SoC04 Tanzania Tuitakayo: Maoni ya kuboresha na kukuza elimu Tanzania

SoC04 Tanzania Tuitakayo: Maoni ya kuboresha na kukuza elimu Tanzania

Tanzania Tuitakayo competition threads

BATSON

New Member
Joined
Jun 15, 2024
Posts
1
Reaction score
1
MAONI KATIKA KUBORESHA NA KUKUZA ELIMU TANZANIA
(Nini kifanyike ili kuboresha na kukuza Elimu yetu ya Tanzania ?)
Naitwa Batson R. Msigwa kutoka Njombe-Tanzania. Mimi ni mhitimu Kutoka Chuo Kikuu Cha Dar-es-Salaam, niliyesomea Ualimu katika tawi la Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa-Iringa katika masomo ya Shahada ya kwanza ya Elimu katika sanaa somo la Kiingereza ambapo Kwa sasa najitolea kufundisha katika shule mojawapo ya sekondari iliyopo katika mkoa wa Njombe wilaya ya Wanging'ombe, Ni mtoto wa kwanza kutoka familia duni yenye mama na watoto watatu baada ya baba yetu kufariki tangu mwaka 2007; pamoja na ugumu wa maisha na hali ya kuwa mama yetu hana kazi maalumu mbali na ukulima mdogo bado anaipambania familia ambapo hata sisi tunapambana kwa kulipigania taifa letu pendwa la Tanzania;

Kwanza namshukuru Mungu kwa uzima alionipa na afya tele ya kuweza kushiriki katika jukwaa hili kutoa maoni yangu kuhusiana na maendeleo ya Taifa letu kwa miaka 5, 10, 15, 20 na hata 25 ijayo ; naiona Tanzania ikistawi hapo baadae hasa katika suala la ELIMU ambapo ningependa kutoa maoni yangu katika sekta hii. Pili namshukuru Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazofanya ili kuboresha elimu na sekta zingine kwa ujumla hali ambayo hata sisi tutokao katika familia masikini tunaweza kusoma kwani hata mimi nilipewa Mkopo na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kwani bila hivyo nisingeweza kusoma. Si hivyo tu lakini pia namshukuru na kumpongeza sana Waziri wetu wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ndugu Mh. Adolf Mkenda kwa jitihata anazozifanya katika kuboresha na kukuza elimu yetu.

Ni ukweli usiopingika kwamba Elimu ndio msingi wa mambo yote na sekta zingine zote zinatokana na kitovu hiki kupitia shule na walimu, hivyo elimu ndio msingi wa taaluma zote duniani niko hapa kutoa maoni yangu kuhuiana na nini kifanyike ili kuboresha na kukuza elimu yetu ya Tanzania ?

Udhibiti wa Walimu waingiao na waliopo kazini kwa ujumla.
Ni dhahiri kwamba chakula kizuri ni matokeo ya maandilizi mazuri ya viambata kabla ya mchakato mzima wa upishi lakini hivyo vyote si bora pasipokuwepo na mpishi bora, Ndugu wadau napenda kusema kwamba, elimu yetu ya Tanzania itaweza kuboreshwa kupitia walimu kwani wao ndio daraja hivyo uwepo wa ukaguzi wa mara kwa mara utasaidia kwa kiasi kikubwa, Nikiungana na wazo la Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mh. Adolf Mkenda, Kwamba walimu wanaotarajia kuajiriwa wanatakiwa kupimwa kabla ya kupewa nafasi hii itasaidia kupata walimu bora na wenye weledi wa kufanya kazi; upimaji huo uhusishe nadharia kwa maana ya mitihani ya kitaaluma kwa ujumla na umahili wake katika somo husika lakini pia upimaji wa vitendo unahitajika ikiwemo kuandaa somo kwani walimu walio wengi hawafanyi maadalizi ya vipindi vyao, hivyo maandalizi na mipango ni kitu cha msingi kwa kila hatua. Pia walimu waliopo kazini pia kufanya mitihani, kwa mfano walimu wanaweza kufanya mitihani ya maoni kuhusiana na mitazamo na mapendekezo yao katika kuboresha na kukuza elimu
yetu.

