Tanzania ipo njia panda

Tanzania ipo njia panda

kipanga85

JF-Expert Member
Joined
Apr 15, 2024
Posts
2,459
Reaction score
6,466
Maoni

Tanzania iko kwenye njia panda ya kuogofya

Kuna dalili za kutia doa ahadi za Rais Samia – baada ya kuingiamadarakani, kuwa atahakikisha Tanzania inaheshimu misingi yahaki na kuimarisha demokrasia. Hata hivyo,bado hajachelewa kutimiza aliyoahidi, licha ya nchi kugubikwa na matukio yakuchafua taswira ya uongozi wake.

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifaya Vijana, mwezi uliopita, baadhi ya vyama vya siasa vilipanga kuitumia siku hiyo kufanya mikutano na maandamano, kama ambavyo imekuwa ikifanyika kila mwaka.

Pamoja na vyama vyote vikuu vilivyoomba kuadhimisha siku hiyo kwa njia mbalimbali kuruhusiwa, chama kikuu cha upinzani - Chadema, kilizuiwa kufanya mikutano na hata maandamano yaliyopangwa kufanyika Jiji la Mbeya na maeneo mengine.

Muda mfupi kabla ya maadhimisho hayo kuanza, Jeshi la Polisi lilipiga marufuku kufanyika kwa mikusanyiko yeyote na kukamata viongozi wa juu wa Chadema waliokuwa Mbeya na maeneo mengine walikokuwa wamepanga kuadhimisha siku hiyo.

Jeshi la Polisi lilieleza kuwa lilizuia kufanyika kwa mikutano na maandamano ya wafuasi wa Chadema baada ya “kupata taarifa za kiintelijensia” kuwa chama hicho kilipanga kuhamasisha wafuasi wake kufanya fujo.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadh Juma Hajji, alisema jeshi lake litafanya kila linalowezekana kuzuia fujo kwa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.

Pia soma: Ally Mohamed Kibao auawa na mwili kutelekezwa Ununio ukiwa umeharibika sana

Alidai kauli ya kiongozi mmoja wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha); kwamba wafuasi wa CHADEMA na vijana wote, “waache uteja na wajifunze kudai haki
kama wenzao wa Kenya.”

Ikumbukwe kuwa nchini Kenya, kwa miezi kadhaa, vijana waliitisha maandamano makubwa maeneo mengi ya nchi hiyo wakilaani na kupinga kuwepo kwa ugumu wa maisha, kuongezwa kwa kodi na kuminywa kwa demokrasia.

Kufuatia maandamano hayo, serikali ilitumia vyombo vya usalama kuzuia, lakini ilishindikana – hata baada ya kuua raia. Kuendelea kwa shinikizo kutoka kwa vijana hao, maarufu kwa jina la Gen-Z, hatimaye kumlazimisha Rais William Ruto kuvunja baraza la mawaziri na kuweka zuio la ongezeko la kodi.

Ni kutokana na hofu hiyo, kwambakunaweza kutokea machafuko, hasa katika maeneo ya Dar es Salaam, Zanzibar na Mbeya, Serikali ya Tanzania ilipiga marufuku mikutano ya Chadema na kuwakamata zaidi ya vijana 500 wengi wakiwa wafuasi wa Chadema walipokuwa wakijaribu kukusanyika kinyume na marufuku hiyo.

Katika kamatakamata hiyo, Jeshi la Polisi pia liliwashikilia baadhi ya viongozi wakuu wa Chadema akiwemo Katibu Mkuu, John Mnyika, Makamu Mwenyekiti Taifa, Tundu Lissu na Mjumbe wa Kamati Kuu, Joseph Mbilinyi.

Viongozi hao walidai kudhuriwa na kupelekwa katika vituo vya Polisi vya Mbeya, Iringa na Njombe , kabla ya kusafirishwa kwa magari kuelekea Dar esSalaam.

Matukio hayo yanayominya demokrasia, uhuru na haki za kikatiba, yanakumbusha utawala wa “kibabe” wa Rais (awamu ya tano), John Magufuli, ambaye aliamua kuzuia kufanyika kwa maandamano na mikutano ya vyama vya siasa; kwa waliohoji ama kukaidi msimamo huo wa kauli ya Rais Magufuli, walikamatwa, kuteswa na kujeruhiwa, kama ilivyotokea kwa Tundu Lissu, ambaye alinusurikia kifo baada ya kupigwa risasi 16.

Baada ya Rais Magufuli kufariki dunia mwaka 2021, mrithi wake, Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye awali aliahidi kuwa tofauti na mtangulizi wake, akaanza uongozi kwa kuruhusu kuwepo uhuru wa vyombo vya habari na kufungulia magazeti yaliyofungiwa. Januari 2023, alibatilisha marufuku ya Magufuli dhidi ya mikutano ya vyama vya upinzani.

Hii ilimaanisha kuwa vyama vya siasa sasa vikawa na haki iliyopokwa - ya kufanya mikutano na maandamano kwa uhuru, baada ya miaka sita ya marufuku, kuanzia mwaka 2016.

Kutokana na msimamo wa Rais Samia na kuanza kutekeleza baadhi ya ahadi zake, Watanzania na jumuia ya kimataifa “walimwaga sifa” kwa kiongozi huyo wa Tanzania, ambapo pia mazingira mazuri ya biashara yalivutia kiasi kikubwa cha wawekezaji.

Screenshot 2024-09-08 115057.png

Rais Samia alionekana kuwa tofauti na mtangulizi wake, Rais Magufuli ambaye alifika mahali akapingana na ukweli wa kisayansi kuhusu maambukizi ya UVIKO-19. Badala yake, aliunda timu ya wataalamu walioongoza mabadiliko ya sera juu ya janga hilo.

Katika uongozi wa Rais Samia, alianza pia kwa kutangaza mageuzi kwenye masuala ya haki kwa kuunda Tume ya Haki Jinai na kikosi kazi juu ya demokrasia na kuahidi kurejesha misingi ya demokrasia.
Mapema mwaka huu, gazeti maarufu la The Economist, liliandika; “kwa hakika, sasa Tanzania ina kiwango kidogo cha uonevu kwa raia wake na imepunguza kwa kiasi kikubwa mambo yaliyokuwa yakiitia aibu kwa kuminya haki.”

Uamuzi hatarishi

Wakati Tanzania inajiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba, mwaka huu na uchaguzi mkuu wa kuwapata rais, wabunge na madiwani, uliopangwa kufanyika mwaka kesho, uongozi wa Rais Samia unaonekana kurejea kwenye baadhi ya mienendo hatarishi ya mtangulizi wake, Rais Magufuli.

Baadhi ya matukio mabaya ambayo yanaonekana kumelea kwa sasa ni pamoja na kutekwa, kupotea kwa watu na kuzuia haki ya kukusayika na kufanya siasa; mfano mzuri ikiwa ni kupigwa marufuku kwa mikutano ya Chadema hivi karibuni.

Mbali na matukio hayo, kauli ya hivi karibuni ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad, inaashiria kurejea kwa ubabe wa dola dhidi ya vyama vya siasa.

Kauli yake kwamba jeshi hilo litafuatilia kwa karibu kauli za wanasiasa wote wanapokuwa majukwaani ili kubaini endapo zina viashiria vya kuchochea wananchi kuchukia serikali limeibua maswali kuliko majibu.

Hakika kauli hiyo inabeba viashiria kuvitisha vyama vya siasa na viongozi wao ili wasizungumze, jambo ambalo linakinzana na maono ya Rais Samia wakati akiingia madarakani.

Kauli hii inaonekana kuelekezwa kwa viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, ambao wamekuwa wakikemea rushwa na kutuhumu kuwepo kwa mipango michafu ya kuvuruga uchaguzi inayofanywa na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), hata hivyo, chama hicho kimekuwa kikikanusha madai ya ACT.

Kuwepo kwa matukio ya kupotea na kuteswa kwa wanachama wa vyama vya upinzani na wakosoaji wa mienendo ya serikali, ni hatua nyingine inayoongeza shaka kwenye ahadi za Rais Samia.

Julai, mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani Tanga, lilithibitisha kumshikilia Kombo Mbwana, kiongozi wa Chadema wa wilaya – kwa siku 30, baada ya kutoweka. Pia viongozi wengine wawili wa Chadema; Dioniz Kipanya kutoka Rukwa na Deusdedith Soka kutoka Temeke, Dar es Salaam - wametoweka hadi leo, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja, bila taarifa yoyote kutoka kwa mamlaka.

Sambamba na matukio hayo, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kilitoa orodha ya watu 83, wakiwemo Mbwana na Kipanya, ambao walitoweka katika mazingira ya kutatanisha.

“Jeshi la Polisi limekuwa likikanusha mara kwa mara kutokea kwa matukio hayo, lakini baadaye inabainika kuwa matukio hayo ni kweli, halafu kitu cha kushangaza, Polisi inakamata raia wema wanaoripoti matukio haya, wakiwatuhumu kwa kueneza habari za uongo kwenye mitandao,” kilisema chama cha wanasheria hao.

Mwelekeo wa hatari

Kuwepo kwa idadi inayoongezeka ya matukio maovu – yaliyozoeleka wakati wa utawala wa Magufuli, na sasa yakirejea, kunafanya watu washindwe kuona tofauti kubwa kati yake na wakati wa sasa wa uongozi wa Rais Samia.

Kibaya zaidi, kurejeshwa madarakani kwa marafiki wa Magufuli, ambao awali Rais Samia “aliwaweka pembeni,” nako kunajenga picha kuwa huenda Tanzania inaelekea “kulekule” kwenye mazingira ya uonevu, kuminywa kwa demokrasia, kuteswa na kutofuatwa kwa katiba.

Kurejeshwa kwa Paul Makonda kwenye nafasi ya uongozi ndani ya CCM na baadaye kupelekwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, hakujaondoa makovu aliyoacha kwa kuumiza watu wakati akifanya kazi chini ya Magufuli.

Makonda akiwa kiongozi wa Dar es Salaam, alidaiwa kuunda vikosi kadhaa vilivyokuwa na malengo maovu ya kushambulia watu kwa madai ambayo mengi hayakuweza kuthibitishwa.

Njia zilizokuwa zikitumika kufuatilia watu zilikuwa zikionea, kutesa na hata kuminya haki ya kuishi kwa wengine.

Kuibuka kwa matukio haya ya hovyo yanachafua taswira ya nchi na sifa za Rais Samia, kwa wananchi wake na hata mbele ya jumuia ya kimataifa. Hata hivyo, bado Rais Samia hajachelewa.

Anao muda wa kureke na kukomesha mambo hayo ili kuendelea kujenga imani na matamanio aliyoahidi wakati akiingia madarakani.

Kitu kingine kikubwa kinachoweza kujenga imani zaidi, ni kwa Rais Samia kutekeleza mambo muhimu yanayopendekezwa na tume za mageuzi ya haki jinai na mageuzi ya kidemokrasia - ambayo aliyaasisi mwenyewe.

Endapo mambo mengi yatatekelezwa kutoka kwenye mapendekezo ya tume alizounda Rais Samia, uhakika ni kwamba kutakuwa na mabadiliko makubwa kwa viongozi kutekeleza majukumu yao, kuimarishwa kwa demokrasia na kutetea misingi ya haki za binadamu.

Pamoja na kwamba kuridhia kutekelezwa kwa mageuzi hayo kutamfanya asionekane “kiongozi wa maana sana” ndani ya chama chake - CCM, lakini Rais Samia atakuwa ameacha alama katika uongozi uliotukuka kwa Tanzania na kuheshimiwa kuwa kiongozi wa mageuzi makubwa.

Akiridhia na kusimamia mambo hayo, Rais Samia atajijengea sifa binafsi na pekee ya kuwa kiongozi aliyeamua kufuata misingi ya haki na demokrasia kwa lengo la kuwa na Tanzania yenye amani, utulivu wa kweli na maendeleo jumuishi.
 
Back
Top Bottom