Ojuolegbha
JF-Expert Member
- Sep 6, 2020
- 1,278
- 797
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Said Yakubu amekutana na kufanya mazunguzo na Mhe. Youssoufa Mohamed Ali, Katibu wa Rais Mwenye Dhamana ya Wizara ya Ulinzi nchini Comoro. Lengo la mazungumzo hayo ilikuwa ni kujitambulisha na kugusia mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mhe. Youssoufa Mohamed Ali amegusia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Comoro na Tanzania ili kuwawezesha wananchi kunufaika na historia ya ushirikiano mwema uliopo baina ya nchi mbili hizi. Alibainisha kwamba Comoro ina kila sababu ya kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta za ujenzi wa miundombinu, barabara, nyumba za gharama nafuu, shule na vituo vya afya.
Amebainisha pia kuwa Comoro inakabiliwa na changamoto ya usafiri wa anga wa ndani ya nchi. Hivyo amekaribisha sekta binafsi kutoka nchini Tanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya ujenzi, kuwekeza katika usafiri wa anga kwa safari za ndani pamoja na kuanzisha safari kati ya nchi hiyo na nchi jirani ikiwemo Madagascar, Mauritius, na Seychelles.
Kadhalika, alibainisha kuwa Tanzania ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula nchini Comoro iwapo nchi hiyo itaweka mkakati wa kuuza mchele nchini kwake.
Naye Mhe. Balozi Saidi Yakubu amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. amebainisha kuwa Ofisi yake itaendelea kushirikiana na Mamlaka zote nchini humo kuhakikisha malengo ya ushirikiano uliopo yanatimizwa.
Akigusia mwito kwa sekta binafsi kutoka nchini Tanzania kushiriki katika harakati za maendeleo nchini humo, Mhe. Balozi Yakubu amebainisha kuwa wafanyabiashara wa Tanzania wameanza kuiangalia Comoro. Amejulisha kuwa Ofisi yake iliratibu Kongamano la Biashara na Uwekezaji katika sekta za Kilimo, Mifugo na Usafirishaji tarehe 21 Agosti, 2024. Kongamano hilo limepelekea Kampuni mbalimbali kutembelea nchi hiyo ili kutafuta fursa za kibiashara.
Mwisho alitumia fursa hiyo kubainisha kuwa Shirika la Ndege la Tanzania limepata kibali cha kufanya safari za ndege ya mzigo kati ya Comoro na Tanzania kwa kutumia ndege yake yenye uwezo wa kubeba tani 54. Hivyo Shirika hilo lipo tayari kutoa huduma.
Soma Pia: Comoro na Tanzania kushirikiana katika kilimo na uvuvi
Alijulisha pia Kampuni ya Precision inatarajia kuongeza safari kati ya Tanzania na Comoro ndani ya mwezi Oktoba, 2024. Hatua hiyo itafanya kuwa na usafiri wa uhakika kati ya nchi mbili hzi siku zote za wiki, na kuongezeka safari za ndani. Aidha, Kampuni hiyo inakamilisha upembuzi yakinifu iweze kuanza safari za kwenda kisiwa cha Moheli, pamoja na baadae kuanzisha Kampuni ya Precision Comoro.