Tanzania inaendelea ila maendeleo ya baadhi ya watu na viongozi bado

Tanzania inaendelea ila maendeleo ya baadhi ya watu na viongozi bado

Kichpox

JF-Expert Member
Joined
Feb 19, 2017
Posts
361
Reaction score
397
UNDP inaendelea na tafsiri kwamba maendeleo ya watu ni kutanuka kwa machaguo. Uhuru na uwezo ni maeneo yenye tafsiri pana kuliko mahitaji ya lazima. Hapo maana yake ni kwamba maendeleo ya watu hayapimwi kwa kupata yale mahitaji ya lazima, kwa maana ya chakula, mavazi na malazi.


Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kupitia Ripoti ya Maendeleo ya Watu (HDR) ya mwaka, linatafsiri kuwa maendeleo ya watu ni kutanuka kwa uhuru wa watu na uwezo wa kuongoza maisha wanayoyathamini na wawe na sababu ya kuthamini maisha yao.

UNDP inaendelea na tafsiri kwamba maendeleo ya watu ni kutanuka kwa machaguo. Uhuru na uwezo ni maeneo yenye tafsiri pana kuliko mahitaji ya lazima. Hapo maana yake ni kwamba maendeleo ya watu hayapimwi kwa kupata yale mahitaji ya lazima, kwa maana ya chakula, mavazi na malazi.

Turejee tafsiri; maendeleo ya watu ni kutanuka kwa uhuru wa watu (mosi). Watu hao wawe na uwezo wa kuongoza maisha yao (pili). Wawe wanayathamini maisha yao (tatu). Wawe na sababu ya kuona maisha yao yana thamani (nne). Wawe na wigo mpana wa kuchagua kuhusu maisha yao (tano). Mwisho unaona kuwa uhuru na uwezo ni maneno yenye kubeba tafsiri ya jumla.

Tujiulize; je, Watanzania wanaona maisha yao yana thamani? Jawabu la swali hilo linajielekeza kwenye matukio kadhaa ya hivi karibuni ya askari wa jeshi la polisi kujiua mfululizo. Kisha swali linafuata; aliyepewa sababu ya kuyaona maisha yake kuwa yenye thamani anaweza kujiua? Matukio ya watu kujiua ni kipimo cha uwepo wa kundi kubwa la watu ambao hawaoni thamani ya maisha yao.

Maendeleo ya watu ni kielelezo cha watu kujiona wana sababu ya kuishi. Hivyo, kama sababu ya kuishi haijapandikizwa vizuri kwenye baadhi ya makundi, maana yake nchi au jamii ina watu ambao hawajaendelea.

Sababu za kuishi huonekana kwa watu jinsi ambavyo walivyo na matumaini. Nyuso na miili yao inazungumza nini baada ya shughuli za kila siku? Asubuhi panapokucha, nishati za miili zinatoa ari kiasi gani kwa watu kuanza siku? Nyuso zao zipoje kipindi wanapoyaacha makazi yao kuelekea yale maeneo yao ya utafutaji riziki?

Bashasha kazini huchagizwa na mambo matatu; mosi ni mapenzi kwa kazi husika. Pili, kipato. Tatu ni uwezo wa kumudu mahitaji. Mambo mawili hasa huondoa bashasha ya mtu kwenye kazi yake. Kwanza ni kutoipenda kazi yenyewe na kukosa uwezo wa kumudu mahitaji.

Hata kama unapata kipato lakini hakitoshelezi mahitaji, moja kwa moja utapoteza furaha, hali ikiendelea utapoteza matumaini.

Ipo barua ilisambaa ikidaiwa iliandikwa askari polisi, Nelson Mkonda, aliyejiua Tarime, Mara. Kilichoelezwa ni kwamba aligombana na mpenzi wake. Katika ugomvi wao Nelson aliharibu vitu vya ndani ambavyo alivinunua yeye mwenyewe. Baadaye mpenzi wake alimtaka avilipe.

Nelson akawa hana pesa, ikabidi aende kukopa Sh1.5 milioni ambazo alizitumia kununua vitu hivyo. Hata hivyo, baada ya kutafakari akaona inamuuma, kwa nini ameingia deni kulipia vitu ambavyo alivinunua mwenyewe? Uamuzi wake ukawa ni kujiua ili yule mpenzi alipe hizo fedha.

Akaacha maagizo kuwa hata vitu vingine vya ndani vilivyopo kwa pale ambavyo ni vyake, apewe kaka yake.

Kama polisi, yaani mtu mwenye ajira inayoeleweka serikalini anaweza kuona Sh1.5 milioni ni mzigo mkubwa kuubeba, kiasi cha kupoteza matumaini, kukata tamaa, kisha kuona bora kufa, vipi yule asiye na ajira, anayeelemewa na mzigo wa mahitaji kutokana na kuandamwa na majukumu binafsi na familia?

Vigezo vya maendeleo

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika mahubiri yake ya falsafa za maendeleo, alisema ili nchi ipige hatua kimaendeleo inahitaji mambo manne – watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Hapo alikuwa na maana kwamba kukosekana kwa kitu kimoja kati ya hivyo, ni vigumu kupatikana maendeleo ya kweli.

Ardhi Tanzania ipo, kubwa na nzuri kabisa. Watu wanazidi kuongezeka, inakadiriwa hivi sasa wamefika 52 milioni, kutoka 44.9 milioni kutokana na sensa ya 2012. Mjadala hapa ni kama watu wenyewe wanaendelea. Hali ni kugusa uhuru na uwezo wao. Je, wana wigo mpana wa kuchagua? Wanao uhuru wa kutosha na uwezo wa kujichagulia maisha yao?

