TCRA hatuwaelewi kwanini hamjazima simu zisizosajiliwa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Miaka minne iliyopita, serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), iliutangazia umma kuwa kila anayemiliki simu, lazima ahakikishe kuwa anaisajili.

Ili kuhakikisha kwamba zoezi hilo linafanikiwa, TCRA ilitoa muda maalum wa miezi sita kuwa namba zote za simu za mkononi zisajiliwe kuanzia Julai Mosi hadi Desemba 31, mwaka 2009.

Hata hivyo, baada ya kuonekana kuwa zoezi hilo ni gumu na linagusa watu wengi, TCRA iliamua kuongeza muda wa kusajili namba za simu kwa miezi sita zaidi yaani hadi Juni 30, 2010.

Wakati muda huo ukiongezwa, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, alisema wamechukua hatua hiyo baada ya kufanyika tathmini kwa kuzingatia maslahi ya watumiaji na watoa huduma na wadau wengine nchini.

Alisema licha ya kwamba zoezi lilikuwa likiendelea vizuri, lakini lilikabiliwa na changamoto kadha wa kadha.

Profesa Nkoma alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni uandikishaji katika sehemu za vijijini, uhakiki wa kutambulika, ukosefu wa umeme kwa ajili ya kutolea nakala vivuli vya vitambulisho na kuingiza namba zilizosajiliwa katika database za mitandao ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa Profesa Nkoma, kwa wakati huo, idadi ya namba za simu nchini zilikuwa zikiongezeka maradufu kutoka 284,109 mwaka 2000 hadi kufikia 14,903,024 mwaka 2009.

Kwa msingi huo, alisema idadi ya namba za simu zilizosajiliwa kwa wakati huo, zilikuwa zimefikia asilimia 43.

Profesa Nkoma alisisitiza kuwa kazi ya kuweka utaratibu wa kusajili namba za simu katika sheria ulikuwa unaendelea na ikikamilika itakuwa ni lazima kwa mtu yeyote anayemiliki namba za simu kujisajili.

Mkurugenzi huyo alisema sababu ya kuanzisha utaratibu wa kusajili namba za simu ni kuwalinda watumiaji na matumizi mabaya ya huduma za mawasiliano, kuwawezesha kuwatambua watumiaji wa huduma za ziada za simu, kuimarisha usalama wa taifa na kuwezesha watoa huduma za mawasiliano kuwafahamu vizuri wateja wao na kuwahudumia ipasavyo.

Kama hizo ndizo sababu alizozitoa Profesa Nkoma za kusajili namba za simu, sisi kwa hakika tunaona kama hazijafikiwa.

Tunasema hivyo kwa sababu hadi sasa yapata miaka minne tangu zoezi la usajili wa namba za simu lianze lakini bado tunashuhudia watu wasio waaminifu, wakiendelea kutumia namba za simu zisizosajiliwa kufanyia vitendo viovu huku TCRA iliyoweka utaratibu huo, ikiwafumbia macho.

Baadhi ya watu wanatumia namba hizo kutukana watu wengine, tena kwa bahati mbaya sana wanawatukana hata viongozi, kufanyia utapeli wa aina mbalimbali pamoja na kutoa vitisho vya kila aina.

Hakika inasikitisha kuona kwamba yote hayo yanatokea huku mamlaka zinazohusika zikishuhudia katika kipindi chote hicho cha takriban miaka minne.

Tulitarajia kwamba kusajiliwa kwa namba za simu, kungesaidia sana kama siyo kumaliza kabisa vitendo kama hivyo.

Hata hivyo, jana Profesa Nkoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema uchunguzi uliofanyika nchini kote, umegundua kuwa pamoja na usajili wa namba za simu kuwa wa lazima kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (Epoca) ya mwaka 2010, kuna ukiukwaji mkubwa wa matakwa ya sheria na kanuni za usajili wa namba za simu.

Profesa Nkoma alikuwa akisoma tamko la pamoja kwa umma la TCRA na kampuni zinazotoa huduma za simu kuhusu usajili wa namba za simu za mkononi nchini.

Alisema kutokana na hali hiyo, Aprili 4-11, mwaka huu, TCRA na kampuni za simu, walikutana na kukubaliana juu ya hatua za kumaliza kabisa tatizo la usajili wa namba za simu.

Alisema jambo jingine walilokubaliana na kampuni hizo ni utaratibu wa kufungia namba zote za simu ambazo hazikusajiliwa.

Profesa Nkoma alisema TCRA ikishirikiana na kampuni za simu na vyombo vya usalama, imeanza kampeni endelevu yenye lengo la kuwabaini wote wanaohusika na uvunjifu huo wa sheria.

Alisema kampeni hiyo pia inalenga kuwalinda watumiaji wema na jamii kwa jumla kwa ajili ya kuimarisha usalama na kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi.

Hata hivyo, sisi tunadhani hatua hii imechelewa kuchukuliwa kwani madhara yake tayari yameanza kujitokeza katika jamii.

Tulichotarajia ni kwamba, mara baada ya agizo la mwisho la kusajili namba za simu, kusingekuwapo na namba zozote za simu ambazo hazijasajiliwa ziendelee kufanya kazi.

Hata hivyo, licha ya kwamba TCRA imechelewa kuchukua hatua hiyo muhimu, tunashauri kwamba ni muhimu kwa sasa kuwa makini kuhakikisha kwamba namba ya simu isiyosajiliwa, inafungwa.

Kwa kufanya hivyo kutasadia sana kupunguza vitendo mbalimbali vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikifanywa kupitia namba za simu zisizosajiliwa.






CHANZO: NIPASHE

 
Bongo kila kitu usanii
zaidi Bongo tambarare.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…