SoC02 Tanzania kuwa kama Singapore inawezekana endapo itafanya haya...

SoC02 Tanzania kuwa kama Singapore inawezekana endapo itafanya haya...

Stories of Change - 2022 Competition

Mirrey Nchimbi

New Member
Joined
Jul 19, 2022
Posts
3
Reaction score
5
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...!

Ni kawaida kusikia Tanzania kufananishwa na nchi mbalimbali barani Afrika hasa katika nyaja za kiuchumi, kisiasa, kijamii na utamaduni. Na tumeziona nchi za Magharibi kama mfano katika nyanja hizo na muda mwingine imekuwa ngumu kujilinganisha nao. Hii ni kwa sababu nchi hizo za Magharibi zimepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika sekta mbalimbali. Tanzania haipo pabaya sana, kama tunavyofikiria, mfumo wa elimu ukifanyiwa maboresho kadhaa utafanana na kuwa na mchango chanya kama ule wa Singapore.

Singapore ni moja ya nchi duniani inayosifika kwa mfumo bora wa elimu. Kabla ya Singapore kufikia mafanikio haya, mfumo wake wa elimu ulikuwa unafanana kabisa na mfumo wa Tanzania hivi sasa. Singapore ni mfano bora kwani historia zetu zinashabihiana; nchi zote mbili zilitawaliwa na Uingereza, Singapore ilipata Uhuru mwaka 1965 na Tanganyika mwaka 1961, huku Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulikua mwaka 1964.

Yafuatayo ni mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa na Serikali ya Singapore ili kuboresha mfumo wa elimu nchini humo, ambayo yakichukuliwa kwa uzito ndio majibu ya changamoto zinazokabili sekta ya elimu Tanzania;

Elimu na Maisha; Baada ya kupata uhuru (1965), elimu iliyotolewa nchini Singapore ilikuwa na lengo la kutoa wafanyakazi wenye ujuzi mbalimbali ili kwendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya viwanda duniani. Hivyo basi, elimu rasmi ilitolewa ikiambatana na elimu ya ufundi. Lakini pia lugha ya kiingereza ilipewa kipaumbele kama lugha ya kwanza ili kuongeza nafasi ya wananchi wao kuajiriwa katika nchi mbalimbali duniani kwani Kiingereza ni lugha ya Kimataifa hivyo kusaidia wahitimu kutoka Singapore kuwa na nafasi kubwa kuajiriwa katika nchi za magharibi kulinganisha na nchi nyingine zilizoko bara la Asia. Tanzania pia, mnamo mwaka 1967 ulianzisha mfumo wa elimu ya kujitegemea. Tofauti iliopo ni kuwa lengo la elimu ya kujitegemea ni kutumia rasilimali zilizopo nchini kuikomboa nchi na kuboresha maisha ya Mtanzania mmoja mmoja. Elimu hiyo haikulenga kuteka soko la kimataifa kama ile ya Singapore.

Elimu na ubora wa kazi; Baadae ikaja kuonekana kuwa, mfumo ule wa elimu uliweza kuzalisha wafanyakazi katika nyanja mbalimbali lakini ubora wa ufanyaji kazi wao ulikua hauridhishi. Hivyo Serikali ya Singapore, ikaboresha tena mfumo wa elimu nchini humo kwa lengo la kuongeza ufanisi wa wafanyakazi waliokuwepo nchini humo, lakini pia kuhakikisha kuwa wanafunzi walioko shuleni, vyuo vikuu na vyuo vya ufundi wanahitimu wakiwa na uwezo wa kufanya kazi kikamilifu pale watakapoajiriwa au kujiajiri. Kabla ya maboresho haya kufanyika katika mfumo wa elimu ya Singapore ilionekana kuwa wafanyakazi nchini humo hawakuweza kushindana katika soko la ajira, na wafanyakazi wa mataifa mengine kama Amerika na Japan.

Maboresho yalijikita kuongeza ubora wa elimu ya ufundi na viwanda, lakini pia kusaidia wanafunzi ambao kwa namna moja au nyingine walishindwa kufaulu vizuri ili kuweza kuingia katika soko la ajira au kujiajiri. Tanzania pia ina programu mbalimbali zinazoweza kuambatana na semina elekezi kwa lengo la kutoa ujuzi fulani kwa wafanyakazi hao. Lakini hakuna mpango wa kudumu kama ule wa Singapore kuhakikisha kuwa hata wanafunzi ambao bado hawajaingia katika soko la ajira kuwa na ufanisi katika kazi zao lakini kuwawezesha kushindana kimataifa. Kwani Tanzania inashindana kimataifa katika la soko la ajira na nchi mbalimbali katika jumuiya ya Afrika mashariki , Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Umoja wa nchi za Afrika na duniani kwa ujumla. Ni muda muafaka kwa Tanzania kutengeneza kizazi ambacho kitakuwa kimelimika na wabunifu kama ilivyo Singapore.

Elimu kama mfumo wa Maisha; Badiliko hili lililofanywa na Singapore, ni mpango wa kudumu wa kufanya elimu kuwa mfumo wa maisha wa kila siku ya watu wake wa rika zote. Kwa kuendeleza mikakati ya kuongeza ujuzi, ubunifu na uvumbuzi katika nyanja mbalimbali hasa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kiujumla. Singapore imeweza hili, kwa kupunguza msisitizo na mkazo kwenye mitihani ya kuandika shuleni na katika taasisi mbalimbali za kujifunzia kama vyuo vya ufundi na vyuo vikuu. Na kuweka mazingira madhubuti ya kupima uelewa wa wanafunzi wao kwa vitendo, lakini kumsaidia mwanafunzi kufurahia na kufanya kwa majaribio vile anvyofundishwa darasani. Hivyo kuongeza chachu ya kusoma zaidi , kuwa wabunifu na kuvumbua stadi mbalimbali zinazohusiana na masomo husika. Msisitizo huu, haujajikita kwenye masomo rasmi pekee. Sekta kama michezo, saana na mambo mbalimbali ya kijamii yanapewa kipaumbele.

