Gavana wa Kaunti ya Nyeri nchini Kenya, Dr. Wahome Gakuru, amefariki mapema leo Jumanne kufuatia ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Kabati, katika barabara kuu ya Thika-Sagana katika Kaunti ya Murang'a.
Alikimbizwa katika Hospitali ya Thika Level 5 kwa matibabu ya dharura lakini akaaga dunia.
Kamishna wa Kaunti Murang'a John Elungata alithibitisha kifo cha hicho.
Bwana Elungata alisema kuwa Kabati ni eneo hatari sana na madereva hukosa mwelekeo kila mvua inaponyesha.
Maafisa wa polisi wamesema kuwa gari la Gavana huyo lilikuwa na abiria wanne wakati wa ajali hiyo, akiwemo msaidizi wake wa kibinafsi, mlinzi wake na dereva.
Mkono na mguu wa msaidizi wake wa kibinafsi ilivyunjika huku miguu ya msaidizi wake ikijeruhiwa vibaya huku dereva akidaiwa kuwa katika hali nzuri.
Polisi wanasema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gurudumo moja la gari hilo kupasuka wakati mvua kali ilipokuwa ikinyesha.
Mwili wa Gavana huyo umesafirishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee mjini Nairobi.
Inadaiwa kuwa Gavana huyo alikuwa akielekea kuhudhuria kipindi kimoja cha redio na runinga wakati gari lake lilipokumbwa na ajali hiyo.
Dr. Gakuru ni Gavana wa pili wa Nyeri kufariki dunia wakati yupo madarakani baada ya Gavana Nderitu Gachagua kufariki mwezi Februari mwaka huu.