SoC04 Tanzania tuitakayo: Mikakati thabiti inayotekelezeka ya kupunguza tatizo la ajira hapa nchini

SoC04 Tanzania tuitakayo: Mikakati thabiti inayotekelezeka ya kupunguza tatizo la ajira hapa nchini

Tanzania Tuitakayo competition threads

Msafie

Member
Joined
Sep 7, 2017
Posts
17
Reaction score
8
UTANGULIZI
Changamoto ya ajira hapa nchini imekua tatizo linalokua kwa kasi huku vijana wakiwa ni waathirika wakubwa. Hivyo serikali iweke mikakati madhubuti itakayotokelezeka haraka ili kupunguza changamoto hii. Katika mada hii tutaona mambo mbalimbali yanayochangia ongezeko la ukosefu wa ajira na namna ya kukabiliana nayo kwa kuzingatia mikakati mbalimbali inayoweza kutekelezwa na serikali, sekta binafsi, na jamii kwa ujumla.

CHANZO CHA TATIZO
Baadhi ya mambo ambayo yanachangia uwepo wa tatizo la ukosefu wa ajira hapa nchini ni:

Ongezeko kubwa la Idadi ya Watu, Kuulingana na sensa ya mwaka 2022 idadi ya watu inaongezeka kwa wastani wa 3.2% kwa mwaka, Hali hii hupelekea kuongezeka kwa shinikizo kwenye soko la ajira. Watu wengi wanahitaji kazi lakini nafasi za kazi haziongezeki kwa uwiano sawa.

Ukosefu wa Ujuzi na Elimu: Watu wengi hawana elimu na ujuzi unaoendana na mazingira yao, hivyo wanashindwa kubaini fursa za ajira zinazopatikana. Kwa kiasi kikubwa hali hii imechangiwa na Mfumo wa elimu wa sasa ambao unamlazimisha mwanafunzi kusubiri ajira baada ya kuhitimu na sio kujiongeza kulingana na mazingira yanayomzunguka.

Mabadiliko ya Kiteknolojia: Matumizi ya teknolojia ya kisasa yanapunguza nafasi nyingi za kazi, hasa katika sekta za viwanda, ujenzi na huduma. Mfano katika ujenzi shughuli kama kuchanganya zege, kupaka rangi n.k zinafanywa na mashine kama mbadala wa kuajiri watu kufanya kazi hizo.

Sera mbovu za Kiuchumi, ambazo hazijajikita katika uzalishaji endelevu. Tumeshuhudia Sera mbovu za serikali za kuongeza pato la Taifa kwa kuweka Tozo katika baadhi ya bidhaa mfano mafuta na huduma za miamala ya kibenki na simu na kwenye kumbi za starehe.
Lakini pia kudhihirisha Serikali haijajipanga, Bado baadhi ya wabunge wanaendelea kupendekeza Tozo katika line za simu kwa ili kupata fedha kwa ajili ya mpango wa Bima ya Afya kwa wote, Badala ya sera za uzalishaji na uwekezaji.

Kufungwa kwa Biashara na Makampuni kwa sababu mbalimbali, kama ukosefu wa malighafi, usimamizi mbaya, ukosefu wa masoko au sera mbovu za serikali zinachangia kupunguza nafasi za ajira. Mfano Januari 2024 kiwanda cha Raha Beverage Co. kilitoa tamko la kufunga kiwanda kutokana na ukosefu wa sukari sanjari na bei holela ya sukari huku ikielezwa kua zaidi ya ajira 200 zitapotea.

Ukosefu wa Mikopo na Mitaji, Bila mikopo na mitaji, ni vigumu kwa watu binafsi na wafanyabiashara kuanzisha na kukuza biashara mpya ambazo zingeweza kutoa ajira. Kuna changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wadogo ambao serikali haijawawekea mpango maalumu utakaowawezesha kunufaika na fursa za mikopo yenye riba nafuu katika kukuza biashara zao.

Mazingira Duni ya Biashara: Biashara zinaweza kushindwa kustawi ikiwa kuna urasimu mwingi, rushwa, na sheria ngumu ambazo zinakwamisha ukuaji wa biashara. Tumeishuhudia mwaka 2023 wafanyabiashara wa soko la kimataifa Kariakoo waligoma wakilalamikia urasimu bandarini, Rushwa na kunyanyaswa na Mamlaka mbalimbali za serikali kama vile TRA.

NINI KIFANYIKE?
Kuboresha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi
:
Moja, Serikali na jamii zinapaswa kuondoa dhana potofu kwenye jamii ya kwamba wanaoenda mafunzo ya ufundi stadi ni wale waliofeli.

Pili, Kwa miaka 5 ijayo, ni vyema serikali ifanye maandalizi ya kufundisha ufundi stadi na ujuzi unaohitajika sokoni kwenye shule za sekondari na msingi, ili kuwasaidia watoto kuweza kujiajiri pindi wamalizapo shule. Maandalizi haya yahusishe Miundombinu, Vifaa vya kufundishia, Wataalamu wa mafunzo hayo na kuandaa mitaala.

Mafunzo kama vile ufundi wa simu na computer, ujenzi, ufundi wa magari, pikipiki, umeme (wiring), Ushonaji, ufundi bomba ni muhimu kwani fursa zipo nyingi huku kukiwa na upungufu wa wajuzi.

Kukuza Sekta ya Kilimo kwa kuhimiza matumizi ya Teknolojia za Kisasa:
Kilimo ni sekta muhimu ya kukuza uchumi wa Taifa letu. Ndani ya miaka 10 ijayo, Serikali iandae idara maalumu ambayo itahimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kukuza sekta ya kilimo ikiwemo utoaji wa elimu ya kilimo kuanzia hatua za upandaji wa mbegu, palizi, mavuno mpaka hatua za kuhifadhi nafaka.

Baadhi ya wakulima bado wanatumia mbegu zisizobora, hatua duni za upandaji mbegu na matumizi ya kemikali kuhifadhi mazao yao dhidi ya wadudu, njia ambayo huhatarisha afya za walaji, kushusha thamani ya mazao na kuishia kukata tamaa.

Sambamba na utoaji wa elimu, Idara hiyo itumike kubaini changamoto zinazowakabili wakulima na kutoa mapendekezo kwa serikali ili hatua stahiki zitumike kuwasaidia wakulima.
Mfano kutoa ruzuku kwenye teknolojia ya kisasa, mikopo nafuu na kuwasaidia kutafuta soko la kimataifa la mazao yao.

Kuwekeza katika Elimu ya usindikaji kwa lengo la kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao hali ambayo itasaidia kuongeza ajira

Mazingira Bora ya Biashara Sheria na Kanuni:
Kutokutoza kodi zaidi ya mara moja na Kurahisisha taratibu za kuanzisha na kuendesha biashara, Kulipa kodi kwanza isiwe kigezo cha kupata vibali vya kuanzisha biashara, Kwa sababu tunategemea biashara kupata fedha ya kodi.

Serikali iandae mazingira rafiki ambayo yatasaidia kurasimisha biashara kwa njia ya mtandao.
Kutokana na ukuaji wa teknolojia, Biashara inaweza kufanywa kwa njia mbalimbali, Ukiachana na mfumo wa kupanga bidhaa kwenye fremu na kusubiri wateja, kwa sasa biashara inaweza kufanywa kwa njia ya mtandao bila kuwa na ofisi.
Hivyo Serikali itoe leseni maalumu ambazo zitapatikana kwa kujisajili kwenye mfumo maalumu utakaoundwa na serikali, utakaomwezesha mfanyabiashara kutambulika popote atakapotoa huduma, ambapo licha ya kuwezesha ukusanyaji wa mapato kutoka kwa wafanyabiashara hawa, pia itaongeza usalama kwa mteja kwa kumuhakiki mfanyabiashara kabla ya manunuzi.

Kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa Mikopo midogo kwa wajasiriamali. Kwa kutumia mfumo wa kitambulisho cha Taifa ambao tayari umeunganishwa na benki, sambamba na mfumo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo niliopendekeza uanzishwe, itumike kuwapatia wafanyabiashara wadogo mikopo ambayo inaweza kuongezeka kadiri mteja anapokua anafanya marejesho bila usumbufu. Hii itasaidia kupunguza tatizo la ajira kwani vijana wasiokua na mitaji ndiyo wadau wakubwa wa biashara za mtandaoni.

Serikali na jamii kwa ujumla zishirikiane kuhimiza umuhimu wa uzazi wa mpango, ili kudhibiti kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu.

Serikali iandae Sera za Ajira na Mpango wa Kitaifa wa Ajira, unaolenga kupunguza ukosefu wa ajira, iwe ni mpango wa lazima na sio sehemu ya siasa kama ilivyo kwa sasa, ambapo viongozi wanachukulia ajira kama sera wakati wa uchaguzi.

Kukuza Teknolojia na kuendeleza ICT, Kuwekeza katika teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuunda nafasi mpya za ajira. Serikali itoe uhuru kamili kwa vyombo vya habari na kuweka masharti nafuu ili vijana wawekeze katika sekta ya habari na mawasiliano.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom