STORIES OF CHANGE 2024
TANZANIA TUITAKAYO
WAJIBU WA ASKARI WA USALAMA BARABARANI KWA JAMII - (TRAFFIC POLICE PUBLIC LIABILITY)
Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani linapaswa kuboreshwa ili wawezeshwe kutoa huduma zaidi ya wanazotoa kwa sasa. Tunawaona wakiongoza magari, kukagua magari, kupima ajali, kupunguza msongamano wa magari barabarani, upitishaji wa wahitimu wa mafunzo ya udereva, kusimamia misafara ya viongozi na pia kutoza faini za papo kwa papo kwa makosa wanayoona wao kuwa yanafaa kutozea faini.
Jeshi hili lingeifaa sana jamii kama lingetoa huduma za ziada kadhaa, na kwa sasa nitaje mbili tuu kati ya nyingi.
Kwanza: Ingefaa sana kama kitengo hiki kingejihusisha na utoaji wa taarifa zinazihusu maeneo korofi ya Barabara yanayosababishwa na miundombinu hatarishi na iliyoharibika kama vile kuwepo kwa shimo/mashimo hatarishi ambayo baadhi ya madereva hupata ajali wakijaribu kuyakwepa maana yanakuwa ya ghafla na wala hayana vibao/viashiria vya tahadhari.
Utawaona askari wa usalama barabarani wakija kupima ajali maeneo kama hayo na kwa haraka sana utasikia “….sababu ya ajali ni mwendokasi wa dereva” na hawataji kabisa kuhusu shimo au handaki alilokuwa anajaribu kukwepa dereva.
Askari hawa walipaswa kuwa na mfumo wa kidigitali wa kutoa taarifa za maeneo kama hayo TANROADS au TARURA na mfumo utoe fursa kwa jamii kufuatilia hatua zinazochukuliwa na wahusika wanapopata taarifa hizo. Uwepo ukomo wa muda ambao tatizo litafanyiwa ufumbuzi wa haraka, uwe wa muda au wa kudumu, na taarifa itolewe kwenye mfumo kwa ajili ya ufuatiliaji kuonyesha kitafanyika nini, lini, wapi, na ni nani atakayefanya.
Pili: Kumekuwepo kero kubwa sana ya magari yanayoharibikia barabarani na kusababisha foleni kubwa sana inayokuwa kero kubwa kwa watumiaji wa Barabara. Ukifika hapo kwenye gari bovu utakuta mtu kafungua “cabin” au “bonett” ya gari na nyuma ya gari lake ameweka pembetatu ya kuashiria hatari au ameweka majani mabichi barabarani kuashiria ubovu wa gari lake. Wakati mwingine gari laweza kuwa zima ila dereva kaamua “akaage kidogo hapo nyumbani wajue anaondoka”. Kuna wakati magari hayo yanakaa kwa masaa au hata siku hapo kusubiri kinachoaminika kuwa ni “matengenezo” huku wakisababisha hatari, foleni, ajali, na kila aina ya usumbufu kwa watumiaji wengine wa Barabara. Askari wa Usalama Barabarani hata wakija kwenye tukio wanaishia “kufanya mazungumzo”. Sanasana watapiga simu ili zije “breakdown” zile wanazozijua wao (na huenda wanazomiliki wao) wanaivuta gari kwa malipo wanayokubaliana. Hapo serikali haipati mapato yoyote hata kama hiyo gari imefanya uharibifu hapo barabarani kama vile kumwaga mafuta kwenye lami, kugonga nguzo, kugonga vigingi au vizuizi vingine.
Katika hili, Kitengo cha Usalama Barabarani kingeweza kuimarishwa kwa kupewa mamlaka ya kufanya mambo mawili.
- Wawe na mamlaka ya kuondosha mara moja gari lililoharibika barabarani na kuliegesha mahali Jirani, lakini palipo salama. Gharama za kufanya hivyo atalipa mmiliki wa gari.
