SoC03 Teknolojia inavyoweza kusaidia kutoa mikopo (ya Halmashauri) kwa vijana, wanawake na walemavu na kuwa na urejeshwaji mzuri

SoC03 Teknolojia inavyoweza kusaidia kutoa mikopo (ya Halmashauri) kwa vijana, wanawake na walemavu na kuwa na urejeshwaji mzuri

Stories of Change - 2023 Competition

Prof Janabi wa JF

Senior Member
Joined
Jul 7, 2023
Posts
165
Reaction score
450
Bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2023/24 imeondoa 10% ya kuwakopesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambapo wataangalia utaratibu mzuri wa kutoa fedha hizo kama mikopo kwa kuwa kwa sasa walikuwa na changamoto ya utoaji na urejeshwaji wa mikopo hiyo.

Nimeona ni vyema niandike kitu ili kusaidia namna bora ya kutoa fedha hizo kwa kundi lengwa na kuwa na urejeshwaji mzuri hali ambayo inaweza kufanya mikoo hiyo iendelee kuwanufaisha watu wengi zaidi na kuondoa umasikini nchini.

Kwanza naomba niseme kuwa mbali na kuwa na changamoto kwenye urejeshwaji wa mikopo hiyo, pia kuna changamoto ya mahusiano kwa kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa makundi ambayo mara nyingine hulazimika kuungana hata kama hawana lengo la pamoja. Hali hii imechangia kushindwa kujua wa kumfuata kwa kuwa ni suala la kundi ni suala la mtu.

Hata hivyo uwepo wa teknolojia umerahisisha mambo na tunaweza kufanya vizuri katika kufikia kundi lengwa bila kuwa na hofu ya namna ya ukusanyaji wa mikopo hii ambayo kwa mwaka huu haitatolewa, hivyo mwaka huu wa fedha uwe ni mwaka wa kuweka mipango sawa kwa mwaka ujao wa fedha au muda wowote tutakaoona unafaa.

Namna ya utoaji Mikopo

Nashauri mikopo hii itolewe kwa mtu mmoja mmoja kupitia mitandao ya mawasiliano, yaani Tigo, Voda, Airtel nk. Ambapo mtu wa kupata mikopo hiyo sio tu awe mteja yoyote bali awe mteja mwenye lipa namba (Ambayo inamtambulisha kuwa ni mjasiliamali) na akaunti yake iwe ni ile ambayo imewahi kupokea malipo kwa muda fulani mathalani miezi sita, ili tuwe na uhakika kuwa tunamkopesha mtu ambaye hajachukua namba tu kwa ajili ya mkopo bali ana biashara ambayo inafanya kazi.

Aidha, kuwa na uhakika wa umri, hali ya ulemavu na jisnia ya muomba mikopo ni rahisi kwa kuwa mtu huyu atakuwa ametumia namba ya NIDA kujisajili, pia anapochukua lipa namba taarifa zaidi zichukuliwe ili kuwa na uhakika wa hali yake. Hapa tutakuwa na uhakika kuwa mikopo inawafikia kundi lengwa.

Aidha, mikopo hii iwe inahamishika, yaani mtu akibadili lipa namba kwa namna yoyote deni linamfuata na kama ataamua kuacha biashara, bado tunamjua kwa kuwa ametumia namba ya NIDA, kwa hiyo deni litakuwa kwenye namba ya NIDA haijalishi atatumia mtandao gani kujisajili upya tutamjua na tutamkata fedha yetu hadi inapoisha.

Hapa utaona suala la kuwa kundi halina nafasi, kwa kuwa anakopeshwa mtu mmoja mmoja ambapo wao wakiona haja ya kuungana wataungana na kuwa kundi kutokana na biashara yao bila kuwa na nia ya kupata mkopo bali ni nia ya kutumia mkopo waliopata, hii italeta kitu kiuchumi kinachoopendekezwa sana ”Voluntary union” yaani ni uamuzi sio kwa kuwa ni sharti.

Mfumo huu, ni muhimu ili kuepuka mambo mengi ikiwemo kushindwa kurejesha mikopo, kwa mfumo huu mtu atapewa grace period kama kawaida, ila baada ya hapo fedha itakuwa inakatwa kwa lipa namba au namba yake ya simu ya kawaida ili kurejesha mkopo, hapo itakuwa inapunguza gharama za ufuatiliaji na hatari(risk) ya kupoteza fedha kama ilivyokuwa kwa miaka mingi baada ya kuanzishwa mikopo hii.

Umuhimu wa ziada

Kwa muda mrefu tumekuwa tukihangaika kulipa kodi kwa kuwa wengi wanatumia cash kulipia bidhaa, kwa namna hii wanaotaka mikopo watawaomba watu wao walipe kupitia lipa namba ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata mikopo mikubwa hali ambayo itaongeza mapato ya serikali kwa kuwa ni ngumu mtu kukwepa kodi kwa malipo ya kielectronik.

Aidha mfumo huu utatuweka katika nafasi nzuri ya kuufikia uchumi wa kidigitali kama ilivyo katika Digital Economy Frame Work, ambapo pia tutaibua fursa nyingine za ufanyaji wa malipo na kuendelea kufaidi fursa hizo huku tukipunguza gharama za ukusanyaji wa mapato.

Fiada za mikopo ya halmashauri kwa njia ya kielekroniki

Faida kubwa ni kuwa ni rahisi kuwafikia kundi lengwa na ni rahisi kukusanya marejesho kwa kuwa watu wanatumianjia za kielektroniki kupata malipo na pia kwa kuwa tunasajili kwa NIDA ni rahisi kufahamu kila taarifa muhimu ya mtu tunayempa mkopo.

Faida nyingine ni kuwa tunakuwa na uhakika wa fedha ambazo mfanyabiashara anazizungusha kwa kuwa kabla ya kumpa mkopo tunabidi kuangalia miezi sita iliyopita mzunguko wake ulikuwaje kupitia namba yake ya kupokea malipo ya biashara (Lipa Namba). Hii italeta ugumu mtu kughushi kwa kuwa namba lazima iwe na jina lenye uhusiano na yeye, tofauti na sasa watu wanaweza kuomba workshop ya mtu kujidai yao ili wapewe mikopo. Biashara iangalie mzunguko wa hela sio masuala ya kama mtu ana kibanda, hii ni enzi ya kidigitali.

Mfumo huu ni rafiki kwa kukusanya mapato kutoka kwa sekta isiyorasmi (Informal Sector) kwa kuwa watu watahamasishana wenyewe kutumia malipo kwa lipa namba hali ambayo ni muhimu kwa mamlaka za ukusanyaji kodi.

Wazo hili linatekelezeka, wala halihitaji utaalamu mkubwa, wala halitaingilia mfumo wa kawaida wa ukopeshaji uliopo wa mtandao kwa kuwa riba yake na namna yake ya ukopeshaji ni tofauti na mikopo inayoendelea mtandaoni, mathalani mikopo ya mtandao inaangalia tu transactions hata kama hana biashara(lipa namba).

Namna nyepesi itakavyofanya kazi
Menu ya huduma za serikali itakuwa na sehemu ya kuomba mkopo, ambapo muombaji ataweka Lipa namba yake na system itaangalia miamala ya Lipa namba, na asili yake ili kujua Halmashauri anayotokea. Kisha itaangalia kama fedha zipo za kuweza kumpatia. Uwezekano unapokuwepo, muombaji atatakiwa kuweka namba yake ya NIDA(ili kuhakiki kuwa LIPA NAMBA anayotumia ni yake, umri na jinsia ya mwombaji) na kuweka taarifa nyingine zinazotakiwa kuhusu biashara yake kisha atapokea mkopo ndani ya muda mfupi.

Changamoto
Changamoto ni changamoto kutambua hali ya ulemavu wa mtu kwa system. Hata hivyo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inaweza kusaidia katika kutambua hali za ulemavu wa watu na kuwapa namba maalumu inayotaja aina ya ulemavu alionao. Aidha, taarifa ya ulemavu inaweza kuwa inawekwa kwenye taarifa zinazokusanywa na NIDA au wasajili wa biashara ili kuweka wepesi katika hilo.

Nipeni Kura zenu
 
Upvote 3
Back
Top Bottom