Hivyo kuongeza wigo wa ajira binafsi kupelekea kupunguza wimbi la kukosa ajira kwa vijana nchini Singapore. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakitu cha kujifunza hapa ili kuboresha mfumo wa elimu utakaopelekea matokeo chanya ikiwemo kupunguza wimbi la vijana kukosa ajira, kuwa na kizazi kinachotambua umuhimu wa elimu katika maisha, na sio umuhimu wa vyeti tu.

Nini kifanyike Tanzania iwe kama Singapore?
Kuboresha mitaala ya masomo katika shule za awali na msingi. Elimu ya awali “ chekechea” kama tulivyozea kusema ni muhimu sana katika kuweka msingi mzuri wa kielimu kwa watoto wanaoanza shule. Waswahili wanasema “Samaki mkunje, angali mbichi” , mitaala ya masomo katika shule za awali na msingi zimuandae mtoto wa Kitanzania kupenda shule na kutambua umuhimu wa elimu kama hazina yake binafsi na taifa zima na sio kama nyenzo ya ajira rasmi maana vijana wengi wanahitimu vyuo na vyuo vikuu wakiwa na mategemeo ya ajira rasmi na sio kutumia elimu na ujuzi katika kuletea mabadiliko chanya katika jamii zao, na kuwaletea faida kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Lakini pia, kuhakikisha viwango na ujuzi wa walimu na wakufunzi katika taasisi mbalimbali za elimu. Ubora wa elimu inayotolewa shuleni na vyuoni una uhusiano wa karibu na uwezo wa walimu husika. Ubora wa walimu usipimwe tu kwa kuangalia ufaulu wao lakini namna wanavyowasilisha mada za masomo kwa wanafunzi. Kuwajengea uwezo walimu, kuwasilisha mada kwa vitendo hasa katika masomo ya Sayansi na Teknolojia.
Kuona Sanaa kama fursa.

Serikali, kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuandaa mpango maalumu wa kuratibu na kupima uwezo wa vijana kwenye sekta hii ili kuweza kuongeza nafasi za ajira na kujiari.

Kusema Tanzania kama uko Singapore, inawezekana!
 
Upvote 6
Ni nzuri lkn unazani serikali yetu inakosa kuhusu huduma y elimu kwa jamii?
 
Ni nzuri lkn unazani serikali yetu inakosa kuhusu huduma y elimu kW jamii?
Ni wajibu wa serikali kuhakikisha watu wake wanapata Elimu Bora. Haikosei lakini kufanya maboresho kwenye sekta ya Elimu kutasaidia jamii na taifa kiujumla.
 
Ni nzuri lkn unazani serikali yetu inakosa kuhusu huduma y elimu kW
Ni wajibu wa serikali kuhakikisha watu wake wanapata Elimu Bora. Haikosei lakini kufanya maboresho kwenye sekta ya Elimu kutasaidia jamii na taifa kiujumla.
hapana ukisema “Haikosei” ili kumridhisha mtu unakosea. Serikali inakosea sehemu nyingi sana katika elimu. Kwanza mfumo wanaotumia umewafanya wanafunzi wengi wasome kufaulu na sio kuelewa na hii ni kwa sababu hakuna elimu kubwa ya practical kila kitu tunafundishwa in theory. Ingekua mtu anaanza kutumia computer kuanzia primary unadhani kungekua na ujinga mkubwa kama uliopo? Sio tu computer kuna kutumia maabara imagine tunakuja kutumia maabara tuko form 3 afu at the same time tunategemewa kufaulu physics, chemistry na biology..tunaanzia wap kuyafaulu mambo mageni ivi hatukupewa ata introduction nayo ya practical ata kidogo uko primary tunakua hatuna passion hata wanaofaulu ni kwakuhangaika sana kuelewa. Ubongo wa mtoto uko vizur kuelewa na kukumbuka vitu hivyo tungeanza kufundishwa ivi vitu tangia primary huezi kujenga nyumba bila msingi serikali ingeeka focus yake kwa shule za msingi zaidi ya iliyoweka huko ndo kuna determine future. Imagine mtu yuko chuo halafu hajui kutumia computer na ni kitu ambacho tumekua comfortable nacho sana. Sio hayo tu kuna swala la kudrop out wanafunzi wana drop out PRIMARY jamn kweli, wenzetu wana drop out highschool Yani inabidi serikali ijiulize kwann elimu ni bure lakin bado wanafunzi wana drop out, ni tatizo laki saikolojia zaidi ya kifedha yani nna mambo mengi sana yakuongelea kuhusu elimu lakin wacha niishie hapa ila jua yakwamba nakusupport na kura yang unayo 👍🏾👍🏾👍🏾
 
Asante kwa kuniunga mkono. Nakubaliana na wewe Kuna madhaifu mengi katika mfumo wetu wa Elimu. Na kwenye andiko , nililoandika nimegusia umuhimu wa kuboresha elimu ya awali yaani chekechea pamoja na Elimu ya msingi. Kuboresha elimu za juu na kuacha ya awali ni kukata matawi na kuacha mizizi ya tatizo.
Jukwaa hili liwe chachu Kwa serikali na wadau mbalimbali wa Elimu kuchukua mawazo chanya na kuboresha sekta ya Elimu.
 
Back
Top Bottom