Maonesho ya uagizaji ya China (CIIE) yamemalizika hivi karibuni mjini Shanghai. Maonesho haya ambayo safari hii ni ya awamu ya saba, yamefanyika kwa mafanikio makubwa kwani nchi nyingi zaidi zimeshiriki na kupiku idadi ya nchi shiriki za mwaka uliopita. Likiwa ni jukwaa la ufunguaji milango na kutangaza bidhaa katika dunia nzima, maonesho ya CIIE ambayo yameanza kufanyika tangu mwaka 2018 yamekuwa yakitoa kipaumbele zaidi kwa nchi za Afrika ili kuweza kuingia kwenye soko la dunia kwa urahisi zaidi.
Kwa baadhi ya nchi kama vile Tanzania, maonesho haya hayakuwa ya kutafuta soko la bidhaa ama uwekezaji kwenye biashara tu, bali yalikuwa ni maonesho ya kimkakati zaidi, ambapo fursa nyingi za uwekezaji kwenye miundombinu ya sekta mbalimbali zilitumiwa na nchi hii.
China na Tanzania mwaka huu zinaadhimisha miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia, ili kuenzi maadhimisho haya, Tanzania safari hii imeteuliwa kuwa miongoni mwa nchi mgeni wa heshima kwenye maonesho haya. Na katika kuheshimu nia ya China, Tanzania ilileta ugeni mzito kwenye maonesho haya ya uagizaji ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Dokta Hussein Ali Mwinyi aliongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki kwenye maonesho na kuhudhuria sherehe za ufunguzi.
Alipokuwa Shanghai Dokta Mwinyi alipata fursa ya kukutana na makampuni makubwa ya China ambayo yameonesha nia ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali za viziwani Zanzibar. Hii ni habari njema kwa Tanzania kwani licha ya maonesho haya kuipatia fursa kubwa nchi hii kupata soko la bidhaa zake nchini China, pia matunda yake yameonekana kwenye sekta ya utalii.
Ifahamike kuwa mbali na vyanzo vingine Zanzibar pia inategemea mapato yake kupitia utalii. Hivyo kupitia maonesho haya. Dk. Hussein Ali Mwinyi, alikutana na ujumbe kutoka Kampuni ya Wuhan Guangfu Tangyuan Buer Cultural Development chini ya mwenyeji wake, Bwana Wenbao Tan, Mkurugenzi Mkuu kutoka Shirika la China-Africa Industrial Cooperation Promotion Center.
Kampuni ya Wuhan Guangfu Tangyuan Buer Cultural Development, inayojishughulisha na kukuza na kuboresha utamaduni wa Kichina, uwekezaji katika utalii, uandaaji wa matamasha ya sanaa, utamaduni, na ubunifu wa kidijitali, imeonesha nia ya kuwekeza Zanzibar kupitia mradi wa Eneo Maalumu la Mabadilishano ya Utamaduni kati ya Chinana Tanzania.
Lengo la mradi huu wa kijiji cha utalii ni kubadilishana tamaduni na utakuwa na vituo vya Muziki, Kazi za Mikono, Uchoraji, utamaduni wa makabila mbalimbali, pamoja na utamaduni wa jadi kutoka China. Ujumbe wa China unatarajiwa kutembelea Zanzibar mwezi Disemba 2024 ili kuweza kukamilisha taratibu za mradi ho.
Maeneo mengine ambayo yalifuatiliwa na Tanzania kwenye maeonesho haya ya CIIE ni ujenzi Bandari ya Mangapwani, Unguja ambapo Dkt Mwinyi alifanya mazungumzo na Bw. Bai Yin Zhan na ujumbe wake kutoka kampuni ya China Harbour Engineering Co. Ltd yenye uzoefu wa kujenga miradi ya kimkakati kama vile ujenzi wa bandari, upanuzi, na uboreshaji wa miundombinu kwa viwango vya kimataifa. Hivi sasa serikali ya Mapinduzi Zanzibar ipo katika mchakato wa kuipa dhamana kampuni hiyo ya China kujenga Bandari hii ya Mangapwani.
CIIE imeonesha dhamira thabiti ya China ya kufungua mlango, ambayo imeongeza imani ya makampuni mengi ya kigeni kutaka kuwekeza katika nchi mbalimbali za Afrika. Kutokana na dhamira hii ya China hata nchi zinazowekezwa za Afrika pia zimekuwa na imani kubwa na makampuni ya China yanayowekeza. Ndio maana Tanzania inaichukulia China kama rafiki namba moja anayeaminika hasa katika kutekeleza ahadi zake inazotoa kwenye majukwaa mbalimbali yakiwemo Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) na Mpango wa “Ukanda Mmoja Njia Moja”.