SoC02 Tatizo la Njaa Bara la Afrika

SoC02 Tatizo la Njaa Bara la Afrika

Stories of Change - 2022 Competition

M GABAGAMBI

New Member
Joined
Oct 2, 2020
Posts
2
Reaction score
1
Bara la Afrika kwa kipindi kirefu sasa pamekuwa pakikabiliwa na tatizo au baa la njaa japo kuwa nchi za Afrika ni wazalishaji wa mazao ya chakula kwa asilimia kubwa yaani uti wa mgongo wa uchumi wa nchi za Afrika umekuwa ukitegemea katika kilimo.Ni jambo la aibu sana kwa nchi za Afrika pamoja na waafrika tokea kupata Uhuru kutoka kwa wakoloni mpaka sasa hivi bado tunakabiliwa na tatizo la njaa wakati nguvu kubwa ya watu wa Afrika imeegemea zaidi kwenye kilimo.

Licha ya kuwa na kila aina ya utajiri bado watu wa Afrika tatizo ambalo limekuwa likiwasumbua ni njaa, mfano kuwepo kwa utajiri kama:-

Mito na vyanzo vingi vya maji.
Kwa kiwango kikubwa nchi nyingi za Afrika zimezungukwa na vyanzo vingi vya maji ambavyo msimu mzima wa mwaka vimekuwa vikitiririsha maji. Chemchem, mito, mabwawa, maziwa ni moja ya vyanzo vya maji ambavyo katika bara la Afrika tumejaliwa kuwa navyo tena vyanzo hivi ni vya asilia kabisa na sio vya kutengenezwa; kwa mfano ziwa Victoria, ziwa Tanganyika, ziwa Chad, ziwa Nubia, ziwa Albert, ziwa Edward, ziwa turkana, ziwa Kariba, ziwa cabora bassa, kwa upande wa mito kuna mto Nile, mto Zambezi, mto kagera, mto kongo, mto Niger mto Limpopo, mto orange. Licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji bado watu wa nchi za Afrika tumekuwa tunakabiliwa na tatizo la njaa kuanzia nchi zetu zilipopata Uhuru na kuanza kujitawala hadi hivi sasa.

Mabonde makubwa kwa ajili ya kilimo.
Utajiri mwingine ni kuwa na ardhi kubwa yenye rutuba kwa ajili ya kilimo.Katika maeneo mengi ya bara la Afrika ardhi inayo uwezo wa kutoa chakula kwa misimu yote ya mwaka; yaani kipindi cha masika, vuli na kiangazi.

Mbali na mazao ya chakula tu pia vile vile ardhi ya nchi za bara la Afrika pamekuwepo na ustawi wa matunda ya aina nyingi sana mpaka matunda pori, ndizi, miwa, maembe, machungwa, matango, nazi, parachichi, matikitiki maji ni baadhi ya matunda ambayo hupatikana kwa wingi katika bara la Afrika. Licha ya kuwa na mabonde mengi kwa ajili ya kilimo na watu kujishughulisha katika kilimo kwa asilimia kubwa bado watu wa Afrika wanakabiliwa na tatizo la lishe bora, utapia mlo, njaa pamoja na kutokuwa na utaratibu mzuri wa kula chakula.

Hali ya hewa nzuri.
Katika majira yote ya mwaka yaani masika,vuli na kiangazi pamekuwepo na hali ya hewa nzuri yenye kustawisha mazao kwa kiwango kikubwa; kwa bara la Afrika ni tofauti na mabara mengine ambayo yamekuwa na kuanguka kwa barafu kiasi cha kukausha mazao vile vile kwa upande wa jangwa Afrika ni tofauti na mabara mengine. Hivyo hali ya hewa nzuri iliyopo Afrika ni moja ya utajiri uliopo wenye kuruhusu kustawi kwa mazao mengi lakini bado watu wa Afrika wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la njaa kiasi cha kupewa na kupokea misaada na nchi za kigeni.

Nguvu kazi.
Watu wa Afrika wanasifika kwa kuwa na nguvu,miili yenye kuvumilia changamoto ya hali ya hewa;yaani jua,joto na baridi. Katika familia za kiafrika ndio familia zenye idadi kubwa ya watu, kwa familia moja idadi yake inaweza kuwa na watu kuanzia 5-9. Hivyo bara la Afrika tunayo nguvu kazi ya kutosha, nguvu kazi ni moja ya utajiri ambao tunao katika nchi za bara la Afrika ambapo kwa maksio ya haraka mtu mmoja barani Afrika anaweza kulima nusu hekari mpaka hekari nzima kwa siku nzima kwa kutumia jembe la mkono. Hivyo mbali na kuwa na utajiri huu wote wa kuwa na nguvu kazi ya kutosha katika kuzalisha chakula bado bara la Afrika tumekuwa tukikabiliwa na tatizo la njaa.

Matatizo ambayo yanasababishwa na kuwepo kwa tatizo la njaa katika bara la Afrika ni mengi kiasi kwamba kinafanya tusiweze kupiga hatua za kimaendeleo katika bara la Afrika na kuzidi kuwa wategemezi wa misaada kutoka nchi za kigeni, miongoni mwa matatizo hayo ni:-

Vifo.
Vifo vingi ambavyo vimekuwa vikitokea katika nchi za Afrika husababishwa na kuwepo kwa njaa iliyokithiri mfano.malawi, Burundi, Zimbabwe, DRC Congo, Somalia, Ethiopia,erithrea, Sudan kusini ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimekuwa zikikabiliwa na tatizo la vifo vingi vikisababishwa na kuwepo kwa njaa njaa ambapo idadi kubwa ya watu wamekuwa wakitegemea misaada ya chakula kutoka shirika la umoja wa mataifa.Lakini pia kwa nchi ya Tanzania katika miaka ya 1980 tulikabiwa na hali mbaya ya kuwepo kwa njaa.

Ulemavu.
Mara nyingi vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuwepo kwa watu ambao wamekuwa wakipata ulemavu katika kugombania chakula.Kuchomana visu,kukatana mapanga,kurushiana mawe pamoja na kupigana marungu imekuwa ndio mtindo wa watu wengi wa nchi za Afrika katika vurugu.Hivyo kukatika kwa viungo,majeraha na kuwekana alama katika miili imekuwa ikisababishwa na kuwepo kwa tatizo la njaa; yaani kugombania chakula miongoni mwa wahanga.

Ugomvi, kutokuelewa pamoja na kusambaratika kwa ndoa.
Migogoro mingi ambayo husababisha kusambaratika kwa familia na kutengana kwa ndoa pia husababishwa na kuwepo kwa tatizo la njaa. Mume au baba kushindwa kuhudumia au kuipatia familia mahitaji ya chakula imekuwa ndio chanzo migogoro, ugomvi na kutokuwa na maelewano mazuri katika familia.Na pia mara nyingi pamekuwepo na vitendo vya kikatili ambavyo vimekuwa vikitokea pindi mume au baba anaposhindwa kuleta au kutimiza mahitaji ya chakula.

Ukahaba na wizi.
Biashara ya ukahaba katika maeneo mengi ya miji na vijijini katika nchi za Afrika zimeshamiri kwa kiwango kikubwa,kwa sasa biashara ya ukahaba sio siri tena ambapo biashara hiyo hufanywa mpaka kwenye mitandao.Kwaharaka tafiti zinaonesha kuwa wengi hujiingiza katika biashara ya ukahaba kwa ajili ya kutafuta chakula au pesa kwa ajili ya kujinunulia chakula chao binafsi au cha familia. Vilevile katika wizi vijana wengi wamekuwa vibaka na wakwapuaji wa mali ndogo ndogo za watu wengine, kwa mfano maeneo ya mbagala, mabibo, manzese, keko na sinza kwa mkoa wa Dar es Salaam ni maeneo ambayo kumekuwepo na kukithiri kwa vitendo vya wizi mpaka wa nguo ndani kwa lengo la kuuza ili wapate pesa kwa ajili ya kununua chakula.

Hivyo ni aibu sana mpaka sasa mataifa ya Afrika kupokea misaada ya chakula kutoka nchi za kigeni.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom