Utangulizi
Kwenye ukuaji wa taifa lolote lile duniani, linahitaji kuwa na viongozi wenye maono mapana kwa taifa lao. Pia kuwa na sera dhabiti kwa taifa lao ni muhimu, mfano kwenye elimu, afya na nishati.Elimu
Elimu ndio msingi mkubwa kwa ukuaji wa taifa lolote. Ili taifa liweze kukua kiuchumi, haina budi kuwa na sera dhabiti juu ya elimu kuanzia msingi hadi vyuo vikuu isiyo badilika badilika. Ili tuandae Tanzania ya miaka 25 ijayo, hatuna budi kufanya mapinduzi makubwa sana kwenye hii sekta ya elimu, hasa kuandaa mitaala ambayo inaanda watalamu mahiri kwa taifa.Changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya elimu Tanzania ni:
- Uhaba wa walimu wenye sifa - Hasa kwenye maeneo ya vijijini, ukosefu wa walimu bora na wenye sifa husababisha wanafunzi kufundishwa na walimu wasio na sifa/mafunzo stahili. Ili kuzalisha watalamu wazuri, inatubidi taifa liwekeze zaidi kuandaa walimu mahiri ambao wataweza kuzalisha wataalam mahiri.
- Miundombinu - Katika ufundishaji na ufunzaji, yatupasa kuwa na miundombinu rafiki kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa ili walimu wawe na morali ya juu wakiwa wanaandaa watalamu wa miaka 25 ijayo.
- Mitaala - Mitaala imekuwa na changamoto kubwa sana hapa nchini ya kubadilika badilika. Ili kuwa na mtaala usio badilika kila mara, yatupasa tuandae mtaala ambao utachukua muda mrefu kubadilika, hata baada ya miaka 20 tunafanya marekebisho kuendana na kasi ya dunia. Pia, mitaala iwe rafiki kufundisha wanafunzi elimu bora ya kujitegemea kuanzia chini hadi juu, kuliko mitaala ya sasa ya kukariri kuja kujibia mitihani. Tukiwa na mitaala bora, tutapunguza kwa kiasi changamoto ya ajira.
Afya
Taifa lolote lile ili liweze kukua kiuchumi, ni lazima liwe na sera imara kwenye sekta ya afya kwa watu wake. Sekta hii inakabiliwa na changamoto nyingi sana hasa kwa mataifa yanayoendelea kukua kiuchumi. Yatupasa kufanya mapinduzi makubwa kwenye hii sekta kwa baadhi ya maeneo:- Vifaa tiba - Kuwa na vifaa vinavyotosheleza kwenye hospitali zote kuanzia zahanati za vijiji ili kila mwananchi akiwa anahitaji huduma inapatikana kwa urahisi, sio kwenda kununua dawa kwenye maduka ya nje.
- Miundombinu - Kuwa na miundombinu rafiki na ya kutosheleza kwa wananchi kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa ili huduma zinazotolewa ziwafikie wananchi pamoja na watoa huduma kwa ufanisi.
- Matibabu - Ili jamii ipate huduma bora na inayostahili, inahitajika sera bora kwa taifa ambayo kila mwananchi anaweza kumudu gharama za matibabu hasa kwa watu wanaoishi vijijini/mazingira magumu waweze kupata huduma bora.
- Madaktari/Wauguzi - Kuandaa madaktari na wauguzi mahiri na ambao watakuwa na morali ya kutoa huduma inayostahili kwa jamii inayowazunguka bila kujali rika wala kabila.
Nishati
Ili taifa liweze kukua kiuchumi, linahitaji kuwa na nishati inayotosheleza kwa matumizi ya viwandani na majumbani. Sera mbovu ndio changamoto kubwa hasa kwa taifa letu ambalo limejaliwa kuwa na vyanzo tofauti vya kuzalisha nishati ya umeme hasa maji, upepo, gesi, mafuta na jua.Ili kuandaa Tanzania ya miaka 25 ijayo, hatuna budi kama taifa kuandaa sera nzuri hasa ya kutokutegemea chanzo kimoja cha nishati, ambapo asilimia kubwa ya nishati hapa nchini inatokana na maji. Tugeukie upande mwingine wa kuzalisha nishati, mfano kuna baadhi ya maeneo hapa nchini yana uwezo mkubwa kuzalisha nishati ya umeme kutoka kwenye upepo au jua. Hii itasaidia kutatua kidogo changamoto ya umeme na kuweza kuzalisha umeme kwa njia ya upepo au jua na kuunganisha kwenye gridi ya taifa.
Ili maeneo mengi ya nchi hasa vijijini yaweze kuunganishiwa umeme kwa maendeleo yao na taifa, maana asilimia kubwa ya malighafi yanatokea vijijini. Hivyo, pakiwa na umeme wa uhakika wataweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo.
Upvote
4