- Wawe na mamlaka ya kuwasiliana na wahusika wa miundombinu, (pale inapokuwa imeharibiwa) na mmiliki wa chombo kwa muda huohuo apewe madai ya uharibifu na usumbufu uliosababishwa na gari lake mara moja ili alipe.
Haya yatakuwa ni magari yenye vifaa vya uokozi kama vile gesi ya kukatia vyuma, misumemo ya umeme ya kukatia vyuma, nyundo nzito, winchi, mitambo ya kuunganisha vyuma, mifumo imara ya mawasiliano,… nk ili waweze kutoa msaada hasa penye ajali. Ni magari yenye ving’ora ambayo yatafika eneo la tukio kwa muda mfupi sana na kutoa msaada kwa wahanga wa tukio au kuondosha hatari ya athari za gari lililoharibika na kufunga njia au kusababisha msongamano wa magari barabarani. Mfumo utaandika makadirio na kutoa hati ya madai (INVOICE) kwa namba ya gari moja kwa moja. Mfumo kama wa GPS utumike kukadiria umbali ambao magari-mitambo yamesafiri kuja eneo la tukio na kama gari bovu limevutwa, mfumo utajua limevutwa kwa umali wa mita ngapi. Umali utasaidia katika kuzalisha hati ya madai. Hati hii itakuwa na taarifa za mambo kama vile: Madai ya kusafirisha gari-mitambo toka kituo chake hadi eneo la tukio (shs…….Madai yatokanayo na kuvuta gari kwa umbali wa mita ….. (shs…..; madai yatokanayo na uharibifu wa Barabara/miundombinu ya Barabara (shs……; madai yatokanayo na huduma nyingine (shs….(zitaorodheshwa) na kisha jumla kuu (shs…..
Ankara hii atapewa mwenye gari au mwakilishi wake (dereva). Madai haya hayatakuwa na mjadala, na yatatakiwa kulipwa ndani ya siku 30 na yasipolipwa yatabeba riba. Mmiliki atalipa madai haya na kisha yeye atakwenda kudai BIMA endapo kama BIMA yake inahusika. Akishindwa kulipa madai hayo gari litataifishwa na kuuzwa kwenye mnada ndani ya siku nyingine 30, na mapato yatafidia kwanza gharama husika, kisha kiasi kinachobaki (kama kipo) atapewa mmiliki wa gari.
Kwa kufanya hivi, kitengo hiki kitaweza kujiendesha kibiashara, na pia itaokoa mali na muda wa watu, huku tukitunza miundombinu yetu. Kwa sasa unawezakuta Daraja lililojengwa kwa fedha nyingi kingo zake zote zimeshagongwa na magari lakini si rahisi kujua ni magari yapi na utengenezaji wake unasubiri bajeti kuu ya serikali. Kwa kufanya hivi tutahakikisha kuwa kila miundombinu inayogongwa na magari kwa ajali inatengenezwa ndani ya siku 14 tangu kutokea kwa tukio maana tuna uhakika wa kupata malipo ya fidia kwa matengenezo hayo.
Kitengo hiki kikiimarishwa kidigitali, itakuwa rahisi kwa askari kitengo cha Usalama Barabarani kuwasiliana na wadau wa miundombinu kama vile TANROARS na TARURA ili kila uharibifu upate makadirio stahiki, na pia matengenezo yachukue muda mfupi kardi iwezekanavyo. Pia ni vyema kikawepo kiunganishi cha taarifa hizi kwa jamii, kwani miundombinu hii ni mali ya wananchi, na wanayo haki ya kufuatilia kujua uharibifu kama unashughulikiwa.
Ili kufanikisha hili ni lazima jeshi la Polisi lijipange kuandaa bajeti kubwa yenye raslimali watu na ununuzi wa mitambo hii hata kama ni kwa awamu ili hatimaye uwe ni utaratibu wa nchi nzima. Hii pia itasababisha umakini mkubwa kwa wamiliki wa magari na madereva, kutotumia magari yenye hitilafu hata zikiwa ndogo kwa kuogopa kuwa inaweza kuwagharimu zaidi endapo kama gari litaharibikia barabarani.
Upvote
5