Kuna msemo kwamba "kwa kadiri vitu vinavyobadilika, ndivyo vinavyobakia vile vile". Kuna mabadiliko makubwa yametokea nchini lakini ni mabadiliko ambayo bado yanaonesha kuwa vitu vimebakia vile vile japo kuwa vilipaswa kubadilika pia. Lakini kubwa zaidi ni je mabadiliko tunayoyaona yamesababisha taifa kubadilika kwa ubora zaidi au yanapaswa kusababisha taifa kubadilika kwa ubora zaidi? Lakini swali kubwa zaidi ni tunaweza kupima vipi matokeo ya mabadiliko hayo?
Kwangu mimi naamini mabadiliko makubwa yametokea upande wa Bunge. Kwanza upande wa ubora na uthubutu wa uchangiaji lakini pia kufungiwa kwa Zitto kulisababisha watu kuliona Bunge kwa jinsi lilivyo hasa kuwa limejaa wabunge wa CCM ambao wako tayari kufanya lolote kutetea serikali yao.
Jinsi Bunge lilivyotumika kumfungia Zitto kulisababisha wananchi kuelewa kuwa Bunge linaweza kufanya lolote lile hasa likiwa limejaa watu wa chama kimoja. Hata hivyo CCM baada ya kugundua jinsi walivyoboronga wakageuka na kufanya triangulation ya upinzani na wao wenyewe wakaanza kuzungumza kama wapinzani na matokeo yake ni mashujaa wa Februari, na kuibuka kwa wabunge kama yule wa Sikonge, n.k Hivyo, utaona kuwa matokeo makubwa ya suala la Buzwagi ni kuimarika kwa wabunge wa CCM na hivyo CCM kujijengea mashujaa wapinzani ndani yake na kuwakubali.
Huko nyuma ilikuwa mbunge au kiongozi wa CCM akisema kitu kinyume na "vikao vya chama" basi atakabwa na lile dubwasha la "nidhamu ya chama". Kuanzia sakata la Buzwagi na baadaye mjadala wa Richmond, CCM imepoteza uwezo wake wa kuzima mijadala kinyemela. Imejaribu Butiama lakini pasipo mafanikio makubwa na sasa ndani ya CCM kuna new alignment of political positions. CCM imewahi kuwa na makundi lakini hakuna wakati ambapo imewahi kuwa na makundi yenye milengo ya kibinafsi kama wakati huu. Hii alignment inayoendelea ndiyo (naamini) kiini cha kuvunjika na kuanguka kwa CCM.
Lakini jingine ambalo limedhihirishwa tangia mwaka jana ni kuwa wapinzani bado hawajajua mchezo wa siasa. Naamini hakuna wakati ambapo upinzani Tanzania ungeweza kujijenga na kukita katika mioyo ya Watanzania kama wakati wa sakata la Buzwagi.
Na hasa upande wa Chadema. Chadema ilishindwa kutumia nafasi waliyopewa na fate ya kujipatia wanachama wapya, kutangaza sera zake na kusahihisha mambo yote yaliyokuwa yanakisonga chama hicho toka ndani na kuibuka better, bigger and stronger. Kosa kubwa walilolifanya ni kudhania (kwa makosa) mjadala wa Buzwagi ulikuwa ni suala la "Kitaifa" tu na siyo la chama. Na kosa hilo (nilisema wakati ule) linadhihirika sasa hivi katika ushirikiano wao wenye mashaka na vyama vya TLP, CUF na NCCR.
Sasa hivi kufuatia msiba wa Wangwe vyama vya TLP, CUF na NCCR vimeamua kutumia nafasi hii kujijenga na kujitafutia jimbo kule Tarime na kuna uwezekano mkubwa kwa NCCR kuchukua jimbo hilo wakikubaliana na TLP kuwaunga mkono kule Biharamulo. Wakifanya hivyo vyama hivyo viwili vitarudi na angalau mbunge mmoja mmoja Bungeni.
Lakini pia kuna jingine limedhihirika nalo ni kutokana na hilo la Buzwagi; Chadema na wabunge wake walionekana (kama bado sijui) kuwa ndio watetezi wa raslimali za nchi na wabunge wake vinara katika vita dhidi ya ufisadi. Wanasiasa wake walisimama kama wajenga hoja wakubwa pale Temeke, na wakasimama Bungeni kama mashujaa wasio na mzaha. Kitu kimoja kilikosekana na naamini bado kinakosekana. Uongozi.
Nasema uongozi na hapa simaanishi watu wenye vyeo vya uongozi kwani nitakuwa si mkweli. Uongozi ninao uzungumzia ni uwezo wa kutambua tatizo, kulichambua katika sehemu zake, kuona uzito wake na kutafakari njia za kulikabili. Uongozi huo ni wa kuweza kutafuta usuluhishi wa matatizo ndani ya chama na kuhakikisha kuwa chama bado kinaendelea kuwa kimoja, imara, na chenye msimamo mmoja.
Binafsi naamini kuwa suala la hoja za Wangwe na watu waliokuwa wanamuunga mkono lilikuwa ni suala la hoja dhidi ya hoja na lingeshughulikiwa kwa kujibiwa na mazungumzo na siyo mabishano na tuhuma. Ninaelewa watu wako tofauti na personalities tofauti. NI wazi kulikuwa/bado upo mgongano wa personalities za Wangwe na Mbowe. Mgongano huu ulikuwa ni laana kwa Chadema ingawa ungeweza kutumika kuwa baraka kubwa sana. Waswahilli wanasema "mafahali wawili hawaki zizi moja"; lakini naamini "mafahali wawili wanaweza kulima pamoja".
Wangwe na Mbowe wasingelazimika kukaa pamoja lakini walipoamua kufungwa nira pamoja (Mwenyekiti na Kaimu Makamu Mwenyekiti) kama ng'ombe wa maksai katika kulima shamba la Chadema lilikuwa ni jukumu lao kuhakikisha wanalima pamoja. Hilo halikuwezekana kwani inaonekana katika kufanya hivyo mmoja alitaka aanzishe juu na mwingine alitaka aanzie chini. Na kwa kufanya hivyo ku polarize the party. Ni wazi kuwa wanasiasa hao wawili wasingeweza kukaa katika nafasi hizo wakiwa wanarushiana tuhuma nzito kama tulizozishuhudia. Binafsi naamini ilikuwa ni ukosefu mkubwa wa kiuongozi hadi kufikia walipofikia. Labda ililazimu kufika huko lakini naamini kuna mambo ambayo yangeweza kufanywa na mwisho wake ingawa ungeendeleza tofauti ya mambo fulani kwa hakika ungefanya chama chao kiendelee kuonesha mfano.
Kosa ambalo naamini bado lipo katika Chadema ni wao pia kwa namna kubwa kufuata mfumo wa muundo wa CCM kama chama. Muundo huu umepitwa na wakati kwani unafuata mfumo wa kikomunisti na una lengo kubwa la control of party machinery. Hauko loose enough to allow dissent while maintaining unity.
6.1.1 Kutakuwa na ngazi saba za uongozi wa Chama kama ifuatavyo:
(a) Ngazi ya Msingi (Shina kwenye CCM)
(b) Tawi
(c) Kata/Wadi
(d) Jimbo/Wilaya
(e) Mkoa
(f) Jimbo.
(g) Taifa - Katiba ya Chadema
Je ingeweza kuwa na muundo mwingine tofauti? ndiyo. Sitalizungumzia hilo kwa sasa.
Kwa upande wa chama cha CUF kwa kweli ni chama ambacho naamini kiko kama na kigugumizi. Kinataka kusema kitu lakini hakisemi ingawa kimsingi kinapaswa kusema jambo hilo. Ndicho chama Kikuu cha upinzani nchini chenye wabunge wengi na wawakilishi wengi.
Lakini mabadiliko tunayoyazungumzia hayajakigusa sana chama hicho na matokeo yake hayaonekani sana upande wa Tanzania bara. Binafsi naamini kuwa CUF ingeweza kuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko na kuwa tishio la CCM Tanzania bara endapo kingeweza kujijenga zaidi bara. CUF kinapokea fedha nyingi zaidi za ruzuku kuliko chama kingine cha upinzani na kina uwezo mkubwa wa kuwa tishio la CCM bara.
Lakini kwa namna wanayoielewa wao inaonekana maslahi yao makubwa yako Zanzibar kuliko bara na hivyo kujikita zaidi Zanzibar. Bado sijajua ni jinsi gani CUF inaweza kusimama na kuwa mtetezi wa maslahi ya Taifa zima na kuongoza vita dhidi ya ufisadi nchini? Kikiwa na raslimali zaidi ya kifedha, kikiwa na wabunge wengi zaidi (kwenye Bunge la Muungano) ni kwanini sauti ya CUF inasikika kama mwangwi tu?
Ndio maana utaona hata juzi walipotoa kauli ya kuwalalamikia wafadhili haikuchukua muda Ubalozi wa Marekani ukajibu. Nina uhakika CUF ni lile "JITU LILILOLALA) (the sleeping giant). Naamini kwenye mjadala mzima wa ufisadi CUF imekuwa ni kama mpiga makofi wakati wa ngoma na yeye mwenyewe hataki kucheza. Sielewi kama ulikuwa ni mkakati kuwa Chadema ndio wacheze na CUF washangilie au ni kuwa CUF hawataki kuingilia sana kashfa zinazohusu bara?
CUF inaweza kabisa kuwa chama mbadala wa CCM kwanza kwa sababu hakijagubikwa na kashfa nzito au misuko suko ya juu ya uongozi na ile iliyotokea imekuwa ikihusu Zanzibar zaidi kuliko CUF bara. Na hata wakati wanachama wake walipomeguka na kurudi CCM CUF haikupigiwa kelele sana. Inawezekana ni kutokana na uongozi wa Seif na Dr. Lipumba au uthabiti wa jinsi ambavyo viongozi hao wawili wamekuwa wakiiendesha CUF kwani hata wakati ambapo unaweza kufikiri CUF inaweza kulipuka Zanzibar utaona kuwa mambo yanaziimwa chini kwa chini.
Nilitarajia kuona CUF baada ya kupitia migogoro ya kiuongozi na tuhuma za hapa na pale wangeweza kujikita katika kukiimarisha chama chao bara na kufanya siyo tu wakubalike zaidi lakini waonekane ni chama cha kitaifa zaidi. Hili bado halijatokea. Lakini swali kubwa kuhusu ni CUF ni je CUF inaweza kuendelea kuwa na nguvu na sura ile ile ya mtetezi wa Zanzibar pasipo Maalim Seif katika nafasi ya uongozi? Je Seif akiondoka CUF itaendelea kuwa moja au itakuwa ni kama yaliyotokea baada ya kifo cha Alexander the Great?
Kwa upande wa CCM, nimekwisha elezea kidogo hapo juu mabadiliko ambayo yametokea. Lakini naamini kuna kubwa zaidi ambalo linatokea ndani ya CCM ni kujiimarisha kwa CCM kutoka ndani. Kwa nje mtu anaweza kuona CCM inagawanyika lakini naamini kinachofanyika sasa ni mkakati wa kujiimarisha kutoka ndani kwa kukubali internal dissent bila kulazimishwa kutoka ndani ya Chama.
Siamini kama sasa hivi CCM itamfukuza mtu kwa kuwa na maoni yasiyo kuwa sera au yasiyo lingana na ilani ya CCM. CCM itamfukuza mtu kwa kula fedha za chama au kuliharibia jina chama kwa vitendo fulani lakini si kwa maoni. Ni kwa sababu hiyo anayetegemea kuwa mama Kilango au Dr. Mwakyembe watatoka CCM kwa sababu ya kupingwa maoni watakuwa wanaota. Wana CCM watatoka pale watakapotambua kuwa hawakaribishwi tena CCM. Sasa hivi CCM inajiandaa kwa kuruhusu wagombea huru na ili kuhakikisha watu wake wanabakia ndani basi ina jiandaa kuruhusu mawazo na fikra tofauti.
Kwa kufanya hivyo, CCM naamini itarudisha nguvu za uamuzi wa mwisho kwa wagombea kufanyika kwenye kura za maoni na ya kuwa kura za maoni zitakuwa ni za mwisho. Watalifanya hili kwa sababu wameshatambua kuwa kuwalazimisha wananchi wamchague mtu wasiyemtaka kumewagharimu sana na gharama kubwa ambayo naamini hadi kesho watakuwa wanaijutia ni kumuengua Dr. Slaa mwaka 1995 licha ya kukubalika kwake Karatu kuliko Patrick Qoro.
Siyo hilo tu hata Tarime ni somo kubwa kwao na pia kilichotokea Bunda watu wanakumbuka. Umaarufu wa wabunge wa kuchaguliwa na kuamka kwa wananchi kifikra kutalazimisha CCM kujenga mazingira ya kutambua kura za maoni kama uamuzi wa mwisho na ya kuwa hakuna tena kubeba wagombea wake.
Nimesema vitu vimebadilika lakini pia vimeendelea kubakia vile vile. Je mabadiliko yote haya tunayoyaona kwenye upande wa siasa yamesababisha mabadiliko ya kiutendaji? Kwa kiasi inawezekana lakini kiukweli bado utendaji wetu uko vile vile kwani bado watendaji hawajajitahidi kushikamana na mabadiliko ya kisiasa.
Matokeo yake, kiutawala na kiutendaji serikalini bado tunahangaika na mambo yale yale, maamuzi mabovu, utawala wa kibabe, na sheria zile zile ambazo zimetufikisha hapa tulipofika leo. Hakujawa na haraka ya kubadilisha vitu kwa haraka. Sheria ya Madini bado ni ile ile, sheria ya Usalama wa Taifa ni ile ile, Mkataba wa Buzwagi ni ule ule, n.k Hatujafanya hima kubadilisha matendo yetu ya kiutawala. Hadi leo hakuna mtu aliyefikishwa mahakamani kwa kosa lililotokana na tuhuma mbalimbali na kuna uwezekano wa kutofikishwa mahakamani.
Safari bado ni ndefu, lakini hata safari ndefu huanzwa kwa hatua moja. Naamini tumepiga hatua moja mbele, tuilinde tusije tukapiga hatua mbili nyuma halafu tukashangilia kuwa "tumepiga hatua tatu"!