SoC04 Tanzania Ijayo

Tanzania Tuitakayo competition threads

Joseph Nyoni

Member
Joined
Apr 21, 2024
Posts
5
Reaction score
2
TANZANIA IJAYO
Joseph Nyoni

Nikiwa kama mtanzania, napenda kuchangia mambo kadhaa ambayo yatakuja kuinua taifa hili na kufanya liwe na maendeleo makubwa. Endapo mambo haya yatafanyika basi miaka 25 ijayo hatutatembea tena bali tutakuwa katika marathoni ya maendeleo;

Kwanza serikali ishawishi watanzania kufungua makampuni nje ya nchi na makampuni hayo yanunue zaidi bidhaa za Tanzania kwa kuzingatia ubora na kuziuza nchi husika. Yaani serikali izungumze na wafanyabiashara wa kitanzania na kusajili makampuni hayo nchi kama Uingereza, Marekani, Ujerumani, China na nchi nyingine. Na wakiwa huko wanaweza kununua kwa wingi bidhaa nyingi hasa kilimo na zile zitokanazo na misitu kama asali na mbao wakizingatia ubora; kisha kuziuza huko kwani ndizo bidhaa zitokazo kwa wingi nchini. Hii itanyanyua wananchi wengi wa Tanzania kwani wengi hutegemea kilimo na mwishowe itafanya tupate zaidi mitaji ambayo itainua na sekta nyingine nchini.

Pili, taifa liandae mfumo utakaowapokea wahitimu na kuwatengeneza waweze kujitegemea. Yaani kama ni kidato cha nne basi akimaliza shule na kushindwa kufanikiwa kuendelea na masomo basi aende kusoma VETA bure kama ilivyo elimu bure, na huko achague fani aipendayo. Na yule ambaye anaendelea vyuoni anapomaliza tu apokelewe na mfumo ambao utamwendeleza ili aweze kujitegemea, mwishowe taifa litegemee vijana na si vijana kuwa tegemezi ihali wanaweza kujengewa uwezo wa kulitumikia taifa.

Kwa kufanya hivyo tutapunguza wimbi la vijana kutegemea zaidi bodaboda kama moja ya sekta kimbilio ambayo wakati mwingine inadumaza vijana kuwaza zaidi katika sekta nyingine ambazo huenda zikawa msaada zaidi kwa taifa. Kwani vijana hawa wangekuwa na uwanja mpana wangekuwa na vitu vingi mbadala vya kufanya na hata kulitangaza taifa nje ya mipaka yake.

Tatu, kila kata litengwe eneo la kilimo cha umwagiliaji la hekta zisizopungua elfu moja, hii ni kwa kata zote zinazojishughulisha na kilimo. Yaani eneo hilo lifikishiwe miundombinu ya umwagiliaji na watu hao walime mwaka mzima. Kwa kuwa nchi ina kata zaidi ya 3000, na kata nyingi zipo vijijini. Basi taifa linaweza kuwa na hekta 3, 000, 000 za kilimo cha umwagiliaji hivyo kulima mwaka mzima. Mwishowe tukajitengenezea kilimo cha uhakika na si kutegemea mvua, ili wananchi wakodi na kulima. Wananchi wanaweza kukodi eneo hilo watakapo kulima na pesa ipatikanayo iendelee kuboresha miundombinu ya mahali hapo; hili lifanyike kama ilivyofanyika umeme vijijini ili kuyafikia maeneo yote nchini.

Nne, kila kata iwe na kiwanda kimoja cha ushirika na kifanye uzalishaji wa bidhaa ambayo wanachama wa chama hicho cha ushirika wataona inafaa kuizalisha. Tena pawepo na bodi maalum ambayo itahakikisha inasimamia viwanda hivyo vya ushirika. Kufanya hivyo tutawafundisha watu kupenda vya kwetu kwani mteja wa kwanza atakuwa mwanakata husika na pia itaweza kutanua zaidi sekta ya viwanda nchini na kupunguza utegemezi wa kuingiza hata bidhaa ndogo nchini.

Pia tunaweza kuanzisha vituo, na shule za viwanda kila kanda nchini. Bila kujali umri, watu wafundishwe kutengeneza bidhaa za viwandani kwa kutumia wataalamu wa ndani na hata nje ya nchi. Ili kukuza sekta ya viwanda na kupunguza kutegemea zaidi kilimo.

Sita, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ikusanye vijana mbalimbali wenye ubunifu wa kisayansi na teknolojia na kuwakuza kupitia projeti zao mpya hasa za sayansi na teknolojia. Huko wafundishwe kupitia wataalamu mbalimbali ili wakimaliza mafunzo waende mtaani na kugeukia uzalishaji.

Saba, kwakuwa sijawahi kusikia taifa letu lina sera inayohamasisha ongezeko la watu, basi sasa tuhamasishe wananchi wazaliane ili kuongeza soko la ndani, wavumbuzi na nguvu kazi. Siyo siri mataifa mengine yamepiga hatua kupitia idadi kubwa ya watu lakini nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikiaminishwa kuwa na ongezeko kubwa la watu ni tatizo kuliko faida. Tatizo kubwa huwa tunatazama zaidi changamoto na tunasahau kuwa watu wakiwa wengi pia watafanya tupate masoko ya uhakika tena ndani ya nchi yetu; wakati huohuo watanzania wengi watakwenda nje ya nchi ambako wanaweza kuitangaza nchi vizuri katika sekta nyingine kama leo wafanyavyo wanigeria au wachina; wanajulikana hata katika mataifa makubwa kama Marekani, Uingereza kwani wamejazana katika biashara na shughuli nyingi za uchumi kitu kinachoongeza kuwafungulia na kuwaongezea kufungua milango nje ya nchi.

Hivyo kama taifa tujitathimini kwani moja ya sababu ya China kuwa na ongezeko la watu wengi Ni kwamba walipromote sera hiyo, sisi tunaweza hata kupromote kwa kuruhusu binti ambaye yuko nje ya mfumo wa shule kuzaa akiwa na mri wa miaka 16. Kwani wapo wengi huzaa lakini hawapati madhara makubwa cha msingi ni kufuata kanuni za afya ya uzazi, haitoshi tunaweza kutoa huduma bure kwa wazazi na watoto hadi umri wa miaka mitano ili watanzania wengi wasione kikwazo kuwa na watoto wengi.

Nane, kila kanda ya nchi iwe na smart city ( mji unaoongozwa kielekroniki) Yaani kwa kanda ya Kaskazini yaweza ikatengewa eneo lake nje ya mji wa Arusha, Kusini yaweza ikawa Mbeya, Mashariki ni Dar es salaam, na Magharibi yaweza kuwa Tabora au Kigoma na Kanda ya kati ni Dodoma. Hii itawasaidia wataalamu kufanya tafiti na kuwaandaa wananchi wa Tanzania na maendeleo yajayo katika teknolojia. Pia itachochea ubunifu na kukuza utalii wa ndani.

Tisa kuhusu elimu, kuwe na nusu ya muda wa masomo katika siku wanafunzi wajifunze nadharia darasani na nusu ya muda wa masomo inayobaki wanafunzi wafanye mafunzo ya vitendo. Kama haitoshi walimu wafundishe kwa kutumia teknolojia zaidi kuliko mifumo ya zamani waachane na chaki watumie projekta kwani umeme upo kila pembe ya nchi saahizi. Wanafunzi watume kazi zao kwa walimu kwa kutumia email hata kama kwa kutumia smartphone za watu wengine ili kuwaandaa katika mifumo mipya ya mawasiliano na kuwasaidia walimu kwenda katika mbinu za kisasa zaidi za ufundishaji na ujifunzaji.

Kumi tuwe na, sheria kali. Mataifa mengi yaliyoendelea haraka yamesaidiwa pia na sheria kali ambazo nchi hizo ziliamua kutunga na kuzitumia ili watu waheshimu mali za nchi, taratibu, kanuni na hata kuchochea uzalendo. Hivyo hapa kwetu mfumo wa mahakama uboreshwe na hizo sheria ziote meno. Mifumo iweze kudhibiti mali za umma, hiyo itachochea uwajibikaji. Ukiachana na maendeleo ya haraka ya China pia sasahivi kuna taifa la Indonesia ambalo lina kimbia haraka. Moja ya mambo makubwa na ya msingi ni kwasababu Indonesia wameweza kuongeza udhibiti na kuboresha mifumo hasa mfumo wa mahakama. Nasi tukifanya hilo tutapiga hatua mbali kwani pesa zetu zitakwenda zaidi kwenye maendeleo kuliko kuingia mifukoni mwa watu.

Mwandishi: Joseph Nyoni
Simu; +255766875334
Email: superbrainjojo@gmail.com
 
Upvote 2
Soko la mojakwamoja la uhakika. Kama Ghadaffi alivyouza mafuta mojakwa moja ulaya eeeh!
Bonge la idea.


, kila kata iwe na kiwanda kimoja cha ushirika na kifanye uzalishaji wa bidhaa ambayo wanachama wa chama hicho cha ushirika wataona inafaa kuizalisha. Tena pawepo na bodi maalum ambayo itahakikisha inasimamia viwanda hivyo vya ushirika.
Hakika
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…