujali ni nani anafanya ugaidi huo, na bila kujali ni nani analengwa na ugaidi huo. Isionekane tena kuwa gaidi ni yule anayeshambulia nchi za magharibi tu, na kama akishambulia nchi nyingine anapewa jina tofauti na kutendewa tofauti.