SoC02 Tanzania ya Sanaa

SoC02 Tanzania ya Sanaa

Stories of Change - 2022 Competition

clever_kid

New Member
Joined
May 8, 2018
Posts
1
Reaction score
0
Sanaa inaweza kutumika kuwasilisha fikra au mawazo yaliyo ndani ya akili ya mtu. Wasanii hutumia ufundi na ujuzi mbalimbali kubadili fikra na mawazo yao kuwa vitu vinavyovutia kwa hadhira zao.
Kazi za Sanaa zinaweza kuonekana kupitia tanzu za fasihi, uchoraji, ususi, uchongaji, ufinyanzi, uimbaji, uigizaji n.k.

Zifuatazo ni umuhimu wa kazi za Sanaa:
• Sanaa hutumika kudumisha mila na desturi za nchi husika. Mfano, ngoma za asili, mavazi ya asili, nyimbo na maigizo kwa lugha ya kiswahli zenye maadili ya kitanzania n.k.
• Sanaa pia hutumika kama nyenzo ya kutengeneza jamii yenye maadili kupitia maonyo au mafunzo mbalimbali yaliyopo ndani ya kazi ya Sanaa husika.
• Kutumika kubadilisha muonekano wa mahali kwa mfano, picha za ukutani
• Inaleta mvuto wa vipaji kwa wengine, biashara na uwekezaji
• Ni kivutio kwa watalii
• Inachochea hali ya uchumi na ubunifu
• Kuunganisha jamii mbalimbali ndani na nje ya nchi
• Kuzipa jamii mawazo mapya au mageni
• Hubadilisha namna ya watu kufikiri, kutenda, kuona kwa upande mwingine

Katika nchi ya Tanzania Sanaa bado haijapewa kipaumbele kama fani zingine. Chuo cha Sanaa kinachotoa elimu hasa ya Sanaa na utamaduni ni kimoja tu nchi nzima, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuBa) na kinahudumia Afrika mashariki nzima lakini bado hakina viwango vya kimataifa. Vyuo vingine vinavyotoa elimu ya Sanaa na utamaduni ni Chuo Kikuu cha Dar es salaam (Udsm), Chuo kikuu Makumira, Chuo kikuu Mount Meru, na Chuo kikuu cha Dodoma zenye idara ndogo ndogo za sanaa.

Wazazi na walezi wengi huona Sanaa kama uhuni hivyo hulazimisha Watoto wao kujiunga na fani nyingine wanazotaka wao. Hii hupelekea kuzalisha kizazi cha wafanyakazi wasio na weledi, upendo na uzalendo katika fani au kazi wanazofanya, matokeo yake ni ufisadi na kiwango duni cha utendaji kazi.

Kuna mifano mingi ya watu waliofanikiwa kwa kufanya kazi na vitu wanavyovipenda ikiwemo katika Sanaa. Hivyo badala ya kukatisha tamaa za Watoto wenye ndoto katika Sanaa na kufikiria kwamba ni uhuni ni vyema kuwapa moyo na motisha stahiki ili kuwasaidia kukuza kile wanachokipenda kwanzia wakiwa na umri mdogo ili wanapokua wakubwa wawe na ujuzi wa viwango vya juu Zaidi kuliko kuanzia kujifunza ukubwani ambapo akili huwa imechoka,Mambo mengi ya kimaisha ambayo yanachangia kushindwa kubuni kazi sahihi na zenye ubora ukilinganisha na vipaji vya umri mdogo.

Serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya maendeleo yanaweza kuboresha vyuo vya Sanaa na kuvifanya kuwa na viwango Bora vya (kimataifa) katika Nyanja zote, majengo, rasilimali watu, mazingira, elimu inayotolewa, wakufunzi na pia kutoa motisha Zaidi katika Sanaa mbalimbali ili watu waweze kufanya vitu vikubwa Zaidi.

Kwa mfano, TaSuBa hufanya matamasha kila mwaka yenye lengo la kukuza vipaji, ambapo huleta wasanii wakubwa kwa kushirikiana na wanafunzi kutumbuiza na wengine huchukuliwa kwenda kukuza na kuonesha Zaidi vipaji na kazi zao.

Mfano mwingine ni taasisi ya Twaweza ikishirikiana na Nafasi Art Space kuandaa mashindano ya Sanaa na maonesho 2017, ambapo mshindi wa kwanza alipewa kompyuta mpakato na nafasi ya kazi kwa vitendo Nafasi Art Space na mshindi wa pili na wa tatu kupewa kompyuta mpakato kila mmoja.

Hivyo serikali kushirikiana na mashirika mengine ya binafsi yanaweza kubuni njia Zaidi za kuhamasisha Watu mbalimbali katika kujihusisha na Sanaa mbalimbali kwa kutoa motisha nono. Kwa kufanya hivyo Sanaa itakua Zaidi na hata kufungua njia kwa wanafunzi kwa ufadhili, kualikwa kufanya kazi sehemu kubwa na zinazotambulika na kutanua wigo Zaidi kwa kuwakutanisha na wasanii wakongwe ndani na nje ya nchi na hata kukuza uchumi wa taifa kupitia kazi za Sanaa zitakazozalishwa kama matokeo ya mwingiliano huo.

Tena kunatakiwa kuwe na mwingiliano baina ya taasisi na vyuo vya Sanaa na utamaduni, sio vya ndani ya nchi tu bali hata vya nje ya nchi ili kuweza kutanua wigo wa elimu na ujuzi mbalimbali katika Sanaa.

Sanaa za aina zote zinapaswa kupewa kipaumbele na motisha ileile ionekanayo kupewa wasanii wa muziki au katika uigizaji kwasababu ukweli ni kwamba Sanaa zingine zimesahaulika mfano uchoraji, ubunifu wa mavazi, uchongaji, ufinyanzi, ambazo zote huweza kuleta mabadiliko chanya kwa watu binafsi na hata taifa kwa ujumla.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom