SoC04 Tanzania tuitakayo - mabadiliko katika sekta ya elimu

SoC04 Tanzania tuitakayo - mabadiliko katika sekta ya elimu

Tanzania Tuitakayo competition threads

Emaswai

Member
Joined
Jan 28, 2016
Posts
14
Reaction score
9
TANZANIA TUITATAKAYO

MABADILIKO KATIKA MFUMO WA ELIMU.

MUDA WA ELIMU. Kupunguza MUDA unaotumika kwenye mfumo wa elimu wa sasa wa Darasa la kwanza hadi Kidato cha Sita. Miaka saba (7) ya elimu ya msingi, minne (4) sekondari ya awali na miwili (2) sekondari ya juu ni mingi kulinganishwa na ujuzi/maarifa wanayoyapata wahitimu wa Elimu hizo. Wengi wa wahitimu wa Elimu hii ya miaka kumi na mitatu (13) hawafahamu kwa vitendo yale waliyofundishwa bali wamepewa ujuzi wa jumla wa masomo ya biashara, hesabu, sayansi, lugha, mazingira na historia. Muda huo upunguzwe na kuwa jumla ya miaka kumi (10), yaani Elimu ya msingi miaka sita (6) na ijikite zaidi kwenye ujuzi wa lazima (basic knowledge). Elimu ya sekondari ya awali iwe miaka miwili (2), hii imejidhirisha kuwezekana kupitia Elimu zitolewazo mtaani kwa waliokosa fursa ya kuendelea na mfumo rasmi wa Elimu kwa njia ya Qualifying Test (QT) na Elimu ya Sekondari ya Juu iwe ni miaka miwili. Kwa utaratibu wa wengi, mtoto huanzishwa shule akiwa na miaka sita/saba, hivyo kwa mfumo huu wa Elimu, mhitimu wa umri wa miaka kumi na saba (17) atakuwa na maarifa sawa na mhitimu wa miaka ishirini (20) wa elimu itolewayo kwa sasa. Elimu ya Chuo Kikuu iendelee kutolewa kwa muda wa angalau miaka mitatu (3) kutegemeana na aina ya Ujuzi na Fani kama ilivyo sasa.

ELIMU YA KOMPYUTA. Somo la Kompyuta lifundishwe kwa lazima (Not Optional) kuanzia ngazi ya Elimu ya msingi ya darasa la nne ambapo mtoto anakua ameshajengewa uwezo mzuri wa Kusoma, Kuandika na Kutafsiri alama za kiuandishi. Kila shule ya Sekondari ya Awali na Sekondari ya Juu iwe na maabara ya kompyuta ambapo wanafunzi watapata muda wa ziada wa kujifunza kompyuta kivitendo. Serikali na watoa huduma za Mitandao wajitahidi kusambaza huduma ya mtandao (Internet) kurahisisha ufundishaji wa somo hili. Kuwe na mtihani wa kitaifa kupima uwezo wa wanafunzi kinadharia kwa shule za Msingi kwenye Mtihani wa Taifa wa darasa la Sita (6), Kinadharia na Kivitendo (theoritically and practically) kwa Darasa la Nane (8) na Darasa la Kumi (10).

LUGHA YA KUFUNDISHIA. Kubadili lugha ya kufundishia na kuwa Kiingereza. Kutokana na muingiliano mkubwa uliopo na Dunia kuwa kama kijiji (Globalization), ni muda muafaka sasa kuhakikisha tunajenga kizazi chenye kujua kusoma, kuandika na kuongea lugha ya kiingereza kwa ufasaha. Hatuna budi kuweka kiingereza kuwa lugha rasmi ya kufundishia kuanzia ngazi ya chini ya elimu ili wahitimu wawe na fursa sawa na wengineo duniani kote. Kwa mfumo wa elimu wa sasa, wahitimu wa shule za serikali wana ufahamu mdogo wa lugha ya kiingereza hususani kwenye kuongea ukilinganisha na wale wa shule binafsi. Sambamba na hilo, tunahitaji pia kujifunza kwa wingi lugha zizungumzwazo na walio wengi duniani hasahasa Kichina na Kifaransa.

