BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Tahariri:
Mwanahalisi
Mwanahalisi
KATIBU Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Chiligati amejenga mazingira ya kutumbukiza taifa katika janga kubwa la vita.
Aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam wiki iliyopita kwamba Watanzania hawataki kusikiliza taarifa za wizi wa fedha zao serikalini.
Chiligati anasema wananchi wakizisikia taarifa hizo, hasa wanachama wa CCM aliodai wanazidi milioni nne, watachukizwa na hivyo kuamua kuchukua hatua za kulipiza kisasi kwa kuanzisha mapambano.
Hoja ya Chiligati ni kwamba yeye na viongozi wenzake katika CCM, wanakerwa kusikia viongozi wa upinzani wakihusisha chama hicho na ufisadi uliotamalaki serikalini na nchini kote.
Anataka wakome, vinginevyo watasababisha wanachama wa CCM kukasirika na matokeo yake watachukua hatua ya kulipiza kisasi.
Kauli ya Chiligati inaashiria hatari. Ni kauli ya kuchochea wanachama wa chama chake. Kuwajaza pumzi, jeuri na kiburi ambavyo ni silaha za awali katika vita dhidi ya wananchi wenzao. Mauaji ya kimbari huanza hivyo.
Chiligati ni mtu mkubwa serikalini; ni waziri anayekaa kwenye Baraza la Mawaziri. Vilevile ni kiongozi mkubwa katika chama anayeeneza sera, ilani na matakwa ya chama ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya robo karne.
Uzoefu tulionao ni kwamba mara nyingi, kauli-amri za chama tawala zimechukuliwa kuwa maagizo ya kufanyia kazi. Ni kauli hizo ambazo zimewaelekeza wananchi na hata vyombo vya ulinzi na usalama: fanya hili, acha lile. Ni utamaduni uliojengeka.
Leo hii, kwa kauli ya sasa ya Chiligati, hatuna sababu ya kutoamini kwamba anaandaa jeshi kubwa la wanachama milioni nne wa CCM, la kupambana na kila anayekosoa, anayekejeli, anayelaumu, anayelalamikia, anayetuhumu na hata anayeshitaki chama hicho kwa lolote lile.
Hii ni hatari inayotokana na mchoko na kuishiwa uvumilivu wa kisiasa, wakati ambapo chama husika kingekuwa kinatumia shutuma na tuhuma kujisafisha na kujiandaa kwa ushindani na kwenye uwanja linganifu usio na vitisho.
Ubabe huu, siyo tu utazaa vita alivyotangaza Chiligati, bali pia utaendelea kuthibitisha hulka ya chama hicho ya kutaka kushinda kwa vyovyote vile.
Mara hii Chiligati anaahidi utawala wa kibabe utokanao na vita. Tunaukataa!