SoC04 Tanzania tuitakayo katika miaka 25 ijayo

SoC04 Tanzania tuitakayo katika miaka 25 ijayo

Tanzania Tuitakayo competition threads

FikiriMeku

New Member
Joined
Sep 2, 2017
Posts
1
Reaction score
0
Tanzania ni inchi iliyobarikiwa kuwa na utajiri wa rasilimali anuwai kama vile ardhi yenye rutuba, uoto wa asili , bahari , mito , maziwa, mbuga za wanyama nakadhalika. Tanzania pia imejaliwa kuwa na watu wenye upendo na amani. Mambo yote haya yanaifanya Tanzania kuwa na uwezekano mkubwa wa kustawi na kuendelea. Ni wazi kuwa Tanzania imepiga hatua nzuri kwenye Nyanja mbalimbali lakini bado yapo mengi ya kufanya. Nataka kuwa na Tanzania yenye mambo yafuatayo ndani ya miaka 25 ijayo:

Afya. Afya njema ni kiini cha mafanikio katika maeneo mengine ya maisha. Na kama isemwavyo , “Afya ni utajiri” na “akili yenye afya hutokana na mwili wenye afya” na hivyo Tanzania niitakayo ni ile itakayowekeza vizuri kwenye afya ili kuwa na watu ambao ni wazalishaji wazuri na wanaoweza kuchangia vema kwenye maendeleo. Uwekezaji kwenye afya wapaswa kufanywa kwa kuhakikisha kuna huduma nzuri za kiafya na hii itawezekana tu kwa kuwepo na hospitali, zahanati na vituo vya afya vya kutosha si tu katika kila mkoa bali kila Kijiji nchini. Sambamba na hili tutahitaji kuwekeza katika kuwa na vyuo vya afya katika kila wilaya ili kuhakikisha tuna wataalamu wa kutosha watakaohudumu katika mahospitali na vituo vya afya vitakavyojengwa. Yote haya yataenda sambamba kwa kuhakikisha panakuwepo na dawa na vifaa tiba vya kutosha katika kila hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Elimu. Elimu ni muhimili mmojawapo wa maendeleo ya taifa lolote. Hivyo basi, serikali inapaswa kuwekeza vema katika sekta hii kwa kuhakikisha tuna vyuo vikuu, vya kati na vya ufundi vyenye ubora vitakavyozalisha wataalamu kwenye maswala mbalimbali kama vile afya, elimu, sayansi, teknolojia, hisabati, uchumi na mengineyo. Zaidi sana serikali itapaswa kuwekeza kwenye hisabati, sayansi na teknolojia ya taarifa na mawasiliano kwa kuwa ndilo eneo linalokua sana duniani na linaloendesha maendeleo ya mataifa mengi. Vile vile serikali inapaswa kuhakikisha inajenga maktaba katika kila Kijiji na kuhamasisha watanzania kuwa na utamaduni wa kujisomea. Hii itawezesha kuwa na taifa la watu wenye maarifa na uwezo wa kukosoa na kuhoji maswala yanayohusiana na maisha na taifa lao kwa ujumla pamoja na maarifa yanayoweza kujenga Maisha yao na jamii zao.

Uchumi. Tanzania inaweza kuwa na maendeleo ya kutosha na kufikia malengo ya maendeleo endelevu. hii itawezekana endapo tutawekeza vizuri katika afya na elimu na kuwa na uongozi bora. Tutahitaji kuwekeza katika kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika kutokana na vyanzo mbalimbali kama vile maji, gesi asilia, upepo , jua , jotoardhi nakadhalika. Pia tutahitaji kuwekeza kwenye kilimobiashara cha kitaifa na kimataifa kwa kutumia mazao kama vile kahawa, pamba, sukari, katani na mazao mengine tuliyonayo. Pia uzalishaji na uuzaji wa mbogamboga na maua ndani na nje ya nchi vyaweza pia kuimarisha uchumi wetu. Sekta ya utalii itapaswa kuboreshwa kwa kuhakikisha vituo vyote vya kitalii(tourist destinations) vinalindwa na kutunzwa. Yote haya yataimarisha uchumi wetu na kutengeneza ajira kwa watu wetu na hivyo kupunguza umasikini.

Mazingira. Tanzania iliyo bora itapaswa kuwa na mazingira mazuri kwa ajili ya kurahisisha maisha ya binadamu na viumbe wengine. Hii ni pamoja na kuwa na taifa lenye mipango na mifumo madhubuti ya kufanya mazingira yawe safi ikiwa ni pamoja na kuwa na mifumo thabiti ya utupaji taka ili kuondoa uwezekano wa kusababisha milipuko ya magonjwa itokanayo na mazingira machafu. Tutahitaji pia kuwa na miti ya kutosha na kutunza uoto wa asili tulio nao ili kuhakikisha kuwa tunapata mvua kwa wakati na hatupotezi viumbe tulio nao. Hifadhi zetu na mbuga za Wanyama zapaswa kulindwa ili kuendelea kuvutia watalii na kujenga uchumi wetu.

Miundombinu. Tunapaswa kuhakikisha tuna barabara za lami katika kila mkoa kuanzia mijini hadi vijijini. Pia tutahitaji kuwa na reli zitakazohudumia kila mkoa Tanzania na vile vile tutahitaji usafiri wa uhakika wa maji katika maziwa yetu na bahari zetu. tutahitaji pia ndege za kutosha kuhudumia kila mkoa Tanzania. Yote haya yatarahisisha mawasiliano na biashara baina ya watu na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wetu.

Utamaduni. Nataka kuiona Tanzania itakayodumisha utamaduni wake na utambulisho wake duniani na kuzuia kabisa watu wake kumezwa na tamaduni za kigeni zinazohatarisha utambulisho wetu kama taifa. Iwe ni sheria kuwa kila mtanzania ni lazima afahamu kuandika na kukiongea Kiswahili na kuielezea na kuitetea nchi yake akiwa na wageni popote pale. Pawepo pia na vazi la kitaifa litakalomtambulisha mtanzania popote alipo. Tutahitaji pia kuenzi miziki na nyimbo zetu za asili Pamoja na kuhakikisha kuwa wasanii wetu wanaimba nyimbo zenye kuelimisha jamii mambo mazuri tofauti na ilivyo sasa.

Maadili na uwajibikaji. Tunahitaji kuwa na taifa lenye watu wenye maaadili mema na ambao watakuwa wazalendo kwa ajili ya taifa lao. Tutahitaji Tanzania yenye viongozi na watu wenye maadili ambao watapinga kutoa na kupokea rushwa pamoja na kuhakikisha kuwa watu wa taifa hili wanaishi kwa kuzingatia haki na utawala wa sheria kwa ajili ya maendeleo ya taifa. Tutahitaji uwajibikaji kuanzia kwenye ngazi ya familia hadi kwenye viongozi na tutahitaji kuona viongozi wakiwajibika ama kuwajibishwa pindi wanapokosea. Inapaswa kuwa lazima kwa elimu ya maadili na uwajibikaji kufundishwa tangu shule za awali hadi vyuo vikuu ili kuwa na watanzania wenye maadili mema kwa ajli ya taifa lao

Demokrasia na uhuru wa maoni. Tanzania ya miaka 25 ijayo itapaswa kuwa na ukomavu wa kutosha na yenye demokrasia ya kweli. Vyama vyote viruhusiwe kuwa na mihadhara ya kisiasa kama katiba inavyoruhusu. Wananchi pia waruhusiwe kuwa na mikutano huru kujadili maswala yao na mustakabali wa taifa lao bila kuzuiwa ama kuingiliwa. Tanzania ya miaka 25 ijayo inapaswa kuwa na polisi watakaolinda haki za raia badala ya kuwakandamiza. Tutapaswa kuwa na katiba itakayotokana na watanzania na itakayolinda demokrasia na uhuru wa maoni.

Imani. Ongezeko la viongozi wa dini kiholela limechangia kwa kiasi fulani kuwa na watanzania wengi wanaoamini katika maombi na miujiza pasi na kufanya kazi ipasavyo na hivyo kutengeneza taifa la watu wavivu na wasiofikiri vizuri. Jambo hili linahatarisha ustawi wa taifa letu. Ni muhimu viongozi wa dini kuwa wamesomea maswala hayo na wasimamiwe, kuongozwa na kufuatiliwa na mamlaka za kiserikali. Tutahitaji kuwa huru kutoka kwenye Imani potofu za kishirikina zinazohatarisha maisha ya binadamu kama vile watu wenye ualbino na wazee.
 
Upvote 9
Back
Top Bottom