KUZINGATIA HITAJI LA KISHERIA LA KUSAJILI NA KUTUMIA MAJINA YA DOT TZ (.TZ DOMAIN NAMES) NCHINI
Kwa mujibu wa Kifungu cha 79 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Cap. 172 R.E. 2023, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ina wajibu wa kusimamia uendeshaji wa rajisi ya majina ya vikoa vya .tz (.tz domain names registry) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kanuni ya 3(1) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Usimamizi wa Majina ya Vikoa) 2020, iliyorekebishwa mwaka 2023, inazitaka kampuni, taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, ubia, au mashirika ya kijamii yaliyosajiliwa na kufanya biashara nchini Tanzania ambayo yanafanya mawasiliano kwenye mtandao wa intaneti, kusajili na kutumia majina ya kikoa cha dot tz.
Vilevile, Kanuni ya 3(2) inataka jina la kikoa lililosajiliwa litumike kwa mawasiliano yote rasmi ya kielektroniki isipokuwa kama imethibitishwa kitaalamu kuwa haiwezekani.
Pia, Kanuni ya 25 inatamka kwamba mtu yeyote mwenye jina la kikoa ambalo halizingatii Kanuni iliyotajwa hapo juu atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni tano au kifungo kisichopungua miezi kumi na mbili au vyote kwa pamoja.
Kwa muktadha huu, TCRA inazikumbusha kampuni, taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na kijamii yaliyosajiliwa na kufanya shughuli nchini, kutekeleza matakwa ya kisheria yaliyotajwa hapo juu kwa kusajili na kutumia majina ya vikoa vya dot tz.
Usajili wa majina ya dot tz (.tz) unaweza kufanywa kwa kutembelea
Karibu.TZ | .TZ Domain names registration portal. Kwa maelezo zaidi kuhusu usajili huo na masuala mengine yanayohusiana nayo, tafadhali wasiliana na TCRA kupitia anuani iliyopo hapa chini.
Imetolewa tarehe 29 Julai 2025.
Digitally Signed by JABU KUVE BAKA
Dkt. Jabiri K. Bakari MKURUGENZI MKUU