EasyFit
JF-Expert Member
- Jul 4, 2011
- 1,269
- 1,082
Imefahamika kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Tume ya katiba kuwa kiongozi wa Serikali ya Tanganyika atajulikana kama Waziri Mkuu, vile vile kiongozi wa Serikali ya Zanzibar atajulikana kama Waziri Mkuu au anaweza kuendelea kujulikana kama Rais hii itategemea mapendekezo yao, hili litaondoa mgongano wa kuwa na marais watatu bila sababu za msingi walisema baadhi ya wajumbe waliohojiwa na Gazeti hili.
Source: Gazeti la Rai.
Source: Gazeti la Rai.
Alhamisi, Juni 06, 2013 06:43 Na Sarah Mossi
WAKATI wananchi wa Tanzania wakijiandaa kurejea tena kwa Serikali ya Tanganyika kama ilivyoainishwa kwenye rasimu ya Katiba mpya, kiongozi wa Serikali hiyo atajulikana kama Waziri Mkuu, Rai imebaini. Wanazuoni na baadhi ya wajumbe wa Tume ya Katiba wameieleza Rai kuwa, Katiba ya Tanganyika inayotarajiwa kutungwa, ndio itakayotamka jina la kiongozi wa nchi na kwa vyovyote vile ataitwa Waziri Mkuu, ambaye chama chake au kwa kushirikiana na vyama vingine anaweza kuunda Serikali kwa kuwa na wingi wa viti bungeni.
Wanazuoni hao wamesema nafasi hiyo ya Waziri Mkuu itaondoa ukakasi wa kuwa na marais watatu katika Serikali tatu zitakazokuwapo mara baada ya kukamilika kutungwa kwa Katiba mpya.
Rasimu ya Katiba mpya iliyotangazwa juzi na Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, imeainisha namna Jamuhuri ya Muungano itakavyokuwa yenye muundo wa shirikisho lenye Serikali tatu.
Serikali hizo ni Serikali ya Jamhuhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huku shughuli zote za Muungano zikisimamiwa na Serikali, Bunge na Mahakama ya Jamuhuri ya Muungano.
Akizungumza na RAI, Mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, alisema Serikali ya Jamhuri ndio itakuwa na mamlaka ya juu ya Dola na itaongozwa na Rais, kama itakavyoainishwa kwenye Katiba mpya.
Profesa Baregu alisema Serikali za Tanzania Bara na Serikiali ya Mapinduzi Zanzibar zitakuwa na viongozi wao ambao watatamkwa kwenye kwenye Katiba zao.
Alisema, ingawa Zanzibar tayari inayo Katiba yake inayotamka jina la kiongozi mkuu wa nchi hiyo ambaye ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lakini bado ipo nafasi ingawa si kwa ulazima kuwapo kwa marekebisho mengine ya Katiba ya Zanzibar, ambayo itatoa nafasi kwa Katiba kutamka jina jingine litakalopendekezwa.
Kwa upande wa Serikali ya Tanzania Bara, Profesa Baregu alisema huu ndio wakati wake wa kutunga Katiba ya nchi ambayo itatamka jina la kiongozi mkuu wa nchi.
"Kwa upande wa Zanzibar, Katiba inaweza kutamka kiongozi aitwe, Waziri Kiongozi na kwa Tanzania Bara litaweza kuwa Waziri Mkuu, hili litaondoa mgongano wa kuwa na marais watatu bila sababu za msingi.
"Ni matumaini yangu Katiba za Tanzania Bara na Zanzibar zitakazotungwa zitapata majina muafaka na kuondoa utata huo," alisema.
Mjumbe mwingine wa Tume ya Marekebisho ya Katiba kutoka Zanzibar, Ally Saleh, aliiambia RAI kuwa, upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari wanayo Katiba yao inayomtaja kiongozi wake kuwa ni Rais, hivyo hakutakuwa na ulazima wa kulibadili jina la kiongozi huyo.
"Tukumbuke hatuwezi kuwachagulia Wazanzibar jina la Rais wao, tayari wanaye Rais, hii ni fursa zaidi kwa Serikali ya Tanzania Bara itakayoundwa kuamua Rais wao aitwe jina gani," alisema Saleh.


