SoC04 Tanzania Tuitakayo ni ile yenye Hospitali Maalum za Kitaifa kwa kila Kanda

SoC04 Tanzania Tuitakayo ni ile yenye Hospitali Maalum za Kitaifa kwa kila Kanda

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
May 6, 2024
Posts
7
Reaction score
3
UTANGULIZI:
Hospitali Maalum ni Hospitali zinazotoa huduma ya kimatibabu na kiuguzi kwa ugonjwa au tatizo fulani pekee mfano ugonjwa wa moyo, saratani, macho, akili, pumu n.k. Nchini Tanzania tunazo Hospitali Maalum 5 tu za Kitaifa kama vile Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) yenye kutibu magonjwa ya Moyo, Hospitali ya Kibong’oto(KIDH) yenye kutibu Magonjwa ya Kuambukiza, Taasisi ya Mifupa Muhimbili(MOI) yenye kutibu Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu, Hospitali Afya ya Akili Mirembe(MMHH) yenye kutibu Afya ya Akili na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road(ORCI) yenye kutoa huduma za magonjwa ya Saratani.

MGAWANYO WA KANDA:
Nchi yetu imegawanyika katika Kanda 7 za Kanda ya Mashariki, Kanda ya kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Hadi sasa katika hizi kanda 7, Hospitali maalum za Kitaifa zilizopo zinapatikana katika Kanda 3 tu (Mashariki, Kaskazini na Kati) ambapo Kanda ya mashariki inazo Hospitali maalum 3 kati ya 5, Kanda ya kaskazini ina Hospitali Maalum 1 kati ya 5 na Kanda ya Kati ina Hospitali Maalum 1 kati ya 5.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuboresha huduma za Afya kwa kila kanda kwa kuongeza Hospitali za Serikali za Kanda kwa miaka ya hivi karibu kama vile Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara, Hospitali ya Benjamin Mkapa Kanda ya Kati, Hospitali ya Kanda Mbeya ambazo zimerahisha upatikanaji wa matibabu ya kibingwa katika kanda husika, lakini ili kufikia Tanzania Tuitakayo yenye Maendeleo endelevu hatuna budi kuwa na Hospitali Maalum za Kitaifa kwa kila Kanda ingawa matibabu ya kibingwa yanatolewa pia kwenye Hospitali za Kanda zilizopo.

NINI UMUHIMU WA KUWA NA HOSPITALI MAALUM ZA KITAIFA KWA KILA KANDA?

Kusogeza huduma za matibabu maalumu kwa wananchi wa kanda husika
Uwepo wa Hospitali maalum katika Kanda utarahisisha upatikanaji wa huduma ya matibabu maalumu katika kanda husika na kuokoa Maisha ya watu wa eneno hilo kwa urahisi, leo hii mtu akihitaji huduma ya Upasuaji wa mifupa au Ubongo kama yupo kanda ya Nyanda za Juu kusini atalazimika kuifuata huduma hiyo hadi MOI jambo ambalo linaweza kuhatarisha Maisha yake kwa kukosa huduma kwa haraka sababu ya umbali hadi kufika MOI.

Kupunguza gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma
Kwa kuwa hospitali hizi zitakuwa karibu na wakazi wa kanda husika, wagonjwa hawatahitaji kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma ya matibabu. Hii itapunguza gharama za usafiri na itawezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa urahisi. Pia gharama kubwa za matibabu ya mbali zinaweza kupelekea jamii kuingia katika umasikini kwani wakati wa kujiuguza inapunguza uzalishaji, hivyo matibabu yakiwa karibu inapunguza gharama kubwa na kuepuka kuingia kwenye umasikini bila kutarajia.

Kuchochea maendeleo katika kanda husika na Taifa
Wananchi wenye Afya njema kutokana na huduma bora ni nguzo katika maendeleo nchini maana wataweza kujishughulisha na shughuli za kimaendeleo na uzalishaji mali. Afya Bora inasaidia kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji kazi. Hivyo uwepo wa Hospitali Maalum kwa kila kanda utachochea maendeleo katika eneo husika na kwa Taifa.

Kuimarisha utoaji wa huduma za nje ya kituo (outreach services) kwa urahisi zaidi
Miongoni mwa huduma zinazotolewa na Hospitali Maalum ni huduma ya nje ya kituo (Outreach services) kwa jamii ili kuelimisha jamii kuhusu kuzuia magonjwa na namna ya kujikinga. Kituo kikiwa karibu na jamii inakuwa rahisi kuifikia jamii nyingi kwa gharama nafuu. Kwa sasa wataalam wa Afya wakitaka kwenda kutoa huduma ya Outreach mkoa wa Katavi kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road watalazimika kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa hadi kuifikia jamii iliyoko Katavi tofauti na ambapo Wataalamu wangekuwa katika Kanda ya Nyanda za Juu kusini.

Kuvutia uwekezaji katika kanda husika
Mwekezaji yeyote yule makini lazima azingatie hali ya usalama wa wafanyakazi wake, Nchi zenye mfumo na huduma bora za afya zinavutia wawekezaji. Wawekezaji wanajua kuwa wafanyakazi wao watakuwa na afya njema na wataweza kufanya kazi kwa ufanisi palipo huduma bora za Afya na zilizopo karibu. Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu kusini zenye kujihusisha na shughuli za Madini kuna umuhimu sana wa kuwa na Hospitali Maalum ili kuweza kuvutia wawekezaji.

Kuimarisha utafiti wa magonjwa husika katika kanda
Hospitali maalum ni sehemu za utafiti wa magonjwa kwa kushirikiana na watafiti kwa kutoa fursa za kufanya majaribio kwa lengo la kuboresha matibabu. Tafiti kutoka kanda mbalimbali zitasaidia kutoa majibu mbalimbali kwa Watafiti na Wizara ya Afya ili kuwezesha kutunga sera zilizo bora za matibabu ya ugonjwa husika kwa kutumia taarifa jumuishi kutoka kanda mbalimbali. Hii itasaidia kuepuka kutumia taarifa kutoka sehemu moja katika kufanya maamuzi ya kisera.

Kuimarisha utoaji wa huduma za kitaaluma za afya katika kanda husika
Miongoni mwa malengo ya Hospitali maalum ni kuwa Hospitali za Ufundishaji (Teaching Hospital), kwa kuwa Taaluma ya Afya inaendelea kukua kwa kuongezeka vyuo vya kati nchi nzima vinavyotoa mafunzo kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada. Ili kukidhi mahitaji katika utoaji elimu kwenye hizi ngazi za kielimu inahitajika mafunzo kwa vitendo ambayo lazima yapatikane kwenye vituo vya Afya. Kuwepo kwa Hospitali Maalumu kwa kila kanda itarahisisha mafunzo kwa vitendo kwa vyuo vilivyo karibu kwa kutoa fursa ya wanafunzi kwenda kujifunza katika eneo husika.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom