SoC04 TASAF ianzishe benki ya maendeleo ya jamii

SoC04 TASAF ianzishe benki ya maendeleo ya jamii

Tanzania Tuitakayo competition threads

Frajoo

Member
Joined
May 28, 2024
Posts
12
Reaction score
3
Utangulizi.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza kutekeleza mradi wa mfuko wa maendeleo ya jamii yaani Tasaf, kuanzia mwaka 2000.Lengo ni kutokomeza umasikini kwa wananchi.

Mpango ukawa ni kujenga kinga ya jamii kiuchumi,na katika katika maboresho ilipofika mwaka 2012 kama sijakosea walianza mpango mpya wa Kunusuru Kaya masikini.Madhumuni ni yalikuwa ni kuongeza kipato na fursa za kujikimu .

Hakika Tasaf imekuwa ikitoa msaada mkubwa kwa wananchi hususani walio masikini kupata huduma za msingi za maisha kama chakula na mahitaji muhimu ya kilasiku.Tasaf imekuwa mlezi wa wajane na mayatima na walemavu,ambao kwa miaka mingi waliishi maisha yasio na uhakika.

Naweza kusema mpango huu wa makusudi umeleta matumaini makubwa na imani ya wananchi kwa Serikali.

Hii ni hatua ya msingi au ya awali katika maendeleo ya wanajamii, lakini kwa muendelezo wake ni pale Kaya masikini zitaweza kujikwamua zenyewe kwa kupata nyenzo za kutengeneza kipato ili kuwa na uchumi imara au tuseme Kujitegemea kiuchumi.

Uhalisia wa Maisha.

Kutokana na changamoto ya kukosa mitaji pia kimsingi Tasaf inawiwa vigumu kumnyanyua kila mwananchi mwenye uhitaji wa kujikwamua kiuchumi.Hapo ndipo wawekezaji wa kiuchumi waliona fursa hio yakaanzishwa makampuni binafsi mengi sana kwa miaka ya 2010 kwenda mbele,yenye kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo.

Kwakuwa kwenye taasisi za ki fedha yaani mabenki wananchi wasio waajiriwa hawakopesheki kwa kukosa sifa au vigezo stahiki vya kupata udhamini,ikapelekea makampuni hayo yakawa ndio mkombozi.

Mikopo hii itolewayo na makampuni haya ya kukopesha imepewa jina jipya maarufu kama’Kausha damu’ kwa kile kinachosemekana kwamba inatoza riba kubwa,hasa ukizingatia mwananchi masikini inakuwa ndio mara yake ya kwanza kufanya biashara , inapotokea ameshindwa kurejesha fedha pamoja na riba hufilisiwa kwa kunyang’anywa mali zilizoorodheshwa kama udhamini, pia hufedheheshwa hivyo huleta matatizo katika familia na hata kusababisha matatizo ya Afya ya akili.

Nafahamu Tasaf inahitaji maboresho ya utekelezaji wa mipango yake, hivyo sio swala geni kuchukua mrejesho kutoka kwa jamii inazozihudumia.

Nikiwa ni mmoja wa mwananchi kutoka kwenye kaya masikini nimeona kuna haja ya Tasaf kujiongeza zaidi ili kuleta taswira halisi ya kuwa Kinga ya jamii au kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa jamii.
Mrobaini wa ‘Mikopo kausha damu’ kwa jamii ni kuanzishwa kwa Benki ya Maendeleo ya Jamii ,kwa lugha ya kigeni tuiite (Community Development Bank.) ambayo dhumuni lake kubwa ni kutoa mikopo kwa riba nafuu zaidi ya taasisi zote zakifedha na makampuni ya kukopesha nchini.

Natambua kila halmashauri kuna fursa ya mikopo kwa vijana na makundi maalumu,lakini kiuhalisia mikopo ile haijawa na tija kwa kukosa usimamizi na ufatiliaji mzuri,upendeleo (Urasimu) kigezo cha kwenda kama kikundi hukwamisha wengi na mapungufu mengi.

Benki hii itakuwa imejikita katika kuwasaidia wajasiriamali hasa kutoka kwenye Kaya masikini,hivyo mfumo wake wa utoaji huduma utakuwa ni tofauti na benki zingine ambazo kimsingi zinajikita kwenye biashara zaidi.Haitakuwa benki ya kutaka faida bali kuongoza rasilimali fedha ziweze kuwafikia Watanzania walio wengi.

Watoa huduma wengi wawe ni wabobezi wa Ujasiriamali,Masoko pamoja na Usimamizi wa fedha kama ilivyo kwa taasisi nyingi.Ieleweke msisitizo upo kwenye kushauri,kufatilia,kusimamia biashara ndogondogo ili kuwainua masikini kwenye jamii zetu.

Umuhimu wa kutekeleza Mpango huu.

1. Kwanza itaziba mianya ya iliojitokeza kwenye mikopo inayotolewa katika halmashauri kwa vikundi vya vijana na makundi maalumu.Pale halmashauri hakuna ufatiliaji mzuri kwa vikundi vinavyopokea mikopo kwaajili ya kuwekeza kwenye ujasiriamali.

2. Kutokana na uhalisia kwamba katika jamii kuna vikundi vichache sana ambavyo vimejipanga kwa kuwa na wazo moja la uwekezaji, kujisajili na kuwa na maelewano ya muda mrefu, hivyo hii benki itatoa mikopo kwa Kaya moja moja na hata vikundi pia.Kama ilivyo kwenye programu zao zingine wanavyofatilia kwa utaratibu mzuri basi hata hii mikopo itafatiliwa kwa mfumo maalumu na kufatilia maendeleo ya biashara zitakazoanzishwa na walengwa na kupata mrejesho kila wanapohitaji.

3. Ni msaada mkubwa kwa vijana wasio na ajira wanaotokea kwenye Kaya masikini,ambao kimsingi hawadhaminiki pale wanapohitaji mikopo ya kuwekeza kwenye biashara ndondogo au kilimo-biashara.Fedha hizo hazitatolewa kwa matumizi tofauti na kuizalisha fedha.Hii itatimiza jukumu la Tasaf kwa Kaya masikini.

4. Itawakomboa wanawake kwenye mikopo ambayo ni mwiba kwenye maisha yao.Kama nilivyogusia hapo juu kwamba mikopo itatolewa kwa riba nafuu,na kuweka fedha yaani Deposit itasaidia kutoa fursa kwa wengine wenye uhitaji.Nadhani mfumo utazingatia mfumo wa teknolojia hivyo kila baada ya mauzo ya siku au wiki mtu atahitajika akaweke fedha yaani ….

5. Itarahisisha zoezi la kuwasaidia wananchi kwenye miradi ya maendeleo na fedha za kujikimu kila mwezi,kwani hali ilivyo sasa fedha zinazotolewa pasi na kuwapa jukumu la kurejesha lakini kupitia benki hii ya kijamii tayari kuna kundi kubwa la watu ambao watashiriki kuzalisha fedha na kuzirejesha baada ya kupewa elimu ya biashara sanjari na kusimamiwa kwa ukaribu.

6. Benki ya jamii itapunguza makato na urasimu wa fedha zilizotengwa kwaajili ya wahitaji.Nina shuhuda za mapungufu yaliyojitokeza kwenye miradi ya kijamii iliyofadhiliwa na Tasaf ,baadhi ni utaratibu mbovu wa utoaji ,kuna kikundi kilipitishwa ili kipate fedha za mradi wa ufugaji lakini fedha zilipitia kwa Afisa Maendeleo wa wilaya ambaye,alihusika na miamala ya kibenki,alitoa maelekezo hadi duka la kununua vifaa vya ujenzi wa banda,bado aliongeza vifaa kwenye invoice na akawaambia vilivozidi ni vyake.Huu ni mfano unaodhihirisha umuhimu wa Tasaf kuja na benki yao.

7. Zitaongezeka fursa za ajira kwa wasomi waliohitimu kozi za Ujasiriamali,Masoko,Usimamizi wa fedha,biashara,Utunzaji kumbukumbu,Maendeleo ya jamii na Ustawi wa jamii na zinginezo.

8. Pia walengwa wa mpango wa kunusuru Kaya masikini kwa kuwapa fedha za kujikimu na kufanya miradi mbalimbali,watarahisishiwa zoezi la kupokea fedha zao kwa wakati na bila kuwa na maswali yasiyo na majibu ,maana ofisi za benki itakuwa ni sehemu sahihi ya kupata taarifa rasmi.

Hitimisho.

Kwa kuhitimisha ieleweke kwamba benki hii haitazuia benki za kibiashara kupata wateja kwakuwa hii ya jamii itahusika na Kaya masikini na haitakuwa ya kujinufaisha, hivyo itakuwa ni kama taasisi ya kijamii yenye mlengo wa kuwainua wananchi wa chini kiuchumi.Kwa kuwapa mikopo yenye riba rahisi zaidi na elimu ya uwekezaji na ufatiliaji wa karibu katika biashara zitazoanzishwa na walengwa.Hili ni moja ya mabadiliko ambayo natamani kuyaona yakitekelezwa,ni matumaini yangu baada ya miaka 10 hadi 15 mbele Tanzania itakuwa ni nchi ya mfano kati ya zingine zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo kwa sasa zinajulikana kama nchi masikini.

Asanteni kwa muda wenu.

Nawasilisha.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom