The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Katika ulimwengu wa kisasa unaozingatia teknolojia, kuna uvumbuzi mwingi sana wa kurahisisha maisha yetu. Teknolojia saidizi imekuwa muhimu sana kwa watu wenye ulemavu, wazee, na watu walio na maradhi mbalimbali.
Teknolojia saidizi (assistive technology) ni vifaa au programu yoyote ambayo inakusudiwa kuongeza, kudumisha, au kuboresha uwezo wa utendaji wa watu wenye ulemavu, wazee, watu wenye mbalimbali kama vile kiharusi n.k. Vitu hivi vinaweza kuwa ni kiti cha magurudumu, programu ya kompyuta, kibodi (keyboard) au kipanya (mouse) maalum inayoweza kumsaidia mtu mwenye ulemavu kufanya kazi ambayo vinginevyo ingekuwa ngumu au isiyowezekana.
Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa zaidi ya watu bilioni 2.5 wana uhitaji wa kifaa kimoja au zaidi cha usaidizi ili kusaidia mawasiliano na utambuzi, ila watu bilioni moja kati yao hawana/hawawezi kupata huduma hizo.
Hii inatokana na sababu kama vile gharama kubwa, ukosefu wa ufahamu, upatikanaji, sera na ufadhili.
Uchambuzi wa nchi 35 iliofanywa kuhusu teknolojia saidizi unaonesha pengo kubwa kati ya nchi tajiri na zinazoendelea ambapo wakati ufikiaji ukiwa asilimia 3 katika mataifa maskini na ya kipato cha kati, kwenye mataifa tajiri uwezekano wa wananchi kupata vifaa hivyo vya usaidizi ni asilimia 90.
Teknolojia saidizi inaweza kuwa na matokeo chanya kwa afya na ustawi wa mtu na familia yake, pamoja na manufaa mapana ya kijamii na kiuchumi. Zinasaidia pia kumpatia mtu uhuru, kuweza kufanya mawasiliano, kufurahia na kufikia mazingira mbalimbali, burudani, na hatimaye kuleta furaha.
Matumizi sahihi ya visaidizi vya kusikia kwa watoto wadogo, kwa mfano, vinaweza kusaidia kuimarisha ustadi wa lugha. Hii inaweza kumsaidia mtoto katika maisha yake ya kijamii na ya baadaye kwani kama tunavyojua, watu wenye changamoto za ulemavu – hasa ulemavu wa kutosikia – wana fursa ndogo sana za kielimu na ajira. Ingawa si wanafunzi wote wenye ulemavu wanahitaji au wanastahiki teknolojia saidizi, lakini aina mbalimbali za ulemavu zinahitaji zana hizo.
Teknolojia saidizi pia inaweza kuwawezesha wazee kuendelea kuishi nyumbani na kuchelewesha au kuzuia hitaji la kuhudumiwa kila kitu. Kupunguza utegemezi wa matunzo kunawafanya wawe huru zaidi.
Vifaa/zana hizi zinaweza kuongeza usalama na kuboresha maisha ya kijamii. Inasaidia kuleta amani, si kwa wale wanaozitumia tu, bali pia kwa familia zao na marafiki, wafanyakazi wenzao, na walezi.
Kwa ujumla, manufaa ya teknolojia saidizi yanaweza kuchukua jukumu muhimu katika kuboresha maisha kwa watu wengi.
WHO inapendekeza kuwa utoaji wa teknolojia saidizi unahitaji kuunganishwa katika sekta zote muhimu za maendeleo: afya, elimu, kazi n.k. Kila nchi inahitaji kuwa na sera na mpango na usaidizi wa kutosha wa kibajeti ili kuboresha ufikiaji wa teknolojia saidizi kwa kila mtu, kila mahali bila matatizo yoyote.
Pia inapendekezwa kuwa inapohitajika, kipaumbele maalum kinapaswa kutolewa kwa watoto wenye ulemavu, watu walio na ulemavu zaidi ya mmoja au ule mbaya zaidi, wazee na watu wengine walio hatarini.