AINA YA ELIMU. Kubadili Mitaala ya Elimu na kuwekeza zaidi kwenye Elimu ya Vitendo (Practical Learning) na Elimu ya Ufundi (Vocational Training). Kuondoa baadhi ya MADA (Topics) zilizopitwa na wakati katika masomo ya Historia, Sivikia, Jiografia, na Baiolojia. MADA hizo ziwekwe kwenye vitabu vya ziada kwa ajili ya mwanafunzi kujiongezea maarifa inapobidi. Kuyapa kipaumbele masomo yanayohusu Biashara na Uchumi yaani Commerce, Accounting na Economics. Kama somo la Hesabati lilivyowekewa mkazo vivyo hivyo mkazo uwekwe kwenye masomo ya biashara kwani ni msingi mkubwa wa wahitimu kujiajiri. Elimu ya Ufundi iwe ni kwa vijana wenye ndoto na malengo yategemeayo elimu ya Ufundi.

MAFUNZO YA JESHI LA KUJENGA TAIFA (JKT-MUJIBU WA SHERIA). Mafunzo ya (JKT) yawe ni LAZIMA. Tofauti na sasa, mafunzo ya JKT yatolewe kwa kipindi cha mwaka mmoja kamili. JKT wajikite zaidi kwenye kutoa Elimu ya Vitendo na Shughuli za Uzalishaji Mali hususani Kilimo, Ufugaji na Utunzaji wa Mazingira. Wanufaika wa Mafunzo haya wawe ni vijana wote waliohitimu ngazi ya Darasa la Nane (Form Four ya Sasa) na Darasa la kumi (Form Six ya sasa). Yaani, wanafunzi wote wanapomaliza darasa la nane (8) wanapaswa kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa lazima katika kambi watakazopangiwa, majibu ya ufaulu wao yatawakutia kambini, wale watakaokuwa wamefaulu wataruhusiwa kuondoka makambini kwenda kuendelea na masomo ya Sekondari ya Juu yaani darasa la tisa na kumi. Watakaokuwa wamefeli wataendelea na mafunzo kwa kipindi cha mwaka mmoja na watakapohitimu watakuwa na sifa ya kuja kujiunga na Vyuo vya Ufundi na Vyuo vya Elimu kwa ngazi ya Astashahada (Certificate). Vivyo hivyo kwa watakaojiunga mafunzo ya JKT wakiwa wamehitimu darasa la kumi (10), waliofaulu wataruhusiwa kwenda kujiunga na Vyuo Vikuu kwa ajili ya masomo ya Shahada ( Bachelor Degree), wale waliofeli wataendelea na mafunzo ya JKT kwa kipindi cha Mwaka mmoja. Watakapohitimu mafunzo hayo ya JKT watakuwa na sifa ya kujiunga na Vyuo vya Ufundi (Vocational Training) au Kujiunga na Vyuo vya Elimu kwa ngazi ya Stashahada (Diploma).

PROGRAMU ZA KUBADILISHANA UJUZI NA WATAALAMU. Kuendeleza na kukuza programu za kubadilishana ujuzi na mataifa yaliyoendelea. Tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa mataifa mengine. Kumekuwa na programu ya muda mrefu kwa Chuo Kikuu cha Kilimo SUA (Morogoro) kupeleka wahitimu wake nchini Israel kujifunza Kilimo na Ufugaji. Mafunzo ya mwaka mmoja katika mashamba darasa nchini Israel yamekuwa chachu kubwa ya kupata wajuzi wenye weledi na ubobezi wa Kilimo na Ufugaji nchini Tanzania. Tunaweza kutumia njia iyo iyo kupeleka wahitimu wa fani ya mbalimbali ikiwemo Udakitari kutoka vyuo vikuu vya Muhimbili, Hubert Kairuki Memorial University, n.k katika nchi zenye sifa ya Utabibu ikiwemo India, Marekani n.k. Kutengeneza mahusiano baina ya vyuo vikuu vyetu na vyuo vikuu vya nje kwa ajili ya kubadilishana ujuzi.

KUZISIMAMIA TAASISI ZA KUTOA ELIMU. Kuboresha na kuongeza usimamizi kwenye Taasisi za Elimu. Taasisi za Elimu za Serikali na Taasisi Binafsi zinapaswa kuwa na ndoto moja ya kuhakikisha Elimu bora inapatikana ndani ya Nchi. Kuondoa mitaala ya Elimu iliyopitwa na wakati, Kuongeza zana za kisasa za ufundishaji, Kuboresha mazingira ya ufundishaji, Kudhibiti ujengaji holela wa shule na mabweni usiozingatia usalama wa wanafunzi na walimu, kupambana na udanganyifu wakati wa mitihani ya kitaifa, kupambana na rushwa ya ngono mashuleni. Kuboresha maslahi ya Walimu n.k ni baadhi ya hatua muhimu ili kuijenga jamii ya Kitaanzania Iliyoelimika na kustaarabika.

Emanuel William Swai.
0659745511
 
Upvote 5
Back
Top Bottom