SoC04 Tanzania tuitakayo isiwe mfano wa mpishi apikae chakula chake kisha asikile mwenyewe aenda kula cha wengine

SoC04 Tanzania tuitakayo isiwe mfano wa mpishi apikae chakula chake kisha asikile mwenyewe aenda kula cha wengine

Tanzania Tuitakayo competition threads

The Lost Boy

JF-Expert Member
Joined
Nov 24, 2020
Posts
248
Reaction score
311
Namuomba Mwenyezi Mungu ajaalie andiko hili liwe lenye manufaa kwa Nchi yangu na kwa kila atakayebahatika kulisoma.

Ama, kwakuwa ni mpenzi wa lugha asharafu ya kiswahili na pia ni Mtunzi wa mashairi, andiko langu ningependelea nilifungue kwa utangulizi wa shairi langu, lenye kichwa MPISHI GWIJI. shairi hili nalo ni sehemu ya andiko langu.

Ewe gwiji wa magwiji, mtopezi wa mapishi
Ulokirithi kipaji, kwa babu zako wakushi
Nimekuja kukuhoji, unijibu kwa utashi
YAWAJE MPISHI GWIJI, USIONJE LAKO PISHI?!

Kwenye hiki kitongoji, sifa zako kama moshi
Wasifiwa na walaji, kupika hubahatishi
Hata upikapo uji, utamu wake hawishi
YAWAJE MPISHI GWIJI, USIONJE LAKO PISHI?!

Ndiwesi mvamiaji, hunao ubabaishi
Mjuzi kwa uokaji, pishi lako lashawishi
Huzidishi nayo maji, yakaleta utoteshi
YAWAJE MPISHI GWIJI, USIONJE LAKO PISHI?!

Pindi kipika soseji, walao hawabakishi
Nazo chapati za maji, kinywani hazikifishi
Ajabu muandaaji, waenda kula kwa Shishi
YAWAJE MPISHI GWIJI, USIONJE LAKO PISHI?!

Nipe majibu siraji, nitokwe utatanishi
Nami nikuvike taji, lilodaliziwa nakshi
Nikari kuwa umbuji, kwa ulimi na mandishi
YAWAJE MPISHI GWIJI, USIONJE LAKO PISHI?!

************************************
Tanzania yetu leo inajifakharisha kuwa na madaktari, wafamasia, wauguzi, wataalamu wa maabara, na wataalamu wa miozi ambao iliyowasomesha yenyewe.

inajipiga kifua kwa uwepo wamainjia wa barabara, majengo, viwanda, makanika, kemikali, umeme n.k. ambao wengi waliosomeshwa kwenye vyuo vya ndani tena kwa kuwapa mikopo asilimia mia.

inajitamba kuwa na wana wataalamu wafani nyingine ambao hata wapo waliodiriki kupelekwa nje za nchi kwenda kupata ujuzi zaidi. Huko walipelekwa kwa kodi za walala hoi.

Ajabu ni kuwa, licha ya kuwa na hazina ya wajuzi wengi, hutopo tayari kuwatumia kwa manufaa ya nchi. Ama niseme kama nikutumika basi sio vile ilipaswa ukilinganisha na uhitajikaji wao kwa jamii, pia uwekezaji tulioweka kwao.

Nastaajaabu nionapo viongozi wetu hukimbilia kutibiwa nje za nchi au vituo vya afya binafsi pale wanapougua, ilhali vipo vituo vya afya wanavyonadi wamejenga wao. Kwanini wasiliende kutibiwa huko?

Leo miradi mikubwa ya serikali kama vile, ujenzi wa barabara, madaraja, mabwawa, reli na majengo tunaona tenda anapewa mchina au mturuki. Yani hata niandikavyo hivi kuna wachina wanajenga barabara ya mtaani kwetu. Mainjia wetu wakitanzania tuliosomesha wameugeuzwa kuwa Saidia-fundi inakasirisha sana!

AJABU, UNAPIKA PISHI LAKO MWENYEWE, KISHA HUTAKI KULIONJA WENDA KULA PISHI LA MWINGINE?!

MAONO YANGU JUU YA TANZANIA TUITAKAYO MIAKA KWA MIAKA 5- 25 IJAYO.

Kwanza, Tuamini pishi letu-hilo ndio fahari yetu.
Tunaona ni bora leo bila shaka hapo mwanzo hawakuwa hivyo. Walikuwa hatamaniki. Hawakuwa na uzoefu.

Serikali zao ziliwaamini nakuwapa nafasi. Wakaanza kuimarika kidogo kidogo na hatimaye wakawa bora. Mambo yapo hivyo, kama wasemavyo "Practise make you perfect". Kwa tafsiri isiyo rasmi 'kadri utavyozidi kulifanya jambo, ndivyo utalifanya kwa kwa ubora zaidi’.

Tusiwabeza na kuwatweza wajuzi wetu tukaona hawafai mbele ya wengine. Tusifanye wajihisi watoto wakufikia nyumbani kwao wenyewe. Ama ikiwa tutawapuuza kisha wakapata wakuwathamini basi watatukimbia na kwenda wakafaidisha huko bala yetu, kisha tutakuja kusema hawana uzelendo ilihali nchi ndio ya kwanza kufanya usaliti kwa kuamini wageni badala yao.

Tuamini pishi letu ndilo litakalotushibisha na kutunawirisha na wala sio pishi alokujanalo mgeni

Pili. Tuonje chakula chetu kwanza kabla kuwapa wengine wa kile.
Siamini kwamba kweli hatuwezi kujenga nchi yetu wenyewe wakati tuna vijana wengi wenye ujuzi. Sidhani kama nchi za nchi zetu walizijengewa na vijana toka nchi nyingine! Naamin walitumia wajuzi wao wenyewe. Basi na nasi fahari yetu iwe ni kutembea kwenye barabara iliyojengwa na Injinia Mtanzania, shani tumuone mainjinia wetu wakijenga reli na sio tena mturuki.

Vile Viongozi, wetu wawe wa kwanza kupata huduma kwenye ofisi za umma ambapo huko kuna wanataalumu wetu na ndio watawahudumia. Pia ingepemdeza wapeleke watoto wao wakasome shule za msingi za serikali, sekondari za serikali na vyuo kama UDOM, SOKOINE au UDSM isiwe tena kukimbilia nje ya nchi hata kwa vitu ambavyo tunavyo humu humu kwetu.

Upande wa matibabu nao viongozi waende kwenye vituo vyetu vya afya ya umma sio binafsi na nje za nchi. Hii ingewepesisha kuona changamoto zilizopo huko. Ingekuwezekana tusiwe na sehemu mahosusi hospitalini kwao, nao watibiwe sawa na wananchi, pengine hii ingeleta chachu ya kuboresha hospitali zote. Tusipo kuwa tayari kula chakula chetu wenyewe hata mgeni hatokila pindi tumkaribishapo.

Tatu, kama tunataka chakula chenye radha nzuri, basi hatuna budi jikoni tupeleke malighafi na kuni nzuri.
Ikiwa tunataka tupate wajuzi wazuri basi hatuna budi tujue kwamba wanaowafunza nao wawe bora. Walimu/wakufunzi wapewe mazufunzo bora ili wakawafunze vizuri wanafunzi. Shule na vyuo, majengo yaboreshwe vizuri, maabara bora na za kisasa zitawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo. Hospitali vipelekwe vifaa na dawa za kutosha walau madaktari wetu wazoe namna ya kutumie hivyo hata huduma zitakuwa nzuri.

Biriani haipikwi kwa mchele wa chenga chenga, tupeleke basmati na jogoo wa kienyenji uone kama mlaji hatojilamba

Nne, Tuboreshe jiko letu.
Badala ya kuwasema wanatalamu wetu kuwa hawana uwezo ilitakiwa tuhoji juu ya mfumo mzima wa elimu, ambao yamkini ndio huzalisha hao wanataalumu. Mzizi wa fitna ni huu mfumo wa elimu. Tufanye maboresho ya hali ya juu kuendana na mabadiliko ya sasa. lazima tuupitie upya huu mfumo wetu wa elimu.

Iundwe tume ipitie upya mfumo mzima wa elimu. Tuchunguze tuone madhaifu yetu ni yapi ukilinganisha na nchi nyingine! Kama madhaifu ni kwenye mafunzo ya vitendo basi tutengeneze mtaala ambao utagusia huo upande. Na mara tukishapambanua shida ilipo, hatua za haraka zichukuliwe, zisianze tena siasa nyingi zisizo na utekelezaji.

Tuboreshe jiko likiwa bora bila shaka hata kitakachopikwa kitakuwa bora na salama kwa walaji

HITIMISHO
Sio haramu kutumia wajuzi toka nchi nyingine kwenye miradi mbali mbali ya nchini mwetu. ila hili pia sio swala la kuendekeza hasa kwa mambo ambayo tunaweza kufanya wenyewe.

Tunategemea Tanzania yetu ijayo iwe na mikakati ya kuhakikisha inatumai wataalamu wetu ambao naamini watakuwa wazalendo zaidi kuliko wageni lakini pia hii itasaidia kupunguza tatizo la ajira linalozidi kushika hatamu kila kukicha
 
Upvote 1
Back
Top Bottom