Tamko la Masauni Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu madai ya kusambaa kwa matukio ya utekaji wa Watoto, asema Nchi ipo salama

Tamko la Masauni Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu madai ya kusambaa kwa matukio ya utekaji wa Watoto, asema Nchi ipo salama

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760

View: https://www.youtube.com/watch?v=3S9QuDpJOx0



Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni amesema taarifa za kuwa kuna matukio ya utekaji hasa kwa Watoto Nchini ni sehemu ya kuzua taharuki ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wachache kwa manufaa yao binafsi na kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kudhibiti matukio ya uhalifu ambayo yanatokea Nchini.

Amesema Serikali imefanya maboresho ya mifumo na mikakati ya kuyakabili. Kauli hiyo ya Serikali inakuja katika kipindi ambacho kumekuwa na taharuki inayosabababishwa na madai ya kukithiri kwa vitendo vya utekaji dhidi ya watoto.

Amesema “Nchi ipo salama na kuna Watu wana malengo ya kutoa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, ajenda hazipo Mama anauburuza mwingi kweli, sasa haya ni maneno yanayotaka kututoa kwenye malengo tuache kujadili mafanikio ya Awamu ya Sita."

Aidha, kusambaza taarifa zisizo za ukweli ni kosa Kisheria na kuwa Wizara yake inashirikia na Vyombo vingine vya Dola pamoja na Wizara nyingine kwa kutoa elimu kwa Jamii ikiwemo kuanzia ngazi ya Polisi Kata ili kudhibiti matukio ya unyanjasaji kwa Watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa.

Waziri Masauni amesema hayo Jumapili, Julai 28, 2024 katika mkutano wake na Waandishi wa Habari, uliofanyika ofisi ndogo za wizara hiyo Jijini Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa matukio ya kihalifu mwa mwezi Julai.

Katika maelezo yake, Waziri Masauni amesema Serikali inatambua kuwepo kwa matukio hayo, ingawa si kwa ukubwa kama inavyoripotiwa.

"Siwezi kukaa mbele yenu nikasema eti hakuna matukio ya ubakaji na ukatili wa Watoto, nadhani nitakuwa muongo kupitiliza na pengine sitapaswa hata kuwepo hapa mbele.

Amesema "Uhalifu katika nchi yetu upo, ulikuwepo na utaendelea kuwepo kwa sababu binadamu hatujaumbwa kufikiria sawa, isipokuwa tunaunda mkakati na kutafuta mbinu za kupambana nao."


======

TAARIFA YA MHE. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHANDISI HAMAD M.Y MASAUNI KWA AJILI YA KUZUNGUMZA KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 28/7/2024 JIJINI DAR ES SALAAM

Mhe. Daniel Sillo, Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Ndugu, Ally S. Gugu, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Cammillus Wambura, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,
John Masunga, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Nchini,

Ndugu Waandishi wa Habari,

Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutukutanisha hapa leo.

Ndugu Waandishi wa Habari, nipende kuwajulisha kuwa hali ya usalama wa nchi yetu kwa ujumla iko vizuri. Nivipongeze vyombo vyetu vya usalama vikiongozwa na Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kuzidi kuimarisha hali ya utulivu nchini kudhibiti matukio ambayo yanachafua taswira ya nchi yetu kwa kuwa yanahatarisha usalama wa raia na mali zao.

Hivi karibuni, yamekuwa yakiripotiwa matukio mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mengine kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu tuhuma mbalimbali ya vitendo vya kihalifu vinavyohusisha upotevu na utekaji hususan wa watoto wadogo. Taarifa zinaonesha baadhi ya watoto hao kufanyiwa vitendo vya kikatili na hata kupelekea kuuawa. Matukio hayo yamezua taharuki kubwa kwa wananchi katika baadhi ya Mikoa ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Arusha na Kagera.

Ndugu Waandishi wa Habari, Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kamwe haikubaliani na haitakubaliana na vitendo vyote hivi vya uhalifu wanavyofanyiwa baadhi ya watoto wetu kwani sio tu ni vitendo viovu bali vinaenda kinyume kabisa na utamaduni wa Taifa letu lenye sifa ya Utu, Ustaarabu, Amani na Utulivu. Kwa msingi huo, napenda niwahakikishie ndugu wananchi kuwa Serikali imechukua hatua stahiki wale wote waliobainika na itaendelea kuwachukulia hatua wale watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote na matukio haya ya uhalifu.

Tunaungana na Mheshimiwa Rais na watanzania wote, wakiwemo wa wazazi na walezi, kukemea vikali matukio na aina hii ya uhalifu unaopaswa kukemewa na kila mtanzania na kila mzazi ama mlezi kwani watoto wetu ni taifa la kesho na wanapaswa kulindwa kwa namna zote na wazazi, walezi na kila mtanzania. Tunaendelea kutoa rai kwa wananchi kushirikiana na Serikali, hususan Jeshi la Polisi, kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa washukiwa wote wa matendo haya ya kihalifu. Hii ni pamoja na kuendelea kutoa malezi bora na kuwa karibu na kuwafuatilia watoto wetu wakati wote.

Ndugu Waandishi wa Habari, napenda kuwahakikishia kuwa Serikali kupitia vyombo vyake vya Usalama hususani Jeshi la Polisi inaendelea kufanya uchunguzi juu ya yeyote yule anayejihusisha na vitendo hivi vya uhalifu kwa kuwa wanaotekeleza uhalifu huo ni watanzania wenyewe na wala hawatoki mbali na watu ambao tunaishi nao ama majirani zetu na wengine hata wazazi, hivyo Jeshi la Polisi na vyombo vya dola kwa ujumla wake vitachukua hatua za haraka kwa yeyote ambaye atabainika kujihusisha na uhalifu wa aina hii na aina zingine.

Wakati tukifanya hivyo, kumeibuka tabia ya baadhi ya watu kutumia vibaya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuzusha taarifa za uongo kwenye jamii zinazohusisha uhalifu ukiwemo wa watoto kupotea au kutekwa na hivyo kuzua taharuki na hofu kubwa kwa jamii ya watanzania. Watu hao wamekuwa wakitumia taarifa za zamani na kuleta taharuki kwa jamii. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia Jeshi la Polisi, inafuatilia kwa karibu na itawachukulia hatua wote watakaobainika kujihusisha na tabia hiyo. Ikumbukwe kuwa kusambaza taarifa za uongo na zisizo na uhakika ni kosa kisheria na ikibainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yako.

Ili kudhibiti matukio yote hayo na kuepusha taharuki iliyojitokeza nchini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi na kwa kushirikiana na Wizara nyingine na Vyombo vingine vya dola imeweka Mkakati madhubuti. Mkakati huo unahusisha mambo mablimbali ikiwemo kuongeza elimu kwa umma kuhusu utoaji wa malezi bora na ulinzi kwa watoto.

Kwenye hili tutaongeza nguvu zaidi kwa Polisi Kata nchini nzima na pia kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Elimu Maalum kufikia na kutoa elimi kwa wananchi kwa urahisi. Tutaimarisha doria za mara kwa mara na kutoa kipaumbele kwenye taarifa wezeshi kutoka kwa wananchi wema. Hii ni pamoja na kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa haraka pale matukio kama hayo yanaporipotiwa Jesho la Polisi. Vilevile, tutaharakisha uchunguzi wa kesi zote za watuhumiwa ambao watabainika kujihusisha na masuala ya uhalifu wa watoto ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukulia haraka.

Aidha, pamoja na Mkakati huo, ningependa kubainisha kwa umma wa watanzania kuhusu mifano michache ya baadhi ya hatua mahsusi ambazo Jeshi la Polisi limechukua kukabiliana na hali niliyoeleza hapo awali.

Tarehe 24 Julai 2024 iliripotiwa katika Kituo cha Polisi Ngaramtoni jijini Arusha, kupotea kwa watoto wawili baada ya mama yao kuwapakiza kwenye daladala kwenda shule.

Baada ya Jeshi la Polisi kufuatilia imebainika kuwa watoto hawa wawili walichukuliwa na Baba yao Mzazi na wapo Migori nchini Kenya na mama yao mzazi amezungumza nao kwa njia ya simu. Tukio hili linaonesha uhusika wa wazazi hao ambapo wamezua taharuki isiyo ya lazima.

Tukio jingine ni lile lililotokea tarehe 12 Julai 2024 la kupotea kwa mtoto jijini Dar es Salaam. Tukio hilo lililoripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam. Baada ya uchunguzi wa Polisi tarehe 15 Julai 2024 mtoto huyo alipatikana huko Mikumi mkoani Morogoro ambapo alichukuliwa toka shuleni na msichana wa kazi ambaye aliwahi kufanya kazi kwenye familia hiyo.

Waliofanikisha ni wazazi wa msichana wa kazi baada ya kuona taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam. Tunatoa shukrani na pongezi kwa wazazi hao wa msichana wa kazi na tukio hili linaonesha ushirikano na wananchi unavyoweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo hili na mengine ya uhalifu.

Mfano mwingine ni wa tukio lilitokea Mkoani Geita Kata ya Lwamgasa Mkoani Geita ambapo Jeshi la Polisi lilimkamata Flora Mapolo (33) Mkazi wa Kitongoji cha Mlima namna tano akidaiwa kumnyonga mmoja wa watoto wake wawili aliowazaa mapacha wakiwa na miezi miwili kisha kumtupa porini ambapo mwili huo ulikutwa umenyofolewa mguu n mkono hali iliyozua taharuki kwa jamii.

Tukio lingine ni lile lilitokea katika kijiji cha Kwazoka Halmashauri ya Chalinze ambapo Mwenyekiti wa Kijiji cha hicho cha Kwazoka na Mwalimu wa Shule ya Msingi Vigwaza walikamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani Pwani kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo kuhusu wizi wa watoto ambapo watu wengine wawili walikamatwa na Jeshi na Polisi kwa tuhuma za kurekodi clip na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ikieleza kuwa kuna gari aina ya Noah inayopita maeneo mbalimbali an kuwateka watoto wadogo ambapo taarifa ilieleza watoto wawili wa shule ya msingi Vigwaza wameshatekwa, Ambapo Jeshi la Polisi lilifuatilia na kubaini kuwa taarifa za Uongo, walituhumiwa waliosambaza taarifa hizo ni pamoja na Aishi Thomas Ally (32) Mkazi wa Vigwaza Mkoa wa Pwani, Shomari Tengeneza Zinga (64) ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwazoka Mkoani Pwani, Alphonce Bonifasi Temba (54) Mkazi wa Vigwaza Mkoa wa Pwani na Mwalimu Didas Mwendelezi ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Vigwaza. Tukio hili linadhihirisha kuwa Wizara kupitia Jesho la Polisi haina muhali kwa yeyote yule ambaye atabainika kuhusika na uhalifu wa kusambaza taarifa za uongo na uzushi.

Tukio lingine lililotokana na kusambazwa kwa taarifa za uongo na kuzua taharuki ni lile lilitokea katika Shule ya Msingi Vingunguti na Miembeni jijini Dar es Salaam, baada ya watu kusambaza taarifa za kuongo kuwa kuna watoto wamechinjwa katika shule hizo jambo lililozua taharuki na kusababisha wazazi na walezi kuwafuata watoto wao kwenye shule hizo, ambapo baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kufuatilia taarifa hizo ilibainika taarifa hizo si za kweli na zilisambazwa wa watu waovu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii.

Usalama wa watoto wetu unamhusu kila mtanzania, hivyo nirejee kutoa raia kwa wananchi wote kushirikiana na Serikali katika suala zima la ulinzi na usalama wa watoto wetu kwa kuwa jukumu hili linaanzia katika ngazi ya familia. Kila mwananchi anapaswa kumfichua mtu yeyote, bila kujali nafasi yake katika jamii, inapobainika anashiriki katika vitendo hivi vya kihalifu ukiwemo upotevu na utekaji wa watoto nasi hatutosita kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.

Aidha, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia vyombo vyake vya Usalama inaendelea kuimarisha mikakati ya kukabiliana na uhalifu huu na kuwasihi wananchi kufika katika vituo vya polisi vilivyo karibu pamoja na kutumia namba za simu za bure “toll number” ambazo ni 114 na 112 ili kutoa taarifa mapema iwezekanavyo pindi mwananchi anapohisi kuna viashiria vya utekwaji wa mtoto au watoto mahali popote au uhalifu mwingine wowote.
 

Quran na Haki kwa Kila Raia:

Quran, Kitabu kitakatifu cha Uislamu, ni chanzo kikuu cha mwongozo wa kiroho, kisheria, na kijamii kwa Waislamu duniani kote. Inatoa misingi ya haki, usawa, na uadilifu kwa wote. Haki hizi zimewekwa wazi katika aya mbalimbali za Quran, zikijumuisha haki za binadamu, haki za kijamii, na haki za kiuchumi.

  1. Haki za Binadamu: Quran inasisitiza sana juu ya haki za binadamu. Kila mtu ana haki ya kuheshimiwa na kutendewa haki. Quran inasema:
    • "Enyi watu! Hakika Sisi tumewaumba nyote kutokana na mwanamume na mwanamke, na tumewafanya mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye mtukufu zaidi miongoni mwenu kwa Mwenyezi Mungu ni yule mwenye kumcha Mungu zaidi miongoni mwenu..." (Surah Al-Hujurat, 49:13).
    • "Na kwa hakika tumewatukuza wanadamu..." (Surah Al-Isra, 17:70).
  2. Haki za Kijamii: Quran inafundisha usawa na uadilifu katika jamii. Inakataza ubaguzi wa aina yoyote na inahimiza kusaidiana kati ya wanajamii.
    • "Na saidianeni katika wema na uchamungu, wala msisaidiane katika dhambi na uadui..." (Surah Al-Ma'idah, 5:2).
    • "Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi wa haki kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kwa ushahidi wa haki..." (Surah An-Nisa, 4:135).
  3. Haki za Kiuchumi: Quran inatoa mwongozo wa haki katika masuala ya kiuchumi, ikisisitiza juu ya uadilifu katika biashara, kuepuka riba, na kuwasaidia wasiojiweza.
    • "Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na amekataza riba..." (Surah Al-Baqarah, 2:275).
    • "Na wapeni watoto yatima mali zao, wala msibadilishe cha kizuri kwa kibaya..." (Surah An-Nisa, 4:2).
Quran inatoa msingi thabiti wa haki na usawa kwa kila raia, bila kujali jinsia, kabila, au hali ya kiuchumi. Kwa kufuata mafundisho haya, jamii inaweza kujenga msingi wa haki na amani kwa kila mwanachama wake.
 
Atumbuliwe.
Screenshot_2024-07-27-17-04-22-1.png
 
Mpaka atekwe mtoto wake ndio serikali itashtuka wanasiasa wa ccm wanatuona sisi raia wengine ni mbwa au kuku au swala kupotea kwetu kwao sio big deal ila akipotea mwana uvccm au ndugu zao ndio watajua utekaji upo.
 
Kwakweli nawachukia sana watu aina ya Masauni, unawezaje ku dismiss tatizo ambalo liko wazi kabisa??

Kwamba watanzania ni wapumbavu sana au labda amadhani bado wanaishi zama za kupata habari kupitia RTD??

Aache upuuzi huyu mtu.
 
Kwakweli nawachukia sana watu aina ya Masauni, unawezaje ku dismiss tatizo ambalo liko wazi kabisa??

Kwamba watanzania ni wapumbavu sana au labda amadhani bado wanaishi zama za kupata habari kupitia RTD??

Aache upuuzi huyu mtu.
Ana matatizo ya afya ya akili, muacheni.

Uwendawazimu siyo mpaka mtu avae chupi kichwani.
 

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni amesema taarifa za kuwa kuna matukio ya utekaji ni sehemu ya kuzua taharuki ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wachache kwa manufaa yao binafsi na kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kudhibiti matukio ya uhalifu ambayo yanatokea Nchini.

Amesema “Nchi ipo salama na kuna Watu wana malengo ya kutoa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, ajenda hazipo Mama anauburuza mwingi kweli, sasa haya ni maneno yanayotaka kututoa kwenye malengo tuache kujadili mafanikio ya Awamu ya Sita."

Aidha, kusambaza taarifa zisizo za ukweli ni kosa Kisheria na kuwa Wizara yake inashirikia na Vyombo vingine vya Dola pamoja na Wizara nyingine kwa kutoa elimu kwa Jamii ikiwemo kuanzia ngazi ya Polisi Kata ili kudhibiti matukio ya unyanjasaji kwa Watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa.

Raia kutokea kizimkazi huyo. Tutegemee nini kutoka kwake?
 
Kwa hiyo huyu jamaa hili agizo halijui? Ina maana hajalifanyia kazi na wala hatalifanyia kazi.
Alitakiwa atolee ufafanuzi kuhusu hili tukio na sio kuropoka maneno ya kujichanganya.
Kwa nini Mhe Rais atumie fedha za umma kugharamikia matibabu ya huyu kijana ambaye bado jamii ina shahuku ya kufahamu kilichomsibu alivyopotea. Itakuwa amevimbirwa na kodi zetu hadi hajitambui.

 
Waziri haioni hili lakini Raisi kaliona hilo. Ngumu kuamini kuwa tunasonga mbele badala ya kurudi nyuma au wakishinda ndani ya masuti wanajipna wako karibu na Mungu!!!
 

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni amesema taarifa za kuwa kuna matukio ya utekaji ni sehemu ya kuzua taharuki ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wachache kwa manufaa yao binafsi na kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kudhibiti matukio ya uhalifu ambayo yanatokea Nchini.

Amesema “Nchi ipo salama na kuna Watu wana malengo ya kutoa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, ajenda hazipo Mama anauburuza mwingi kweli, sasa haya ni maneno yanayotaka kututoa kwenye malengo tuache kujadili mafanikio ya Awamu ya Sita."

Aidha, kusambaza taarifa zisizo za ukweli ni kosa Kisheria na kuwa Wizara yake inashirikia na Vyombo vingine vya Dola pamoja na Wizara nyingine kwa kutoa elimu kwa Jamii ikiwemo kuanzia ngazi ya Polisi Kata ili kudhibiti matukio ya unyanjasaji kwa Watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa.

Sija wahi kimuelewa huyu jamaa. Na sitakaa nimuelsws. Namshangaa sana Rais kuendea kumkumbatia huyu boya na IGP wake. Hawa ndio wanao haribu malengo mazuri ya Rais.
 
Back
Top Bottom