SoC02 Tanzia: Runinga ni muuaji mwenye sura ya kuvutia

SoC02 Tanzia: Runinga ni muuaji mwenye sura ya kuvutia

Stories of Change - 2022 Competition

Salum Makamba

Member
Joined
Feb 26, 2018
Posts
7
Reaction score
6
Mara nyingi ni ngumu kwa binadamu wengi kuchukua hatua mpaka jambo zito linapotokea aidha kwao au kwa watu wao wa karibu. Tena katika wakati tuliopo ambao wengi wetu tunaongozwa na hisia kuliko tafakuri za kina, imefikia hatua hata balaa linapomtokea mtu wa karibu tunayemfahamu basi hatujifunzi.

Wengi hunyanyua vidole vyetu vya shahada na kumnyooshea. Tutamtuhumu ni mzembe, asiye mwajibikaji na mwenye kujifanya mjuzi ilhali hakuna ajuacho. Ile hekima tuliyoachiwa na wazee wetu kuwa, “Mwenzako akinyolewa zako tia maji” sisi tumeichimbia shimo na kuizika. Na kama haitoshi pahali tulipoizika tumepajenga kwa zege na kupasakafu kwa saruji ili tu ibaki huko milele, kisha sisi na vizazi vyetu tuendelee kuishi katika mtindo wa “sahau” na “puuzia” tuliouchagua.

Ndugu zangu,

Nakumbuka wakati wengi wetu tunakua, muda wa kulala ilikuwa ni baada ya kusikiliza au kutazama Taarifa ya Habari. Nyakati zimebadilika. Kama ambavyo heshima ya kwenye harusi imetoweka, ndivyo ambavyo hata nidhamu ya malezi tumeisukutua kinywani na kuitema mchangani. Leo hii imekuwa kawaida kwa Bi. Harusi kuvaa mavazi yenye kuonyesha sehemu kubwa ya maungo mbele ya Baba na Mama Mkwe wake na kama haitoshi akashindua na kuidengua nyonga yake bila haya ukumbini. Akitokea wa kuhoji ataishia kushushuliwa kuwa ni siku yake aachwe ainjoi (afurahi).

Si hilo tu, sasa ni mwiko hata kumkanya mtoto uliyemzidi umri pindi unapomwona amepotoka au anaelekea katika mwendo huo. Wazazi wasio na soni utasikia wakipaza sauti kuwa mtoto wao asiguswe kwani hakuna mtu anayefahamu uchungu waliopitia wakati wakiwa leba (Chumba cha Kujifungulia Wajawazito). Hekima nyingine ya wazee wetu, “Mtoto wa mwenzio ni wako” nayo tumeibinya na kuisiliba kwa hasira mithili ya kunguni tuliyemkuta amejificha kwenye kona ya kitanda baada ya kututaabisha usiku kucha na kutusababishia usingizi wa mang’amung’amu.

Ndugu zangu,

Kuna msemo unasema, "Usiwalee wanao kama ulivyolelewa wewe, kwa sababu wamezaliwa katika wakati tofauti na ule uliozaliwa wewe." Kauli hii naiunga mkono, lakini isiwafanye wazazi wasichukue tahadhari inavyopaswa. Maana mchelea mwana kulia hulia mwenyewe na siku atakayochuma janga popote awapo, basi hapatakuwa wa wakushiriki naye karamu isipokuwa wazazi wake.

Si siri. Kuna nyumba nyingi sana siku hizi ambazo wazazi wanapelekeshwa na watoto wao (tena wala si watoto walio katika balehe). Na tunayaona! Yaani mtoto anabishana na mzazi wake na anashinda. Na mzazi anamtazama tu huku akisema, "Mtoto ana kiburi sana huyu," kisha anamwacha na alitakalo. Hili jambo ni moto mkali na balaa!

Leo hii si ajabu kukutana na mzazi ambaye katika ukuaji wake, sikukuu alikuwa akinunuliwa magauni ya kumwaga (ambayo hujichanua watoto wakijizungusha) akiwa na mtoto wake wa kike aliyepevuka ambaye kavaa chupi na vesti au pensi ya juu ya mapaja wakizunguka Mlimani City huku wakizungumza vingereza. Hii inachukuliwa kama kwenda na wakati, ufahari na utajiri. Ila kiuhalisia ni moja ya vitu hatari sana. Kisingizio cha utandawazi na “exposure” kimetuondoshea haya na heshima ambazo wazazi wetu walisimama kidete kutujengea. Tunafanya mengi yasiyofaa ili kuwafurahisha marafiki na jamii, wasije kutuita “washamba” na tusiokwenda na wakati hata kama tuendako ni kwenye kina cha upotevu kilichojaa tope.

Ndugu zangu,

Niachane na utangulizi huo ambao ulidhamiria kuiweka sawa akili yako kwa ajili ya dhumuni kusudiwa. Lengo hasa la andiko hili ni kuhusiana na Vipindi vya Runinga ambavyo wazazi mnawaacha watoto wenu wavitazame. Je! Mmejiridhisha ni sahihi kwa umri walionao? Au liwalo na liwe.

