SoC04 Tanzania tuitakayo

SoC04 Tanzania tuitakayo

Tanzania Tuitakayo competition threads

Hassan Mambosasa

JF-Expert Member
Joined
Aug 2, 2014
Posts
3,359
Reaction score
4,528
TANZANIA TUITAKAYO

_eda45dcb-697e-476b-b5b2-09b1729a9663.jpeg

Asubuhi na mapema unaamka ndani ya nyumba yako ya wastani, kutokana na kipato chako kutokuwa toshelevu. Homa nayo inakushika, unasita kwenda mihangaikoni siku hiyo. Suluhu pekee ni kuelekea hospitali, uende walau ukachunguzwe na kujulikana ni kipi kinachousibu mwili wako. Huna namna isipokuwa ni kukimbilia huko, ili kama kuna ugonjwa au tatizo kubwa mwilini mwako usaidiwe.


_c76b4ae3-0a04-4a3e-9992-ffa0efd77fc3.jpeg


Hamu yenyewe ya kwenda huko inakujaa hasa, pasipo kuingiwa na ugumu wowote ule. Utaanza vipi kuingiwa na mashaka, wakati hospitali kwenye huduma ni bure, unafanyiwa vipimo vyote na kupewa dawa zote muhimu ikihitajika.

Serikali yako ndiyo inahusika na gharama zote, neema lukuki ya rasilimali ilizonazo imefanya kukaingizwa kiasi kikubwa cha mapato. Wachilia mbali kodi rafiki inayokusanywa kwa wafanyabiashara, ambayo haiwezi kuathiri wala kuwafanya wakwepe kwa kuogopa kukosa faida.

Cha kuhitajika kwako wewe ni kitambulisho cha taifa, ambacho umekipata bure. Hicho ndiyo kiingilio pekee cha kukuwezesha kutibiwa kwako hospitalini. Nacho unacho unaamua kukichukua na kuelekea kituo cha afya moja kwa moja, ukitaka kuwahi zaidi. Si sababu ya kuwepo wagonjwa wengi, la hasha kutokana na ubora wa huduma unayopewa mpaka unatamani kurudi tena na tena.

Kituo cha afya unaingia unakutana na matabibu wanyenyekevu, wauguzi ambao ni wenye nidhamu zote. Wakiwa wengi kiasi kwamba, mlolongo mrefu wa wagonjwa ni nadra sana kuukuta. Inakuchukua muda mfupi sana kupewa huduma kwa unyenyekevu, na pia kuondoka baada ya kumaliza.

Utaacha vipi kutokuwa na hamu ya kukimbilia kituo cha afya? Yaani hata ukijihisi hata uchovu unaweza kudhani ni ugonjwa, unaenda haraka sana ukatibiwe upimwe na vipimo bora vya kisasa viendavyo na wakati.

Basi huko kituoni unatibiwa kwa unyenyekevu mkubwa, mpaka hata kabla ya kupewa dawa unajihisi upo nusu ya kupona. Unaondoka na nguvu kubwa ya kuendelea na mihangaiko mingine, kutokana na huduma kumalizika mapema kuliko kawaida. Huku kumbukumbu kubwa iliyopo kichwani mwako, ikiwa ni kuhusu biashara yako ambayo ulichelewa kwenda kisa ugonjwa.

Inakubidi kutoa simu yako kuangalia saa, unajua wazi hukupoteza muda mwingi kupewa tiba. Kila ukiangalia simu yenyewe napo unajiwa na hamu ya kuingia mtandaoni inakujia upesi sana, kuangalia yaliyopita ya mjini, kuchangia mada mbalimbali za kijamii na zinginezo. Utaachwaje na shauku ya kupita huko? Ilihali unanunua huduma ya mtandao kwa bei nafuu, bado huko mitandaoni serikali yako imekuwezesha kutoa maoni kwa uhuru zaidi, na kuchangia mada mbalimbali. Si hilo tu bali imekuwekea sera imara sana na zisizo kandamizi, mpaka unaweza kutangaza biashara yako na kuifanya nyingine kwa njia hiyo, pasipo hata kuhitaji gharama kubwa.

Serikali ishajiwezesha yenyewe kwa kuingiza mapato mengi kutokana na rasilimali zilizopo, kodi, pia kuwekeza zaidi kwenye vitega uchumi vingine. Mapato yamekuwa yakibaki mengi kwa asilimia kubwa. Kutokana na kuwa bajeti ya kujiweza yenye kufanya wakajiweza vilivyo, kiasi kwamba wakaboresha huduma zingine, sambamba na kupunguza mkopo na uepukaji kukopa.

Hamu ya kuingia mtandaoni kila mara lazima iwepo hapo, unaishia kuingia wakati huo ukichukua usafiri wa umma kuelekea ilipo biashara yako. Unakaa kwenye siti ukiutazama mji unayoishi. Uliyosheheni miundombinu ya kisasa, kiasi kwamba msongamano wa magari haupo kabisa, inakuchukua muda mfupi sana hadi kufika katikati ya mji.


OIG1.jpeg

Mjini hapo na hata vijijini kuna chaguzi ya usafiri wa umma wa kuutumia, kati ya basi au treni vyote ni rahisi kuvipata kutokana na miundombinu yake kujengwa kila mahali. Kiasi kwamba raia waligawanyika na kutumia mahali walipoona, kunawafaa wao kufika huko waendapo. Yote ni matunda ya serikali kusimamia mapato vyema na kupunguza matumizi yasiyo maana, asilimia kubwa ya miradi ikikulenga wewe na changamoto zako kuliko kuboresha maisha ya viongozi pekee.


OIG4.3DTsnHrvCCH05nCv.jpeg

Hadi unajivunia wazi kuishi nchi uliyopo, ambayo viongozi wake hukujali wewe kwanza kabla ya kuangalia mengineyo. Kiasi kwamba unakaribia kupita kituo ulichotakiwa kushuka, kisa tu kushangaa neema za mji uliyopo na huduma zake.

Taifa ambalo sera zake za kodi hadi nyinginezo zimekuwa ni rafiki kwa asilimia kubwa, mpaka ubunifu wa ndani umekua na kupelekea kuibuka viwanda mbalimbali. Ukafanya uagizaji bidhaa kutoka nje upungue tena, si hilo tu umepelekea zilizozalishwa hapa ndani zipate soko ndani ya nje ya nchi.


Kituoni unaposhuka unakaribishwa na eneo zuri la kupumzikia abiria lililopo mkabala na duka la biadhaa mbalimbali za umeme, zilizozalishwa ndani kutokana na uwezeshaji uliyowafanya wabunifu kuendelea kuzalisha vitu vipya vitokavyo ndani ya nchi. Unaishia kutabasamu ukikumbuka nyumbani kwako unazo baadhi ya bidhaa zao lao, ambazo ni imara na zimekuwa zikikusaidia kwa namna moja ama nyingine.


OIG1 (1).jpeg

Hatimaye unafika kwenye biashara yako, ndani ya soko maarufu hapo mjini ukiusika na uchuuzi wa vyombo mbalimbali vya majumbani. Napo unajihisi kama vile upo peponi, kila unapoangalia jengo hilo lililojengwa kwa mapato ya ndani, ukafanikiwa kupata eneo la kufanyia biashara ambalo ndiyo linalokupa ulaji wa kila siku. Lenye mifumo safi ya taka na masuala mengine yote, kiasi cha kuepuka magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

Taifa lako sikivu lenye kufanyia kazi kila kero yenu, na pia kufuata maoni mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa. Ndiyo hilohilo limekuja kuwafikisha hapo, kutokana na kukubali mapungufu waliyonayo na kuyafanyia kazi. Kutoruhusu watumishi wazembe kuendelea kuwepo, zaidi ya kuwaadhibu wote na kuchochea uwajibikaji kwa asilimia kubwa.


OIG2.jpeg

Haki zako zote za msingi unapatiwa na pia kusikilizwa pasi na kujali una hadhi gani kijamii. Bado watoto wako wanasomeshwa bure kuanzia msingi mpaka kufikia chuo kikuu, wakipitia masomo ambayo huchochea ubunifu kwa asilimia kubwa. Si hilo tu wanaoajiriwa napo ajira nazo zikiwa na uhakika. Kiasi kwamba hali za watu wa chini, ambao nao ni wachangiaji wakubwa wa mapato imeboreshwa.

“Samahani kaka, daktari hana nafasi kwa leo njoo wiki ijayo”, maneno ya muuguzi aliyepo mbele yangu, niliyekuwa nikipanga kuomba kuonana na Daktari bingwa, ndiyo yakanirudisha kwenye uhalisia.

Kwamba nipo nchi ambayo yenye mambo tofauti na niliyoyawaza. Nipo mahali ambapo nimepata shida sana ya usafiri mpaka kuja kufika hapa kituo cha afya. Ninapohitajika kugharamia kwa kiasi kikubwa cha pesa kuja kuonana na mtaalamu, ila napo ana idadi maalum ya wagonjwa anaonana nao, na imeshatimia, napawa kurudi nilipotoka bila huduma.


OIG3.jpeg

Shida hizi nazo zimenifanya nikaota huku nimefumbua macho, nikisubiri kujiandikisha kupata huduma. Mahali ambapo hata nikiuliza kwanini kuna utaratibu huo wa idadi maalum, nahofia ninaweza kupokea kauli isiyo rafiki nikaishia kuongeza shinikizo la damu.

Lau kama tungekuwa na watu wenye maono tungefika hatua zile nilizoziwaza, na ile ndiyo Tanzania tuitakayo. Sielewi tutakuja kufikia lini, tuondokane na adha hizi.
 
Upvote 3
Mods naomba ubadilishe kichwa cha uzi kiwe TANZANIA TUITAKAYO simu yako imepost kimakosa sijamaliza kukiandika
 
Back
Top Bottom