TANROADS kwa kushirikiana na NIT waanzisha kituo cha umahiri cha usalama barabarani

TANROADS kwa kushirikiana na NIT waanzisha kituo cha umahiri cha usalama barabarani

Pfizer

JF-Expert Member
Joined
Mar 25, 2021
Posts
590
Reaction score
807
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wameanzisha kituo cha umahiri (Centre of Excellence) cha usalama barabarani, hatua inayolenga kuimarisha elimu, tafiti na teknolojia katika kupunguza ajali za barabarani.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya wataalamu wa usalama barabarani leo Ijumaa Machi 07, 2025, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha usalama wa barabara nchini na kikanda.

"Taasisi hii itasaidia sana kujenga uwezo wa wadau mbalimbali wanaohusika na usalama barabarani. Suala la usalama barabarani ni jukumu la pamoja, na ni muhimu katika kupunguza ajali lakini pia katika kujenga miundombinu salama," alisema.

Mradi huo ni sehemu ya mpango mpana unaohusiana na ujenzi wa barabara ya Kabingo - Manyovu - Kasulu, unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Fedha za mradi huo zimetumika kununua vifaa vya kisasa vya TEHAMA, kompyuta na vifaa vingine vya kusaidia utoaji wa mafunzo bora katika chuo cha NIT.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha NIT, Dkt. Prosper Mgaya, kituo hicho kitahudumia si Tanzania pekee bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

"Tuna vifaa vya Tele-Conferencing ambavyo vitasaidia wataalamu wetu kufundisha wanafunzi wa mataifa mengine ya Afrika Mashariki kwa wakati mmoja," alisema.

Aidha, kupitia kituo hicho, NIT itaanzisha kozi za Shahada ya Kwanza na Shahada ya Uzamili zitakazohusiana na usalama barabarani ili kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta hiyo.

Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SSP), Wakili Deus Sokoni, amesema kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho ni hatua chanya kwa kuwa ajali nyingi zinatokana na ukosefu wa elimu ya usalama barabarani.

Katika kuthibitisha maendeleo ya Tanzania kwenye usalama barabarani, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Besta kuwa, wiki tatu zilizopita nchi ilitunukiwa tuzo ya heshima ya kimataifa ya iRAP Gary Liddle Memorial Trophy kwa kutambua mchango wake katika kupunguza ajali kupitia Mpango wa Ten Step Plan Tanzania, ikiwa ni nchi ya kwanza kutekeleza mpango huo.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetajwa kama mshirika mkuu wa mafanikio haya kupitia TANROADS, huku wadau mbalimbali wakiahidi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha barabara za Tanzania zinakuwa salama zaidi kwa watumiaji wake.
 
Ninaona kama lengo la taarifa hii lilikuwa ni kutaja jina la dokta Samia na si vinginevyo.
 
Ninaona kama lengo la taarifa hii lilikuwa ni kutaja jina la dokta Samia na si vinginevyo.
Hata mimi sijaelewa madhumuni mahsusi ya huo usalama wanaouzungumzia maana hiyo kazi ni ya traffic police, uhusika wa NIT ni unakujaje wao wafundishaji wa madereva na TANROADS wajenzi wa barabara
 
Back
Top Bottom