IMG_20230618_213858_075.jpg

Matumizi ya Mbinu shirikishi katika ufundishaji na ujifunzaji.
Katika ulimwengu huu wa karne ya 21 unaotawaliwa na matokeo ya utandawazi wanafunzi wengi wamekuwa wakiongezeka maarifa kwa hali ya juu sana tofauti na hapo awali, hivyo hii inapelekea wanafunzi wengi kujihusisha na mambo mengine tofauti na malengo ya elimu yetu, wanafunzi wetu wanahitaji elimu ya saikolojia inayohusisha mbinu shirikishi, mbinu mbalimbali zinahitajika kutumika kama vile uhusishaji wa teknolojia wezeshi na mahusiano yaliyo bora kati ya mwalimu na mwanafunzi ili kujua changamoto za wanafunzi kiurahisi, hii ni mbinu ya kisaikolojia ambayo inamsaidia mwanafunzi kuhamisha upendeleo wake kutoka katika masuala mengine yasiyo mema kurudisha katika maendeleo ya elimu yake kwa kutumia teknojia ile ile inayomvuta kuelekea katika mambo yasiyokuwa na maadili hivyo teknolojia hiyohiyo itumike kumpa motisha katika ujifunzaji wake.

Kujitegemea kwa utendaji katika bodi ya taaluma ya ualimu.
Haina maana kwamba kusiwepo na ushirikiano, lahasha ! Ni kwamba bodi ya taaluma ya ualimu ijitegemee katika majukumu yake bila kuingiliwa na vyama au tume zingine za ualimu kama vile Chama Cha walimu Tanzania(CWT) na Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC), uhusino wao uwe ni katika dhana ya uangalizi na usawa wa mgawanyo kimadaraka kama ilivyo kwa mihimili ya serikali yaani Bunge, Mahakama na Watendaji wakuu wa serikali; hii itasaidia kufanya kazi kwa ufanisi na kushughulikia madai ya walimu pamoja na mahitaji yao hali ambayo inawezesha walimu wengi kufungua mioyo yao ya utayari wa kufanya kazi kwa bidii na ustadi mkubwa.

Uboreshaji wa michepuo ya ufundishaji na ujifunzaji.
Naishukuru sana serikali katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika jitihada za kuanza kusoma somo la kiingereza kwa wanafunzi wa shule za misingi wakiwa darasa la kwanza, kwani hii inawasaidia kuwajengea msingi wa mapema na kuondokana na dhana potofu ya ugumu wa lugha ya kiingereza ili kuendana na mchepuo wa kiingereza hata wanapofika katika daraja la shule ya upili; lakini pamoja na hayo ingefaa zaidi kutumia lugha yetu mama ya Kiswahili kama nyenzo ya mchepuo katika ufundishaji na ujifunzaji ili kurahisisha maendeleo ya elimu yetu.

Uboreshaji wa miundo mbinu na rasilimali watu.
Mara nyingi kumekuwa na kasumba ya wataalamu wengi wa masuala ya elimu kupenda kufanya kazi mbali na nchi yetu kwa manufaa yao hii inapunguza utaalamu katika elimu, kuwepo na sera ya motisha kwa wataalamu wa juu katika kuwajengea uwezo na msukumo wa kusaidia kwanza nchi yetu ni njia inayoweza kutuleletea maendeleo katika elimu yetu, si hivyo tu pia uhuru na mamlaka ya hali ya juu wanayopewa wakufunzi katika elimu za juu unapaswa kudhibitiwa ikiwa ni pamoja na kuboresha namna ya kuwaandaa walimu wenye weledi katika ngazi zote za elimu kuanzia msingi mpaka vyuo.

Mwisho; napenda kuwashukuru waanzilishi wa jukwaa hili pendwa kama kitovu cha maoni katika sera ya maendeleo ya nchi yetu kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Naiona Tanzania ikiendelea katika elimu na sekta zingine kwa ujumla zikiwa ni matunda kutoka kwenye mzizi mkuu wa elimu. Naitazamia Tanzania mpya katika miaka 5, 10, 15, 20 na hata 25 ijayo katika kuboresha na kukuza Elimu yetu; Ahsante naomba Kuwasilisha.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom