Ni kweli ni VICOBA na siyo VIKOBA, na tafsri ni sahihi. VICOBA ni utaratibu wa watu mnaofahamiana wa kujikusanyia pesa kwa ajili ya maendeleo yenu wenyewe. Wazo hili lilianzia "vijijini" kwa utaratibu huo lakini baadaye likaboreshwa na kufanyiwa mabadiliko makubwa ili kuendana na mahitaji ya watu wote - wa mijini na vijijini. Utaratibu huu unawawezesha watu waliokubaliana, kwa hiari yao wenyewe kujikusanyia pesa kwa njia ya HISA NA MFUKO WA JAMII. Kiutaratbu, na
traditionally, kikundi hiki kinaweza kuwa na watu hadi 30 na mnakuwa na uongozi uliochaguliwa wa Mwenyekiti, Katibu, Mweka Hazina, Wakusanya au Wapokea Pesa na Mtunza Nidhamu.
Kila mkutanapo, hususani mara moja kwa wiki, mtanunua hisa kwa thamani mtakayo amua, inaweza kuwa shilingi 2,000/= au 3,000/= au kiasi chochote kwa hisa moja kufuatana na uwezo wa wana kikundi.Kila mwanachama anatakiwa anunue angalau hisa moja (1) kila mkutanapo, hiki ni kiasi cha chini na cha juu ni hisa tano (5). Huu ndio mchango wa mwana kikundi binafsi na hisa hizi ndiyo kama amana yake mtakapoanza kukopeshana. Kuhusu Mfuko wa Jamii, huu ni kwa ajili ya kusaidiana katika kikundi chenu na kila mwanachama analazimika kuuchangia kila wiki kwa kiasi mlichokubaliana aidha sh.1,000/= au 2,000/= n.k. Kitu kimoja au jambo moja la muhimu ni kuwa VICOBA siyo Biblia au Msahafu kwa hiyo mnaweza kupanga mambo yenu kufuatana na mahitaji na uwezo wenu (nimesikia kuna VICOBA moja huko Oysterbay, wanunua hisa kwa sh. 50,000/=!) Hayo ni maelezo machache ya utangulizi, kama una maswali zaidi au kuna mahali hapajaeleweka uliza, ila naweza kuwa nachelewa kujibu kwani siingi JF kila siku. Asante na ubarikiwe.