Siku hizi nyumba nyingi hazitazami Taarifa ya Habari. Ni tamthiliya mchana hadi jioni. Mpaka watoto wadogo wamekuwa waathirika wakubwa wa tamthiliya hizo. Unaweza kukutana na mtoto wa Darasa la Tano asiyejua hata hadithi kumi kichwani ila anaweza kukuelezea tamthiliya zote zinazoendelea katika televisheni tofautitofauti.

Si hivyo tu, baadhi ya wazazi huwaambia watoto wao watazame kisha baadaye kuomba wawasimulie. Je! Una hakika na anachokitazama mwanao? Ikiwa kinaijenga au kuibomoa akili yake?

Ndugu zangu,

Tamthiliya, filamu na hata baadhi ya habari huwa hazifai kwa watu wa umri fulani. Nchi zilizoendelea ni jambo ambalo huzingatiwa sana. Tamthiliya zilizo maarufu katika majumba yetu pamoja na kuhaririwa ili kupunguzwa baadhi ya maeneo hatari bado nyingi hazifai kutazamwa na watoto.

Watu wengi hudhani watoto hawapaswi kutazama "ngono" tu. Akiambiwa filamu au tamthiliya fulani ni "Over 18" basi hufikiri imesheheni "ngono" mwanzo mwisho. Si hivyo! Kuna mambo mengi yanayotazamwa ili kuamua filamu au tamthiliya inawafaa watu wa umri gani. Baadhi ya mambo hayo ni:-

•Uoneshwaji wa tabia zisizofaa kama 'bullying.'

•Tabia na matendo ya hatari ambayo watoto wanaweza kuiga.

•Kuhamasisha tabia mbaya kama utumiaji wa madawa, utumiaji wa silaha etc

•Matumizi ya lugha kali zinaweza zisiwe za matusi ila ni lugha nzito. Pamoja na matendo ya kibaguzi na unyanyapaa.

•Vitisho, mauaji pamoja na vitendo ambavyo vinaweza kuwatia hofu watazamaji (mliowahi kutazama filamu za kutisha mnajua hili).

•Uzungumzaji wa wahusika, mitembeo yao na mambo mengine kadha wa kadha.

Je, tamthiliya zilizo mashuhuri majumbani mwetu zina mambo hayo au hazina? Unatazama na mwanao au peke yako? Tafakari chukua hatua.

Nimeandika andiko hili kwa sababu, kwa wale mnaofuatilia tamthiliya. Ipo moja pendwa sana yenye kurushwa na moja ya kampuni mashuhuri sana hapa nchini kwetu (Tanzania) ambayo, kuna siku ilionyesha mtu amening'inizwa na kamba kama anataka kunyongwa lakini hakufa. Alifanikiwa kuteremka salama na kutoroka.

Mtoto mmoja wa jirani yangu amefariki kwa kujinyonga na kamba. Alichukua na kwenda kujining'iniza mtini. Mlezi wake anasema, "Wakati tunatazama ile tamthiliya aliniuliza; Mbona huyo amewekwa kama kunyongwa ila hajafa. Kumbe mtu anaweza kunyongwa na asife?"

Yeye alipuuza akiamini ni akili za kitoto. Mtoto kajaribu kwenye mpera wa nyumbani kwao. Sasa hatunaye. Watu wengi msibani wanamlaumu yule mtoto kwamba alikuwa amezidi sana "utundu." Je! Nawe unaungana nao?

Leo kwa huyu, kesho kwangu, mtondogoo kwako. Chukua hatua. Hata kama unamlea mtoto wako kizunguzungu na kimayaimayai. Usisahau miiko na taratibu walizokufunza wazazi wako ambazo zimekufanya uwe na tabia njema waliyokusifia wengine na ambayo hata wewe unaipenda.

Utandawazi, misukumo ya marafiki na jamii visikufanye uipuuze miiko ya muhimu katika malezi. Siku ukichuma janga utakula mwenyewe na wa kwenu. Uwafurahishao watakupa pole na kuendelea na maisha yao.

Kuwa macho na watazamavyo wanao runingani.

Change or Perish!

Mwanagenzi.
 
Upvote 5
Andiko zuri sana hili. Naunga mkono hoja. Hili linaenda sambamba na matumizi ya smarphones.

Ni vema wazazi wafanye ukaguzi wa mara kwa mara kujua namna watoto wanavyotumia smartphones zao.
 
Andiko zuri sana hili. Naunga mkono hoja. Hili linaenda sambamba na matumizi ya smarphones.

Ni vema wazazi wafanye ukaguzi wa mara kwa mara kujua namna watoto wanavyotumia smartphones zao.
Kabisa mkuu. Ni jambo la muhimu sana kuzingatiwa. Nyongeza makini sana hii.
 
Back
Top Bottom