Kutoka mambo manne ambayo Mwalimu Nyerere aliyaeleza, matatu yanategemea watu moja kwa moja. Watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Ardhi watu wameikuta imeshawekwa na Mungu. Ni wajibu wao kuitunza na kuiendeleza. Utunzaji na uendelezaji wa ardhi unafanywa na watu. Hivyo, maendeleo kwa nafasi kubwa yanahitaji watu ambao wanaendelea.

Siasa safi inaundwa na watu. Uongozi bora hupatikana kwa watu. Viongozi hutokana na watu, pia huchaguliwa na watu. Kwa msingi huo, watu ndiyo kiini cha siasa safi na uongozi bora. Hivyo basi, Mwalimu Nyerere angeweza tu kusema kwamba ili nchi ipate maendeleo inahitaji ardhi, vilevile watu huru na wenye uwezo.

Watu huru na wenye uwezo wataifanya nchi iwe na siasa safi pamoja na uongozi bora. Hata hivyo, siasa safi pia ndiyo hujenga taifa la watu huru na wenye uwezo. Kwa msingi huo, siasa safi ikisimikwa kwenye nchi, itajenga uwezo wa watu, watajiona wapo huru na wanaothamini maisha yao. Siasa safi hutoa sababu nyingi kwa wananchi kuyaona maisha yao ni yenye thamani.

Sasa basi, siasa safi na ujenzi wa watu huru walio na uwezo wa kuyaongoza maisha yao ni mambo yenye kupaswa kuwekewa mkazo ili taifa lifikie maendeleo ya kweli.

Utaona kwamba uongozi bora ndiyo hasa unaweza kusimika siasa bora na kujenga watu. Hivyo, upo wajibu wa watu wenyewe kuona umuhimu wa kuchagua watu wazuri miongoni mwao ambao watasimika au kuendeleza siasa safi na maendeleo ya watu.

Wigo wa kuchagua

Katika tafsiri ya maendeleo ya watu, kipengele kimojawapo ni wigo mpana wa kuchagua. Kuwa na wigo mpana pasipo watu kujiona wapo huru kuchagua hilo ni tatizo. Inatakiwa watu wawe na machaguo mengi. Na katika kuchagua basi kuwepo na hali ya kuheshimiana kwa namna kila mmoja anavyofanya uchaguzi wake.

Mwalimu Nyerere alizungumzia siasa safi. Tafsiri ya siasa, maana yake ni mchakato wa kufanya uamuzi. Kwa mantiki hiyo, siasa safi ni mchakato mzuri wa kufanya uamuzi. Watu wanakuwa na wigo mpana wa kuchagua, wanajisikia huru na wana sababu ya kuthamini mchakato wenyewe.

Tujiulize; miaka 56 baada ya uhuru, miaka 26 tangu kuruhusiwa kwa mara nyingine mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, lakini unafanyika uchaguzi, wagombea wengine wanaondolewa kwa hoja kwamba wamekosa sifa, kisha mmoja anapita bila kupingwa. Je, nchi ina siasa safi? Watu wanaendelea?

Hivi sasa malalamiko ni mengi kutoka vyama vya siasa, kuhusu wagombea wao wa udiwani katika kata mbalimbali kuondolewa kwenye mchakato kwa maelezo kwamba hawana sifa. Uchaguzi mdogo wa udiwani unafanyika kujaza kata 77 zilizo wazi na jimbo la Buyungu ambalo aliyekuwa mbunge wake, Kasuku Bilago (Chadema) alifariki dunia Mei 26, mwaka huu. Uchaguzi huo utafanyika Agosti 12, mwaka huu.

Kitendo cha kuwepo na madiwani kadhaa wenye kupita bila kupingwa baada ya washindani wao kuenguliwa, ni kuonyesha namna ambavyo maendeleo ya watu ni suala ambalo bado halijafikiwa.

Iwe hoja za viongozi wa vyama ambavyo wagombea wao wamekatwa ni sahihi au ukatwaji wa wagombea umekidhi vigezo na masharti ya kisheria, jawabu linaangukia kwamba maendeleo ya watu bado sana.

Je, nchi mpaka leo ina wasimamizi wa uchaguzi au mamlaka za uchaguzi zina watu ambao wanapendelea chama fulani? Kweli miaka 26 tangu mfumo wa vyama vingi uruhusiwe, viongozi wa vyama bado wanateua wagombea ambao hawakidhi sifa za kugombea uongozi? Kwamba wateuliwa hawajui utaratibu wa kuapa mpaka kutenguliwa? Je, hakimu akikataa kumwapisha mtu kuna njia nyingine mbadala? Maswali yote hayo yanatuleta kwenye kukiri kuwa maendeleo ya watu bado hayajafikiwa.

Malalamiko mengi kila zinapofika nyakati za uchaguzi, maana yake hakujawa na maendeleo ya kisiasa. Hivyo hatujawa na siasa safi. Na kwa vile mahitaji ya siasa safi ni watu huru na wenye uwezo, unapata jibu kwamba kuna shida ya watu sahihi ili kujenga mfumo mzuri wa kufanya uamuzi.

Mwisho unabaini kwamba siasa za nchi zinakosa viongozi wenye maendeleo mazuri kisiasa ili kuruhusu mbegu ya siasa safi kuchipuka.

By Luqman Maloto
 
Back
Top Bottom